Make your own free website on Tripod.com

 

 

 

 

Bagamoyo Wamwandikia Kikwete kugoma kulipa kodi

lNakala zapelekwa kwa Sumaye na Mkuu wa Polisi

Na Mwandishi wetu, Bagamoyo

WANANCHI wa kata ya Miono wilayani Bagamoyo katika mkoa wa Pwani, wamemwandikia barua Mbunge wa jimbo la Chalinze, Luteni Kanali Jakaya Mrisho Kikwete ili kumfahamisha kwa maandishi kuwa wamegoma kulipa kodi ya maendeleo hadi watakapopewa taarifa sahihi za makusanyo na matumizi ya fedha hizo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita na iwe imethibitishwa rasmi na yeye mwenyewe.

"Mheshimiwa Mbunge tunasitisha kulipa kodi ya maendeleo kuanzia leo hadi tutakapopewa taarifa sahihi na ya wazi ya matumizi ya kodi hiyo", inasema barua hiyo iliyoandikwa Oktoba 27, mwaka huu.

Jumla ya wananchi 30 kutoka vijiji 14 vya kata hiyo wamejiorodhesha majina yao na kutia saini waraka huo na kuitaja miaka wanayotaka wapewe maelezo ya kina ya matumizi ya kodi ya maendeleo waliyolipa kuwa ni 1995/96, 1996/97, 1997/98 na kusisitiza; 'ni vyema taarifa hiyo ikathibitishwa na wewe kwanza kabla hatujaipata'.

Wakionyesha kuwa wanathamini ulipaji wa kodi, wananchi hao wamemwambia Kanali Kikwetu wanatambua umuhimu wa jambo hilo kwa vile ni wajibu wa kila raia kwa taifa lake mahali popote duniani, na kwamba katika kufanya hivyo ndipo Serikali inapokuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu kwa watu wake na kuwaletea maendeleo yao wenyewe katika sehemu wanazoishi.

Wameongeza kuwa pamoja na kulipa kodi hiyo kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini hawapati huduma yoyote kutoka Serikalini na kwamba asiyekuwa na fedha hapati matibabu na kuitaja hali hiyo kuwa inatisha.

"Mheshimiwa Mbunge, bado tuna imani na wewe japo tunajua kuwa ni Waziri unayewajibika kuitetea Serikali unapokuwa Bungeni, lakini kutokana na hali tuliyokueleza tunasitisha kutolipa kodi kuanzia leo", wanasisitiza na kumtaka Kanali Kikwete asilipuuze suala hilo licha ya shughuli zake nyingi.

Wananchi walioandika na kutia saini barua hiyo ni Bwa. Jamal Karim, Msafiri Chanyoya, Mtunze Msakamali, Ally gonzo, Hasimu seif, Yenga Mohammed na Bibi Siwatu Hussein ambao wote wanatoka katika kijiji cha Miono.

Wengine ni Bw. Ramadhani Baquari, Jumane Juma, Jumanne Mchuka, Mayanga Juma na Kasukwa Salumu wanaotoka kijiji cha Kikalo wakati kutoka katika kijiji cha Mafungo ni Bw. Charles Mgamwe na Mwevumbo Juma.

Wanaotoka katika kijiji cha Kwa Makocho ni Bw. Bakari Mgaza na Mbelwa Haji wakati Bw. Hassan Kauzeni anatoka kijiji cha Kwa Mwala na kutoka Msimbani ni Bw. Zuberi Rajabu na Mbelwa Juma.

Orodha hiyo pia ina jina na saini za Bw. Ally Mohammed wa kijiji cha Kwekonye, Jamal Mkali wa Mandela, Ally Mziwanda wa Mihuga, Khamis Juma wa Hondogo, Hussein Juma wa Mchiga, Ramadhan Haji wa Mihuga, Sadiki Rajabu wa Kimange, Khamisi Mohammed wa Kisangasa, Saidi Khamis wa Maehalo, Majuto Kabelwa na Mzee Mbaluma ambao wote kwa pamoaj wanatoka kijiji cha Kilemela.

