HEADLINES

 

Papa asifu uenezaji wa ujumbe wa Biblia kupitia redio

Wakatoliki watakiwa kushikamana na watu maskini

Sikukuu ya mavuno kufanyika Novemba 21

Askofu sendoro ahimiza uwekaji kumbukumbu

Mafundisho ya Dini yaimarishwe

Mkutano wa UEM kufunguliwa kesho

Kanisa Lasifiwa Mkoani Mara

Maelfu wamzika Askofu Mustaafu Jimbo Kuu Mwanza 8.10.98

Matanda V.T.C. wafanya Mahafali

Paroko wa Upanga atimiza miaka 50 ya utawa

 

 

Papa asifu uenezaji wa ujumbe wa Biblia kupitia redio

PAPA Yohane Paulo wa Pili amesifu juhudi zinazofanywa za kueneza ujumbe wa Biblia kupitia vyombo vya habari.

Baba Mtakatifu alitoa sifa hizo alipokutana na washiriki wa kongamano la kimataifa lililokuwa likijadili mada ya 'Lugha ya Kibiblia na Mawasiliano ya kisasa'.

Kongamano hilo liliandaliwa na Kampuni ya Lux Vide na walikaribishwa kuonana na Baba Mtakatifu kwenye makao yake Castelgandolfo.

Baba Mtakatifu alielezea kuridhishwa kwake na juhudi zinazofanywa na kampuni hiyo kuueneza ujumbe wa Biblia kwa watu wote kupitia vyombo vya habari vyenye nguvu hasa sinema na televisheni.

"Muunganisho wa Ufunuo wa Kimungu na vyombo vya habari vya kisasa," alisema Baba Mtakatifu, "unapohitimishwa kwa kuheshimu ukweli wa Biblia na kutumiwa vizuri na teknolojia, inaleta matunda bora."

Aidha alisema hali hiyo inavifanya vyombo vya habari viwe huru zaidi na kuleta uwezekano wa kuleta neno la Mungu karibu zaidi na watu.

Pongezi hizo zilitolewa na Baba Mtakatifu kutokana na nia iliyoonyeshwa na sinema kuonyesha habari za agano la kale na jipya.

"Ninatumaini kuwa huduma yenu ya kueneza ujumbe wa Biblia itaendelea kwa nguvu mpya kwa nia ya kuzalisha kazi itakayoweza kuunganisha uisanii na ufunuo was kidini ili kuamsha ndani ya watazamaji hisia nzuri na kuwashirikisha kikamilifu na kuwawezesha kukua kiroho," alimalizia Baba Mtakatifu.

 

Wakatoliki watakiwa kushikamana na watu maskini

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amewataka waumini wa Kanisa Katoliki kuwa na mshikamano na idadi kubwa ya watu maskini ulimwenguni.

Rai hiyo aliitoa wakati wa sala ya Malaika wa Bwana kwenye makazi yake ya mapumziko ya Castelgandolfo ikiwa ni seheme ya maadhimisho ya siku ya Mt. Vincent wa Paulo aliye msimamizi wa vyama vya misaada.

Aliwakumbusha waumini juu ya ukweli kwamba changamoto kubwa lililo mbele yetu ni tofauti kubwa kati ya wale wanaofaidi hali bora ya uchumi na maendeleo ya kisayansi na wanaoishi katika hali mbaya.

Aliongeza kusema kuwa ukichukulia tofauti iliyopo kati ya matajiri na maskini, Mungu yuko upande wa Maskini wasio na chochote.

Alisema kuwa haitakuwa haki kuwa watazamaji na washuhudiaji wa ulimwengu ambao bado kuna watu wanaokufa kwa njaa, wasio na makazi, wanaokosa hata haki ya msingi ya elimu, wasiokuwa na msaada wowote wanapokuwa wagonjwa na wasio na kazi.

Aidha alisema kuwa ni jambo la muhimu kuinua mshikamano wa kitamaduni na kisiasa na hasa kuangalia kwa makini ugumu wa matatizo, kwani kujitoa kwa mtu b9inafsi hakutoshi kumaliza hali hiyo.

"Kwa matatizo kadhaa, kama vile madeni nya kimataifa ya nchi maskini, kuna haja ya kupata jibu kutoka upande wa jumuiya ya kimataifa.

