Kardinali Pengo aonya biashara huria ya silaha

Na Mwandishi wetu

KIONGOZI wa kanisa Katoliki nchini mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameonya dhidi ya kubinafsishwa kwa biashara ya silaha na kuitaka serikali kuendelea na utaratibu wake wa zamani.

Akizungumza na gazeti hili jana, muda mfupi kabla ya kuondoka Kwenda Roma, Italia kuhudhuria mkutano wa mahusiano ya kidini, Kardinali alisema sio kila biashara itaachiwa kwenda huria kwa kuwa inaweza kuhatarisha maisha ya binadamu na kuweka viumbe wote katika hali ya tashwishi na maisha yao.

Kardinali alisema kauli ya serikali kwamba watu wanahitaji silaha kwa hiyo lazima zitafutiwe watu wa kuziuza, haifai kwa kuwa haijitoshelezi na kwamba haishiki maji.

Akifafanua zaidi alisema kwamba kauli hiyo ya serikali inafanana kabisa na utoaji wa ruhusa kwa mauzo huria ya mihadarati kwa kuwa inahitajika.

"Mihadarati katika udhibiti ni dawa, lakini ukiacha hivihivi itakuwa na madhara makubwa kwa binadamu" alisisitiza na kuongeza kuwa biashara ya silaha ni sawa na biashara ya mihadarati haina budi kudhibitiwa.

Kiongozi huyo wa kidini amesema kutokana na mashaka katika utaratibu mzima wa biashara huria, hana budi kukemea hatua hiyo ya serikali, hatua ambayo inaweza kuileta madhara makubwa kwa taifa.

Alitolea mfano kuwa silaha hizo si rahisi kufikia kwa watu wema pekee kwani hata wabaya watazipata kwa kuzingatia hali yenyewe halisi ya masoko huria hasa hapa nchini.

Amesema biashara ya silaha inapashwa kubaki serikalini kama zamani kwa kuwa ni huko tu inakuwa rahisi kujua idadi ya silaha zilizoingia na nani wameuziwa.

"Angalau kwa utaratibu wa zamani serikali ilikuwa na uhakika wa kitu fulani, lakini kwa hili uhakika haupo" na hivyo kutokuwepo na sababu za msingi za kujitetea.

Aidha kiongozi huyo wa Wakatoliki amesema kwamba wananchi ni lazima waamshe sauti yao kuiomba serikali kufuta kusudio lake hilo.

Akitolea mfano wa Marekani, alisema taifa hilo kwa sasa linatafuta mbinu nyingine ya kukabiliana na uwingi wa silaha mikononi mwa watu , silaha ambazo zinatumiwa hata na watoto wadogo kuwachachafya wengine.

 

CCM Zanzibar wasambaratika

lDK. Omari, Ameir, Salmin, Karume wazua mvutano

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

WANACHAMA na wana Masikani wa CCM pamoja na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wamegawanyika katika makundi manne juu ya nani awe mgombea wa Urais wa Zanzibar mwaka 2000.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kuna kampeni zinazoendeshwa kisirisiri na makada wa chama hicho ambapo kila kundi likitaka mtu wao ndiye awe mgombea wa urais wa Zanzibar katika uchaguzi ujao.

Viongozi wanaodaiwa kupigiwa kampeni za chini chini na wanachama pamoja na jumuiya za chama hicho ambazo ni Vijana, Wazazi na U.W.T na hivyo kusababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho ni Rais wa Zanzibar Dk.Salmin Amour, Makamu wa Rais Dk. Omari Ali Juma, Waziri wa Mambo ya ndani Ali Ameir na Waziri wa Mawasiliano wa Zanzibar Amani Abeid Karume.

Uchunguzi huo umeonyesha makundi hayo yamesababisha upinzani mkali kati ya kundi la Dk. Salmin linaloongozwa na wazee na kundi la Dk. Omari Ali Juma linaloungwa mkono na idadi kubwa ya vijana .

Habari zilizopatikana kutoka kwa watendaji wakuu wa Serikali na masikani mbalimbali zinadai kuwa Dk. Salmin kampeni zake zinaendeshwa na wazee ambao wamekuwa hawabadunki makao makuu ya CCM Kisiwandui.

Mwanachama mmoja wa chama hicho ambaye alikataa kutaja jina lake alisema kwamba kundi la Dk. Salmin linaongozwa na mwanasiasa wa zamani aliyemtaja kwa jina la Mzee Kwacha ambaye amekuwa akitamka hadharani DK. Salmin lazima agombee mwaka 2000.