Nakala za barua hiyo zimepelekwa kwa Waziri Mkuu, Bw Frederick Tluway Sumaye pamoja na Mkuu wa Polisi wa wilaya ya bagamoyo kuwataka walinde haki na uslala wa wananchi hao endapo viongozi wa serikali wanaohusika na suala hlo wataamua kutumia nguvu kujaribu kulitatua.

 

Mtuhumiwa amkataa wakili

Na Mwandishi wa PST, Hirondelle

MAHAKAMA ya Kimataifa ya mauaji ya Rwanda iliyopo Arusha (ICTR) imelazimika kuahirisha kusoma mashitaka ya mauaji dhidi ya mkuu wa zamani wa mkoa wa Cyangungu nchini Rwanda, EmanuelBagambiki, baada ya mtuhumiwa kumkataa wakili aliyechaguliwa na ofisi ya msajili wa mahakama hiyo ili amtetee .

Shirika la habari la Hirondelle lilishuhudia bagambiki akimweleza Jaji Wiliam Sekule aliyekuwa anaendesha kesi hiyo kwamba hayuko tayari kusomewa mashitaka wala kujibu lolote juu ya mashitaka hayo hadi atakapompata wakili atakayemchagua yeye mwenyewe kumtetea.

Ofisi ya Msajili wa mahakama hiyo walimpatia mtuhumiwa wakili, Jacques Fierens kutoka Ubelgiji amtetee Bagambiki lakini wakati wa kutambulishana mahakamani hapo, wakili huyo alitamka wazi kuwa hayuko tayari kumtetea kikamilifu mtuhumiwa huyo hadi hapo atakapokubaliwa rasmi naye.

'Sina imani na wakili huyu kwani sikumchagua mwenyewe', alijieleza Bagambiki na kuongeza kuwa 'siko tayari kujibu lolote mpaka nipate wakili wa kutetea haki zangu'.

Bagambiki alikamatwa nchini Togo Juni 6, mwaka huu na hatimaye kupelekwa katika kizuizi cha ICTR Arusha, Tanzania na kusubiri kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuhusika kwake katika mauaji ya watu wa kabila la watusi nchini Rwanda mwaka 1994.

Kutokana na malumbano hayo yaliyojitokeza, Jaji Sekule aliamuru kuahirishwa kwa kesi hiyo kwa muda usiojulikana ili mtuhumiwa apate wasaa wa kutatua tatizo la kumpata wakili wa kumtetea.

Wiki mbili zilizopita mfungwa mmoja, Jean Paul Akayesu aliyekwisha hukumiwa kifungo cha maisha kwa kuhusika katika mauaji hayo pamoja na watuhumiwa 32 waliopo katika kizuizi cha mahakama hiyo mjini Arusha, waligoma kula kupinga kitendo cha kuchaguliwa mawakili na uongozi wa ICTR.

Hata hivyo mgomo huo uliachwa na watuhumiwa hao pamoja na mfungwa huyoambapo walianza tena kula chakula kwa sababu ambazo mpaka sasa hazijaelezwa wa wakuu wa ICTR.

Wanakijiji walalamikia kuuzwa eneo la madini

Na Echela Kongola, PST, Dodoma

WAKAZI wa kijiji cha Kingiti wilayani Mpwapwa wameulaumu uongozi wa kijiji na Wilaya kufuatia kuuzwa kwa eneo la madini lililopo katika mlima kijijini hapo bila kuwapa taarifa.

Hayo yamo katika taarifa iliyotolewa na baadhi ya wanakijiji iliyotolewa kwenye vyombo vya habari wakitaka wasaidiwe ili kuweza kujua watajulishwa lini kuhusiana na swala hilo la kuuzwa kwa eneo hilo.