Baada ya sala hiyo Papa Yohane Paulo wa Pili alikutana na wanajeshi wa kikosi cha 31 cha jeshi la anga la Italia, ambao aliwashukuru kwa kujitoa kwao kumsaidia katika safari zake za anga anapokuwa anasafiri nchini Italia.

Aliwakabidhi pia tuzo kama ishara ya shukrani zake kwa wanajeshi hao.

 

 

Sikukuu ya mavuno kufanyika Novemba 21

Na Justin Mwereke

MAADHIMISHO ya pili ya siku ya Mavuno Jimboni Dar es Salaam yatafanyika Novemba 21 mwaka huu, imeelezwa jijini mwishoni mwa wiki.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kamati y maandalizi zimesema maandalizi yanaendelea vizuri na kuna matumaini ya kupapta mafanikio makubwa zaidi ya mwaka jana kutokana na parokia zote kupata taarifa mapema zaidi kuweza kuandaa waamini wao.

Habari hizo zilisema maadhimisho hayo yatafanyika katika kituo cha Maendeleo cha Msimbazi (Msimbazi Centre) kama mwaka jana na yataongozwa na Ibada ya Misa itakayosomwa na Mhashamu Askofu Mku wa Jimbo Polycarp Kadinali Pengo.

Siku ya mavuno ilibuniwa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo mwaka jana katika jitihada za kutafuta njia za kuliwezesha jimbo liweze kujitegemea kwa hali na mali badala ya kutegemea zaidi misaada kutoka kwa wafadhili au wahisani wa nje ambao tayari wameshaionyesha kuchoka.

Katika maadhimisho ya siku ya mavuno mbaka jana yaliyofanyika Novemba 29, zilipatikana zaidi ya shs. milioni 22.4 kutokana na michango ya fedha taslimu na vitu vya parokia zipatazo 24au waamini binafsi wa parokia hizo.

Ofisi ya jimbo kuu la Dar es Salaam imesema ilipokea shs. 22,427,295 ikiwa ni mapato halisi baada ya kutoa matumzi yote ya maandalizi.

Vitu mbali mbali ikiwa ni pamoja na vyakula, mifugo na vifaa vya kazi za mikono vilichangwa na waamin waliofurika kwenye uwanja wa Msimbazi Centre ambavyo baadaye siku hiyo hiyo vilinadiwa.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana kutoka ofisi kuu ya jimbo, Parokia ya St. Joseph iliongoza kwa kutoa mchango mkubwa zaidi wa shs. 2,180,100 ikifuatia Parokia ya St.Peter iliyotoa shs. 1,750,450. Nafasi ya tatu ilishikwa na Parokia ya Upanga kwa mchango wa shs. 1,578,050.

Parokia nyingine zilizoko katika 'Kumi bora' ni Msimbazi (shs. 1,331,100), Mburahati (shs. 1,055,320), Chang'ombe (shs. 1,041,600), Kurasni (shs. 914,300), Ubungo (shs. 881,100), Magomeni (shs. 839,450), na Manzese (shs. 798,200).Sista Ruth wa ofisi kuu ya jimbo alisema alifurahishwa sana na mahudhuri mazuri ya waamini mwaka jana na anatarajia mwaka huu yatakuwa mazuri zaidi na kutoa mchangomkubwa zaidi

 

Askofu sendoro ahimiza uwekaji kumbukumbu

Na Mwandishi Wetu

ASKOFU mkuu wa Kanisa la kiijili la kilutheri Tanzania,(KKKT) Elinaza Sendoro ameyataka makanisa kutunza kumbukumbu ya historia ya kanisa kwa vile makanisa mengine yanashindwa kuweka kumbukumbu zao.

Askofu Sendoro aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa kuweka jiwe la msingi katika kanisa jipya linalojengwa na wananchi huko Tabata Kimanga, Jijini.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa DK.Kakule Moro ambaye ni naibu mkurugenzi wa mission ya pamoja (UEM), ambao ni muungano wa makanisa 32 yakiwemo 14 ya Bara la Asia, 12 Afrika na makanisa saba ya Ulaya na Ujerumani.

Akitoa risala yake mgeni rasmi aliwaomba wazee wa kanisa kushirikiana na mchungaji aliyekabidhiwa Kanisa hilo na aliwaasa waumini kuacha maovu kwani siku za mwisho zimekaribia.

