Kilombero wagoma kupinga kunyanyaswa na wageni

lBodi ya ILOVO yakutana kupooza makali

Na Said Mmanga,MSJ, Morogoro

WAFANYAKAZI wa kiwandani na mashambani wa kiwanda cha kusindika sukari inayotiokana na miwa, Kilombero jana walitarajiwa kumaliza mgomo wao waliouanza Oktoba 14 mwaka huu baada ya kufikiwa kwa muafaka na menejimenti.

Mgomo huo ambao uliitishwa na chama cha wafanyakazi wa hapo kwa mujibu wa katiba kwa ajili ya kushinikiza mazungumzo unasadikiwa kuingiza kiwanda hasara ya mamilioni.

Baada ya kuona wanaingia hasara menejimenti ya kiwanda cha sukari cha Kilombero kimekubali matakwa ya wafanyakazi hao na hivyo kumaliza mgomo wa siku tatu ambao ulikuwa ukiuunguruma kiwandani hapo.

Menejimenti hiyo imewaahidi wafanyakazi kuwatimizia matakwa yao yote ifikapo Novemba mwaka huu.

Uamuzi huo umefikiwa na bodi ya kiwanda hicho ambayo ililazimika kukutana kwa dharura kujadili mgomo huo ambao unadalili zote za kutibua hali ya uendeshaji kiwandani hapo.

Akiongea kwa njia ya simu na gazeti hili kutoka Mkoani humo mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi kiwandani hapo (T.P.A.W.U) Bw.Stephen Mbuye alisema mgomo wa wafanyakazi uliokuwa umeanza Oktoba 14 ulimalizika juzi baada ya uongozi kuahidi kutekeleza baadhi ya madai yao yakiwemo ya kurekebvisha saa za kazi.

Imedaiwa kuwa waajiriwa hapo tangu wageni hao kutwaa kampuni hiyo huwafanyisha kazi nyingi waajiriwa kwa mshahara kidogo.Aidha imedaiwa kuwa wafanyakazi wa mashambani wamebadilishiwa kipimo na hivyo kuwafanya na wao wajaribu kutumbukiza familia zao ili kukidhi miraba mipya iliyoongezwa.

Aidha yamekuwapo na madai ya wafanyakazi kunyanyaswa na wageni waliotwaa kiwanda hicho maarufu kwa utengenezaji wa sukari inayotumika hapa nchini.

Alisema bodi ya Kiwanda hicho iliyokutana juzi chini Mkurugenzi wa kampuni ya ILOVO ya Afrika Kusini iliyonunua kiwanda hicho ambaye hata hivyo hakuweza kulifahamu jina lake aliyewasili nchini Oktoba 14 asubuhi ili kuja kuzima mgomo huo, ilikubaliana kutekeleza baadhi ya madai yao kama kulipa pesa za likizo kwa wafanyakazi,nauli,kuboresha huduma kwa wafanyakazi, kuondoa unyanyasaji na kuongeza mishahara ambapo wamekubaliana hadi kufikia Novemba 30 madai hayo yawe yametekelezwa na kama yasipotekelezwa watagoma tena.

Bw.Mbuye alisema kuwa kampuni ya ILOVO ambayo ilinunua kiwanda hicho iliahidi kutekeleza madai mbalimbali ya wafanyakazi lakini mara baada ya kukinunua kiwanda hicho walianza kukataa kutimiza ahadi zao na kuanza dharau kwa wazawa hali ambayo alisema iliwafanya waamue kugoma ikiwa ni njia moja wapo ya kudai haki zao.

Alisema hali ya maisha ya wafanyakazi kiwandani hapo imekuwa mbaya ambapo alisema ubaguzi wa rangi umekuwa ni wa hali ya juu ambapo alisema uongozi wa kiwanda hicho umeajiri kikosi maalumu cha ulinzi kutoka nchini kenya kinachojulikana kama (K.K.Security) ambao wamekuwa wakiwanyanyasa wafanyakazi wa Kitanzania kwa kuwapiga.

Akielezea zaidi Bw. Mbuye alisema wafanyakazi wazalendo wamefukuzwa katika nyumba walizokuwa wakiishi kiwandani hapo na nyumba hizo kupewa wazungu wenye asili ya Afrika kusini ambapo imewekwa mipaka ambayo ni marufuku kwa Watanzania (waafrika) kufika katika maeneo wanayoishi wazungu hali ambayo alisema inasababishwa na wazungu hao kuzoea hali ya ubaguzi nchini kwao Afrika kusini.