Akiongea na PST mmoja wa wanakijiji hao Bw. Samweli Chihimba amesema wameamua kuandika barua ya malalamiko kwenda Mkoani, kwani imekuwa muda mrefu tangu kuuzwa kwa eneo hilo.

Amesema eneo hilo liliuzwa 1985 kwa kampuni moja ambayo inajulikana kwa jina la Kilimanjaro Mine na mpaka sasa linaendelea kuchimbwa madini aina ya Peridort.

Bw. Chihimba alisema wamejaribu kuuliza uongozi wa kijiji lakini wamekuwa wakizungushwa bila kupewa jibu la uhakika ikiwa ni pamoja na uongozi wa wilaya kwa hiyo wameona ni vyema kuliweka swala hilo wazi.

Alisema kuuzwa kwa eneo hilo kumewasababishia vijana wengi kukosa ajira kwani wengi wao walikuwa wakitegemea kufanya kazi katika eneo hilo na sasa wamekuwa wakizurula mitaani.

Mkuu wa Mkoa Bw. Isdori Shirima amemtaka Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Flugence Saria kuandaa taarifa kuhusu kuuzwa kwa eneo hilo ili kuweza kupata ukweli na kuweza kuwafahamisha wanakijiji hao.

Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Flugence Saria amekanusha kuwa si kweli kuwa wanakijiji hao hawakufahamishwa kuhusiana na swala hilo la kuuzwa kwa eneo hilo.

Kufuatia taarifa ya wanakijiji hao inayotoa malalamiko inasema kuwa uongozi wa kijiji na wilaya ungekuwa umewataarifu kuhusu swala hilo wasingetoa malalamiko hayo.

Temeke hawana madawati

Na Said Mmanga

JUMLA ya shule kumi za msingi wilayani Temekejijini Dar es salaam zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati ambapo nusu ya wanafunzi wa shule zote wilayani humo wanakaa chini.

Akiongea na gazeti hili ofisini kwake mwishoni mwa wiki mkuu wa wilaya ya Temeke kepteni John Chiligati alisema wilaya yake ina wanafunzi 77,009 wa shule za msingi ambao wanahitaji madawati 22,434 ambapo yaliyopo ni nusu ya idadi ya madawati yanayohitajika.

Bw. Chiligati alisema wilaya yake ina madawati 10,993 yakiwa ni upungufu wa madawati 11,441 hali ambayo imesababisha nusu ya wanafunzi wote wa shule za msingi zilizopo wilayani humo.

Alizitaja shule ambazo zina upungufu mkubwa wa madawati kuwa ni shule ya msingi Mbagala ambayo ina upungufu wa madawati 1125 kati ya 1663 yanayohitajika,Mabatini 1026 kati ya madawati 1485,na shule ya Mgulani ambayo ina upungufu wa madawati 875.

Shule nyingine ambazo zina upungufu wa madawati ni Rangi tatu yenye upungufu wa madawati 673,Sokoine inayohitaji madawati 635 , Mtoni ambayo inahitaji madawati 609 ili kukidhi mahitaji ya madawati kwa wanafunzi wake.

Bw. Chiligati alizitaja shule nyngine kuwa ni Yombo Vituka,Kurasini Keko Mwanga na Shule ya msingi Temeke. Wakati shule ambazo hazina uhaba mkubwa wa madawati ni Chekeni,Mwisongo,Kisarawe II, Kisiwani , Pemba mnazi,Tuangoma na Jeshi la wokovu.

Ili kuondoa tatizo hilo sugu hapa nchini wilayani mwake Bw. Chiligati alisema kila mzazi anatakiwa hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu anatakiwa awe amekamilisha utengenezaji wa madawati kwa ajili ya kukalia watoto wao.

Mbinu nyingine ambazo wilaya hiyo inazitumia katika kutatua tatizo hilo ni kuwaelimisha na kuwabana wazazi juu ya umuhimu wa madawati kwa watoto wao katika kuboresha elimu hapa nchini.

