KAULI YETU

Ufanisi unahitaji moyo wa kujituma

KUNA hali au mambo kadhaa ambayo huhitajika mtu anapoamua kuchagua kazi yake ya kufanya katika maisha.

KWANZA kabisa karibu kila kazi huhitaji elimu ya namna fulani. Elimu hiyo huweza kupatikana shuleni kwa kukaa darasani na kumsikiliza mtaalamu au mwalimu katika fani hiyo.

NI jambo baya sana mtu kufanya kazi ambayo hana elimu juu yake. Hatuwezi kutegemea kupata ufanisi wowote ikiwa mtu asiye na elimu akikabidhiwa kazi ambayo hakusomea.

NDIYO sababu watu wanakwenda shuleni kusoma, wanaenda kwenye kozi kujifunza na hata wanahudhuria mikutano na makongamano mbali mbali ili mradi wanajikamilisha vizuri kielimu

LICHA ya mtu kuwa na elimu katika fani fulani inatakiwa pia kuwa na wito katika fani hiyo.

KWA mfano mtu anaweza akasomea vizuri fani ya uganga. Anaweza akafahamu njia na mbinu zote za matibabu ya magonjwa mbali mbali, lakini kama atakosa ule msukumo wa ndani wa kufanya kazi yake hiyo itakuwa haileti ufanisi wowote ule. Kumbe licha ya mtu kuwa na elimu katika fani yoyote ile huhitaji ule msukumo wa ndani yaani moyo wa kujituma.

MOYO huo wa kujituma na ile hali ya kufanya kazi kwa hiari bila kujali muda. Jambo analolizingatia ni ule ufanisi wa kazi yake. Pengine hata mshahara huwekwa mahala pa pili. Mahali pa kwani ni kuangalia zaidi ufanisi wa hiyo kazi. Kwa lugha ya kiingereza tunasema mtu anaangalia "job satisfaction". Hapo mtu anapenda kuona na kuridhika juu ya kazi yake aliyoifanya.

KUNA manung'uniko mengi katika jamii yetu na hata kwa watendaji wasomi kwa kuwa wengi wao wanafanya kazi bila ule moyo wa kujituma au msukumo wa ndani.

HALI hiyo inajionyesha kwa namna mbali mbali.

KWA wale wanaofanya kazi maofisini, kunakuwa na ile tabia ya kutokutulia na kufanya kazi hadi mwisho na kuikamilisha ile kazi inayotakiwa kufanya.

TUNASHUHUDIA pia kwa wale mafundi mbali mbali wanapotengeneza kitu kwa kulipua lipua. Hawaangalii kama mtumiaji atafaidika namna gani na kwa kiasi gani.

MOYO wa kujituma na kufanya kazi wa kumridhisha mtendaji na wale anaowafanyia hiyo kazi ni jambo la msingi. tunasema huo ndio ustaarabu. Hicho ni kitu kinachokosekana kabisa katika jamii yetu kwa wengi. Madereva wanaopeleka tu magari bila uangalifu hukosa ule msukumo wa ndani katika kazi yao.

MTU anapoamua kufanya kazi vizuri kwa kumwongopa askari au sheria hapo hukosa ule msukumo wa ndani na ule moyo wa kujituma. Kazi inayofanyika katika hali ya woga haileti mafanikio mazuri.

MARA kwa mara watu wanafanya kazi ili mradi ni kazi na kumbe siyo wito wao. Katika kufanya kazi ambayo mtu siyo wito wake tunajikuta tuna malalamiko mengi sana na hata utendaji mbaya.

TUNATOA rai kwanza kwa wazazi na walezi. Imewapasa kutambua miito ya kazi kwa watoto wao. Wazazi na malezi wawaandae watoto wao kulingana na miito yao pia msukumo yao ya ndani.

HAITAKIWI kijana aseme kuwa amechagua kazi fulani kwa sababu mzazi wake alitaka aifanya kazi hiyo. Yeye mwenyewe hakuipenda bali alifanya kulazimishwa tu.

TUNAWAPONGEZA wale watoto ambao wansema wazi kuhusu mito yao ya kazi katika maisha yao ya baadaye.

MARA nyingi ikiwa watoto wamelazimishwa kuchukua kazi fulani mapato yake huwa au kuiacha kazi hiyo, au kutofanya kazi hiyo kwa moyo.

TUSISAHAU yale maneno ya Hekima ya Mwalimu J. Nyerere kuwa "Taifa litajengwa na wenye moyo wa kujituma".Tunahitaji vijana walioandaliwa vizuri katika fani mbali mbali kulingana na miito yao.

HATA kama kuna upungufu wa ajira tujitahidi sana kukwepa kuwasukumiza vijana wetu kwenye fani ambazo siyo wito wao. Mapato yake kama tulivyosema hapo awali ni ule utendaji mbovu wenye kuleta hasara kwa taifa na hata kwa mtu mwenyewe binafsi

 

BARUA ZA WASOMAJI

Katibu mtedaji kata huyu ni hatari

Mheshimiwa Mhariri

NAPENDA kutoa masikitiko na malalamiko yangu kwa kile nilichokiona jinsi wananchi wanavyoteswa, kupigwa, kudhulumiwa na hata kuswekwa rumande na baadhi ya viongozi wetu bila sababu eti kwa vile kiongozi kaamua hivyo.