Gazeti hili lilipotaka kuongea na meneja mkuu wa Kiwanda hicho lilielezwa kuwa amesafiriki kuja jijini na viongozi wengine pia wamesafiri na hawajulikana wameelekea wapi isipokuwa aliyekuwepo alikuwa ni meneja wa kiwanda aliyetajwa kwa jina la Jchang ambaye naye hakupatikana kuongelea juu ya tatizo hilo.

 

Magari yaliyobeba mabomu yatambuliwa

lNi Nissan na Suzuki Samurai

Na Dalphina Rubyema

JESHI la Polisi nchini kwa kushirikiana na Maafisa wa Upelelezi kutoka Marekani (FBI) pamoja na vyombo vingine kutoka ndani na nje ya nchi wamefanikiwa kutambua gari lililotumika kubeba bomu lililolipua Ubalozi wa Marekeni nchini hapo Agosti 7, lilikuwa aina ya Nissan, iliyotengenezwa mwaka 1987 na pia gari jingine aina ya Suzuki Samurai iliyotengenezwa 1989 lilitumika kuwabuba baadhi ya watuhumiwa.

Akizungumza na Waandishi wa habari hapo jana kwenye ofisi za Wizara ya mambo ya ndani, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai Bw. Adadi Rajabu alisema kuwa gari lililotumika kubeba bomu, ni lenye rangi nyeupe na sehemu ya kuhifadhia mizigo ikiwa na rangi ya fedha.

Bw. Adadi alisema kuwa gari hilo limetengenezwa maarufu kwa kuhifadhi barafu au samaki wasiharibike ambapo gari lililotumiwa na watuhumiwa aina ya Suzuki, imeelezwa kuwa rangi yake ni nyeupe.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakutaja namba za magari hayo kwa madai kuwa uchunguzi zaidi unaendelea." Siwezi kutaja namba za magari hayo kwani uchunguzi zaidi unaendelea," alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha Mkurugenzi huyo wa Upelelezi amewataka wananchi walioyaona magari hayo siku ya tukio, kutoa taarifa zao kupitia kwenye kitengo cha Crime Stoppers'.

Kitengo hicho kinapokea habari za matukio mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuwahifadhi ili wasitambulike. Amewataka wananchi wapige simu namba 995 au kwa kupleleka taarifa moja kwa moja kwa Mkuu wa Upelezi wa Makosa ya jinai Mkoa wa Dar-es-salaam.

Bw. Adadi alisema kuwa siyo kwamba wapelelezi hawajui sehemu ambazo magari hayo yalipita bali wanachotaka kufahamu zaidi ni uhakika kutoka kwa wananchi.

Agosti 7 mwaka huu Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulilipuliwa na bomu hali iliyosabisha watu 11 kupoteza maisha yao na wengine 86 kujeruhiwa vibaya.

 

Wamnyonga mama yao kwa kunyimwa Urithi.

Na Jumbe Ismailly, (PST) Singida.

WAKAZI wawili wa kijiji cha Mtama B, wamekamatwa na Polisi Mkoani Singida kwa tuhuma za kumuua mama yao kwa kumnyonga kwa kutumia kaniki waliyomfunga kwenye matendegu ya kitanda baada ya kukataa kuwagawia ng'ombe za urithi.

Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi mkoani Singida Bw. Simon Dau amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Ibrahimu Iddy Makonde (31) na Fadhili Wawa (32).

Bw. Dau alisema marehemu Ali Asha Sungi (65) alikuwa akiishi peke yake baada ya muke wake kufariki 1980 na kwamba baada ya kifo cha mume wake Bi. Asha aliwachukua ng'ombe 20 ambao aliwauza na kujenga nyumba mjini Singida.

Aidha kamanda Dau alisema kuwa nyumba hiyo ya marehemu ambayo ilijengwa karibu na njia ya treni hivyo shirika la Reli nchini (TRC) waliivunja na kumlipa fedha ambazo zilimwezesha kujenga nyumba nyingine katika eneo la Mitunduruni mjini hapa.

Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Polisi mtoto wa Mke ndogo Ibrahimu Iddy Makonde naye alimuomba marehemu mama yake mkubwa amgawie ng'ombe kiasi ili naye aweze kutumia katika mahitaji yake mbali mbali lakini hata hivyo mtoto huyo hakupewa.

