Polisi Tanga waficha wanaotuhumiwa kuua

Na Mwandishi Wetu

POLISI mkoani Tanga imelaumiwa kwa kuficha mauaji yaliyotokea eneo la Kilindi, wilaya ya Handeni mkoani humo.

Habari zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kwamba, kifo cha fundi seremala mmoja aliyetajwa kwa jina la Athumani Ibrahim Kachuru kilitokea kati ya Aprili 5 hadi 12 mwaka huu eneo hilo la Kilindi katika mazingira ya kutatanisha, kimeonekana kuwatatanisha wakazi wa eneo hilo baada ya polisi wilaya na mkoa kutoshughulikia kesi yake kikamilifu.

Imeelezwa na vyanzo vyetu vya habari pamoja na kufanya mahojiano na baadhi ya ndugu wa marehemu Kachuru kwamba, mpaka sasa baadhi ya watuhumiwa walikuwa wametiwa mbaroni kuhusiana na kifo cha mwananchi huyo lakini wameachiwa katika mazingira ya kutatanisha bila kufikishwa mahakamani kama kifo chenyewe kinavyotatanisha.

Tukio hilo la kuuawa Kachuru, inadaiwa limeshafunguliwa kesi yenye nambari CC/71/98 kutokana na faili la upelelezi wa mauaji hayo la polisi wilaya ya Handeni lenye HAN/IR/339/98.

Gazeti hili lilipowalisiana hivi karibuni kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga ili kujua utekelezaji wa kesi inayohusiana na mauaji hayo, alieleza kutoelewa lo lote na akaomba ndugu wa marehemu waende kuonana naye. Lakini hata baada ya hatua hiyo kuchukuliwa, taarifa zilizolifikia gazeti hili majuzi zimeeleza kwamba bado kuna kitendawili kimetegwa kati ya polisi mkoa na wale wa wilaya ya Handeni ambako ndiko inaonekana kufichwa watuhumiwa wa mauaji hayo ili wasifikishwe kwenye vyombo vya sheria.

Pamoja na polisi kutolichukulia kwa uzito tukio la mauaji hayo, lakini watu wapatao 7 waliokamatwa awali kwa kutuhimiwa kuhusika na mauaji hayo wamejulikana kuwa ni Shaaban R. Nyange, Charles Samwel, Habiba S. Omari ambaye alikuwa mchumba wa marehemu Kachuru, Selemani O. Mgonya ambaye ni baba wa Habiba na Seif Saleh Madiwa.

Wengine ni Charles Samwel Mngema ambaye jina lake linafanana na yule wa pili, na mtuhumiwa mkuu inadaiwa alikuwa Ally Mohamed.

Hata hivyo inadaiwa kwamba pamoja na mazingira ya kutatanisha ya mauaji ya Kachuru kuwahusisha watuhumiwa hao, polisi wilaya ya Handeni iliwaachia huru watu wanne bila kuwafikisha mahakamani na walianza kutamba kijijini Kilindi. Wakielezea jinsi walivyojitoa mikononi mwa dola, kwa kutumia 'kitu kidogo' na kuachiwa kwao ikisemekana kulitokana na kukosekana ushahidi wa kuwatia hatiani.

Walioachiwa tayari wametajwa kuwa ni Ally Mohamed, Selemani Omar Mngoya, Charles Samwel Mngema na Seif Saleh Madiwa.

Waliofikishwa mahakamani mara moja tu siku ya Aprili 28 mwaka huu ni Habiba Omar ambaye alikuwa mchumba wa marehemu, pamoja na akina Shaaban R. Nyange na Charles Samwel ambao inadaiwa ni watumishi wa nyumbani kwa Habiba waliotoka Dodoma.

Imeelezwa na jamaa wa marehemu kwamba, kuna uwezekano watu hao wawili wasihusishwe na mauaji hayo hapo baadaye, na hivyo kupoteza ushahidi wa jinsi ya kuyashughulikia mashtaka hayo kikamilifu mahakamani kwa kukosekana waliohusika.

Akiongea na gazeti hili, mmoja wa ndugu wa marehemu Kachuru ambaye hakutaka kutajwa gazetini alieleza kwamba kinachowashangaza ni jinsi polisi mkoani humo hasa Kamanda wa Polisi wa wilaya ya Handeni aliyemtaja kwa jila B. M. Mbaule, kwamba ameshindwa kabisa kuonyesha mshikamano wa kusimamia suala lao. Hivyo kuonekana akiendelea kuwalinda hadi sasa baadhi ya waliotuhumiwa na wameachiwa wakitamba kijijini kwa kulipaka matope Jeshi la Polisi mkoani Tanga.

Kuhusu mazingira ya mauaji hayo, wanandugu hao wamedai kwamba marehemu Kachuru alipotea katika mazingira ya kutatanisha kati ya April 5 mwaka huu ikiwa ni siku ya Jumapili hadi maiti yake ilipoonekana kwenye maji Jumapili ingine ya Aprili 12 mwaka huu.

"Polisi walifuatwa Handeni Jumatatu Aprili 13, 1998 lakini walikwenda eneo la tukio na daktari tarehe 16, baada ya mdogo wa marehemu ambaye ni mwalimu kuwashinikiza," walieleza ndugu hao kwa uchungu

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, kutokana na mazingira ya utatanishi wa mauaji hayo. Kabla ya siku hiyo, mdogo wa marehemu anayeitwa Said Ibrahim Kachuru aliyekuwa anafundisha shule ya msingi Kilindi, sasa amehamia shule nyingine inayoitwa Mafisa aliikataa barua iliyotolewa na Kituo cha Polisi Handeni kama kibali cha mazishi.