Naye askofu Sendoro aliwapongeza washirika wa Kimanga kwa kujenga kanisa hilo bila kupata msaada wowote .

"Hapo zamani waumini walikuwa hawajengi kanisa hadi wapate msaada ". Alisema askofu Sendoro.

Sherehe za uzinduzi wa kanisa hilo jipya zilianza kwa maandamano ambayo yalianzia shule ya msingi Kimanga ambako walikuwa wanasalia kabla hawajajenga kanisa hilo jipya ambalo lilikuwa linazinduliwa na kumalizikia katika kanisa hilo.

 

Mafundisho ya Dini yaimarishwe

Na Lazaro Blassius

SERIKALI imeombwa kushirikiana na madhehebu ya dini kuimarisha mafundisho ya dini mashuleni ili kuliokoa taifa na mmomonyoko wa maadili unaoendelea nchini licha ya Serikali kutunga sheria kali kwa makosa yatokanayo na kukosa maadili mema.

Wito huo umetolewa na Mkufunzi wa wa Chuo cha Ualimu cha Kigurunyembe Morogoro pamoja na Katekista wa parokia ya Mkuzi Jimboni Tanga waliongea na mwandishi wa habari hii kwenye sherehe za Adhimisho la Jubilei ya miaka 100 ya kanisa Katoliki Jimbo la Tanga Septemba, 27.

Bw. Bathromeo Makoa Mkufunzi wa Lugha na Sayansi ya Jamii kwenye chuo cha Ualimu Kigurunyembe amesema elimu ya dini inayotolewa hivi sasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari nchini ni ndogo kulinganisha na maendeleo ya Sayansi na Teknolojia inayoendelea kukua kimataifa.

Amesema makosa na uvunjaji sheria vinavyoongezeka ni kuashiria kukosekana kwa maadili mema kwa vijana, maadili yanayoweza kupatikana katika mafundisho ya dini. Ameshauri viongozi wa madhehebu ya dini kuacha kulumbana badala yake watumie wakati wao kutoa mafundisho ya kina kwa vijana ili kuliokoa Taifa na momonyoko wa maadili unaotishia Imani za kidini kukosa Waumini wa kweli. Amesema ili kukabiliana na kwenda sambamba na maendeleo ya Teknolojia wafundishaji wa dini wapewe elimu ya kutosha kujua mazingira yaliyopo.

Amesisitiza kuwa jamii ya kitanzania ikiandaliwa kiroho itaweza kupambanua faida na athari za utamaduni wa nchi za nje na kuepuka maovu.

Bwana Makoa alikuwa Tanga kushudia adhimisho la Jubilei ya miaka 100 ya Ukatoliki Jimboni Tanga pamoja na Jubilei ya miaka 25 ya Upadrisho wa Mhashamu Askofu Antony Banzi. Askofu Banzi ni mzaliwa wa Morogoro.

Nae Charles Mdoe Shemdoe wa Parokia ya Mkuzi Lushoto amesema ili Imani ya Kikristu iweze kuchangia kujenga maadili mema, elimu ya dini ni lazima ipewe kipaumbele. Amesema baadhi ya wazazi hawazingatii mafundisho ya dini kwa watoto na kuwaachia walimu wa dini mzigo mzima wa ufundishaji kwa Makatekista. Matokeo yake Imani ya Kikristo inaonekana kuwa cha kupia baada ya kupokea Sakramenti.

Ameshauri kuwepo na utaratibu wa kuweka mtihani wa Jimbo zima kabla vijana hawajapokea sakramenti inayohusika.

 

 

Mkutano wa UEM kufunguliwa kesho

Na Said Mmanga,MSJ

MKUTANO mkuu wa umoja wa Misheni Afrika,Ulaya na Asia (UEM) utafunguliwa kesho katika Kanisa la Azania Front Jijini na utafikia kilele chake Oktoba 25 mwaka huu.

Kwa mujibu wa barua ya KKKT dayosisi ya Mashariki na Pwani iliyotiwa saini na katibu msaidizi wa Dayosisi hiyo Askofu Ngelima katika mkutano huo mambo mbalimbali yatajadiliwa juu ya umoja huo ambapo pia kutakuwa na mambo mbalimbali yatakayokuwa yakiendana na mkutano huo. Mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano huo hapo kesho jumatatu itakuwa ni siku ya tanzania wakati Oktoba 17 kutakuwa na tamasha la kidini litakalofanyika katuika ukumbi wa jumba la utamaduni wa Korea lilipo katika barabara ya morogoro jijini.

