HEADLINES

Matumizi ya kondomu ni kujidanganya - Mada

Wavuvi wadai Magugu maji yanasaidia kurejesha vizazi vilivyokuwa vinatoweka

NCCR - Mageuzi wakiri migongano inakiua chama chao

Sheikh Mtopea aibuka na mpya

Waonyesha kanda za ngono hadharani kukiona

Kizimbani kwa kumshambulia msichana mwenzake

Mzee atuhumiwa kumtukana mwanae

Madawa ya kulevya husababisha unyanyasaji kwa wanawake

Kortini kwa kuugua Kipindupindu

 

 

Matumizi ya kondomu ni kujidanganya - Mada

lIna vitundu vinavyochojoa kuingiza hewa

lVitundu hivyo huweza kupitisha virusi

Na Dalphina Rubyema

 

IMEELEZWA kuwa Kondomu siyo kifaa madhubuti cha kuzuia ugonjwa hatari wa Ukimwi kama wengi wanavyofikiri.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na mtoa mada katika semina ya uelimishaji juu ya ugojwa hatari ya ukimwi,Bibi Zamoyoni Abdalah ,semina iliyoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la PASADA iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Chuo cha Uhasibu (DSA) kilichopo Kurasini Jijini.

Akitoa ufafanuzi zaidi juu ya Kondomu, Bibi Zamoyoni alisema kuwa kondomu zina vitundu (pores) ambavyo vimewekwa kwa ajili ya kupitisha hewa ili zisigandamane na hivi vitundu vinawezo mkubwa wa kupitisha virusi vya ukimwi.

Aliongeza kuwa mbali na vitundu hivyo,kondomu pia zina madhara yake ambapo wakati wa kujamiiana kondomu zinaweza kupasuka,kuvuja,kuteleza na pia kondom hizo baadhi yake zilitengenezwa zamani hivyo zinakuwa zimeisha haribika.

Aidha Mtoa mada huyo alisema kuwa usafiri wa kondomu hizo ni wa taratibu mno ambapo alisema zinasafirishwa katika meli kutoka Marekani hadi Tanzani na zoezi hilo linachukuwa zaidi ya miezi mitatu ambapo zikisha ingizwa nchini zinatolewa kwenye maboksi na kuingizwa kwenye maboksi mengine ambapo uwe kwa nembo ya 'Salama Condom'kitu na kuwekwa nembo ya Tanzania kwa kuimanisha kuwa zimetengenezwa nchini kitu ambacho alikipinga.

Kutokana na madhara hayo ya kondomu,Bibi Zamoyoni amewataka wananchi kuacha kabisa tabia ya uasherati ili kuepukana na ukimwi na kama mtu atashindwa kujizuia basi ni bora kuoa au kuolewa na mtu aliyepimwa ambapo kwa wale waliokwisha kuoana wametakiwa kuwa waaminifu kwenye ndoa zao na wala siyo kujidanganya kwa kutumia kondomu na kuwa na wapenzi zaidi ya mmoja huku ukijiamini kuwa huko salama.

 

WAVUVI WASHANGILIA UJIO WAKE

Wakati wataalamu wahaha kutafuta tiba ya Magugu maji:

 

lWadai unasaidia kurejesha vizazi vilivyokuwa vinatoweka

Na Mwandishi wetu

WAVUVI walioko katika vijiji kando mwa ziwa Victoria na waliomo ndani ya ziwa lenyewe wameelezea kufurahishwa kwao na kuwepo na magugu maji katika ziwa hilo kwa madai kuwa hali hiyo imesaidia kurejesha vizazi vilivyoanza kutoweka vya samaki wenye asili na ziwa hilo.

Zaidi ya aina 200 ya vizazi vyenye asili ya ziwa hilo vimepotea tangu samaki wanaokula samaki wengine Nile Perch maarufu kama sangara kwa upande wa tanzania na mbuta upande wa Kenya kupandikizwa katika ziwa hilo kwenye miaka ya sitini. Tatizo la magugu maji limekuwa kero kwa serikali zote zinazounganika na ziwa Victoria kiasi cha kuomba msaada wa kuyaondoa kwa madai kuwa yanahatarisha vizazi vya samaki.