Barua hiyo inadaiwa alipewa Hadji Mohamed, aliyetumwa na kuchelewa kurudi kutokana na askari hao kutotaka kuonyesha ushirikiano hadi alipokutana naye kwenye basi. Kutokana na hali hiyo, mwalimu huyo inasemekana alichachamaa kituoni huko baada ya kuambiwa kwamba kibali hicho kilitolewa kwa sababu polisi hawakuwa na mafuta ya gari kuweza kuwafikisha huko Kilindi.

Mwalimu huyo alichachamaa kwa kuwaeleza kwamba, kama ni hivyo akirejea Kilindi na kuua zaidi ya watu 10, ndio watapata mafuta. Ndipo inasemekana polisi walimsihi kutulia na alilala na kuondoka kesho yake asubuhi wakiwa na daktari.

Maiti ya Kachuru inaelezwa kwamba ilipatikana ikiwa imefungwa shati chini kwenye maji ili isiweze kuelea juu huku meno yakiwa yameng'olewa, mguu umevunjika na majeraha mengine usoni na mbavu za kushoto zikiwa nazo zimevunjwa uionyesha kwamba alikuwa ameuawa.

Kati ya watuhumiwa saba waliokuwa wamekamatwa, inaelezwa Ally Mohamed Mgaya alikuwa na uhusiano mbaya na marehemu kwa kudaiwa anatembea na mkewe kiasi cha kufikishana kwenye Ofisi ya serikali ya Mtaa. Kutokana na kutishia kumwua marehemu ambako inadaiwa Bw. Mgaya aliomba radhi kwa tishio lake hilo.

Lakini inaelezwa kwamba, mbali ya watu saba waliowahi kukamatwa awali kulikuwa na watuhumiwa wengine wawili waliotajwa kuwa ni Juma Kiyeya na Salumu Kilindi. Mmojawao aliwahi kumsimamisha mdogo wa marehemu Kachuru (Mwalimu Saidi) kwamba wakitaka kumtafuta (marehemu), waende mwelekeo mwingine na sio kule ambako maiti ilipatikana.

Inaelezwa kwamba kati ya hao wawili, mmojawao aliwakimbia polisi na mpaka sasa hajakamatwa kuhusishwa na mauaji hayo. Wakati kuna taarifa za kusikika akitamba alikuwa mmoja wa waliomkomoa marehemu.

Mambo mengine yanayodaiwa kuifanya Polisi Handeni inahusika na kuficha mauaji hayo, inasemekana faili la mauaji hayo halikuwa na orodha kamili ya watuhumiwa wanaoshtakiwa na wale walioachiwa. Ikiwa ni pamoja na watu wa wawili ambao walifaulu kuwakimbia polisi siku ya kumtafuta marehemu ambao ni Juma Kiyeya na Salumu Kilindi. Hatua inayoelezwa na ndugu wa marehemu kwamba, ilisababisha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga akishirikiana na Mpelelezi wake wa Mkoa kuifanya kazi hiyo upya kwa kuliitisha jalada la mauaji hayo kutoka Handeni.

Pia inaelezwa kwamba, kuna ushahidi wa mtoto wa Habiba ambaye aliwathibitishia polisi kuwa ni kweli siku ya tukio marehemu alipigwa na miongoni mwa watuhumiwa hao na baadaye kulazwa nje ya nyumba ya mchumba huyo wa marehemu. Watu hao wanadaiwa baadaye waliondoka naye ambapo hakupatikana hadi siku ilipookotwa maiti yake ikiwa imezamishwa mwenye maji pembeni mwa mto.

Wakati huo huo kuna taarifa nyingine inayohusiana na mauaji katika wilaya hiyo ya Handeni kwamba, mwalimu mwingine wa shule ya msingi Mgellah iliyopo wilayani humo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, ameuawa na mpwawe kutokana na ugomvi wa gari yake aina ya Land Rover.

Imeelezwa kwamba tukio hilo ambalo polisi haijalifanyia kazi, lilitokea baada ya mpwa wa mwalimu huyo kung'ang'ania kukabidhiwa gari hilo na marehemu na baada ya kugoma ndipo alisuka mpango wa kumwuua. Lakini polisi inadaiwa haijalishughulikia tukio hilo.

 Wagoma kulipa kodi kwa kukosekana maendeleo

Na Ancent Nyahore, PST,Shinyanga

WANANCHI wa vijiji vya Ilamata na Mwabayanda katika Tarafa ya Sengerema wilaya ya Maswa, wamegoma kulipa kodi na hawajarejeshewa asilimia 20 ya kodi zinazotozwa.

Afisa Mtendaji wa kata ya Kulumi, Bw. Elias Mulyambelele jana ameiambia PST kuwa hali hiyo imejitokeza katika vijiji hivyo na kusababisha zoezi la kukusanya kodi mbali mbali katika maeneo hayo kuwa gumu.

Katika kijiji cha Ilamata, Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Bw. Nyerere Nkono, amesema kuwa ukusanyaji wa kodi katika kijiji hicho umekwama baada ya wananchi 185 kati ya 345 kijijini hapo kugoma kulipa kodi, kwa madai hawaoni maendeleo.

Wiki iliyopita, Bw. Nkono akiwa na wanamgambo wake walirushiwa mawe na wananchi kijijini humo wanasadikiwa kuwa wanapinga kulipa kodi kijijini hapo, japo katika tukio hilo hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Mapema Septemba mwaka huu, Mkuu wa wilaya ya Maswa Bw. Albert Mnalli aliwaagiza Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwenda vijijini na katika kata kusimamia ukusanyaji wa kodi mbali mbali kufuatia kudorora kwa mapato ya Halmashauri hiyo

 Kardinali Pengo amtaka Kapuya ajiuzulu

Na Dalphina Rubyema

MUADHAMA Polycarp Kardinali Pengo amemtaka Waziri wa Elimu na Utamaduni,Profesa Juma Kapuya kuonyesha ustarabu kwa kujiuzulu kutokana na kuvuja kwa mitihani ya kidato cha nne.

Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa habari juzi katika sherehe za miaka 80 ya uhuru wa Poland, zilizofanyika nyumbani kwa balozi wa nchi hiyo mtaa wa Kisiza Oysterbay Jijini.

Alisema kuwa Profesa Kapuya hawezi kukwepa kwa namna yoyote ile kwamba kuvuja kwa mitihani hiyo siyo kosa lake, hii hali inaonyesha jinsi gani alivyo na udhaifu wa kuwadhibiti watendaji walio chini yake.

"Kwa kweli hapa mimi naona Profesa Kapuya aonyeshe ustaarabu kwa kujiuzulu na wala si vingine"alisema Kardinali Pengo.

Aliendelea kusema kuwa tatizo la kuvuja kwa mitihani ni tatizo la muda mrefu, na kipindi chote hicho Profesa Kapuya ameshindwa kuchukua hatua zinazofaa kudhibiti hali hiyo mpaka lilipotokea tukio kubwa namna hiyo ambalo ni aibu si kwa wizara tu bali Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo ya Askofu Pengo imepata kutolewa na watu mbalimbali ambao wanapendekeza Waziri Kapuya kuachia ngazi, kutokana na uzembe aliouonyesha.

Hata hivyo Waziri Kapuya juzi akijibu maswali ya Wabunge kuhusu suala hilo, alitoa kauli kuwa hayuko tayari kujiuzulu kwa vile yeye hahusiki na suala la udhibiti wa mitihani na kuongeza kuwa huwa inapitia hatua mbalimbali.

Hivi karibuni Waziri wa Elimu alisimamisha mitihani ya Kidato cha nne kuendelea kufanyika, kutokana na kuvuja katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga, Mbeya, Rukwa, Morogoro na Kisiwani Pemba.

Naye Mwandishi Lucy Ngowi wa PST anaripoti kuwa Mkuu wa Kitivo cha Elimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam , Profesa Justinian Garabawa alisema kuwa kuvuja kwa mitihani kunatokana na mfumo mzima wa elimu na jinsi usivyopewa kipaumbele. Alisema kitendo cha Waziri wa Elimu na Utamaduni kuifuta, ni njia madhubuti ambayo itasaidia kutatua tatizo hilo.

Profesa Galabawa alisema kuwa ili kuondoa tatizo hilo, serikali haina budi kuwapa walimu motisha kama vile nyumba, mishahara na kuangalia ukubwa wa darasa na vifaa vitavyotumika kufundishia.

Naye Lucas Raphael kutoka Tabora anaripoti kuwa, Walimu mkoani Tabora wamelaani kitendo cha mitihani kuvuja ambapo wametoa pendekezo kuwa wale wote watakaobainika kusababisha kuvuja kwake wachukuliwe hatua kali.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Wakuu wa Shule za Sekondari mjini hapa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Steven Mashishanga ambapo walisema kuwa kitendo hicho kinarudisha nyuma maendeleo ya elimu nchini na kuwadhalilisha walimu wanaofundisha wanafunzi hao.

 Tamko la maaskofu KATOLIKI juu ya uagizaji NA SOKO HURIA LA silaha

Kikao cha Kamati Tendaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kilichokutana kuanzia Novemba 10 hadi 12, 1998 kwenye kituo cha Mikutano na Mafunzo cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kilichoko Kurasini jijini, kimeelezea wasi wasi wake juu ya uamuzi wa serikali wa kutaka kuruhusu biashara buria ya silaha.

Silaha mara nyingi ni tishio la amani. Hivyo pamoja na serikali kuahidi kudhibiti uingizaji na uuzaji wa silaha hizo, Maaskofu wana wasi wasi na zoezi hilo kutokana na mazoea ya nyuma ya serikali kushindwa kudhibiti uingizaji holela wa vitu mbali mbali na hivyo kuwa na hisia kuwa hata udhibiti wa uingizaji na uuzaji wa silaha hautatofautiana na hali hiyo.

Maaskofu wamesema kwa mfano, vitu vingi vimeingizwa nchini kinyume na taratibu kwa visingizio vya wanaohusika kuwa na vibali, lakini wanaingiza zaidi ya vile walivyoruhusiwa.

Hali hiyo itasababisha kuingizwa kwa silaha zaidi kwa njia ya udanganyifu na kuwa mikononi mwa watu ambao hawastahili kupata silaha hizo na hivyo kuhatarisha amani na maisha ya wananchi.

Silaha ni chombo hatari kwa maisha ya binadamu. Hivyo Maaskofu wanaomba na kuisihi serikali isizifanye kuwa ni bidhaa za kuuzwa kutafuta faida, kitu ambacho ndio lengo la mfanya biashara yeyote. Wafanya biashara wengi hujali maslahi na faida yao zaidi kuliko usalama wa wengine.

Maaskofu wanapenda kuiangalisha serikali kuwa, hata katika nchi zilizoendelea na zinazodhaniwa kuwa na udhibiti mkubwa wa silaha, bado silaha zinatumiwa vibaya na hivi kuhatarisha maisha na amani ya wananchi na madhara yake yanaonekana wazi katika nchi hizo.

Hata hapa kwetu, tuna mifano halisi ya matukio ya matumizi mabaya ya silaha zilizo mikononi mwa watu binafsi.