Hata hivyo uchunguzi huo umeonyesha kuwa kundi la mwanasiasa huyo linaonekana kukosa nguvu kutokana na vijana wengi kuwa na imani kwamba iwapo Dk. Omari atasimama kugombea Zanzibar ana uwezo wa kumaliza siasa za Uunguja na Upemba

Waziri wa mambo ya ndani Ali Ameir Mohamedi hivi karibuni alisema kuwa hivi sasa masikani zimekuwa zikiwapiga majungu viongozi. Alikuwa akichangia mada juu ya hali ya kisiasa Zanzibar katika semina ya siku mbili iliyoandaliwa na CCM huko Wete Pemba.

Waziri huyo hakufafanua wanachama hao wa CCM wanawapiga majungu viongozi gani, lakini inadaiwa kwamba kauli hiyo imekuja baada ya Ali Ameir kuambiwa hafai kugombea Urais kwa mwaka 2000.

Naye Raisi Salmin akifunga semina hiyo alisema kwamba masikani zote zinazopiga majungu viongozi ziache kazi hiyo mara moja na kuahidi kuzishughulikia .

Rais wa Zanzibar inasemekana bado ana hamu ya kugombea nafasi hiyo licha ya Katiba ya Zanzibar kumuweka kushoto kutokana na muda wake wa vipindi viwili kumalizika.

Dk. Salmini alisema Chama cha Mapinduzi hakitakubali kuona viongozi wakiendelea kupigwa majungu na wana masikani na kuwataka wanaoendelea na mchezo huo waache mara moja.

Hivi sasa mitaa mbali mbali ya Zanzibar imetawaliwa na mazungumzo makubwa juu ya suala hilo nani agombee nafasi hiyo kati ya Dk. Ali Omari Juma na Amani Abeid Karume, Dk. Salimin Amour na Ali Amir Mohamedi

 

HEKAHEKA YA WALIOKUMBWA NA MAFURIKO

Kambi ya Buza kuvunjwa kesho

Na Dalphina Rubyema

TUME ya Jiji la Dar-es-salaam kesho inatarajia kuvunja kambi ya watu walioathirika na mafuriko na kuhifadhiwa katika eneo la Buza wilayani Temeke Jijini.

Habari za kuaminika ambazo Mwandishi wa habari hizi amezipata zinasema kuwa Tume ya Jiji imewapatia waathirika wote viwanja vya kujenga katika eneo la Kinyelezi na Buza hapo hapo. Kaya 130 ndizo zilizokuwa zinahifadhiwa katika kambi ya Buza.

Jumla ya familia 120 zimeisha ondoka katika eneo hilo na kuhamia katika viwanja walivyopewa eneo la Buza ambapo familia kumi zilikuwa kwenye maandalizi ya kuhamia Kinyelezi hapo kesho.

Habari zaidi kutoka katika eneo hilo zilizotolewa na mmoja wa waathirika aliyejitambulisha kwa jina la Bibi. Asha Husein zinasema familia hizo kumi zilizokuwa zimebaki eneo hilo zimepatiwa viwanja mnamo Oktoba 21 katika eneo la Kinyelezi na mara baada ya kupatiwa viwanja hivyo zilitakiwa kuhama mara moja.

Aliendelea kusema kuwa kwa vile huko Kinyerezi hakuna nyumba,waliiomba Tume iwape muda wa kuendelea kujihifadhi kwenye mahema hayo hadi hapo watakapo kuwa wamejenga nyumba kitu ambacho Tume ilikubali na kuwapa muda wa siku mbili wawe wameshamaliza kujenga.

"Tuliiomba Tume itusaidie na imetupa muda wa siku mbili hivyo tunajitahidi kujenga na hiyo Jumapili gari la Tume litakuja kutuchukua hadi Kinyelezi"alisema Bibi Asha.

Habari zaidi zinasema kuwa mizigo ya waathirika hao tayari imeshapelekwa Kinyelezi na hiyo kesho gari litabeba watu na vyombo vichache.

 

Katika hali inayoonyesha kupotea kwa mwelekeo:

Wapinzani wapondana wenyewe kwa wenyewe

lMaalim Seif aambiwa ametia ulimi wake puani... Kisa kakubali muafaka na CCM

Na Said Mmanga

WAKATI vyama vya upinzani vikiwa vinaendelea kudai mkutano wa Katiba na kuuponda waraka namba moja wa Serikali wa kujadili mabadiliko ya Katiba nchini White paper vyama hivyo vimeendelea kujichanganya na kusema kuwa viongozi wa vyama hivyo ndio sababu kubwa ya kutofanyika kwa mkutano huo.

Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha National League for Democrasy (NLD) Emanuel Makaidi alisema jijini alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuwa si kweli kama Serikali imekwamisha mkutano wa Katiba bali vyama vya upinzani ndio kikwazo kwa kuwa vviongozi wengi wa vyama vya upinzani hawapo makini.

Alisema kama kweli wapinzani wanataka mkutano wa Katiba basi hawana budi wabunge wa vyama hivyo kujiuzulu ikiwa ni njia mojawapo ya kuilazimisha Serikali kuitisha mkutano wa katiba au kuipinga White Paper.

Kiongozi huyo wa chama cha upinzani ambacho hakina mbunge katika bunge la Jamhuri ya Muungano wala katika baraza la wawakilishi, alisema kuwa badala yake hivi sasa vyama hivyo vimekuwa katika migogoro ya mara kwa mara yenye kila aina ya ubinafsi.

Aidha kiongozi huyo alisema kwa sasa vyama hivyo vimezorota hali ambayo alidai imemfanya rais Mkapa kutaka kuanzisha mdahalo wa kujadili upinzani hapa nchini kwa kuwa anajua bila ya kuwepo kwa vyama hivyo hawezi kuongoza nchi.

Aliwataka viongozi wa vyama vingine kuacha kumlaumu Rais Mkapa na badala yake wajitokeze wakati mjadala huo utakapozinduliwa ambapo alisema mara utakapoanza mjadala huo chama chake kitakuwa cha kwanza kujitokeza.

Akitumia lugha ya mafumbo na majigambo kuwa chama chake ndicho bora zaidi Bw. Makaidi aliwaponda viongozi wa vyama mbalimbali na kutamka kuwa hawawezi kuwa marais wa nchi hii na wala hawawezi kuongoza mageuzi kwa kuwa ni mawakala wa chama tawala.

Naye aliyekuwa mratibu wa mambo ya ndani wa chama cha wananchi (CUF) ambaye amejiunga na NLD Bw. Michael Nyaruba alisema kuwa kitendo cha Makamu mwenyekiti wa CUF Bw. Seif Sharif Hamad kukubali muafaka pamoja na kumtambua Dk. Salmin Amour na Serikali yake ni sawa na kutia ulimi wake puani

Kutokana na sababu hiyo Bw. Nyaruba alisema yeye pamoja na wenzie wameamua kujiunga na NLD ili kuimarisha upinzani ambapo alidai kuwa asilimia sitini ya wenyeviti wa mikoa wa CUF Tanzania bara wanamuunga mkono kutokana na hatua yake ya kujiengua katika chama hicho.

Katika hatua nyingine aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha PONA mkoani Mbeya Bw. John Mwakibinga alisema vyama vya upinzani ni vizuri lakini vinaharibiwa na viongozi au waanzilishi ambao wanatamaa ya pesa. Bw. Mwakibinga naye amejiunga na chama cha NLD.

 

Kinyesi chahatarisha wafanyabiashara wa Sabasaba

Na Gaudence Massati, MSJ, Morogoro

WAFANYABIASHARA wafanyao shughuli zao kuuzunguka uwanja wa Sabasaba mjini Morogoro, wapo hatarini kuambukizwa magonjwa, kutokana na wafanyabiashara hao kuyatumia baadhi ya majengo ambayo hayajakamilika ujenzi wake kwa kujisaidia haja ndogo na kubwa.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, aliyetembelea uwanjani hapo, umeonyesha kuwa sehemu kubwa ya uwanja huo imetapakaa mkojo na vinyesi kiasi cha kusababisha harufu mbaya kwenye baadhi ya sehemu na kuwa kero kwa wapita njia.

Kwa mfnao eneo linalokutanisha barabara ya Kiswanya na ile iendayo jengo la CCM mkoani hapo kuna jengo ambalo halijaisha na karibu wafanyabiashara wote wa soko lililo karibu na uwanja huo hujisaidia hapo na kufanya jengo hilo lifurike mkojo kiasi kwamba kwa sasa mkojo huo unatiririkia barabarani na kuleta kero na harufu mbaya kwa wapita njia, pia eneo la jukwaa kubwa la uwanja huo kwa sasa limejaa vinyesi na mkojo kiasi cha kutisha na kuhatarisha afya za vijana wanaofika asubuhi na jioni kufanya mazoezi kiwanjani hapo.

Mwandishi wa habari hizi alipoongea na mmoja wa viongozi wa soko hilo aliyejitambulisha kwa jina moja tu Bwana Mpeka, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo.

Na aliongeza kwamba imekuwa vigumu sana kuwadhibiti watu wasijisaidie katika maeneo hayo, alidai kuwa wengi hukwepa gharama za vyoo vya kulipia ambazo hutozwa sh. 100 kwa haja kubwa na 50 kwa haja ndogo. Hata hivyo amesema kwamba kukosekana kwa ustaarabu pia ni chanzo cha tatizo hilo na ofisi yake inaandaa mikakati ya kukomesha tatizo hilo.