Amesema kabla ya tukio hilo mtoto mkubwa wa marehemu Bw. Mrunda Iddy aliamua kwenda kuangalia Video katika kijiji cha jirani ndipo watuhumiwa walipokwenda nyumbani kwa Bibi Asha na kumvamia na hatimaye kumuua.

 

Whitepaper haiwezi kuleta katiba inayotakiwa sasa-CUF

Na Said Mmanga,MSJ

WAKATI tume ya kuratibu maoni juu ya katiba ikiendelea na kazi yake vyama vya upinzani vimeendelea kuuponda waraka namba moja wa Serikali, "White paper " na kusema umeletwa kutokana na woga wa chama tawala cha CCM .

Aidha imedaiwa kwamba waraka huo hauwezi kamwe kutoa katiba inayotakiwa sasa.

Akiongea na gazeti hili ofisini kwake mwishoni mwa wiki naibu Mkurugenzi wa vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) Bw. Shaibu Akwilombe alisema kuwa waraka huo hauwezi kuleta katiba itakayokidhi mahitaji ya wananchi kwa kuwa haiwapi uhuru wa moja kwa moja wananchi juu ya maoni yao kuhusu katiba wanayoitaka.

Alisema wananchi wanatakiwa waipuuze white paper kwa kuwa haitakidhi madai ya katiba kwa kuwa serikali haifanyii kazi maoni ya wananchi bali ni ujanja wa ccm na serikali katika kuhakikisha inabaki madarakani milele.

Alisema wajumbe wote wa tume hiyo ni watumishi wa vyombo vya dola ambavyo vinatokana na katiba hivyo ni sawa na kuwaambia watoto wampige baba yao jambo ambalo alisema si rahisi kutekelezeka na kusisitiza kuwa lengo la waraka huo ni kuilinda serikali na chama tawala visiondoke madarakani.

Bw. Akwilombe alisema kuwa hoja ya msingi ni jinsi gani tutapata katiba ambayo itakuwa na maslahi kwa watu wote na sio ujanja unaofanywa na Serikali wa kuunda tume na kuratibu maoni ya wanachi ambayo alidai mara nyingi huwa hayafanyiwi kazi.

Akitolea mfano wa baadhi ya tume zilizoundwa na maoni ya wananchi kupuuzwa ni pamoja na tume ya jaji Mkuu Francis Nyalali ambayo ilipendekeza kufutwa kwa sheria 40 za ukandamizaji ambazo hadi leo hazijafutwa na wananchi asilimia themanini walitaka chama kimoja lakini serikali iliamua kuunda mfumo wa vyama vingi na kusema kuwa suluhu ya kupata katiba ambayo itagusa maslahi ya kila mmoja ni kuitisha mkutano wa katiba.

Aidha, alisema kuwa kuteuliwa kwa tume ya white paper ni kujihusisha na matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi wakati wakiwa wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ya kijamii .

" White paper ni utapeli kwani wewe nikikualika au nikikuomba ushauri ni lazima niufanyie kazi hivyo mwalikwa ni mwalikwa hawezi kuwa ndiye mwenye shughuli". Alisema Bw. Akwilombe na kuongeza kuwa mchezo unaofanywa na Serikali wa kuunda katiba kwa mtazamo wa chama ni hatari kwa kuwa kila chama kitakachoingia madarakani kitakuwa kinaandaa waraka wake hali ambayo itazidi kurudisha nyuma uchumi wa Taifa.

 

Ashikiliwa kwa kupoteza bastola yake

Na Joseph Sabinus

POLISI Mkoani Dar es Salaam wanamshikilia Bw. Mathew Paul Mbaruku kwa tuhuma za uzembe uliosababisha kuibiwa bastola.

Kamanda Gewe alisema jijini jana kuwa mnamo majira ya saa moja na dakika arobaini jana asubuhi Bw. Mbaruku alikwenda kumuangalia mgonjwa muhimbili ambapo aliiegesha gari ikiwa na mkoba wenye bastola ambapo wezi walivunja mlango na kuondoka na bastola hiyo.

Bw. Gewe alisema Bw. Mbaruku ambaye alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Pajero lenye namba za usajili TAS 937 si mkazi wa jijini na alikuwa amefikia mtaa wa Laibon uliopo maeneo ya Oysterbay,Jijini.