"Si kweli kuwa kuna athari za magugu maji kwa samaki? Athari inapandikizwa tu kwa kuwa samaki hao wala samaki na ukubwa wao hawawezi kuishi na hewa kidogo", alisema mvuvi mmoja na kuongeza kuwa magugu hayo yamewezesha sasa kukamata aina mbali mbali za samaki wakiwemo barbus au odhadhu kwa Kenya kwa Kabila la Waluo, ninge, Ochere, Muni na Kambare (wazoefu)

Watafiti wanasema kwamba magugu maji yanatengeneza aina fulani la kapeti ambalo linazuia walaji samaki wadogo kama ndege na samaki wakubwa kuvamia eneo hilo.

Aidha kapeti hilo linazalisha chakula cha samaki wadogo ndio maana kutokana na usalama kuwa mkubwa na chakula kuwa kingi samaki hao wameanza kupatikana.

Mtafiti mmoja wa kituo cha utafiti cha Kenya KEMFRI Bw. Robert Obuga akiongea na mwandishi wa All Africa News Agency, AANA, amesema kwamba kero kwa wataalamu limekuwa ni nafuu kwa wavuvi wadogo na kwa tabia za baadhi ya makabila.

Aidha mtafiti mwingine wa KEMFRI pia Bw. Tsuma Jembe amesema magugu maji yanasaidia pia kuondokana na uvuvi unaopitisha kiwango. Amesema uvuvi wa kokoro umekuwa chanzo cha kuangamiza samaki wote lakini kwa kuwa magugu maji yapo wavuvi hawawezi kutupa nyavu kama wanavyotaka.

Habari zaidi zinasema kwamba wavuvi katika ziwa hili Victoria lenye mzingo wa kilomita za skwea 68,000 sasa hivi wanashuhudia samaki wengi wa asili wa ziwa hilo wakianza kuonekana.

Waluo wanafurahia sana kuwepo kwa samaki odhadhu ambaye hutumika sana katika kuwakarimu wageni hasa mashemeji na wakwe.

Ingawa kurejea kwa samaki wa asili kumewafurahisha wenyeji wengi magugu maji bado yamekuwa kero kwa wavuvi wakubwa ambao wanaviwanda. Wafanya biashara hao wamesema hawaelewi watu wanafurahia nini na magugu maji kwa kuwa mtu hawezi kuishi kwa kutengemea ladha ya samaki wa asili.

Wanadai kuwa uvuvi ni biashara kwa hiyo tishio lolote kwa uvuvi wa kibiashara lazima liondoshwe.

Tayari ipo mipango mbali mbali takribani katika nchi zote kufanikisha uondoaji wa magugu maji kitendo ambacho pia kimeleta hisia tofauti miongoni mwa wakazi wa kandoni mwa ziwa wanaotegemea maisha yao kazi za uvuvi.

 

 

NCCR - Mageuzi wakiri migongano inakiua chama chao

Na Dalphina Rubyema

IMEFAHAMIKA kuwa migogoro ya Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi Taifa,Bw.Agustine Mrema na katibu wake Mabele Marando na kunasababisha ukosefu wa ushirikiano miongoni mwa wanachama hao ambao wengine wanafuata kambi ya Bw.Mrema na wengine kambi ya Bw.Marando.

Hayo yalisememwa hivi karibuni katika mkutano cha Wajumbe wa Hamlamashauri ya chama hicho Jimbo la Temeke uliofanyika ukumbi wa Omax Inn uliopo Keko Magurumbasi Jijini.

Wajumbe hao wakitoa matatizo mbalimbali yanayooneka ndani ya chama chao, walisema kuwa tangu kuwepo na mgogoro baina ya Bw,Mrema na Bw.Marando,kumekuwa na ulegevu wa hali ya juu ndani ya chama ambapo viongozi hata wa kata wanashindwa kuafikiana na hali kama hii zaidi imejitokeza katika kata Mtoni.

"Sisi viongozi wa NCCR-Mageuzi kata ya Mtoni tunashindwa kuelewana kabisa,Mimi kama mwenyekiti wa kata hiyo nikiitisha kikao baadhi ya wajumbe hata viongozi wanakataa kuja lakini kama anayehutubia ni Bw.Mrema hapo kila mmoja anajitokeza,hali kama hii inaonyesha jinsi gani Kata ya Mtoni ilivyo na u-Mrema na U-Marando"alisema Mwenyekiti wa NCCR kata ya Mtoni.