 

Akamatwa Dar na kurejeshwa Kilwa kwa kudhalilisha ajuza

Na Padri Anthony Chilumba,Kilwa Masoko

KIJANA mmoja Kheri Hamza(21) mkazi wa kijiji cha Kivinje wilayani Kilwa katika Mkoa wa Lindi ambaye alikimbilia mjini Dar-es-salaam baada ya kutuhumiwa kumdhalilisha mama mmoja kwa kumbaka(jina tunalo) amekamatwa na kurudishwa Kilwa.

Habari zinasema katika Juma la mwisho la Mwezi Agosti mwaka huu ,katika eneo la Kituba lililopo Kivinje,mutuhumiwa alikamata bibi mmoja mwenye umri wa miaka 70 na kumpeleka kichakani akiwa na lengo la kumwingilia kimwili bila ridhaa yake.

Katika patashika hiyo,mtuhumiwa inasemekana kabla hatatimiza haja yake alikurupushwa na wapita njia.

Katika tukio hilo ambalo liliwashangaza wakazi wengi wa eneo hilo,mtuhumiwa alikimbilia mjini Dar-es-Salaam na alikamatwa Oktoba 10 mwaka huu ambapo alikamatwa na polisi na kumfikisha Kilwa.

Uchunguzi unaonyesha kwamba mutuhumiwa ambaye anashikiliwa na polisi atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa upelelezi.

 

Mkurugenzi apiga marufuku wanafunzi kutumiwa kuuza bidhaa  

Na Moses Kaona, Mbeya

MKURUGENZI wa Manispaa ya Mbeya amepiga marufuku tabia iliyojengeka kwa baadhi ya walimu ambao huwashirikisha wanafunzi kuuza vitu vya biashara kwenye shule za msingi.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Bw. Robert Chidosa alisema walimu na wanafunzi hawaruhusiwi kuuza vitu vya aina yoyote ile nje na ndani ya eneo la shule.

Bwana Chidosa alisema halmashauri yake ilishawakataza walimu hao kuleta vitu ambavyo huuzwa kwa wanafunzi kwenye shule zote zilizopo kwenye Halmashauri yake ilishangazwa na tabia hiyo ambayo inaonekana kupuuzwa na walimu hao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari kwenye baadhi ya shule ambapo aliwakuta baadhi ya wanafunzi wakiuza barafu (ice cream), maandazi, bagia na big-g za walimu wao.

 

Sprint promotion yalalamikiwa Mbeya

lVibarua wasema hawapewi ujira wao

Na Moses Kaona, Mbeya

KAMPUNI ya Sprint Promotion kutoka Kenya ambayo inafanya utafiti wa kuuza sabuni ya unga ARIEL Mkoani Mbeya imelalamikiwa na vibarua wanaouza sabuni hiyo kwa kutowalipa malipo yao kwa wakati unaostahili.

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi baadhi ya vibarua hao walisema kampuni hiyo imekuwa ikivunja makubaliano ya malipo ya 2000/- kwa siku.

Walisema baadhi yao wamefukuzwa na kukosa malipo yao kwa madai ya kuuza sabuni kidogo ambapo paketi kubwa huzwa kwa shiling 300/- na ndogo kwa shiling 200/- walidai kuwa hulazimika kushinda na njaa toka asubuni mpaka jioni wakitembeza sabuni nyumba hadi nyumba.

Aidha walisema kuwa siku ya kwanza kazini haihesabiwi kulipwa hata hivyo walisema malipo yao hayatolewi kwa wakati unaotakiwa mpaka sasa hawajalipwa fedha zao na hawaelewi wachue hatua gani.

Walipoulizwa kuwa endapo kampuni hiyo itaamua kuondoka na kuwaacha bila kuwalipa fedha zao watachukua hatua gani walisema watashindwa kuchukua hatua za kisheria kwa kuwa kampuni hiyo inatoka Kenya na wao ni vibarua wanaotegemea kulipwa kwa siku.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi ulibaini kuwa vibarua hao huuza sabuni hizo kwenye maeneo ya Mwakibete, Isanga, Iyunga, Mabatini, Uwanja wa ndege na mji mdogo wa Mbalizi ambapo hutakiwa kutoa maelezo ya matumizi ya sabuni hiyo na kusimamiwa na viongozi wao.

Alipohojiwa kuhusiana na suala hilo kingozi wa kampuni hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja na Mourice alikataa kusema lolote akidai kuwa yeye si msemaji.