 

Afyekwa sikio kwa panga

Na Neema Dawson

JAFARI Shaweji 32, Mkazi wa Msongola wilayani Ilala amepandishwa kizimbani katika mahakama ya mwanzo Mbagala akikabiliwa na shtaka la kumjeruhi mwenzake kwa kumkata sikio na hatimaye kui ngia mitini.

Mapema ilidaiwa na msoma mashtaka konstebo Fabiana Mariseli alidai mbele ya hakimu Rehema Mohamedi kuwa Mnamo Septemba 22 mwaka huu majira ya saa 2.00 za asubuhi huko Msongola mshtakiwa huyo alimjeruhi Shabani Shamte kwa kumkata na panga katika sikio lake la kushoto na kumsababbishia maumivu makali sana mwilini mwake .

Hata hivyo mshtakiwa huyo baada ya kumjeruhi Shabani sikio lake pia alifanikiwa kumpiga magumi na mateke, kumpiga kwa kutumia rungu kwenye mgongo wake na kutumia panga hilo hilo kumkata katika mguu wake wa kulia hali ambayo ilimsababishia maumivu makali sana mwilini mwake.

Mshtakiwa huyo baada ya kusomewa shtaka hilo alikana kuhusika nalo na amedhaminiwa hadi hapo Oktoba 26 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena na hali ya mlalamikaji huyo inaendelea vizuri.

Katika tukio jingine ; Yusufu Abdalah 38, Mkazi wa Mtoni Kichangani amepandishwa kizimbani katika mahakama hiyo akikabiliwa na shtaka la kuharibu mali .

Mbele ya Hakimu Rehema Konstebo Fabian alidai kuwa Mnamo mwaka 98 ingawa tarehe na mwezi haukumbuki huko mtoni kwa Azizi Ally mshtakiwa huyo aliharibu Redio ya gari ambyo thamani yake ni sh. 50,000 mali ya Rashidi Ally .

Mshtakiwa huyo baada ya kusomewa shtaka hilo alikana kuhusika nalo na amedhaminiwa hadi hapo Oktoba 27 Mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

CCM wajibu mapigo ya NCCR

Na Dalphina Rubyema

WAKATI chama cha NCCR-Mageuzi Jimbo la Temeke kimejizatiti kunyakua viti vingi vya uwenyekiti wa serikali za mitaa na Madiwani katika uchaguzi utakaofanyika mwakani,Chama cha Mapinduzi Wilayani humo kimesema kuwa NCCR haina ubavu wa kupata ushindi huo na yenyewe CCM inauhakika wa kupata ushindi kwa asilimia 99.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi hivi karibuni kwenye ofisi yake,Katibu Mkuu wa wachama cha Mapinduzi Wilaya ya Temeke Bw.Josephat Bwai alisema kuwa ina uhakika wa kupata ushindi kwa vile sera zake zinaeleweka kwa watu na si kama NCCR inayotumia muda wake katika malumbano.

"Unajua sisi chama chetu kinatekeleza ilani zake kwa wananchi na siyo NCCR inayokalia malumbano ya wao kwa wao"alisema Bw.Bwai.

Katibu huyo aliendelea kusema kuwa NCCR imekuwa ikitumia muda wake mwingi kuikandamiza chama tawala yaani CCM kwamba chama tawala hakiwapi maendeleo yoyote wanachi na kujifanya wao wana NCCR wanajua kufanya kazi za maendeleo kitu ambacho amesema siyo cha ukweli.

Aliendelea kusema kuwa CCM imefanya kazi nyingi wilayani humo na inaendelea kufanya kazi nyingi za kimaendeleo na wala haitachoka kufanya hivyo kwa wanachi wake tofauti na Mwenyekiti wa NCCR Taifa na Mbunge wa Jimbo hilo Bw.Agustine Mrema ambaye tangu ashike madaraka ya ubunge hajawahi kufanya shughuli yoyote ya maana jimboni humo.

"Hapa Wanachi wenyewe watapima ni chama gani wakipe kura nyingi maana ukweli unajionyesha wenyewe ,wao wapime na kutoa uamzi wa haraka"alisema Bw.Bwai.

Hata hivyo Bw.Bwai alisema kuwa hadi hivi sasa hakuna taarifa rasmi iliyokwisha tolewa kutoka serikalini kwamba uchaguzi utafanyika lini hivyo anaona maajabu NCCR kuanza kutabiri ushindi.

