HEADLINES

CUF, CCM wapigana vijembe Dar

ATHARI ZA EL NINO ZIKIWA BADO KUSHUGHULIKIWA Jiji halijui litakapopata milioni 600/-

Amuua mama yake kwa kumkatisha kipindi cha televisheni

Ashikwa na kupata kibano baada ya kuiba viatu mskitini

Jiji yafunga Kumbi tano za starehe

SMZ kubadili Katiba

Bomba la Songosongo kuanza kuwekwa Desemba

CUF, CCM wapigana vijembe Dar

Na Said Mmanga

 

VYAMA vya siasa vimetofautiana juu ya sababu za kushuka kwa uchumi hapa nchini.

Wakati CCM inadai kumesababishwa na wafanyakazi wote, Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hali hiyo imesababishwa na sera mbovu za serikali na chama tawala.

Wakichangia mada kwa nyakati tofauti katika kongamano la madai arobaini ya sheria za wafanyakazi ,lililoandaliwa na shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (T.F.T.U) linalofanyika katika ukumbi la Karimjee jijini,Mbunge wa viti maalum(CCM), Dk.Zainabu Gama alisema uchumi unashushwa au kupandishwa na wafanyakazi wa ngazi zote.

Alisema wafanyakazi kuanzia ngazi ya wafagiaji hadi mawaziri wamehusika katika kushuka kwa uchumi kwa kuishauri vibaya serikali na kuongeza kuwa muda mwingi wanakuwa hawafanyi kazi na kujishughulisha na mambo yao.

DK.Gama pia alisema sheria zilizopitwa na wakati zionyeshwe wazi ambapo wafanyakazi wailazimishe serikali juu ya malipo ya pensheni yaendane na cheo cha mfanyakazi na yabadilike kulingana na wakati uliopo.

Naye katibu mkuu wa CUF Bw.Shaban Khamis Mloo alipinga sababu zilizotolewa na Dk.Gama na kusema kuwa kushuka kwa uchumi wa Taifa kumesababishwa na sera mbovu za serikali ambazo pia zimewadumaza wananchi.

Amesema kutokana na sera hizo za serikali zimesababisha wafanyakazi kuwa ombaomba na kuongeza kuwa serikali haiwezi kusikiliza madai ya wafanyakazi kwakuwa haina ziada.

Akichangia mada juu ya madai arobaini ya Wafanyakazi iliyoanzishwa na Katibu wa RAAWU Bw.Nestory Ngula, Mbunge wa Kisesa (UDP), Bw.Erasto Tumbo alisema kilio cha wafanyakazi hakitaisha kama wafanyakazi wenyewe hawatachukuwa hatua madhubuti kupambana na serikali.

Alisema miongoni mwa hatua ambazo wanaweza kuzichukuwa ni kugoma ili kuibana serikali itekeleze madai ya sheria za wafanyakazi ambapo alisema kwa kuwa vyama vingi vya wafanyakazi vina woga na hawataki kugoma basi madai yao hayatafaulu.

Kongamano hilo linalowashirikisha watu mbalimbali wakiwemo Wabunge na viongozi wa vyama vya siasa lilianza juzi na litamalizika leo.

 

ATHARI ZA EL NINO ZIKIWA BADO KUSHUGHULIKIWAJIJI halijui litakapopata milioni 600/-

Na Dalphina Rubyema

 

TUME ya Jiji imesema haijui itapata wapi jumla ya shilingi milioni zaidi ya 600 zinazohitajika kwa ajili ya kukarabati maeneo yaliyoathirika na mafurikio.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hivi karibuni kwenye ofisi za Tume ya Jiji,Afisa mmoja wa ngazi ya juu Tume ya Jiji ambaye hakuta jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa ukarabati huo ungekuwa umeshaanza kitaambo lakini hadi hivi sasa kinachokwamisha zoezi hilo ni pesa.

Alisema kwamba tume ina shughuli nyingi zinazohitaji fedha na kwa sasa ni vigumu kuelewa hali itakavyokuwa hapo baadaye.