Mwanzoni mwa mwezi huu nilikuwa kijijini nilijionea mwenye jinsi wanakijiji wanavyoonewa na kiongozi wao katibu Mtendaji kata jina tunalihifadhi. Kijana mmoja aliagizwa kununua chupa 3 za kinywaji (beer), baada ya kupewa chupa hizo alitokea kiongozi huyo na kuanza kudai kuwa asitoke bila kumpa Katibu chupa moja.

"Kijana alimfahamisha kuwa beer hizo ameagizwa kwa ajili ya wageni" alisema kijana huyo.

Katibu aliendelea kudai kuwa, "hujui kuwa mimi ndiye mtendaji? Hakuna zaidi yangu hapa kijijini" alisema katibu. Katika kubishana watu walianza kutoka kila kona na kumzomea. Gafla Katibu kata alianza kumshambulia hadi kumchania nguo zake, kijana alizidiwa nguvu kutokana na msaada alioupata Katibu Kata kutoka kwa sungusungu wake wawili.

Baada ya kuona kijana anaelemewa zaidi watu waliingilia kati kuwaamua vinginevyo angeuawa. Kijana alishauriwa kwenda polisi, katibu aliposikia hayo alitamba akisema "hata ukienda polisi hawawezi kunifanya kitu" alisema.

Kiajan alipeleka malalamiko yake polisi Kemondo lakini alijibiwa kuwa mtu huyo amewashinda na kusema wanachoweza kumsaidia ni kumpa barua aende polisi Bukoba mjini. Alienda polisi Bukoba na kesho yake niliondoka kijijini nikaacha kesi inaendelea.

Kilichoniuma na ninachoona kwa katibu kata kama kiongozi wa Serikali badala ya kuwatunza na kuwasaidia raia wake anatumia chio chake kuwagandamiza, kuwanyanyasa, kuwanyamg'anya kwa nguvu haki zao.

Serikali inatuelimisha kwamba tuwe wazi na wakweli na tutume sheria, sasa ina kuwa kinyume kwa viongozi wenyewe, haki inakuwa dhuluma, mabavu na unyanyasaji.

Ninabaki katika kujiuliza je viongozi wa ngazi za chini wamepewa msimamo huo ama ni tabia ya mtu mwenyewe. Ikiwa ni tabia ya mtu kwa nini watu wa namna hiyo wanapewa uongozi? Tuelimishe kwamba, ili tuendelee tunahitaji mabo manne (4)

Siasa safi, Uongozi bora, Watu na Ardhi. Sasa siasa vijijini imekuw chungu, uongozi umekuwa wa mabavu, watu wanaongozwa kwa kuburuzwa na ardhi sijui takuwaje?

Ninawaomba viongozi wahusikana nidhamu ya watumishi wa serikali na waajiri wa watumishi Serikalini watupie macho suala hili ili haki itendeke vijijini. Msipo ziba ufa mtagharimu gharama kubwa kujenga ukuta.

Ni mimi mwenye jicho lililopata kuona hayo, sikio lililopata kusikia na moyo uliopata uchungu kwa jinsi wananchi wanavyoteseka vijijini.

Damas Bugwainwe,

SLP 9174,

Dar es salaam

 

 

Misafara ya White paper ni kufuja fedha za walipa kodi

Mheshimiwa Mhariri ,

Naomba unipe nafasi katika gazeti lako tukufu ili niweze kutoa yale ambayo yamekuwa yakinisumbua katika kichwa changu yanayofanywa na viongozi wa Serikali.

Kwa nia njema kabisa Serikali kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipitisha waraka wa Serikali namba moja ambao unajulikana kama "White paper", lengo lake kuu likiwa ni kuwapa nafasi watanzania kutoa maoni yao juu ya Katiba ya nchi ni nini wanakitaka na kitu gani hawakitaki.

Lakini tangu kutolewa waraka huo nimekuwa nikikerwa na tabia ya viongozi wa serikali ambao wao ndiyo waliotoa Waraka huo kupita katika mikoa mbalimbali kwa madai eti ya kuhamasisha wananchi kutoa maoni yao katika tume iliyoundwa na seriali kuratibu maoni kuhusu katiba ya nchi.

Kinachonikera ni kwamba kwa nini wao wapite mikoani na kutumia pesa za wavuja jasho kudai eti wanatuhamasisha tutoe maoni katika kamati iliyoundwa na serikali kwa sababu sisi sio wajinga ambao hatujui linaloendelea kwani kwa kinachoonekana ni kwamba Serikali ina ajenda katika jambo hilo kwani ni lazima wao watuhimize sisi ?.

Kwa kuwa Wananchi tunajua umuhimu wa Katiba hatutaki viongozi wa Serikali watupitie kwa madai wanatuhimiza ikumbukwe kuwa ni rahisi kumlazimisha Ng'ombe kwenda Bwawani lakini si rahisi kumlazimisha kunywa maji kwa hiyo kama waraka umekwisha toka hakuna haja ya Mawaziri kuzunguka mikoani na kutumia fedha za wavuja jasho huku sisi wenyewe tunaolipishwa fedha hizo tukiwa tunakabiliwa na matatizo mbalimbali kama watoto wetu kukaa chini, Hospitali hazina dawa na mambo mengine na hivyo ni bora wakae chini wafanye kazi zao na waache kabisa kutufanyia kiini macho cha kutumia fedha zetu.

Kitu ambacho mimi nimekiona katika ziara za mawaziri hao kuhamasisha White Paper ni kukipigia debe chama tawala cha CCM na pia inaonekana wazi waraka huu wa Serikali ni kiini Macho na kuna ajenda ambayo imekwisha andaliwa .

Wasalamu

Mwananchi Mkereketwa

Dar es salaam