 

Walemavu wataka wizara yao na mahabusu yao

Na Emma Kayuza

WALEMAVU wameiomba serikali iangalie uwezekano wa kuunda Wizara ya Walemavu ambayo inaweza kuwatatulia matatizo yao.

Hayo yalisema na Mwenyekiti wa muda wa Walemavu,Bw.Mohamed Chanzi wakati wa mkutano wa kujadili white paper uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu uliopo Kurasini Jijini.

Bw.Chanzi alisema kuwa kukosa mahali pa kukimbilia pindi wanapopata matatizo wameiomba serikali iangalie uwezekano wa kuwepo Wizara yao.

Alisema pamoja na kuomba Wizara Walemavu wangeomba watengewe mahabusu zao ili kuepuka kuwachanganya na wa tu wasiokuwa walemavu kwa vile wamekuwa wakiathirika na magonjwa mbalimbali pindi wapelekekwapo huko mahabusu.

 

'Kuchelewa kuanza mabaraza chanzo cha migogoro ya ardhi'

Na Charles Masanyika, Mbulu

KUCHELEWA kuanza kwa mabaraza ya ardhi katika wilaya mbalimbali hapa nchini ndiyo chanzo cha kujitokeza kwa migogoro ya ardhi na kuwa kero kwa wananchi.

Akiongea na gazeti hili ofisini kwake mkuu wa wilaya ya Mbulu mkoani Arusha Bi.Esther Malieta alisema migogoro mingi ya ardhi inayojitokeza sehemu nyingi nchini inashindwa kutatuliwa kutokana na kukosekana kwa mabaraza hayo.

Alisema hivi sasa sehemu nyingi wananchi wamekuwa wakidiriki kupigana na hata kuuwana kwa kugombea mipaka ya ardhi au mashamba.

Bi. Malieta alisema kwa kuwa serikali iliazimia kuunda mabaraza hayo ili kutatua migogoro ya ardhi ingekuwa vizuri yaanzishwe haraka ili migogoro yote inayohusu ardhi itatuliwe kisheria.

Akifafanua zaidi juu yasuala hilo mkuu huyo wa wilaya alisema migogoro mingi inawakabili watu wenye uwezo mdogo hasa pale wanapogombea mipaka au mashamba na watu wenye uwezo ambao hutumia uwezo wao kuwakandamiza wanyonge.

Bi. Malieta alisema katika wilaya ya mbulu mipaka ya mashamba imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi ambapo hata hivyo alisema ofisi yake katika jitihada zake za kutatua migogoro ya ardhi imekuwa ikitembelea sehemu zote zenye migogoro na kuwakutanisha wageni wote ili kupta muafaka kutoka pande zote.

 

 

CUF waandaa mabadiliko makubwa kuing'oa CCM

Na Mwandishi wetu

KATIKA hali inayoonekana ni kujijengea mazingira mazuri ya kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na kuing'oa CCM madarakani hatimaye kuingia Ikulu chama cha CUF kinaandaa mabadiliko makubwa katika uongozi wake wa juu.

Habari kutoka ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani Visiwani zilizothibitishwa na kiongozi mmoja wa juu wa chama hicho ambaye aliomba asitajwe jina lake zinaeleza kuwa ili kuimarisha upinzani nchini nzima badala ya sasa ambapo wana nguvu upande wa Kisiwani, mtuhumiwa wa kesi ya uhaini Juma Duni Haji ndiye atakayekuwa mgombea uraisi wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar.

Mabadiliko mengine kwa mujibu wa habari ni kwamba makamu mwenyekiti wa chama hicho Bw. Seif shariff Hamad atakuwa mgombea mwenza wa kiti cha urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania ambapo mgombea wa nafasi hiyo ataendelea kuwa Ibrahimu Lipumba ambaye alikuwa ni miongoni mwa wagombea waliochuana na rais Benjamin Mkapa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995.