Silaha hizo zinatumika kuhatarisha na kuondoa usalama wa mali na uhai wa wananchi na hata kuteketeza mali asili ya Taifa.

Tunaiomba serikali isitishe uamuzi wake wa kutaka kuruhusu biashara huria ya silaha. Badala yake iendelee na mtindo wake wa sasa wa kujihusisha moja kwa moja katika uingizaji na uuzaji wa silaha.

Hekima, Umoja na Amani ndizo ngao zetu.

lLicha ya kauli hii ya maaskofu duka moja tayari limeanza Dar es salaam kwa mujibu wa gazeti la Uhuru. MHARIRI

Kufuatia mgomo uliotia hasara ya mamilioni

Kilombero waanza kulipwa mafao yao

lSUDECO washikwa kigugumizi,wagwaya kutoa ufafanuzi

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya mgomo mkubwa wa wafanyakazi uliokisababishia kiwanda cha kutengeneza sukari cha Kilombero hasara ya mamilioni ya shilingi umezaa matunda na hatimaye wafanyakazi wa Kiwandani na mashambani wameanza kulipwa mafao yao.

Wafanyakazi hao walifanya mgomo uliodumu kwa siku tatu kuanzia Oktoba 14 hadi 17 mwaka huuikiwa ni njia ya kuulazimisha uongozi wa kiwanda hicho kuwalipa mafao yao mbalimbali na kupinga kunynyaswa na wamiliki wa kiwanda hicho kampuni ya ILOVO kutoka Afrika Kusini.

Habari kutoka kiwandani hapo zinasema kuwa wafanyakazi wa mashambani na kiwandani wameanza kulipwa malimbikizo ya mishahara yao pamoja na posho za likizo ambazo walikuwa hawajalipwa kwa muda mrefu.

Wakiongea na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka Kilombero mkoani Morogoro wafanyakazi hao ambao wameomba majina yao yasitajwe gazetini kwa kuhofia ajira yao kuwa matatani na kuchukiwa na uongozi wa kampuni hiyo wamesema posho na malimbikizo ya mishahara imeanza kulipwa kufuatia muafaka uliofikiwa kwa pamoja kati ya bodi ya kiwanda hicho na chama cha wafantakazi (TPAWU ) kiwandani hapo mwezi uliopita.

Pamoja na kuanza kutekelezwa kwa baadhi ya madai yao lakini wafanyakazi hao wametishia kugoma tena endapo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu madai yao yote yatakuwa hayajatekelezwa kwa kuwa hiyo ndio njia pekee ya kudai haki yao kutokana na kile walichoeleza kuwa Shirika la maendeleo ya sukari kushindwa kuwasaidia wafanyakazi hao.

Juhudi za gazeti hili kupata ufafanuzi wa madai ya wafanyakazi hao kupitia Shirika la Sukari nchini ,SUDECO, na hatua gani zitachukuliwa kwa kampuni inayohusika zimegongwa mwamba kwa wiki tatu sasa.

Madai hayo ni pamoja na kampuni hiyo ya Kilombero kuendesha kazi zake kwa ubaguzi wa rangi ikiwa ni pamoja na kuwafukuza wafanyakazi wazalendo katika nyumba walizokuwa wakiishi na nyumba hizo na kukaliwa na wazungu pamoja na kupigwa kwa wafanyakazi.

Aidha walitaka kujua nini kinawapa kiburi kikosi maalumu kilichoajiriwa na kampuni hiyo kutoka Kenya kinachojulikana kwa jina la KK security cha kuwatesa wafanyakazi.

Awali gazeti hili lilipotaka ufafanuzi afisa mmoja wa ngazi ya juu katika kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Msoka aliomba apelekewe maswali ili ayapeleke kwa meneja mkuu atoe ufafanuzi kwa kuwa suala lenyewe lilikuwa nyeti na asingeweza kujibu yeye.

Licha ya kupelekewa maswali watendaji wa kampuni hiyo bado wameendelea kugwaya kutoa ufafanuzi ambapo Kiongozi ilipopiga hodi tena katika ofisi za shirika hilo ilielezwa kuwa anayeshughulikia suala hilo ni mama Haule ambaye naye alisema hajawahi kuona barua ya maswali ya gazeti hili na hawezi kujua ajibu nini kwa kuwa alikuwa ameanza kazi si muda mrefu baada ya kutoka likizo.

Katika kile kinachoonekana ni kujigongagonga na kugwaya kwa watendaji wa shirika hilo kulitolea ufafanuzi ni hatua gani zitachukuliwa kwa kampuni ya Ilovo kama iitathibitika kuwa madai ya wafanyakazi wa kiwanda hicho ni kweli, gazeti hili lilipotaka kumuona meneja mkuu lilielezwa kuwa amefiwa; na katibu muhtasi wake alikuwa ametoka.

Wakati tunakaribia kuingia mtamboni tuliwasiliana tena na SUDECO ambako tuliambiwa kwamba suala hilo amepewa ofisa mmoja kwa jina la Msimbila ambaye kila tulipowasiliana naye tuliambiwa yuko kwenye kikao.

 

Picha za video marufuku-Jiji

Na Said Mmanga wa MSJ

TUME ya Jiji kanda ya Temeke imepiga marufuku biashara ya uonyeshaji wa picha za video katika nyumba za watu binafsi,ofisi za vyama na katika mabaa kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Agizo hilo linakuja siku chache tangu ofisi ya utamaduni wilayani humo kutangaza vita dhidi ya wale wanaoonyesha kanda za ngono hadharani ambapo ilisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wanaovunja maadili ya utamaduni wa Kitanzania kwa kuonyesha mikanda hiyo kiholela.