 

Serikali 'inawatega' wananchi wake

Na Said Mmanga,MSJ

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema hatua ya Serikali kuruhusu mihadhara ya kidini ni mtego.

Chama hicho kimewataka waumini wasikubali hadi Serikali itakapotoa ufafanuzi wa kashfa za kidini vinginevyo watu wataendelea kupigwa risasi na vyombo vya dola.

Naibu Mkurugenzi wa vijana wa chama hicho Shaibu Akwilombe alisema jijini mwishoni mwa wiki kuwa Serikali imekuwa haina msimamo juu ya maamuzi yake na mara nyingi imekuwa ikifumbia macho matatizo na wanapopata malalamiko ndipo huanza kazi na wakati huo hutegemea wamepata malalamiko kutoka wapi kama watakuwa waislamu wamelalamika basi Wakristo wataathirika na wakristo wakilalamika waislamu wataathirika.

Alimtaka mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Luteni Yusufu Makamba kueleza kwa nini Serikali iliipiga mihadhara marufuku ambapo pia alimtaka azungumzie matatizo ya nyuma na kutoa ufafanuzi wake ili kujua ni nani alikuwa na makosa na kama serikali ilikuwa na makosa basi waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria.

Akwilombe alisema kama Serikali itashindwa kutoa ufafanuzi juu ya kashfa basi waumini wa dini zote wakae wakijihadhari na ruhusa hiyo kwani iko siku wanaweza wakajikuta wanakamatwa na vyombo vya dola na kusema jambo bora ni kuweka wazi juu ya mambo ambayo ni kashfa ili kila mmoja atekeleze wajibu wake wa kikatiba wa uhuru wa kuabudu.

Wakati huo huo chama hicho kimesema kuwa vitendo vilivyofanywa na serikali dhidi ya wananchi wa Kazimzumbwi ni matokeo ya mbegu mbaya zilizopandwa na wananchi mnamo mwaka 1995 wkati wa uchaguzi mkuu,na kuongeza kuwa viongozi wa sasa wa serikali ni watu waliochoka kufikiri hivyo hawajui namna ya kutatua matatizo ya wananchi na wanachojua ni kutumia nguvu.

 

Msichana akwapua fedha kujirudisha nyumbani

lKisa hawaelewani na tajiri wake

Na Said Mmanga, MSJ

MFANYAKAZI wa ndani Sikujua Shabani (14) mkazi wa Kimanzichana mkoani Pwani amefikishwa katika kituo cha polisi Magomeni akikabiliwa na tuhuma ya kumwibia mwajiri wake pesa taslimu shilingi 3500, upande wa kitenge na doti tatu za khanga.

Akisimulia mkasa huo dada wa mtuhumiwa Tatu Shabani alisema Sikujua ambaye alikuwa akifanya kazi za ndani jijini alirudi nyumbani kwao Kimanzichana na kuwaeleza kuwa ametoroka kwa sababu alikuwa haelewani na tajiri yake na aliwaeleza kuwa hakumuaga wakati alipokuwa akiondoka.

Alisema siku nne baadaye mwajiri wake alifika na kutaka kujua kama msaidizi huyo alikuwepo nyumbani.

Imedaiwa kwamba mara baada ya mtuhumiwa kumuona mwajiri wake ambaye hata hivyo hakuweza kulitaja jina lake alikimbia .

Tatu alisema kuwa baada ya kukimbia alimuomba mama huyo awe na subira hadi wakati wa jioni kwa kuwa ni lazima atarudi na ndipo waweze kuongea juu ya suala hilo, ambapo mama huyo alikubali kusubiri hadi jioni ambapo mtuhumiwa alirudi na alipoulizwa alikiri kuchukua pesa 3500 ambapo zilikuwa za kununulia maandazi na mboga pamoja na upande wa kitenge.

Kutokana na kutopatikana kwa muafaka baina ya mama huyo na Sikujua alimfikisha kituo cha polisi Magomeni ambako alilala hadi Jumatatu.

Hata hivyo msichana huyo alikubali kulipa gharama za vitu hivyo pamoja na usumbufu ambapo alitakiwa kulipa jumla ya shilingi 34000 ambapo ameahidi kuzilipa.

Naye Sikujua akisimulia kisanga hicho alisema ni kweli alichukua shilingi 3500 na upande wa kitenge lakini si kwa lengo la kuiba bali ni kwa ajili aweze kufika nyumbani kwao kutokana na madai ya kutoelewana na mwajiri wake