Wajumbe hao kutokana na hali hiyo inayojitokeza miongoni mwa wanachama,itafika hatua Wanachama wote washindwe kuudhulia mikutano endapo atakayekuwa akihutubia siyo Bw.Mrema au Marando na hii ni hatari kwa Chama hicho.

Aidha katika Mkutano huo ilielezwa kuwa Mwenyekiti wa NCCR-tawi la Magurumbasi B,hawajibiki kwa vile tawi lake haidi hivi sasa tawi lake bado halijafanya uchaguzi na wala ofisi ya Mwenyekiti wa Jimbo haina taarifa nini zidi kimekwamisha uchaguzi huo.

Kutokana na hali hiyo inayoendelea kujitokeza ndani ya Chama hicho Mwenyekiti wa Jimbo Bw.Peter Chisunga aliwataka wajumbe hao kuzidisha ushirikiano na waachane kabisa na mgogoro wa Bw.Mrema na Bw.Marando.

"Tuzidishe ushirikiano jamani kama kuna mgogoro wowote kwenye kata au tawi fulani tuumalize haraka tusingoje ukomae kwani tumeisha ona ule wa Bw.Mrema na Bw,Marando"alitoa msisitizo Mwenyekiti huyo.

 

 

Sheikh Mtopea aibuka na mpya

lAzungumzia serikali za mitaa na kuahidi kuisambaratisha CCM mwakani

Na Dalphina Rubyema

CHAMA cha NCCR-Mageuzi Jimbo la Temeke,kimejizatiti kushinda katika uchaguzi wa viti vya serikali za mitaa pamoja na Madiwani,uchaguzi utakaofanyika hapo mwakani.

Akizungumza kwenye mkutano wa Wajumbe wa Halmashauri kuu jimboni humo uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Omax Inn uliopo Keko Magurumbasi jijini, Makamu Mwenyekiti wa Wazee NCCR ngazi ya Taifa Sheikh Kassim Mtopea alisema kuwa yeye kama mpiga debe maarufu wa chama hicho atahakikisha kazi yake hiyo ya kupiga debe kwenye Jimbo zima ambapo alisema kutokana na bidii yake hiyo ana uhakika wa chama hicho kuchukua viti vingi.

Sheikh Mtopea ambaye alikuwa Mwenyekiti kwenye Jimbo hilo kabla Bw.Peter Chisunga hajashika madaraka,alisema kuwa NCCR ina wapenzi wengi na hivyo anauhakika wote wakipiga kura Chama tawala cha CCM hakitapata viti vingi kwenye uchaguzi huo.

Katika kufanya maandalizi ya kabla ya uchaguzi huo,Sheikh Mtopea amewataka viongozi ambao ni Mwenyekiti Bw.Peter Chisunga na Katibu wake Bw.Juma Kilimba kuandaa ratiba ya kuzungukia kata zote za Temekeambapo yeye Mtopea ataongozana na viongozi hao kwa kupitia kila kata ambapo watakuwa wanahamasisha wananchi juu ya uchaguzi huo.

Pamoja na kuwa na imani ya kunyakua viti vingi kwenye chaguzi hizo,Sheihk Mtopea ambaye kwa hivi sasa amenyoa ndevu zake zilizokuwa ndefu na nyeupe ambazo alidai zilikuwa zinamfanya aonekane mzee na kuongeza kuwa kunyoa ndevu ni kwenda na wakati,amewataka wanachama wote wa NCCR-Mageuzi kuwa na msimamo wa hali ya juu na chama chao na siyo kushawishiwa kujiunga na vyama vingine.

"Kuweni makini sana watu wa vyama vingine kikiwemo chama tawala cha CCM,wanatutafuta sana wana-NCCR ili tujiunge na vyama vyao,mimi nimeisha shawishiwa na vyama zaidi ya vinne lakini sijakubali na wala sitakubali kujiunga na chama kingine,nitakufa na NCCR,Mtopea ni NCCR na NCCR ndiyo Mtope"alisema Sheikh Mtopea.

