Make your own free website on Tripod.com

TFF mpya ituunganishe - WADAU

Na Machumu Manyama

UONGOZI mpya wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais Leodgar Tenga, umepongezwa kwa kuchaguliwa kwake lakini umetakiwa kwanza, kuunganisha vyama vikuu vinavyosimamia mchezo huo ili kufanikisha azima iliyokusudiwa na Shirikisho hilo.

Wadau mbalimbali wa soka waliyasema hayo, baada ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa kutafuta viongozi wa Shirikisho hilo katika Hotel ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam hivi karibuni walipozungumza na KIONGOZI kwa nyakati tofauti.

Walisema iwapo uongozi huo mpya utayafanya yale waliokuwa wakijinadi wakati wa kuomba nafasi za uongozi, basi huenda soka la Tanzania likafanikiwa na kuepusha ile aibu iliyodumu kwa takribani miaka 10 nchi ikiwa msindikizaji katika mashindano ya kimataifa.

Mwenyekiti wa Kundi la Yanga Asili Bw. Yusuf Mzimba alisema, kutokana na uongozi uliopita kuwa mbali na wadau mbalimbali wa soka pamoja na  Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Umoja wa Vilabu Nchini (UTAFOC), Uongozi huu mpya unapaswa kuwa karibu na vyama hivyo hasa kwa kushirikiana katika kutoa maamuzi ya pamoja ili kuendeleza soka.

Alisema kuwa, katika uongozi uliopita kulionekana kuwepo kwa uhusiano mbovu na vyama hivyo, hali iliyofanya mawasiliano ya pamoja kuwa magumu huku kila mmoja akitoa maamuzi yake binafsi.

“Ni wakati sasa kwa uongozi mpya kuweka uhusiano mzuri ili kuwepo kwa mawasiliano ya kutosha kutoka pande hizo ambazo ndizo wasimamizi wakubwa wa soka letu,” alisema.

Naye mpenda michezo aliyejitambulisha kwa jina la John Richard alisema hivi sasa  jukumu kubwa alilonalo Bw. Tenga na viongozi wenzake ni kuhakikisha matatizo yaliyokuwepo hapo awali ambayo yalikuwa kikwazo katika maendeleo ya soka  yanaondolewa ili watimize matakwa ya Watanzania kuendelea kisoka tunapoanza mwaka huu mpya.

Aliongeza kusema kuwa, viongozi hao wanapaswa kuepuka kupindisha kwa kanuni na sheria za soka zilizosababisha migongano ndani ya shirikisho hilo awali.

Alisema ni wakati sasa kwa TFF mpya, kusimamia kikamilifu sheria na taratibu za soka kwa kuwa ndio muhimili na mwongozo wa maendeleo ya soka karibu katika kila nchi duniani.

Wadau hao walisema hawana wasiwasi na viongozi waliorithi madaraka hivi sasa, kwa kuwa wanawajua kuwa ni wakereketwa na watu wenye uchungu na mpira wa Tanzania, hivyo wamewatakia kila la kheri viongozi hao.

ASHANTI yatahadharisha Ligi Kuu

Na Machumu Manyama

BAADA ya kufanikiwa  kupanda daraja msimu huu na kushiriki Ligi Kuu ya VODACOM Tanzania Bara 2005, timu ya soka ya Ashanti ya Ilala, imepania kufanya kweli katika ligi hiyo inayotarajiwa kuanza baadae mwaka huu.

Katibu Mkuu wa timu hiyo, Arafati Bakari ameliambia KIONGOZI, hivi karibuni jijini Dar es Salaam kuwa, mwendo waliotoka nao katika Ligi Daraja la Kwanza, wanatarajia kuuendeleza hata katika Ligi Kuu.

Alisema, Watanzania wasubiri kuona soka la kisasa kutoka kwa timu yake inayoundwa na wachezaji wasio na majina makubwa kama ilivyozoeleka kwa timu nyingi zinazo shiriki Ligi Kuu.

Katika kuimarisha kikosi chao,  hawatarajii kuwasajili wachezaji wakongwe na walio na majina makubwa katika medani ya soka nchini badala yake, watasajili wachezaji chipukizi ili waoneshe uwezo wao.

“Lengo letu ni kuinua vipaji vya chipukizi, kwa hiyo tutawapa nafasi zaidi, ili nao wauoneshe umma wa Watanzania uwezo wao,  watoto wenye vipaji tunao (Ashanti),” alitamba Bakari.

Aliongeza kuwa, katika kujidhatiti na ligi hiyo kubwa nchini, wanatarajia kuanza mazoezi yao hivi karibuni, huku wakiwa na kikosi cha wachezaji 25.