Maofisa Mambo ya nje wachota wanavyotaka

Na Mwandishi Wetu

MKAGUZI Mkuu wa serikali ameshutumu tabia inayozidi kumea katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ambapo maafisa wachache wamekuwa wakijichotea mamilioni bila kujali voti walizopangiwa wala kufuata utaratibu wa hesabu za serikali.

Aidha mkaguzi huyo mkuu katika taarifa yake, ameeleza kusikitishwa na kutaka hatua za haraka kuchukuliwa kurejesha masurufu yanayofikia takribani sh.bilioni 1.4 ambayo ama hayakutumika ipasavyo au wahusika hawakurejesha kabisa.

Pamoja na kauli hiyo, amesikitishwa na jinsi maafisa 12 walivyoweza kutumbua fedha za serikali kwa fujo bila hata kurejesha risiti wala kueleza matumizi yake .

Aidha katika ripoti hiyo ameshutumu tabia ya maafisa wahusika, kwa kukataa kueleza au kujibu maswali ambayo aliwapelekea.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ukaguzi inayoishia Juni mwaka uliopita, Mkaguzi Mkuu pia alizungumzia vifaa vilivyoagizwa na Wizara hiyo ambavyo kwanza haijulikani kama vimefika , viko wapi na au kama vinafanyakazi: Na pia utoaji wa kondorasi kwenye balozi nje ambao unatiliwa mashaka kwa kuwa unaliingizia taifa hasara kubwa.

Mkaguzi huyo akizungumzia matumizi mabaya ya masurufu, amesema maafisa wanne pekee wametumia kiasi cha sh.106,766,864 na maafisa wengine wanane wametumia kiasi cha sh. 417,820,964 kati ya jumla ya masurufu

 

Sekretarieti iliyompatia ushindi Mkapa yajipanga upya

Na Sadick Mgonja

SEKRETARIETI iliyompeleka Rais Benjamin Mkapa katika madaraka mwaka 1995 imeanza kujikusanya upya tayari kwa maandalizi ya muda mrefu ya kukamilisha ngwe ya pili ya uongozi wa awamu ya tatu.

Habari kutoka ndani ya Chama cha CCM zimesema kwamba chama chochote chenye dhamira ya kutawala ni lazima kijiandae mapema ingawa walikataa kukiri au kukubali kwamba sekretarieti hiyo ambayo iliongozwa na Waziri Mstaafu wa Ulinzi Kanali Abdulrahman Kinana imeanza kazi zake.

Akiongea na Gazeti hili juzi kufuatia uvumi uliozagaa kwenye kambi za wapinzani, ofisa mmoja wa cheo cha juu katika makao makuu ya chama hicho, Jijini Dar, alisema kuwa harakati zinazoendelea ndani ya chama ni kuhakikisha kuwa wanakiweka chama hai kwa ajili ya ushindi mwaka 2000 lakini sio kampeni rasmi kama ambavyo baadhi ya watu wanatafsiri.

Kiongozi huyo ambaye aliomba asitajwe jina kwa kuwa si msemaji rasmi wa chama hicho alisema kuwa ni kweli kuwa CCM, kama vilivyo vyama vingine kinafanya harakati zake za kawaida za kuhakikisha kuwa kinakuwa katika hali nzuri ya kutwaa ushindi kwaka 2000. ''Tukianza kampeni sasa si tutakuwa tunavunja sheria ya uchaguzi''

 

 

 

Jidawi kulipua bomu la bilioni moja za CUF

l Asema wanaogopa kuitisha Mkutano Mkuu

Na Mwandishi Wetu,Zanzibar

ALIYEKUWA mdhamini wa Chama Cha Wananchi (CUF), Bi. Naila Mujid Jidawi amedai anakamilisha vielelezo ili alipue bomu la matumizi mabaya ya shilingi bilioni moja zikiwa ni ruzuku ya serikali na misada ya wafadhili.