Kiongozi huyo alipoulizwa itawezekana vipi kwa Bw. Juma Duni Haji kuwania kiti hicho wakati akikabiliwa na kesi ya uhaini alisema kiongozi huyo amewekwa ndani kutokana na CCM kuhofia kupoteza madaraka na kusema kuwa miongoni mwa masharti ya muafaka wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar ni kufutwa kwa kesi hiyo ambapo alisisitiza itafutwa wakati wowote.

Habari hizo zimesema kuwa mbali na msukumo ambao serikali ya DK. Salmin Amour inaupata kutoka kwa jumuiya za Kimataifa pamoja na chama hicho juu ya kuachiwa kwa watuhumiwa wa uhaini, akiwemo Juma Duni Haji ambaye ni ndugu wa karibu wa DK. Salmini hali ambayo imempa msukumo kiongozi huyo wa Zanzibar kutaka kuwaacha watuhumiwa hao.

Zinasema habari hizo kuwa hivi ndugu hao wa karibu familia zao zimegawanyika na kuwa chui na paka jambo ambalo limemfanya DK. Salmini hivi atafute mbinu za kumaliza tatizo hilo ili kurudisha umoja katika familia yao na kuijengea CCM mazingira mazuri ya kushinda uchaguzi wa mwaka 2000.

Mabadiliko hayo makubwa ndani ya CUF yanakuja huku CCM upande wa Zanzibar ikiwa inakabiliwa na mgawanyiko mkubwa uliopelekea kwa wanamaskani na viongozi wa chama na serikali kugawanyika katika makundi manne ambapo kila moja anataka mtu wake awe mgombea wa urais wa chama hicho mwaka 2000.

Makundi hayo ni lile ambalo linamtaka waziri wa mambo ya ndani Bw. Ali Ameir awe mgombea wa kiti cha urais kupitia chama hicho. Wengine ni makamu wa rais DK. Omari Ali juma ambaye wengi wanamtaka ili kukitia chama hicho nguvu upande wa Pemba

.Mbali na hao pia katika kundi hilo wapo Dk. Salmin mwenyewe ambaye licha ya Katiba kutomruhusu kugombea tena kiti hicho lakini bado ana uchu wa kutaka kugombea tena na mwingine ni waziri wa Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Amani Abeid Karume mtoto wa hayati Abeid Amani karume rais wa kwanza wa Visiwa hivyo.

 

Hakuna mwanasiasa aliyejipachika madarakani-NCCR

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha NCCR - Mageuzi mkoani Dar es Salaam, kimesema kuwa viongozi wote wa vyama vya siasa hawakujipachika madarakani bali wamekabidhiwa dhamana hizo kutokana na ridhaa za wananchi wanaowaongoza na kumtaka Rais Benjamin William Mkapa asijipe mamlaka ya kuwasemea wanachama wa vyama vya upinzani nchini.

Hayo yameelezwa mjini Dar es Salaam na Katibu Mwenezi wa NCCR - Mageuzi wa mkoa huo, Bw. Charles Charles alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusiana na kauli inayotolewa mara nyingi na Rais Mkapa ya kudai kuwa wapinzani hawana haki ya kuzungumzia masuala mbali mbali ya kitaifa kwa madai kwamba hawana ridhaa ya wananchi kwa sababu walishindwa kuingia Ikulu mwaka 1995.

"Hii kauli ambayo Mkapa aliirudia tena Jumatano wiki hii kwamba suala ima la hii "white Paper iachiwe serikali peke yake na kutaka wapinzani wasizungumze lolote eti kwamba hawana ridhaa ya watu ni upotoshaji mkubwa. Hakuna mwanasiasa aliyejipachika madarakani hali wote wamechaguliwa kama yeye. Tofauti iliyopo tu ni wadhifa alionao kila mmoja", amesema kiongozi huyo.

alisisitiza kuwa viongozi wa vyama vya upinzani wana haki sawa na viongozi wa CCM kama Rais Mkapa mwenyewe katika kutoa maoni na maelekezo kwa wanachama wanaowaongoza na kusema neneo "wananchi" linamaanisha watu bila kubagua kabila, dini, rangi, itikadi au mapenzi aliyonayo kila mmoja katika nafsi yake.