Sheikh Mtopea amepinga vikali habari zilizoandikwa na gazeti moja linalotoka kila siku , kwamba yeye amekikimbia chama cha NCCR kitu ambacho alisema siyo cha ukweli,"Mimi sijaikimbia NCCR bado ni mwanachama hai"alisema.

Waonyesha kanda za ngono hadharani kukiona

Na Said Mmanga,MSJ

OFISI ya utamaduni wilaya ya Temeke inakusudia kuwachukulia hatua watu wote wanaoonyesha kanda za ngono kiholela na hivyo kuharibu utamaduni wa taifa.

Akiongea na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake mwishoni mwa wiki afisa utamaduni wa wilaya hiyo Bw. Nestory Wisandara alipotakiwa kutoa ufafanuzi ni hatua gani ofisi yake itachukua dhidi ya watu wanaoonyesha kanda za ngono katika kumbi za starehe na katika ofisi za vyama vya siasa hasa za chama cha mapinduzi, alisema kuwa ofisi yake ilikuwa haina taarifa juu ya vitendo hivyo lakini itachukua hatua za mara moja kukabiliana na hali hiyo.

Alisema kuonyesha kanda hizo kiholela bila kujali watu wanaoangalia kwa kiasi kikubwa kunaharibu tabia za watoto na hivyo kuuvuruga utamaduni wa taifa ambapo moja kati ya hatua watakazozichukua ni kuanzisha msako katika sehemu mbalimbali ambazo zinaonyesha picha za video.

Bw. Wisandara alisema wengi kati ya watu wanaonyesha video hizo hawana leseni ya kufanya biashara hiyo ambapo alisisitiza hata kama mtu atakuwa na leseni lakini hairuhusiwi kuonyesha kanda hizo kiholela ambapo alisema wale watakaopatikana watachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.

Aidha, aliwaomba wananchi wote kutoa taarifa katika sehemu zinazohusika mapema wakati wanapoona vitendo vyovyote vya uvunjaji wa sheria ambapo pia aliwataka viongozi wa serikali wa maeneo yote kuanzia mitaa hadi wilaya washughulikie kulinda maadili katika maeneo yao.

Alisema si vizuri kwa watoto kuonyeshwa picha hizo kwani zitakuwa zikichochea vitendo viovu na kuongeza kuwa si utamaduni wa kitanzania na kufanya hivyo ni kuhatarisha utamaduni na maadili ya kitanzania.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa uonyesha wa kanda za ngono katika kumbi za CCM na sehemu nyingine wilayani humo umekuwa ni wa hali ya juu ambapo waonyeshaji hutumia mbinu mbalimbli ili kufanya watu wasijue kitu kinachoendelea ndani ambapo wakati mwingine huandika maneno pilau, ndombolo au kibinda nkoi na kumbe kinachoonyeshwa ni kanda za ngono ambapo watu wa jinsia mbalimbali hasa watoto wadogo kuanzia umri wa miaka sita na kuendelea wamekuwa wateja wakubwa wa mikanda hiyo .

 

Kizimbani kwa kumshambulia msichana mwenzake

Na Getruder Madembwe

MSICHANA mmoja Rehema Omari mkazi wa Kawe Jijini amefikishwa mahakamani kujibu shitaka la kumshambulia msichana mwenzake Nasra Kanuti.

Mwendesha mashtaka wa polisi konstebo Bakari Bakari aliieleza mahakama mbele ya hakimu Janeth Mnyuwa kuwa mnamo Septemba 17 mwaka huu mshtakiwa akiwa nyumbani kwao alimsukuma Nasra hadi kuanguka chini katika maeneo ya Ukwamani bila sababu yoyote .

Mshitakiwa amekana shitaka na kesi imeahirishwa hadi Oktoba 20 mwaka huu .

Wakati huo huo mkazi mmoja wa Kawe, Benedictor Paul amefikishwa mahakamani kujibu shitaka la wizi wa kuaminiwa.

Mwendesha mashitaka wa Polisi Bakari Bakari aliieleza mahakama ya mwanzo Kawe mbele ya hakimu Janeth Mnyuwa alisema kuwa mnamo septemba 27 mwaka huu majira ya mchana katika maeneo ya Lugalo mshitakiwa alikabidhiwa baiskeli kwa ajili ya kuchotea maji kisha amrudishie mwenyewe Timothy Mwaipopo .