Kwa mujibu wa barua ya tume hiyo kanda ya Temeke kwenda kwa maafisa watendaji kata iliyosainiwa na afisa utamaduni wa wilaya hiyo Nestory Wisandara kwa niaba ya mkurugenzi wa kanda hiyo ilisema kuwa uonyeshaji wa video hadharani ni marufuku nje ya majumba ya sinema ni marufuku na kuongeza kuwa biashara hiyo haina leseni wala kibali .

Alisema wananchi hawakatazwi kuangalia video zao isipokuwa biashara ya kuonyesha picha za video ndiyo iliyopigwa marufuku kwa kuwa zinaendeshwa kinyemela na kinyume cha sheria za nchi ambapo alisema pia wanainyima Serikali mapato yake ambayo yangestahili kupatikana kama wahusika wangefuata taratibu za kisheria.

Akifafanua zaidi juu ya suala hilo alisema biashara ya uonyeshaji wa picha za video kiholela umekithiri wilayani humo ambapo nyingine zinavunja maadili ya Kitanzania hali ambayo alidai inachangia kwa kiasi Akiongea na gazeti hili ofisini kwake afisa utamaduni wa wilaya ya Temeke Bw. Nestory Wisandara alisema ofiasi yake pamoja na tume ya jiji wilayani humo wamepiga marufuku uoneshaji wa picha za video katika sehemu hizo kwa kuwa ni kinyume cha sheria, ambapo alidai kuwa biashara ya uonyeshaji wa mikanda hiyo haitakiwi kufanywa nje ya majumba yaliyoruhusiwa kuendesha biashara hiyo na pia ni ukiukaji wa makausudi wa sheria za nchi pamoja na sheria za tume ya jiji.

kikubwa kuharibu tabia za vijana na hasa watoto ambao ndio Taifa la kesho.

Sambamba na hilo Wisandara alisema pia wenye kumbi za starehe nao wametakiwa kufuata masharti ya vibali vyao na kuonya kuwa mtu ambaye atakwenda kinyume na maagizo ya vibali hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuzifungia kumbi za starehe ambazo zinakiuka utaratibu uliowekwa .

Alisema wenye kumbi za starehe wanatakiwa kupiga disko au dansi hadi saa tano na nusu kwa siku za kawaida na saa sita katika siku za mwisho wa wiki na siku kuu ambapo pia alisema wamewaaagiza kuhakikisha muziki unapigwa katika kumbi hizo hauwabugudhi wananchi wengine .

Hivi karibuni ofisi hiyo ilizifungia kumbi tano za starehe kutokana na kuwabugudhi wananchi wengine kutokana na muziki unapigwa katika maeneo hayo nyakati za usiku.

CCM Kilimanjaro yapigwa jeki

Charles Masanyika, Moshi

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) Bi Doreen Kisamo mapema wiki hii alikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya magari vyenye thamani ya zaidi ya shilingi laki tatu kwa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika hafla hiyo fupi ya kukabidhi mchango huo iliyofanyika katika ofisi ya CCM mkoa wa Kilimanjaro Bi Doreen allisema kuwa baada ya kupata barua ya maombi, yeye kama mjumbe wa NEC aliona ni wajibu kuimarisha chama popote pale.

Alisema kuwa ili kuwa na umuhimu wa kurejea majukumu ya chama chochote cha siasa ni lazima kuongeza idadi ya wanachana na kuhakikisha uhai wa wanachama katika kuimarisha shughuli za chama.

Aidha Bi Kisamo amekitaka chama hicho kutathmini ili kisifanye makosa tena kama uchaguzi mkuu uliopita na kusema hakina budi kuunganisha nguvu za hali na mali ili kuimarisha chama na kuhakikisha kinapata ushindi katika uchaguzi wowote ule.

Awali Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Peter David alisema kuwa kutokana na msaada huo mkoa wake utahakikisha vifaa hivyo vinatumika ipasavyo .

Mkurugenzi wa manispaa ya Moro atakiwa kujieleza

Na Said Mmanga, Morogoro

MKURUGENZI wa manispaa ya Morogoro ametakiwa kutoe maelezo juu ya kushindwa kwa wazabuni kutengeneza barabara na vivuko au la asubiri Halmashauri kumjadili yeye na wenzake kwamba wameshindwa kumudu dhamana walizokabidhiwa.

Kauli hiyo imetolewa na diwani wa kata ya Kingo (CCM) Bw.Omar Simba wakati wa kujadili utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Maendeleo hususani Ujenzi wa barabara na madaraja (Vivuko) katika Manispaa ya Morogoro.

Diwani huyo amesema lawama inabidi ziwaendee watu wa halmashauri hiyo kwa kutoa zabuni kwa wazabuni wasio na uwezo wa kuzifanya kazi hizo.

Akichangia bajeti ya Halmashauri hiyo katika kikao cha bajeti kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa mwishoni mwa wiki Bw. Kingo alisema wazabuni wengi wanaopewa kazi hizo hawana uwezo wa kifedha na kusema kuwa kuwatumia watu hao ni sawa na kufanya kazi na matapeli.

Bw. Simba alisema suala la kutengeneza vivuko halihitaji fedha nyingi ambapo pia alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo hadi kufikia Jumatatu kuelezea kwanini asiwajibishwe kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo, vinginevyo kikao cha halmashauri kiwajadili kuwa wameshindwa kufanya kazi .

Wakati huo huo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 62,430,600 katika mwaka ujao wa fehda.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Emanuel Kalobelo alisema mjini hapa katika kikao cha bajeti ya Halmashauri hiyo, ambapo bajeti hiyo imeongezeka kutoka shilingi milioni 451 hadi milioni 621 na katika uongeza pato hilo halmashauri imepandisha viwango vya kodi ya maendeleo.