Bw. Charles alimtaka Rais Mkapa aache kuwapotosha Watanzania kwamba wapinzani hawana haki ya kuipinga, kuikosoa au kuichambua kwa namna yoyote White paper na kuonya kuwa endapo "hatajirekebisha" atawalazimisha waanze rasmi kumchambua kisiasa .

Bw. Charles Charles ambaye pia ni Msemaji wa Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, Bw. Augustine Lyatonga Mrema, alisema kauli inayotolewa mara nyingi na Rais Mkapa ya kuwataka wananchi wawapuze wapinzani wanapozungumzia masuala muhimu ya kitaifa ikiwemo katiba ya nchi yao ni jitihada mbovu za kutaka kudhibiti na kupora mamlaka waliyonayo wananchi ya kuweka utaratibu wa kuongozwa na serikali yao kwa jinsi wanavyotaka wao.

 

Wanaotuhumiwa 'kuyeyusha' mamilioni Kilimo 'Wageuka mbogo'

Na Mwandishi Wetu

WATUMISHI waliostaafu kazi Serikalini katika Wizara ya Kilimo na Ushirika, wamesema kuwa hawajui hatima ya mafao yao kutokana na kero wanazopata kutoka kwa maofisa wa juu ambapo pamoja na kutoshughulikiwa kabisa kwa namna yoyote, lakini pia wamekuwa wakitukanwa na kukaripiwa kila wanapojaribu kuyafuatilia.

Katika barua yao ya Novemba 2, 1998 waliyomwandikia KatibuMkuu wa Wizara hiyo. Bw, Barie, wawakilishi wanane wa watumishi hao wastaafu, wameleza jinsi wanavyonyanyaswa katika Makao Mkuu ya Wizara hiyo mjini Dar es Salaam na kutaka awakutanishe ana kwa ana na maofisa wanaohusika ili waambiwe mbele yake ni kwa nini wanafanyiwa hivyo na lini watalipwa haki zao.

"Katika zoezi zima la kufuatilia mafao yetu yakiwemo mapunjo yake tumekuwa tukipambana na kero mbali mbali kutoka kwa watumishi na watendaji wa Wizara yako. "Kero tunazopata ni pamoja na kutukanwa na kukaripiwa na baadahi ya maofisa utumishi, wahasibu na watu wa masjala, kitu ambacho kimetufanya hadi sasa tusipate haki zetu toka mwaka 1996", inasema barua hiyo iliyosainiwa na jopo la wastaafu hao wanane kwa niaba ya wenzao wengi kutoka sehemu mbali mbali nchini.

Wastaafu waliosaini barua hiyo wakiongozwa na Bw. George N. Jackson ambaye alkuwa mkufunzi wa Chuo cha Utafiti na Mafunzo ya Kilimo cha Tumbi huko Tabora ni pamoja na Bw. Justine Kisege, Rmadhani Alute, Charles ahmsa, Michael K. Kumoso, Charles H.M. Elieza, Weston B. Mbonile na Gerold K. Ngerangera katika barua hiyo ambayo pia imenakilishwa kwenda tume ya Kudumu ya uchunguzi inayofanya kazi zake ikiwa chini ya Ofisi ya Rais, Ikulu, potevu wa mafaili ya wastaafu hao nalo ni tatizo jingine lililozungumziwa na kutajwa kuwa ni kero nyingine iliyokosa ufumbuzi.

"Baadhi yetu tumekaa Dar es Salaam kwa zaidi ya miezi sita sasa bila kupatikana kwa majadala yetu", inasema barua hiyo ambayo mwandishi wa habari hzi ameiona nakala yake.

Sambamba na hayo, wastaafu hao wameeleza kwamba uchunguzi wa kina walioufanya unaonyesha kuwa baadhi wa hundi za malipo ya mafao wanayodai zilishachukuliwa na watendaji wa Wizara hiyo kutoka Wizara ya Fedha na kupotelea mikononi mwa baadhi ya maofisa wakuu ambao ni watendaji wanaohusika na shughuli hiyo bila kuwafikia wenyewe.