"Unajua Tume ina kazi nyingi sana na hizi kazi zinahitaji pesa hivyo inabidi tuzifanye kwa utaratibu maalum na siyo wananchi wafikirie kwamba tumeshindwa kutekeleza kazi ya ukarabati wa maeneo yaliyoathirika na mafuriko"alisema Afisa huyo bila kufafanua zaidi utaratibu unaofanywa na Tume hiyo.

Hata hivyo Afisa huyo alisema kuwa baadhi ya watu ambao kwa namna moja au nyingine walichangia uharibifu huo itabidi hata wao wachangie katika ukarabati huo.

Alitoa mfano wa wakazi waliochangia uharibifu huo kuwa ni wakazi wa Keko Magurumbasi ambao baadhi yao walijenga nyumba zao juu ya bomba la kupitisha maji machafu yanayotoka viwandani hivyo pamoja na mafuriko hata wao walichangia kumeguka kwa bomba hilo hivyo watachangia kiasi fulani cha fedha na kiasi hicho kitatajwa baadaye.

Maeneo kadhaa hapa jijini yakiharibika kutokana na mvua kubwa za el-nino zilizokuwa zikinyesha tangu Februari hadi Aprili mwaka huu ambapo Makamu wa Rais DK.Omary Alli Juma alipoya-tembelea maeneo hayo aliahidi kuwa shughuli za ukarabati zingeanza mara moja mara baada ya mvua hizo kuacha kunyesha kitu ambacho hadi hivi sasa hakuna hatua yoyote iliyokwisha chukuliwa.

Maeneo yaliyoathirika zaidi ni Tabata Relini, Magomeni, Mwananyamala, Kigogo, Jangwani pamoja na Keko Magurumbasi eneo la Mselelekoni.

 

Amuua mama yake kwa kumkatisha kipindi cha televisheni

HELSINKI, Finland

MWANAMUME mmoja mwenye umri wa miaka 42 amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumuua mama yake bila kukusudia baada ya mama huyo kumkatisha matangazo ya televisheni yaliyokuwa yakionyesha mashindano ya mbio za magari za Formula One.

Gazeti Iltalehti limesema kwamba mtu huyo alimuua mama yake katika ugomvi baada ya mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 68 kuingia katika chumba cha televisheni na kuizima wakati maonyesho ya moja kwa moja ya michuano hiyo bado inaendelea.

Tukio hilo limetokea Agosti mwaka huu katika michuano ya GrandPrix ambapo dereva kutoka Finland Mika Hakkinen alishinda michuano hiyo na kujiweka katika hali nzuri ya kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na michuano hiyo.

Inadaiwa baada ya mama huyo kuzima televisheni hiyo kulitokea kujibizana vikali kwa maneno na mwanaye huyo ambaye ni mpenzi mkubwa wa michuano hiyo inayoangaliwa na wananchi wengi wa Finland.

Majibizano hayo yalifuatiwa na vurumai kubwa ambapo mwanamume huyo alimniga mama yake na kusababisha umauti uliomkuta

 

 

Ashikwa na kupata kibano baada ya kuiba viatu mskitini

Na Said Mmanga, MSJ

KIJANA mmoja wa kiume ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja wiki hii alipata mkong'oto mkali kutoka kwa waumini wa dini ya kiislamu baada ya kutuhumiwa kuiba viatu Msikitini.

Tukio hilo lilitokea Jumatatu iliyopita Novemba 28 katika Msikiti wa Ngazija uliopo katika mtaa wa India Jijini, majira ya saa saba mchana wakati waumini hao walipokuwa katika swala ya adhuhuri ambapo wakati waumini wengine walipokuwa wakiendelea na swala yeye aliinuka na kwenda kuchukua viatu ili aondoke navyo na ndipo mwenyewe alipomuona na kuamua kukatisha swala na kumkamata.

Kijana huyo alipoulizwa anavipeleka wapi viatu hivyo aina ya raba alisema ni vya kwake na ndipo waumini wengine walipoyasikia majibizano hayo na ndipo walipotaka kujua kuna nini ambapo mwenye viatu alisema yule kijana ni mwizi na alikuwa anataka kuiba viatu hivyo na mtuhumiwa akisema ni vya kwake hali ambayo iliwafanya waumini wamuulize kila mmoja kama ni vya kwake vina alama gani.