Bw. Kalobelo alisema kuwa kodi ya maendeleo kwa mwananchi wa kawaida imepanda kutoka shilingi 1,500 hadi 2,000. Mfanyakazi imepanda kutoka shilingi 3,000 hadi 3,500 wakati mfanyakazi ambaye mshahara wake unazidi shilingi 36,000 kwa mwezi sasa atalazimika kulipa shilingi 4,000 za kodi ya maendeleo badala ya 3,500.

Mbinu nyingine zitakazotumiwa na halmashauri hiyo kuongeza mapato yake ni kuwatumia mawakala katika kukusanya uhuru badala ya kuajiri watu wa kufanya kazi hiyo.

Viongozi wa Bakwata wabondwa msikitini

Na Mwandishi wa PST, Bunda

KATIKA hali ya kushangaza, waumini wa Msikiti wa Ijumaa ulioko wilaya ya Bunda, mkoani Mara, mwanzoni mwa wiki, waliugeuza msikiti wao kama uwanja wa masumbwi, baada ya kuanza kuwatwanga makonde viongozi wao kwa tuhma za ubadhiriu.

Viongozi hao waliobondwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Waislam nchini wa Wilaya ya Bunda, Bw. Abdallah Biseku na Katibu wake Bw. Mussa Ibrahim.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, licha ya kuumizwa vibaya na waumini hao, alichaniwa kanzu yake maalum na kuvunjiwa miwani ya macho ambayo ndiyo tegemeo lake kutokana na ubovu wa macho.

Bw. Biseku ameiambia Alasiri kuwa katibu wake Bw. Ibrahim ndiye aliyepata kibano kikali.

"Aliumizwa sana hasa ehemu za usoni", amesema Bw. Biseku na kongeza kuwa kutokana na hali hiyo ilibidi wambdebe mzobemzobe kwenye hospitali moja iliyoko mjini hapa ijulikanayo kama DDH ambako alipelekwa moja kwa moja wodini kulazwa.

Alipoulizwa chanzo cha kubondwa na waumini wenzeo, Mwenyekiti huyo amesema, "wenzetu wametupakazia kuwa tumekula pesa zilizochangwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kiislam, lakini siyo kweli, bali wamamua kututoa kafara tu".

Habari zaidi zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya waumini na kuthibitishwa na Bw. Biseku mwenyewe, zimesema kuwa viongozi hao wanadaiwa kutafuna zaidi ya shs. milioni mbili.

Pesa hizo zilichangwa na watu kadhaa wakiwemo viongozi wa serikali na wabunge kadhaa.

Akisimulia tuko hilo, Bw. Biseku amesema masumbwi hayo hayakuja kama mvua ya kiangazi na kwamba dalili zilikwishaanza kujitokeza siku nyingi.

Kulikuwa na mgogoro mkubwa tena wa siku nyingi kati yetu viongozi na waumini, amesema

"Siku hiyo ilikuwa kama jipu lililoiva, linapotumbuliwa......, mvutano umedumu kwa takriban miezi minne sasa, na waumini walishataka kutudhalilisha siku nyingi tu, lakini Mola akasaidia", ameongeza Bw. Biseku.

Akifafanua zaidi jinsi kasheshe hilo lilivyoanza, amesema awali hali ilikuwa shwari kabisa lakini baadaye katibu wake alivyonyanyuka kutaka kuwasomea barua iliyotoka mkoani, kwa kasi ya ajabu, kama nyuki wavamiapo mtu anayewachokoza kwenye mzinga wao, waumini walinyanyuka na kumvamia na kuanza kumtandika bakora.

Barua hiyo ilikuwa ikiwataka baadhi ya viongozi wanaochchea fujo msikitini hapo kuachia ngazi mara moja kabla ya kufanyika kwa mkutano wa usuluhishi uliopangwa mwishoni mwa mwezi huu.

Kufuatia tukio hilo, habari zimesema muumini mmoja aliyetajwa kwa jina la Kassim Ibrahm anashikiliwa na polisi mjini hapa kwa tuhuma za kufanya fujo.

Hata hivyo taarifa zaidi zimesema polisi bado wanaendelea na uchungu wao juu ya sakata hilo.

 Pwani yapiga marufuku usafirishaji Mkaa usiku

Na Aboubakary Mlawa, PST Bagamoyo

MAGARI yanayobeba mkaa kutoka Mkoani Pwani kwenda Jijini Dares Salaam, yamepigwa marufuku kusafirisha bidhaa kuanzia saa 12 jioni kutokana na magari mengi kutolipa ushuru na hivyo kuzikosesha mapato wilaya.

Hilo ni moja ya maazimio katika kikao cha ujirani mwema baina ya Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam , Wanausalama na Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri za wilaya katika mikoa hiyo kilichofanyika mjini Bagamoyo wiki hii.

Wakuu hao wamesema kuwa kutokana na halmashauri zao kukosa mapato ya kodi ya ushuru wa mkaa, kuanzia sasa magari yanayobeba mkaa ni marufuku kupitia nyakati za usiku.

Wamesema magari hayo yamekuwa yakipita usiku kwa kukwepa wakusanyaji kodi na ushuru, tofauti na mchana ambapo hukamatwa na kulipa ushuru.

Aidha wamesema kuwa doria itaimarishwa kwa wanunuzi wa mbao, kuni, miti ya ujenzi , korosho na mkaa, kuhakikisha kuwa walipa ushuru chini ya usimamizi wa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri.

 Maiti ya Mvuvi yaokotwa baharini

Na Joseph Sabinus

MTU mmoja Godfrey Samwel (30) mkazi wa kijiji cha Mbutu Mkwajuni Wilayani Temeke, amefariki dunia katika ajali ya maji.

Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake jana ,Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Alfred Gewe alisema kuwa mwili wa marehemu ambaye alikuwa katika shughuli za uvuvi uliokotwa baharini juzi mchana.

Katika tukio jingine, mtu mmoja amejeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira alipokurupushwa yeye na wenzake wakivunja nyumba ya Bw.Omary Abdalah maeneo ya Keko Mwanga usiku wa kumkia jana.

Kamanda Gewe alimtaja mtu kuwa ni Beny Luhoga (18) mkazi wa Keko Mwanga na kwamba wenzake wanne walifanikiwa kutoroka na hakuna kitu kilichoibiwa ambapo majeruhi huyo amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Temeke.

Tushirikiane kuinua familia - Akina mama

Na Emma Kayuza

KITENGO cha Maendeleo cha akina mama kinachofanya kazi chini ya Caritas Tanzania na Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC), kimewataka akina mama na akina baba kushirikiana katika kuinua maisha ya familia na jamii.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ofisini kwake hapo jana, Mwakilishi wa Kanda ya Magharibi Bibi Sesilia Kalima alisema kuwa kazi kubwa ya kitengo hicho ni kutoa mafunzo kwa waratibu, kufuatilia shughuli za akina mama majimboni na kutafuta ufadhili kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya akina mama.

Alisema kuwa wanatafuta mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu kwa waratibu waliopo Majimboni kwa akina mama wanaowahudumia, na wanashirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali(NGO's) katika shughuli za kuwaendeleza akina mama na kuhudhuria mikutano mbalimbali kuwakilisha waratibu ndani na nje ya nchi.

 Wizi wa nyaya wakwamisha mawasiliano Kaliua, Urambo

Na Peter Dominic

SHIRIKA la Simu hapa nchini limesema kwamba wizi wa nyaya katika maeneo ya Urambo na kaliua, Tabora yanasababisha kero kubwa kwa watu wanaotaka kuwasiliana na wakazi wa maeneo hayo.

Meneja Uhusiano wa shirika hilo Bw. I.J. Semtawa alifafanu kuwa matatizo yaliyopo sasa ni matokeo ya vitendo vya wizi wa nyaya ambapo hadi sasa kumekuwepo na matukio (7) ya wizi wa nyaya ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

"Tunawaomba wateja wetu kuwa wavumilivu mara yanapotokea matatizo kama hayo hasa mikoa ya mbali". Bw. Semtawa aliongeza na kusema kuwa shirika hilo linajitahidi kurudisha mawasiliano ili kuondoa kero hizo kwa wateja wake.

Bw. Semtawa aliwaomba pia wananchi kutoa taarifa pindi wanapowaona waharibifu hao ili hatua kali na za kisheria ziweze kuchukuliwa na kwamba serikali imekwishatoa tamko rasimi kukamatwa mara moja kwa wezi wa nyaya hizo.

Taarifa ya Bw. Semtawa imefuatia malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa Dar es salaam wanaotaka kuwasiliana na ndugu zao au kikazi na wilaya hizo mbili za Tabora.

Wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti wateja hao ambao wanaishi hapa jijini wamesema wamekuwa wakitafuta kwa muda mrefu jinsi ya kuwasiliana na jamaa zao wanaoishi mkoa wa Tabora bila mafanikio.

Mteja mmoja wa Shirika hilo aliyejitambulisha kwa jina la Kulwa Yahya amelieleza gazeti hili kuwa amekuwa akipiga simu bila mafanikio ili aweze kuwasiliana na ndugu zake walioko maeneo ya Kaliua mkoa wa Tabora.

"Nimekwishapiga simu kwa kipindi cha wiki 3 bila mafanikio sasa sipewi laini na hata simu inapopokelewa na Operata ambaye naye akishafanya hivyo ananiambiri bila mafanikio".

Bw. Kulwa amezitaja namba za mkoa huo maeneo ya Kaliua kuwa ni Namba 4, 13, na 40 ambazo amekuwa akiambiwa hazipatikani, "swala hilo mpaka lini", alihoji .

 Abood aisaidia shule vifaa vya ujenzi

Na Said Mmanga - MSJ Morogoro

SHULE ya msingi Mwene iliyoko Manispaa ya Morogoro, imepatiwa msaada wa vifaa mbali mbali vya ujenzi vitakavyosaidia kufanyia ukarabati wa shule hiyo.

Vifaa hivyo ni mifuko 25 ya saruji na mchanga lori tatu, vyote kwa pamoja vikiwa vimetolewa na Mkurugenzi wa Makampuni ya Abood.

Akikabidhi vifaa hivyo wakati wa mahafali ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba shuleni hapo yalipofanyika kwenye hoteli ya Oasis juzi, Mkurugenzi wa makampuni hayo Bw. Aziz Abood aliyewakilishwa na Afisa Elimu wa Manispaa, Esther Mwangamila alisema kuwa amekubali kuwa mlezi wa shule hiyo na kwamba atatoa msaada kadri hali itakavyoruhusu.

Naye Afisa Elimu wa Manispaa hiyo, Bi. Mwangamila akizungumza kwa niaba ya Bw. Abood, alisema kuwa wanfunzi hawana budi kuyatumia maadili mema waliyojifunza shuleni ikiwa ni pamoja na kujiepusha na vitendo viovu kama vile uvutaji bangi na madawa ya kulevya.

Wakati huo huo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara bibi Shamim Khan ameteuliwa kuwa mlezi wa kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Mission to the Homeless (MHC) cha mjini hapa.