 

Saba wapanda kizimbani kwa wizi wa kuku wa mayai 100

Na Emma Kayuza

WAKAZI saba wa Segerea Jijini,wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Buguruni kujibu shitaka la wizi wa kuku 100 wa mayai wenye thamani ya shilingi 300,000.

Mbele ya hakimu Rukia Katembo,Konstebo Issa Salum alidai kuwa Oktoba 31 mwaka huu saa 9.00 usiku katika eneo la Segerea Msikitini washtakiwa kwa pamoja waliiba kuku hao mali ya mlalamikaji aliyemtaja kwa jina la Johanes Magesa.

Konstebo Salum aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Salum Msemo (25),Daud Bulavi (23),Wailen Peter (19),Stephano Paschael (22),Rajabu Abdalah (28),Simba Juma (34) pamoja na Sufian Said (29).

Washtakiwa kwa pamoja walikana kuhusika na shtaka hilo na wako rumande kwa kukosa wadhamini hadi Novemba 13 kesi yao itakapotajwa.

Wakati huo huo,Christopher Buruno (20) mkazi wa Yombo Minazi mirefu amekiri kosa la kutishia kumchoma kisu mlalamikaji Joseph Mussa .Mbele ya hakimu Rukia Katembo,Knstebo Issa Salum alidai kuwa Novemba Mosi mwaka huu 1.00 usiku katika barabara ya Nyerere ndani ya daladala TZK 9779 ambalo linafanya safari zake kati ya Gongolamboto -Kariakoo ,mshtakiwa alimtishia kumchoma kisu mlalamikaji ambaye ni dereva wa gari hilo ,akiwa kwenye mwendo.

Konstebo Salum alidai kuwa mshitakiwa alichomoa kisu na kumtishia mlalamikaji na kumsababishia hofu mwenyewe pamoja na abiria waliokuwa ndani ya gari hilo.

Konstebo Salum aliendelea kudai kuwa siku hiyo hiyo na muda huo huo katika kituo kidogo cha polisi TAZARA baada ya kufikishwa kituoni hapo kwa kosa la kutishia,wakati akipewa ulinzi,smhtakiwa aliaanza kumrushia ngumi na mateke askari C 6094,Konstebo Peter kwa nia ya kupinga kupekuliwa na kuwekwa mahabusu.

Mshtakiwa alikana kuhusika shtaka la kumfania fujao askari huyo na ametrudishwa rumande kwa kukosa wadhamni hadi Novemba 12 kesi yake itakapotajwa.

 

Wafanyabiashara wanung'unikia ushuru wa asilimia 40 wa sukari

Na Dalphina Rubyema

WAFANYABIASHARA wanaoingiza sukari nchini kutoka nchi za nje,wamesema siku za usoni kutakuwepo na upungufu mkubwa wa bidhaa hiyo hali itakayopelekea bei kupanda.

Wafanyabiashara hao wakubwa ambao kwa kawaida huagiza sukari na ambao hawakupenda kutajwa gazetini wamesema kwa kuwa sukari itakayokuwa inategemewa ni ya kutoka humu humu nchini, huku ikijulikana dhahiri kuwa uzalishaji wetu hautoshelezi.

Walisema Serikali ya Tanzania inafanya kazi zake kwa kuburuzwa ndiyo maana hata inatoa uamzi bila kufikiria madhara yanayoweza kutokea kwa jamii.

"Huyu Mkapa anaburuzwa sana alivyofika Kilombelo na kuambiwa kuwa sukari ya kiwanda hicho hainunuliki hivyo ni hasara kwa Taifa naye akatoa tamko kuwa sukari inayoingizwa nchini kutoka nchi za nje ipandishwe kodi kwa asilimia arobaini bila kujali sisi tunaoiingiza tutapata hasara kiasi gani?"alihoji Mfanyabiashara mmoja anayefanyia biashara yake mtaa wa Living Stone Jijini.