Bi. Jidawi amesema bomu hilo anatarajia kulilipua katika mkutano mkuu ujao wa chama hicho ambao ameeleza kutokana na viongozi wa juu wa CUF kulielewa, wamekuwa wakipiga chenga kuitisha mkutano mkuu ili siri zao zisitobowe.

Ameeleza kwamba tayari amekutana na viongozi wa mikoa zaidi ya 10 huko Dodoma na kuzungumzia mambo mbali mbali, likiwemo hilo la kutumia vibaya ruzuku kutoka serikalini kiasi cha milioni 700 katika kipindi cha miaka mitatu na misaada ya wafadhili milioni 300 kutoka

 

'Wamachinga' kumtapikia nyongo yao Mrema

Na Mwandishi Wetu

 WAFANYABIASHARA ndogo-ndogo mjini Dar es Salaam ambao ni maarufu kwa jina la "Wamachinga", wanakutana na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR - Mageuzi, Bw. Augustine Lyatonga Mrema leo asubuhi katika ukumbi wa Starlight Hotel uliopo barabara ya Bibi Titi Mohammed,

 

 

Maiti mbili zaokotwa Dar

Na Joseph Sanibus

 WATU wawili wamegunduliwa wakiwa wamekufa katika matukio tofauti Jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Bw. Alfred Gewe aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa katika tukio la kwanza, mwili wa mwanaume mmoja wa miaka 28-30 ambao haujatambuliwa uligunduliwa akiwa amejinyonga na kuharibika vibaya katika maeneo ya Mbezi-Msigane juzi.

Katika tukio jingine maiti ya mwanamke mmoja ambaye pia hajatambuliwa, iliokotowa katika maeneo ya Mwenge-Mlalakuwa ikiwa haina jeraha lo lote.

Wakati huo huo Kassim Saleh (27) mkazi wa Ilala, alifariki dunia juzi jioni muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali ya Muhimbili baada ya kugongwa na gari aina ya Toyota TAV 18 katika makutano ya mtaa wa Nyamwezi na Msimbazi alipokuwa akitembea kwa miguu.

Dereva wa gari hilo, Bw. Said Nassor (32) amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili baada ya kushambiliwa na wananchi waliokuwa na hasira kwa kuendesha gari pembeni zaidi.

 Jiji lawapatia kifuta jasho wauguzi wa kipindupindu

Na Justin Mwereke

 

TUME ya Jiji imetoa Sh. milioni mbili kwa ajili ya kuwalipa posho madaktari na wauguzi walioteuliwa kuhudumia wagonjwa wa kipindupindu katika kambi mbalimbali zilizowekwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa huo mwaka jana mwishoni.

Jumla ya madaktani na wauguzi wapatao 300 walidai kuwa walikuwa hawajalipwa posho zao za kufanya kazi katika kambi hizo tangu walipoteuliwa Novemba 24 mwaka jana, na kwamba walikuwa hawapewi maelezo ya wazi juu ya kulipwa posho hizo.

Kamishina wa Afya wa Tume ya Jiji, Dk. Job Laizer alimwambia mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki kuwa fedha hizo zimeishatumwa kwa waganga wakuu wa wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni Oktoba mwishoni mwaka huu kuwalipa wahusika.

Dr. Laizer alisema fedha hizo ambazo ni kidogo kulingangisha na kiasi kinachodaiwa, zilitolewa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kati ya Mei na Juni mwaka huu na zitagawiwa sawa kwa kila mmoja bila kujali cheo wala siku alizofanya kazi ya kuhudumia wagonjwa hao.

 

 

Mama akuta mtoto akila kondomu na kutishia kutoa roho ya mtu

Na Peter Dominic

TABIA za nyumba za kupanga ambapo watu hujifanyia mambo shaghala baghala yameponza mtoto wa mwaka mmoja kutwaa kondomu iliyotumika na kuitafuna.