Mkurugenzi wa Kituo hicho Bw. robert Lameck Simba aliileza kiongozi ofisini kwake kuwa Bibi Khan aliteuliwa kuwa mlezi katika kikao chake cha mwezi Agosti mwaka huu, kutokana na mchango wake mkubwa kwa jamii.

Alisema mbali na kuwa mlezi wa kituo, Waziri Khan ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum (CCM) pia amepewa jukumu la kutafuta wadhamini wa kituo hicho.

Bw. Simba alisema kuwa hadi sasa kituo chake kina watoto 13 kati yao wanane ni wakiume ambapo baadhi yao wapo katika shule za awali, msingi na wengine wapo katika mafunzo ya ufundi magari, kushona na kudarizi .

Mkurugenzi huyo wa MHC alisema lengo la kituo chake ni kuwa na watoto 25 ambapo pia alisema hivi karibuni katuo chake kilipata misaada kutoka kwa Makampuni na watu biafsi ili kukiendesha.

Aliyataja Makampuni hayo kuwa ni mfuko wa Taifa wa hifadhi jamii (NSSF) mkoa wa Morogoro, Shirika la Kihifadhi Misitu (TAFOL), Frateli wa Chuo cha Mtakatifu Gasper, Na Shirika la Misaada la Kikatoliki la Caritas.

 

 Akutwa amekufa kando ya barabara

Na Gaudence Massati - MSJ Morogoro

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Vijana wa TANU mkoa wa Morogoro, Bw. Seleman Malongoza amekutwa amekufa katika mazingira ya kutatanisha jana alfajiri kando ya barabara iliyokuwa mtaa wa Kitamale, sabasaba mjini hapa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Bw. Christopher Shekiondo, marehemu alikutwa na wapita njia alfajiri ya jana na baadaye kuiarifu polisi ambao walifika eneo la tukio baadaye.

Kamanda Shekiondo amesema marehemu mwenye umri wa miaka 51, alikutwa na jeraha chini ya sikio lake la kulia ambalo lilitokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.

Ameendelea kusema kwamba, mpaka sasa hakuna mtu anayeshukiwa kuhusika na tukio hilo na upelelezi unaendelea ili kujua mtu au watu wanaohusika na tukio hilo.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi, mdogo wa marehemu Bw. Abdallah Malongoza amesema marehemu aliaga usiku wa juzi majira ya saa 2.30 kuwa anakwenda kuangalia video kwenye baa ya New York iliyopo jirani na maeneo anayoishi na hakurudi mpaka alipokutwa amekufa. Watu wanaoishi jirani na eneo ulipokutwa mwili wa marehemu, wamedai hawakusikia kishindo wala kelele za mtu anayepigwa, hivyo wanaamini kuwa marehemu aliuawa mbali na maiti yake kutupwa hapo.

Katika uhai wake marehemu aliwahi kuwa Mwenyekiti wa vijana wa TANU Mkoa wa Morogoro kwenye miaka ya sabini kabla hajaachia wadhifa huo, pia alikuwa mwasisi wa TANU na baadaye wa CCM.

 Mkurugenzi wa manispaa ya Moro atakiwa kujieleza

Na Said Mmanga, Morogoro

MKURUGENZI wa manispaa ya Morogoro ametakiwa kutoa maelezo juu ya kushindwa kwa wazabuni kutengeneza barabara na vivuko au la asubiri Halmashauri kumjadili yeye na wenzake kwamba wameshindwa kumudu dhamana walizokabidhiwa.

Kauli hiyo imetolewa na diwani wa kata ya Kingo (CCM) Bw.Omar Simba wakati wa kujadili utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Maendeleo hususani Ujenzi wa barabara na madaraja (Vivuko) katika Manispaa ya Morogoro.

Diwani huyo amesema lawama inabidi ziwaendee watu wa halmashauri hiyo kwa kutoa zabuni kwa wazabuni wasio na uwezo wa kuzifanya kazi hizo.

Akichangia bajeti ya Halmashauri hiyo katika kikao cha bajeti kilichofanyika katika ukumbi wa Manispaa mwishoni mwa wiki Bw. Kingo alisema wazabuni wengi wanaopewa kazi hizo hawana uwezo wa kifedha na kusema kuwa kuwatumia watu hao ni sawa na kufanya kazi na matapeli.

Bw. Simba alisema suala la kutengeneza vivuko halihitaji fedha nyingi ambapo pia alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa hiyo hadi kufikia Jumatatu kuelezea kwanini asiwajibishwe kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo, vinginevyo kikao cha halmashauri kiwajadili kuwa wameshindwa kufanya kazi .

Wakati huo huo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inatarajia kukusanya jumla ya shilingi 62,430,600 katika mwaka ujao wa fehda.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Emanuel Kalobelo alisema mjini hapa katika kikao cha bajeti ya Halmashauri hiyo, ambapo bajeti hiyo imeongezeka kutoka shilingi milioni 451 hadi milioni 621 na katika uongeza pato hilo halmashauri imepandisha viwango vya kodi ya maendeleo.

Bw. Kalobelo alisema kuwa kodi ya maendeleo kwa mwananchi wa kawaida imepanda kutoka shilingi 1,500 hadi 2,000. Mfanyakazi imepanda kutoka shilingi 3,000 hadi 3,500 wakati mfanyakazi ambaye mshahara wake unazidi shilingi 36,000 kwa mwezi sasa atalazimika kulipa shilingi 4,000 za kodi ya maendeleo badala ya 3,500.

Mbinu nyingine zitakazotumiwa na halmashauri hiyo kuongeza mapato yake ni kuwatumia mawakala katika kukusanya uhuru badala ya kuajiri watu wa kufanya kazi hiyo.