Mmliki wa viatu hivyo ambaye naye jina lake halikupatikana mara moja alisema ndani ya viatu hivyo kuna soksi za njano zenye mstari wa bluu wakati mtuhumiwa alionekana kubabaika ambapo awali alisema kuna soksi zenye rangi ya pundamilia ambapo baadaye alibadilisha na kusema zipo soksi za bluu zenye madoamadoa ambapo zilipokuja kutolewa zilionekana ni soksi za njano zenye mstari wa bluu na ndipo waumini hao walipompa kipigo kabla ya kuokolewa na waumini wengine ambao walimrudisha msikitini ili kumnusuru na kipigo kutoka kwa waumini hao pamoja na wapita njia.

Wakati watu wenye hasira walikuwa wakivutana wao kwa wao ambapo kuna ambao walitaka atolewe nje ili waendelee kumsulubu kwa madai kuwa wamezoea kuiba viatu msikitini baadhi ya waumini waliokuwepo msikitini hapo walisema kuwa kijana huyo apigwe picha ili zisambazwe katika misikiti yote ya jijini ili ajulikane ambapo wengine walikuwa wakipinga wakidai hatua hiyo haitoshi dawa ni kumpiga kwa kuwa vitendo vya wizi wa viatua vimekithiri katika misikiti mbalimbali jijini.

Hadi mwandishi wa habari hizi alipoondoka eneo la tukio aliacha bado kijana huyo akiwa mikononi mwa waumini hao wakiendelea kumsaili zaidi.

 

Jiji yafunga Kumbi tano za starehe

Na Said Mmanga,MSJ

 

TUME ya jiji la Dar es salaam imezifungia kumbi tano za starehe Wilayani Temeke kuendesha shughuli za burudani kutokana na kukiuka masharti ya leseni zao pamoja na kupiga muziki kwa sauti ya juu hadi usiku wa manane.

Kwa mujibu wa barua ya tume hiyo iliyosainiwana afisa utamaduni wa Wilaya ya Temeke Nestory Wisandarakwa niaba ya mkurugenzi wa kanda kwenda kwa wamiliki wa kumbi hizo ambayo nakala yake imepelekwa kwa mkuu wa Wilaya hiyo na kwa mkurugenzi wa tume ya jiji kanda pamoja na mkuu wa polisi wilayani humo, kumbi hizo zimefungiwa kutokana na kupiga muziki kwa sauti ya juu hadi usiku wa manane na wakati mwingine kupiga muziki hadi asubuhi jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za vibali vinavyotolewa kwa ajili ya burudani.

Kumbi ambazo zimefungiwa kwa mujibu wa barua hiyo yenye kumbukumbu namba DCC/UT/WT/SM/VOL.V/1/165 ya Septemba 28 mwaka huu imezitaja kumbi hizo kuwa ni Sigara social and Sports Club,Kikolo Inn bar,Kivulini bar,Lambada bar and Guest house na Ngomano night park zote za wilayani humo.

Sababu nyingine ambayo imeelezwa na tume hiyo ya kuzifungia kumbi hizo ni kwamba kutokana na kupiga muziki hadi nyakati za usiku wa manane na wakati mwingine asubuhi zimekuwa zikosesha amani na utulivuna kuwapa kero na usumbufu mkubwa wananchi wanaoishi karibu na baa hizo.

"Kwa kukosesha amani na utulivu na kuwapa kero jirani zako hivyo nina kuamuru kuanzia tarehe ya barua hii usimamishe kabisa na iwe marufuku kupiga muziki wowote ule uwe wa dansi au disko katika ukumbi wako". Inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Akifafanua zaidi Wisandara alisema kuwa wamepata malalamiko kutoka kwa wananchi wa maeneo na baada ya kuyafanyia kazi wamechukua hatua ya kuzifungia kumbi hizo ambapo alisema ni makosa kupiga muziki hadi usiku wa manane kwani kufanya hivyo ni kuwaathiri watu wengine .