Mshitakiwa amekana shtaka na amerudishwa rumande hadi.

 

 

Mzee atuhumiwa kumtukana mwanae

Na Mwandishi Wetu

MZEE mstaafu Bw. Nicolaus Lyimo (60) mkazi wa kinondoni amepandishwa kizimbani na mwanaye katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo akikabiliwa na shtaka la kutoa matusi ya nguoni.

Akisomewa hati ya mashtaka na polisi wa mahakama hiyo Obedi Magoti mbele ya Hakimu Bi. Moga Starford ilielezwa kuwa mnamo 20 Septemba, mwaka huu majira ya saa 3.00 usiku huko mtaa wa Lindi mshtakiwa alimtolewa mwanaye matusi ya nguoni Bi. Debora Somoni ambaye ni mlalamikaji.

Mzee huyo alipohojiwa na hakimu kuhusiana na shtaka hilo kuwa alimtolewa mwanaye matusi ya nguoni akiwa kama ni mzazi wake alisema kuwa yeye alikuwa msuluhuishi wa mdogo wake pamoja na mwanaye.

"Tatizo nilikuwa mimi msuluhulishi wao na hicho ndicho kilichoniponya hadi kufikishwa hapa mheshimiwa". Alisema mzee Lyimo.

Kesi hiyo imeahirisha hadi hapo Oktoba, 9 mwaka itakapo tajwa tena na mshtakiwa huyo nje kwa dhamana ya wadhamini wawili wakiwa na vitabulisho.

Wakati huo huo. Kundi la ('10) wakiwa wanawake kwa wanaume wa kabila la kigogo kwa jina maarufu (Omba omba) waliswekwa ndani wakiwa na watoto wao pamoja na vifurishi vyao kwa shtaka la uzembe na uzuruzaji katika mahakama hiyo hiyo ya Kariakoo.

Wakisomewa shtaka hilo na polisi Obedi Magodi mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Bi. Moga Starford kuwa mnamo 28 Septemba, mwaka huu majira ya 12.00 usiku maeneo ya Bibi Titi Mohamed walikamatwa na askari na N.C 7712 Hamsa pamoja ana askari mwenzake wakiwa wanazurura onyo bila kazi.

Kina mama hao ambao kila mmoja alitoa hoja yake ya pekee wakidai kuwa "sisi tumewafuata waume zetu huko walikuja kufanya kazi huko Dar" walisema kina mama hao.

Kundi hilo ikiwa ni mzee Matonya na wenzake (9) walirundishwa rumande kwa kukosa wadhamini mpaka hapo kesi hiyo itakapotajwa tena 12 Oktoba, mwaka huu.

 

 

Madawa ya kulevya husababisha unyanyasaji kwa wanawake

Na Said Mmanga,MSJ

IMEELEZWA kuwa umasikini katika familia na utumiaji wa madawa ya kulevya na ulevi kwa vijana ni miongoni mwa mambo yanayosababisha unyanyasaji wa wanawake hapa nchini.

Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa idara ya wanawake na watoto katika wizara ya maendeleo ya jamii wanawake na watoto Bi. Priscila Ole Kambainei alipokuwa akifungua semina ya siku tano ya ushauri juu ya ukatili kwa wanawake na vijana,iliyoandaliwa na umoja waushauri wa misheni wa Afrika, Ulaya na Asia iliyokuwa ikifanyika katika ukumbi wa kituo cha kiroho Mbagala, jijini.

Alisema suala la umasikini limesababisha vijana wengi wakose ajira na hivyo kujikuta wakichanganyikiwa na matokeo yake kujiingiza katika vitendo vya ulevi na utumiaji wa madawa ya kulevya hali ambayo aliielezea kuwa ni chanzo cha vitendo vya unyanyasaji wa wanawake.

Bi.Kambainei alisema kuwa wakati umefika kwa viongozi wa Serikali, na mtu mmoja mmoja kuliangalia suala la vijana na kushirikiana kuwapa ushauri kwa kuwa vitendo vya unyanyasaji wanawake huwa vinaanzia nyumbani.

Alisema kuwa sababu kubwa ni kukosekana kwa mahitaji muhimu kwa vijana katika familia na matokeo yake wanamuua kuimbia nyumbani na kwenda mitaani ambako hujiingiza katika vitendo vya kihuni na utumiaji wa madawa ya kulevya.