Mama wa mtoto huyo Malisa anayeishi maeneo ya mburahati Barafu alimanusura amtoe mtu roho baada ya mtoto wake kunusurika kuimeza kondomu (mpira wa kiume) hiyo.

Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 4.00 asubuhi ambapo mama huyo alienda kuteka maji na aliporudi alimkuta mwanae mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ameishikilia kondom huku akitafuna taratibu baada ya kuiokota kwenye debe la takataka ambalo halikuwa mbali na eneo la nyumba hiyo.

Watu walioshuhudia tukio hilo wamesema kuwa mama huyo baada ya kuona hali hiyo alimpokonya mwanae na kushindwa kuizua hasira yake kwa watu aliowaita wanaharamu kwa kutaka kumpeleka ahera mwanae kabla ya siku zake na akaahidi kuwachukulia hatua za kisheria wapangaji wenzake atakaowabaini kutokuwa waangalifu katika mambo yao binafsi yenye kuhatarisha usalama wa wengine.

Aidha mwanamke huyo aliitisha kikao cha dharura ambapo aliahidi kumtoa mtu roho kwa kuwa mtoto wake tayari amepewa Ukimwi kutokana na kumeza uchafu wa kwenye mpira huo.

Hata hivyo wapangaji hao baada ya kuulizwa mmoja mmoja kwa kuogopa mambo yasiwe makubwa mmoja kati yao alikiri kuzitupa kondomu hizo kwenye Debe la takataka lakini alieleza kuwa zilikuwa hazijatumika.

 

 

Wapinzani walalamikiwa kwa ububu

Na Dalphina Rubyema

VYAMA vya upinzani vimekuwa kimya kuwasilisha maoni yake kwemye ofisi ya serikali ya kuratibu maoni Waraka wa serikali maarufu kwa jina la 'White paper'.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi hivi karibuni, katibu wa kuratibu maoni upande wa serikali, Bw.Siegfried Lushagara alisema kuwa ofisi yake ilipeleka barua kwa kila chama na walipeleka barua hizo miezi mitatu iliyopita lakini hadi hivi sasa hakuna chama kilichokwisha toa maoni yake.

Aliongeza kusema kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama cha Wananchi CUF, Bw.Shariff Hamad alileta maoni yake binafsi lakini siyo maoni ya chama chake.

Hata hivyo katibu huyo alisema kuwa hadi hivi sasa kamati yake imekwisha tembelea mikoa kumi na moja ambapo wananchi wengi wametoa maoni kwamba katiba hiyo ifanyiwe marekebisho.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Kagera, Kigoma, Mwanza, Tabora, Mara, Shinyanga, Mtwara, Luvuma, Rukwa, Pemba Kusini, na Pemba Kaskazini.

Hata hivyo mmoja wa viongozi wa NCCR na msaidizi wa Bw. Mrema katika mambo ya Habari Bw.Charles Charles alipinga kauli ya mratibu huyo na kusema kwamba msimamo wa vyama vya upinzani unaeleweka wazi hakuna haja ya kubabaishana.

Amesema kwamba huu si wakati muafaka wa kuburuzana katika kutafuta ridhaa ya wananchi na badala yake uitishwe mkutano wa katiba kama wapinzani wanavyoataka.

 

 

Auza nyumba hewa na kuingia mitini

Na Neema Dawson

MWAKA Bakari Mkazi wa Kongowe hapo Jijini, ambaye anadaiwa kuingia mitini na pesa taslimu 66,000/- baada ya kumtapeli mama mmoja kwa kumuuzia vyumba hewa bado hajapatikana tangu Aprili 27 mwaka huu.

Dada wa Mwaka Bakari aliyefa-hamika kwa jina la Mwalimu Amina Bakari ambaye alikuwa bega kwa bega wakati wa kuandikishana mkataba wa kupatiana vyumba hivyo kati ya mdai na mdaiwa aliieleza mahakama ya mwanzo Temeke mbele ya hakimu Modesti Matenyage ambaye alikuwa anasikiliza kesi hiyo.