Akifafanua zaidi juu ya mkutano huo mmoja wa wakuu wa idara ya wanawake katika dayosisi hiyoRahel Mwakamianda alisema kuwa mkutano huo pia utajadili mapendekezo mbalimbali yatakayotolewa katikasemina ya wanawake na vijana wa umoja huo ambayo imemalizika jana katika ukumbi wa kituo cha kiroho Mbagala ambao ulikuwa ukijadili hali za vijana na mambo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake.

Baadhi ya mambo ambayo yalitarajiwa na mapendekezo yake yatafikishwa katika kikao hicho ni kuwepo kwa wachungaji wanawake kwa makanisa ya umoja huo ambapo wapo wanaokubali na wapo ambao wanapinga juu ya suala hilo.

Bi. Mwakamianda alisema kuwa kumekuwa na mvutano juu ya suala la kuwepo kwa wachungaji wanawake katika makanisa ya umoja huo na katika semina semina iliyomalizika jana kila nchi washiriki pamoja na dayosisi zilizoshiriki katika mkutano huo zilitarajiwa kuwasilisha au kuchangia mawazo juu ya hali ya maisha ya mwanamke katika kanisa,katika jamii mbalimbali na hali ya maisha katika nchi mbalimbali za Kiafrika.

 

Kanisa Lasifiwa Mkoani Mara.

Na Bigambo jeje, PST

 

KANISA Katoliki jimbo la Musoma limekuwa mstari wa mbele katika kusaidia kusambaza chakula cha msaada mkoani Mara, imefahamika.

Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Mara, Balozi Nimrod Lugoe alipokuwa akiongea katika hotuba fupi ya kumkaribisha Mwadhama Polycarp Kardinal Pengo mkoani humo katika uwanja wa Karume.

Balozi Lugoe alisema kanisa hilo kupitia shirika lake la kutoa misaada la CARITAS limeweza kusambaza chakula cha msaada kwa watu wenye njaa mkoani Mara kwa uaminifu na bila kusita.

Akizungumzia kuhusu uhuru wa dini alisema serikali itaendelea kutoa uhuru huo wa kuabudu kila mtu na imani ya dini yake na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo, hakutakuweko malumbano ya kidini.

Akijibu hotuba hiyo Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma Mhashamu Baba Justin Samba alisema kanisa lake liliweza kusambaza chakula hicho kutokana na ushirikiano mzuri kati ya dhehebu hilo la dini na serikali zaidi ya tani 11,000 za chakula zilizpokelewa mkoani Mara na kusambazwa kwa walengwa kama chakula cha msaada kilichotolewa na serikali kati ya mwaka 1998-1998.

 

Maelfu wamzika Askofu Mustaafu Jimbo Kuu Mwanza 8.10.98

Na charles Hililla, Mwanza.

 

MAELFU ya watu kutoka jimbo kuu la Mwanza na majimbo jirani walifurika kwenye kanisa kuu la jimbo la Mwanza parokia ya Bugando kwa ajiri ya kutoa heshima za mwisho, rambi rambi na kuhudhuria ibada ya misa ya mazishi ya Askofu Mkuu mstaafu wa jimbo hilo Askofu Renatus Butibubage aliyefariki dunia Oktoba 2, mwaka huu kwenye Hospitali ya rufaa ya Bugando.

Umati huo wa watu ulianza kufurika tangu Oktoba 7 usiku ulipopokelewa mwili wa marehemu na kufanyika ibada ya kupokea mwili wa marehemu, iliyoongozwa na Askofu Aloysius Balina hadi Oktoba 8 siku ya ibada ya misa ya mazishi.

Ibada ya misa ya mazishi iliongozwa na Askofu Nestor Timanywa wa jimbo la Bukoba, ilihudhuriwa na watu mbali mbali mashuhuri kutoka ndani na nje ya mkoa wa Mwanza wakongozwa na Baba wa Tafia Mwl. Nyerere aliyekuwa ameambatana na mke wake Mama Maria Nyerere.