Bi. Kambainei alieleza kuwa matokeo ya hali hiyo ni magonjwa na umasikini uliokithiri ambapo alisistizza umuhimu wa vijana kuangaliwa kwa ujumla na jamii izungumze nao ambapo alitaka serikali iwaangalie kwa kuangalia baadhi ya sheria na kuwahimiza washiriki wa semina hiyo kutumia mwanga watakaokuwa kuwa wameupata kutatua matatizo yanayoikabili jamii hivi sasa.

Mkurugenzi huyo alisema wakati umefika kwa Serikali, mashirika yasiyo ya Kiserikali,(NGO),namtu mmoja mmoja kushirikiana pamoja katika kuihamasisha jamii juu ya masuala ya wanawake na vijana,ambapo hata hivyo alisema baadhi ya tabia za wazazi zimechangia katika kuwafanya vijana wawe na mwelekeo mbaya ambapo alitolea mfano wazazi kupigana au kutoleana lugha chafu mbele ya watoto.

Lengo la semina hiyo lilikuwa ni kuangalia unyanyasaji wa wanawake na vijana na kuona ni kwa namna gani wanaweza kutatua matatizo hayo ambapo jumla ya nchi sita zilishiriki katika semina hiyo ambazo ni Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya watu wa Congo,Botswana,Cameroun, Namibia , Ujerumani na wenyeji wa Tanzania.

 

Kortini kwa kuugua Kipindupindu

Na Peter Kasonga,PST

Watu 16 wamefikishwa mahakama ya mwanzo na kupingwa faini ya shs. 1,000 kwa kosa la kutozingatia masharti ya afya kwani hao ni waliougua ugonjwa wa kipindupindu na kupona.

Mbele ya hakimu wa mahakama hayo Bi. Elizaberth Pole imedaiwa na Kaimu Afisa wa Afya wa mjini Bi Tatu Masunga kuwa watu hao ni wale waliolazwa katika kituo cha Afya cha Kizumbi na Chamaguha mwishoni mwa mwezi ulipita kwa kuugua ugonjwa wa kipindupindu.

Afisa hayo aliiambia mahakama kuwa baada ya kulazwa katika vitu hivyo na kupona ofisi yake ilichukua hatua ya kwenda katika makazi yao na kushuhudia kuwa watu hao wahawa vyoo na pia hawachemzshi maji ya kunywa.

Alisema kuwa ofisi yake kwa hivi sasa imeamua kuchukua hatua kali za kisheria za kuwafikisha watu wote mahakamani ambao wataugua ugonjwa huo na kupona ili wale ambao hawajaugua ugonjwa huo ili kuwa fundisho kwao.

Katika mahakama hiyo watu waliofikishwa na kupigwa faini ni Edward Gomba, Mipawa Joseph, Keji Mabura, Ester Charles, na Muhoja Ndoto.

Wengine waliofikishwa hapa ni Margreth Mahona, Lumla Magilinga, Swea Daniel, Regina Joseph, Paul Kana, Elizabeth Goje, Shilinde Mungu, Regina Amili na Shija Maazoya.

Wakazi wa mji hu wamekiambia PST kuwa wana shangazwa na kusikitishwa kwa uamuzi huo wa kuwafikisha ambao wanaugua ugonjwa huo mahakamani kuwa ni kitendo cha kukiuka hali za binadamu na ni uonevu. "Kwa kweli inasitikisha sana iweje mtu apatwe na ugonjwa na baadaye ushitakiwe huo ni uonevu mkubwa" Alilalamika mtumishi mmoja wa kampuni ya simu aliyejitambulisha kwa jina Stella.

Wamesema kuwa hakuna mtu anayependa kuugua kwani magonjwa ni matokeo yanayopangwa na Mungu na kama watakuwa wanalazwa kwa ugonjwa huo na kufikishwa mahakamani bora hata wagonjwa wanaougua magonjwa mengine wafikishwe mahakamani.

Kufuatia kulipuka kwa ugonjwa huo mwezi Januari 30, mwaka huu jumla ya watu 53 mpaka, ksasa wamefariki, na waliougua ugonjwa huo ni watu 200 katika halmashauri ya mji wa Shinyanga.