Mwalimu Amina Bakari ambaye alikuwa Shahidi kwa upande wa mdai alikiri kuwa mdogo wake Mwaka Bakari alipewa pesa Taslimu sh. 66,000 kutoka kwa mdaiwa ikiwa ni malipo ya kodi ya vyumba viwili .

Vyumba vilivyokusudiwa inasadikiwa vilikuw na vyombo vya mpangaji mwingine ambaye alifariki na maiti yake ilikuwa imesafirishwa kwenda Bukoba, na hivyo vyumba hivyo kubaki vikimilikiwa na ndugu wa marehemu. Akitoa hukumu hiyo katika kesi hiyo ambayo ilikuwa inasikilizwa upande mmoja baada ya mdaiwa katika kesi hiyo kuingia mitini na pesa za mdaiwa huyo, Hakimu Modesti Matenyange alisema kuwa mdai huyo ana haki ya kurudishiwa fedha zake au kupewa vyumba hivyo.

Hakimu amesema mlalamikaji anatakiwa kusubiri kwa muda wa siku 42 ili mdaiwa huyo akisubiriwa kujitokeza kupinga hukumu hiyo na fedha hizo zitazaa kutokana na muda wate ambao mdai aliutumia kusumbuka kufuatilia kesi hiyo.

 

 

Apata mkong'oto wa nguvu kwa kumwacha mwanafunzi wa kike akining'inia

Na Getruder Madembwe

 

KONDAKTA wa daladala lenye nambari za usajiri TZM 5987 aina ya Hiace alipata viboko vya nguvu kutoka kwa askari MP Oliver wa Jeshi mwanafunzi wa kike akining'inia mlangoni.

Tukio hilo lilitokea maneo ya Makongo kituoni ambako ndiko alikokuwa askari huyo.

Askari huyo baada ya kumwona mwanafunzi huyo alimuuliza konda huyo kwa nini mwanafunzi ananing'inia, kondakta huyo alijitetea kwamba yeye sio kondakta ila ni abiria tu.

Lakini dereva wa gari lile alisema kwamba kondakta alikuwa ndiyo huyo ndipo askari huyo alipoanza kumpiga viboko vya mgongoni hali iliyosababisha kondakta huyo kutoa machozi.

 

 

Badala ya kuwawajibisha kisheria 'waliotafuna' fedha:

Wizara yaamua kulipa mafao ya wastaafu kwa njia ya michango

lMmoja wa watuhumiwa wakuu aandaliwa uhamisho maalumu

 

Na mwandishi wetu

 

WIZARA ya Kilimo na Ushirika, imeamua kulipa mafao ya watumishi wake wastaafu kwa njia ya michango baada ya "kuyeyuka" kwa mamilioni ya fedha ambayo hundi zake zilichukuliwa kutoka Hazina na 'kutafunwa" na baadhi ya "vigogo" wa ngazi za juu.

Habari zilizovuja kutoka ndani ya moja kati ya vikao nyeti, zimeeleza kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Barie alikutana kwa dharura na watendaji wake wakuu Jumatatu wiki hii na kuzungumza nao kwa kina kuhusu tuhuma za kukwama kwa malipo hayo ya mwisho ya watumishi wastaafu kutokana na 'kuliwa' na wajanja wachache.

Katika kikacho hicho ambacho pia kiliwahusisha watuhumiwa wenyewe, iliamriwa rasmi kuwa kwa vile fedha zinazohusika haziwezi tena kupatikana, mafao hayo sasa itabidi yalipwe kwa njia ya michango ambapo kila idara itakatwa sehemu fulani ya fungu kutoka kwenye kasma yake kwa sababu hakuna namna nyingine yoyote inayoweza kulitatua suala hilo.

"Imebidi tukubaliane kufanya hivyo ili fedha za kuwalipa (wastaafu) wale ambao mafao yao yameliwa zipatikane na kuwapa, halafu sisi tutajuana baadaye", alisema mmoja wa maofisa wakuu waliodhuria kikao hicho.