Alisema katika siku za kawaida vibali vya kupiga muziki au disko hutoa ruhusa ya kufanya hivyo mwisho saa tano wakati siku za mwisho wa wiki mwisho ni saa sita na kupiga muziki kinyume cha muda huo ni kukiuka masharti ya leseni walizopewa

 

SMZ kubadili Katiba

Na Mwandishi wetu

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema katiba ya zanzibar itafanyiwa marekebisho ili liende sambamba na wakati huu .

Hayo yameelezwa na waziri wa sheria na katiba Iddi Pandu Hassan alipokuwa akizungumza na wananchi wa habari hizi

Bw. Pandu amesema kwamba pamoja na kuwa katiba hiyo imeshafanyiwa marekebisho nmara kadha bado kunahitajika maeneo kupitiwa upya kwa madai kwamba katiba sio msaafu.

Waziri Pandu ameyataka maeneo ambayo yatahitajika kufaniwa marekebisho kuwa ni pamoja na muundo wa baraza la wawakilishi,mamlaka ya rais na vyombo vya sheria,pamoja na mambo mengine,

Hata hivyo Waziri Pandu hakueleza mfumo utakaosaidia kufanikisha mabadiliko hayo lakini alisema serikali itatoa utaratibu muda muafaka utakapofika.

Aidha kwa kuwa katiba ya jamhuri ya muungano itafanyiwa mabadiliko nayo katiba ya Zanzibar haina budi kubadili ili iende sambamba na wakati ulioopo.

Akizungumzia Tume ya Uchaguzi Zanzibar kufanyiwa marekebisho alisema jambo hilo litategemea maoni ya wananchi kupitia waraka wa serikali white paper.

Hata hivyo akizungumzia suala la wapinzani kuhusishwa na tume ya uchaguzi alisema haoni sababu ya wapinzani kuwemo katika tume za uchaguzi kwa kile alichodai kukaribisha mizozo kwa sababu kila atakeyehusisha atatetea msimamo wa sera za chama chake.

Amesema ni vyema katika tume hiyo wawepo watu wasioshabikia upande wowote badala ya kuwashirikisha viongozi wenye misimamo mikali ya siasa.

 

 

Bomba la Songosongo kuanza kuwekwa Desemba

Na Dalphina Rubyema

 

UCHIMBAJI na uwekaji wa bomba la kupitisha gesi katika Mradi wa Songo Songo utaanza mapema mwaka kesho au mwishoni mwa Mwaka huu (Desemba).

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Afisa wa Kanda katika Mradi huo Bibi Eva Mwingizi wakati alipokuwa akizungumza na Mwandishi wa habari hizi ofisini kwake hivi karibuni.

Bibi Mwingizi alisema kuwa kilichokuwa kinakwamisha uchimbaji na uwekaji wa bomba kuchelewa ni kulipa fidia kwa watu watakaothirika na zoezi hilo ambapo alisema Novemba mwaka jana walitoa fidia kiasi cha shilingi Bilioni 2.6 kwa watu 2,600 na hii ni asilimia 92 ya watu waliolipwa fidia hiyo.

Aliendelea kusema kuwa walikuwa na nia ya kwalipa watu wote lakini hiyo asilimia tano ya watu waliobaki hawakuweza kulipwa kutokana na migogoro waliyokuwa nayo zaidi ni ya kifamilia ambapo walikuwa wanaandaa utaratibu wa mirathi pamoja na watu wengine waliokuwa na migogoro ya mipaka na wale ambao wakuwa mbali na maeneo hayo.

Hata hivyo Bibi Mwingizi alisema kuwa utaratibu umeisha kamilika ambapo alisema asilimia hiyo nane iliyobaki nao wameanza kupewa fidia yao ambapo zoezi la pli la kutoa fidia lilianza tangu Septemba 30 mwaka huu.

Alisema TANESCO na Kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill watakuwa wanapata umeme moja kwa moja kutoka Songas ambacho ndiyo kituo kikuu cha gesi hiyo ambapo watumiaji wengine watakuwa wanapata umeme kupitia katika Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TCPL).