Wengine waliohudhuria Misa hiyo walikuwa ni mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Meja Jenerali James Luhanga, Mbunge wa Magu na Mwenyekiti wa chama cha Siasa cha UDP Mhe. John Cheyo. Viongozi wengine walikuwa ni kutoka serikalini, vyama vya siasa na madhehebu mbali mbali ya dini.

Kwenye mahubiri wakati wa misa hiy, Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza Askofu Anthony Mayala, alimtaja marehemu Askofu Mkuu mstaafu marehemu kuwa yeye alijiita kuwa ni chuma cha pua katika kutetea na kuilinda imani yake kwa kanisa kutokana na moto wake aliokuwa maechagua wakati alipopewa daraja la uaskofu kama mwongozo wake. "UPENDO HUVUMILIA" ndio maana amevumilia yote hadi kifo chake.

Misa hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na maaskofu saba kutoka majimbo ya Jimbo Kuu Mwanza Askofu Anthony Mayala, Shinyanga- Askofu Aloysius Balina, Bukoba Askofu Nestor timanywa, Kigoma Askofu Paul Ruzoka. Wengine walikuwa ni Askofu Severine Niwemugizi Rulenge, Askofu wa Musoma ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Askofu Justin Samba, Askofu mstaafu fortunatus Lukanima na Askofu wa Anglikan Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria Askofu Manase Yona.

Kundi kubwa la mapadri kutoka majimbo ya jirani na mamia ya masista na watawa. Marehemu Askofu Renatus Butibubage amezikwa kwneye kanisa la Nyegezi Seminari.

 

Matanda V.T.C. wafanya Mahafali

Na Charles Hillila, Shinyanga.

 

JUMLA ya vijana 27 wamehitimu mafunzo ya awali ya ufundi mchundo Oktoba 4, mwaka huu kwenye chuo cha ufundi Matanda kinachoendeshwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga. Fani zifundishwazo chuoni hapo ni ufundi wa magari, umeme na ukelezaji wa vyumba na mabomba.

Kwenye mahafali hayo ambayo ilikuwa ni ya saba tangu chuo hicho kisajiliwe na serikali hapo mwaka 1992, kamanda wa polisi wa mkoa wa Shinya Bw. Gumbo aliyekuwa amekaribishwa kwenye mahafali hayo, aliwaasa vijana wanaomaliza kuwa mabalozi wazuri wa chuo na jimbo kwa ujumla kwa kuwa waaminifu kwa kazi watakazopewa na wateja.

Awali vijana hao kwenye risala yao walitaja kuwa: jimbo lifikirie kuongeza idadi ya walimu kwani waliopo hawatoshelezi idadi ya wanafundi. Kingine walisema ni upungufu wa vitabu na vifaa vya kufanyia kazi na kufundishia na wakaongeza kuwa kupatikana kwa mahitaji hayo kutaongeza uwezo wa kitaaluma kwa wanafunzi chuoni hapo.

Aidha vijana hao walisisitiza kwenye risala yao kuwa pawepo na kisanduku cha huduma ya kwanza pamoja na dawa zake kwa vile shughuli wanazofanya zinawiana kabisa na shughuli za viwandani ambapo mtu anaweza kuumia wakati wowote.

Kingine walichosema kwanye risala yao ni kukatiwa bima kwa vipindi wanapokuwa kwenye majaribio kazini na kupewa mtihani ya ushindani na vyuo vingine vya namna hiyo ili wajipime kabla ya mitihani ya taifa.

Akijibu risala hiyo Padri Michael Kumalija aliyekuwa mgeni rasmi siku hiyo kwa niaba ya jimbo aliwaambia vijana hao kuwa, huduma ya kwanza ni ya muhimu sana kuwepo chuoni hapo na akaahidi kulifikisha suala hilo kwa uongozi wa jimbo.

Aidaha Padri Kumalija aliwaomba vijana ho kuwa na moyo wa subira kuhusu madai na maombi yao na kuendelea kusema kuwa mambo mazuri hayaji kwa mara moja. Alitoa ombi kwa uongozi wa chuo hicho kuangalia uwezekano wa kuwapatia vitenda kazi kila kijana anayemaliza chuoni hapo kulingana na fani aliyokuwa anasoma. Kauli hiyo ilipokelewa kwa shangwe kubwa na wanafunzi hao.

Nae mku wa chuo hicho Bw. Mtwangile aliwaasa vijana hao kuwa; wajitahidi kuishi kwa kufuata sheria za nchi na kumuweka Mungu mbele katika shughuli zao zote.

 

Paroko wa Upanga atimiza miaka 50 ya utawa

Na. Stephen Rwehikiza

PAROKO wa Upanga, Padri Mario Meccarini Jumapili, iliyopita 4/10/98 alisherehekea sikukuu ya kutimiza miaka 50 ya Utawa wa Wafransisko, Capuchini.

Sherehe hiyo ilihudhuriwa na wanaparokia wengi wa Upanga, pamoja na wawakilishi wa shirika la Wafransisko Capuchini nchini Tanzania, na kundi la wawakilishi wa wazee na watu wengine wasiojiweza (maskini) ambao Padri Mario amekuwa karibu nao kwa msaada wa kiroho na kuwashughulikia kwa misaada midogo midogo ya kukidhi maisha yao.

Baba Mario mwenye umri wa miaka 68 alizaliwa kijini cha kestirio

Frorentino Italia 1/3/1930 na kujiunga na utawa mwaka 1948

sherehe hiyo ilianza kwa Misa Takatifu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu ambayo aliiongoza yeye mwenyewe pamoja na Paroko Msaidizi Padri Zakayo.

Baada ya Misa waumini walijumuika pamoja katika uwanja wa Parokia kwa kumpongeza kwa zawadi, michezo ya kuigiza, na nyimbo kutoka vikundi vya vijana wadogo na kikundi cha Viwawa parokiani. Sherehe hiyo ilifuatiwa na chakula cha mchana.

Katika tafrija hiyo, Mwenyekti wa Baraza la walei parokia ya Upanga Ndugu John Baptista Mwenda, kwa niaba ya Wanaparokia wa Upanga, alimsifu Padri Mario kwa kujitoa muhanga kumtumika Mungu na viumbe vyake kwa kipindi chote che miaka 50 katika Utawa.

Kwa kipindi cha miaka karibu mitano akiwa Paroko wa Upanga Padri Mario ameleta uhai zaidi kwa vyama vya kitume na jumuiya Parokiani, vyama hivyo ni WAWATA, VIWAWA, CPT na chama cha Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Pia jumuiya za Neo-Katekuminato na Yohane Mbatizaji nazo vimeimarika zaidi chini ya uongozi wake thabiti wa karibu.

Kufuatia ombi la Mwadhama Polycarp Cardinal Pengo kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ajira kwa vijana, padri Mario amekuwa mstari wa mbele kuhimiza jitihada za kupunguza matatizo ya vijana kutoka kazi na tayari kamati na mfuko maalumu vimeundwa Parokiani kwa ajili ya vijana. Mpaka sasa vijana kadhaa parokiani wamefaidika na mfuko huu kwa kulipiwa ada za shule au kupewa mikopo ya kuanzisha biashara ndogo ndogo.

Pia kwa juhudi zake Baba Mario imejengwa shule ya kufundisha kushona. Parokiani ambayo itafunguliwa mwakani.

Pia kuna mipango ya kujenga zahanti Parokiani ambayo itahudumia maskini na wana Upanga kwa jumla

zaidi ya hayo, Padri Mario amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha vijana wa Parokia watafute njia za kujisaidia wenyewe na kusaidiana wao kwa wao.

Katika kutikia wito huo, VIWAWA Parokiani hivi karibuni waliendesha matembezi ya hisani ambayo yaliongozwa na Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Paul Kimiti na yameingiza kiasi kisichopungua shs. Milioni mbili.

Padri Mario alijiunga na Utawa, "Noviciati" Wafransisko Capuchini 8/9/1947 Florentino, Italia na alipata daraja la upadre 17/3/1956

Alikuja Tanzania 1964 na kwa kipindi kirefu alifanya shughuli za kitume katika Parokia mbali mbali, Mpwapwa katika Dayosisi ya Dodoma mpaka mwaka 1994 alipohamishiwa Parokia ya Upanga.

Wanaparokia wa Upanga wanamtakia maisha marefu katika kazi yake ya kuchungaji na kumtumikia Mungu kwa uaminifu na bidii.