Kauli ya wafanyabiashara hao hata hivyo inapingana na ya serikali ambayo imesema licha ya kupandisha ushuru wafanyabiashara hao hawatapa hasara hata kidogo.

Waziri wa fedha Bw.Yona licha ya kukiri kuwa hatua hiyo imelenga kulinda wazalishaji wa hapa nchini, ushuru huo utasaidia kuimarisha bei ya sukari.

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa habari hizi unaonyesha kuwa bei ya sukari bado haijapanda bei ambapo hivi sasa gharama yake ni shilingi 380 katika maeneo ya Yombo na shilingi 400 katika maeneo kadhaa ya Jiji.

 

Amwagia mumewe maji ya moto usoni

Na Getruder Madembwe

SALMA Mohamedi mwenye umri wa miaka (40) mkazi wa Salasala Kunduchi amefikishwa Mahakamani kwa kosa la kumjeruhi mume wake usoni kwa kumwagia maji ya moto .

Akisomewa shitaka hilo na msoma mashitaka wa Polisi Konstebo Bakari Bakari kuwa mnamo Oktoba 2 mwaka huu majira ya saa 4.00 usiku mshitakiwa alimmwagia maji ya moto mume wake na kumsababishia kubabuka usoni.

Akijitetea Salma alisema kwamba yeye alikuwa anataka kupika ugali na kwa bahati mbaya maji yalimwagika. Shitaka hilo lipo mbele ya hakimu Jafari Msensemi.

Wakati huo huo Jackson Evana (32) na anthony John wamefikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na shitaka la kukutwa na pombe haramu ya gongo.

Wakisomewa mashitaka na msomaji mashtaka mbele ya hakimu Msensemi kuwa mnamo Novemba 3 mwaka huu huko Mbezi kunguru majira ya saa sita mchana washitakiwa walikamatwa na pombe hiyo haramu ya gongo lita kumi. Washitakiwa wamekana shitaka na wamerudishwa rumande.

 

LHCR wapinga kuingizwa silaha huria

Na Mwandishi Wetu

KITENGO cha Kutetea Haki za binadamu (LHRC) kimepinga vikali uuzaji binafsi wa silaha kwa madai kuwa hivi sasa polisi imeshindwa kuthibiti silaha chache zilizopo nchini.

Hayo alisemwa na mwanasheri mkuu wa kitengo hicho, Bw. Evod Mmanda alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake.

Alisema kuwa silaha zilizoko mikononi kwa sasa udhibiti wake umekuwa dhaifu kwa sababu silaha hizo pamoja na sare za jeshi na polisi zimekuwa zikitumika katika matukio ya ujambazi.

"Tujikumbushe na tukio la hivi karibuni huko mkoa wa Kagera ambapo majambazi wawili waliokuwa na bunduki za SMG waliteka nyara mabasi manne na kuwaamuru abiria wa mabasi hayo kuvua nguo zao

jambo ambalo kitengo chake kimekiona kitendo hicho ni unyanyasaji wa kijinsia",alisema.

Bw. Mmanda alitoa sababu tatu za kupinga uuzaji binafsi wa silaha ambapo alieleza kuwa silaha zitakazouzwa zimetengenezwa kwa ajili kuulia, sababu ya pili alidai kuwa silaha zilizoko mikononi mwa jeshi na polisi uthibiti wake umekuwa dhaifu na mwisho alidai kuwa kwa nchi zilizoendelea kama Marekani na Ulaya ambako kuna jeshi zuri lakini udhibiti wa silaha hizo umeshindikana.

Alisema silaha hizo zikiwa nyingi mikononi mwa wananchi zinaweza kuliletea taifa vita kama vile Soweto au jimbo la Kwa Zulu Natal Afrika ya Kusini ambapo kupigana ni jambo la kawaida.