Ingawa hakutaka kueleza kwa kina kuhusu hatua zitakazochukuliwa hapo baadaye dhidi ya watuhumiwa wanaohusika na "utafunaji" huo wa mamilioni ya fedha za mafao ya watumishi wastaafu, afisa huyo alisema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo aliwaambia Wajumbe wake kwamba kwa kawaida hapendi kugombana na watu, lakini kamwe hatakuwa na huruma "kwa hili" ingawa hakufafanua.

Bw. Barie aliyeteuliwa wiki chache tu zilizopita kuwa Katibu Mkuu Mpya wa Wizara ya Kilimo na ushirika kuchukua nafasi ya Luteni Kanali magere ambaye sasa ni katibu Tawala wa mkoa wa Kigoma, amekaririwa akiagiza kuwa anataka wastaafu wote wanaoidai Wizara hiyo walipwe haraka ili kuondokana na aibu mbaya iliyokuwa ya kuongoza kwa utendaji mbaya na huduma mbovu.

Wakati huo huo, mmoja wa watuhumiwa wakuu "waliotafuna" fedha za mafao ya wastaafu hao ambazo hundi zake zilichukuliwa kutoka Hazina kati ya Oktoba 22, 1996 na Oktoba 31, mwaka jana ambaye jina na madaraka yake tunayahifadhi kwa muda, anaandaliwa uhamisho maalum kutoka Wizarani hapo kwenda sehemu nyingine badala ya kumwajibisha kwa mujibu wa sheria.

Habari za awali zilizopatikana zimeeleza kuwa afisa huyo huenda akapelekwa Wizara ya Ujenzi ingawa haikufahamika mara moja ataondoka lini na kama atakwenda kuendelea na wadhifa huo mkubwa alionao hivi sasa katika Wizara ya Kilimo na ushirika ama vinginevyo, lakini tayari ameshaanza matayarisho ya kukabidhi ofisi yake.

 

 

'Ukaguzi wa shule ni muhimu kuinua kiwango cha taaluma'

Na Charles Masanyika, Arusha

 

SERIKALI imeagiza kuwa shule zote nchini ni lazima zikaguliwe katika kipindi kisichozidi miaka mitatu ili kunyanyua kiwango cha elimu na kutoa matokeo mazuri ya kufaulu kwa wanafunzi .

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Utamaduni Bw.Abu Bakari Rajabu wakati anafungua warsha ya ukaguzi wa elimu kutoka kanda zote nchini unaofanyika katika ukumbi wa AICC mjini Arusha.

Bw. Rajabu amesema kwamba zipo shule nyingi ambazo tangu zianzishwe hazijaweza kukaguliwa na pia kuna shule nyingine kwa zaidi ya miaka 5 hazijaweza kufanyiwa ukaguzi wowote.

Amesema kwamba hivi sasa inaoneka wazi ni vigumu kufikia lengo la ukaguzi wa shule kutokana na taarifa ya ukaguzi wa shule ya mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu.

Katika taarifa hiyo Bw. Rajabu amesema kwa upande wa vyuo vya elimu utekelezaji wa ukaguzi ulikuwa asilimia 0, Sekondari asilimia 37, elimu ya watu wazima asilimia 34.6, na asilimia 46.2 kwa shule za msingi.

Amesema kwamba wizara inaelewa wazi Idara ya ukaguzi wa elimu inakabiliwa na matatizo chungu mzima ya kiwemo ukosefu wa vitendea kazi, uhaba wa wakaguzi, malazi, usafiri, posho za kujikimu, na ukosefu wa vivutio kwa watumishi.

Bw. Rajabu anaeleza kwamba serikali imeamua kuimarisha idara hiyo kwa kuhaikisha wakaguzi walioko wananolewa kiuwezo kwa kupatiwa mafunzo na pia kuwafundishz wakaguzi wengine 100 kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha.