SHEREHE ZA KUZALIWA MKOMBOZI YESU KRISTO (KRISMAS/NOELI-2004)

 

WAZO kuu la Krismas 2004 ni “Haki na Amani Inayothamini Uhai wa Mwanadamu.” Ndugu zangu waamini, leo tunaadhimisha sherehe za kuzaliwa kwake Yesu Kristo, Mwana wa Mungu. Kanisa linatuongoza pangoni Bethlehemu kutuonesha Neno wa Mungu aliyetwaa mwili (Umwilisho) katika Bikira Maria.

Katika hali ya unyonge, Mungu anakaa nasi- “Immanueli” ili atuondoe katika mauti ya dhambi. “Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangazia” (Isaya 9:2).

Aya hii ya Nabii Isaya inahitimisha matumaini ya wengi wanaotembea katika giza la dhambi. “Mimi ni njia ya ukweli na uhai. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu” (Yoh 14: 6).

Kwetu sisi tuliotembea wiki nne za Majilio tukitafakari umaana na umuhimu wa siku ya leo, bila shaka tuna kila sababu za kuimba kwamba tumefika. Lakini, furaha hii imesongwa na wasiwasi mkubwa, kwani hali ilivyo nchini mwetu na ulimwenguni kwa jumla, si ya furaha tunayotazamia sote kwani watu wengi usiku wa leo wanaomboleza kwa sababu ya kukosa haki na amani iliyo zawadi ya Sikukuu ya Krismas.

Krismas ni Haki na Amani iliyothamini Uhai

 Sababu kuu ya “Umwilisho” ni upeo wa upendo wa Mungu kutaka kutembea nasi kwa hali zote isipokuwa dhambi. Ni Mungu aliyetuumba kwa mfano wake amependa kuturudishia Amani na Uhai uliopotea kwa sababu ya dhambi. Hivyo, uwepo wa Mungu kwa binadamu, ni hakikisho la uwepo wa Haki na Amani iliyo tunda la uhai wetu.

Leo katika mji wa Bethlehemu amezaliwa mtoto. Kitendo cha kuzaliwa katika familia zetu kila wakati ni zawadi na furaha kwa familia nzima.

Uhai ni zawadi inayotoka kwa Mungu kwani Mungu tunayemwabudu yu hai. Hivyo, zawadi ya uhai- Mungu kuzaliwa kati yetu.

Je, ndugu zangu, ni kwa namna gani sisi tunaenzi na kuutunza uhai? Kitendo cha vyombo vya dola kusajili vituo vya kuharibu na kuondoa uhai kwa kisingizio cha “uzazi wa majira” ni kinyume cha sherehe za leo.

Nchini mwetu kuna utitiri wa vituo vya uzazi wa majira na shughuli kubwa za vituo hivi ni kuharibu uhai. Sera ni kwamba, kadiri wanavyoweza kutoa dawa nyingi za kuharibu au kusitisha mimba, ndivyo wanavyo jipongeza na kuzawadiwa na wale waliowatuma.

Enyi viongozi wetu, si kila linalofaa pale China, America na Ulaya linafaa pia Tanzania. Kitendo cha Serikali zetu kufumbia macho vituo hivi ni kutowajibika na kufanya Katiba ya nchi inayolinda uhai wa raia kuwa kejeli! Jueni ya kwamba, mamlaka yoyote ina uwezo wa kugeuza mabaya kuwa mazuri, lakini hamna ruhusa ya kufanya mazuri kuwa mabaya!

Mazingira ya mahali alipozaliwa Mkombozi wa Ulimwenguni tunayemwadhimisha, yanaonesha  wazi kabisa hali ilivyokuwa wakati wake. Alizaliwa horini, mkiwa, masikini aliyekataliwa na wote wenye nyumba za kupanga.

 Kristo alizaliwa katika ulimwengu wa chuki na maovu mengi, haki ilikuwa ni bidhaa ya kununua. Utaifa na kabila la wazazi wake umemfanya Mkombozi wa ulimwengu kuzaliwa katika pango na kitanda chake kuwa hori la ng’ombe!

Ndugu zangu, hali ikoje ulimwenguni na hususani Tanzania yetu? Mara nyingi kipimo cha haki za raia kimekuwa si uraia wake na ubinadamu wake ila chama chake cha siasa, dini yake, kabila lake, uwezo wake wa uchumi na mahali alipotokea au anapoishi.

Kitendo cha wana usalama kuingilia Mahakama ni ashirio wazo la kutokuwa na utawala wa sheria. Mfano mzuri ni wa waamini Wakristo huko Kiuyu Pemba walionyimwa na vyombo vya usalama na utawala kusali katika Kanisa lao baada ya Mahakama ya Mwanzo kuamua vingine?

Je, huu ndio utawala bora wa sheria? Ni zaidi ya miezi 10 sasa tangu ajali ya gari la Skuli ya Tomondo kugongwa; hakuna kesi kwani aliyesababisha ajali hii ni mzito kiuchumi! Mnyonge akimbilie wapi? Na hali kama hii itaendelea mpaka lini? Kiini cha sherehe ya leo ni tangazo kwamba ,maovu hayana nguvu tena ulimwenguni! Tutafanya nini ili haya yawe kweli?

Haki na Amani ya Kweli ni katika Kuwajibika

Changamoto za sherehe ya leo, ni kwa namna gani tunamwishi Immanuel- Mungu pamoja nasi?

Kamwe hatuwezi kusema Mungu yupo pamoja nasi kama hatutashughulikia masuala nyeti ya HAKI za wote na hasa wanyonge. Mboni ya utawala wa sheria ni HAKI kwa wote na uwajibikaji wa vyombo vilivyopewa jukumu la kutekeleza haya. Kutowajibika kwa vyombo vya dola athari zake ni kubwa na za hatari.

Matukio yaliyotokea wakati wa chaguzi za mitaa huko Tanzania bara na mengine yaliyotokea huko Kusini Pemba, wakati wa uandikishaji wa daftari la wapiga kura, ni matunda ya kutowajibika  kwa waliokabidhiwa jukumu hilo.

Kitendo cha kuweka raia katika vituo vya kupigia kura kwa muda mrefu kwa sababu za uzembe au ubinafsi ni kinyume cha utawala wa sheria na demokrasia, na hivyo, Kanisa linalaani kwa hali zote umwagaji damu uliotokea huko Pemba na Dar es Salaam na linaagiza wahusika wawajibishwe kisheria.

Propaganda za kuwagawanya Watanzania kwa nadharia za Uzanzibari na Uzanzibara na vitendo vya kutishia raia juu haki ya kujiandikisha kupiga kura ni kinyume cha Katiba ya Muungano na hivyo, wahusika wawajibishwe.

Enyi viongozi na wana siasa mnaochochea fikra za Uzanzibari na Uzanzibara, jifunzeni kwa majirani zetu. Ujumbe wa Kristo ni iweni wapenda amani wa nchi yenu kuliko wa madaraka kwa njia ya upanga.

Ndugu zangu, wengi wa jamaa zetu wapo magerezani miezi na miaka wakisubiri haki. Vijana wetu wengi wanatumika kama vitega uchumi vya wachache wenye uchu wa mali na madaraka.

Wengi wa wanajamii wameathirika kwa dawa za kulevya si kwa hiari yao, ila kwa shinikizo la umaskini.

Asipofanya hivyo ataishije? Wengi wa jamaa zetu ni waathirika wa UKIMWI kwa sababu ya kutojua, kutowajibika na kwa sababu ya anasa bila wajibu. Haya yote ni kwa sababu ya kutowajibika na hivyo kupotea kwa AMANI. Mungu Immanueli anayetembea nasi anatualika sote tuwajibike ili tupate yale mema aliyopenda tuyaishi.

Umaana wa Mungu Pamoja Nasi- Immanuel:

Kila binadamu aliyeubwa kwa mfano na sura ya Mungu ana uwezo wa kutambua kwamba Mungu ni muumba wa vyote na mbele yake binadamu wote ni sawa. Mungu huyu aliye chanzo cha kila mmoja wetu hatutakii maovu ila mazuri, na ndiyo maana anakuja kwetu kwa hali ya ubinadamu wetu.

Si kweli kwamba Mungu ameumba matabaka ya watu. Matabaka ya watu ni mavuno ya mwanadamu kushindwa kutumia uhuru aliomzawadia Mungu.

Sababu za vita ya kwanza na ya pili ya ulimwengu, ni wanadamu wa nchi za viwanda kutaka kutawala ulimwengu kwa nguvu ya vita ya silaha. Nia ya kutawala ulimwengu na hasa ulimwengu wa nchi maskini bado ipo pale pale lakini, kwa muundo na falsafa nyingine.

Nia hii inatekelezwa kwa kasi mno chini ya mwavuli wa “utandawazi” na “ubinafsishaji” unaolenga kumiliki njia zote za uchumi wa nchi masikini! Je, ni nani asiyejua nguvu ya utawala ni uchumi wenye nguvu? Mungu anayetembea nasi ni Mungu wa haki kwa wote.

Aidha, si kweli kwamba wawekezaji nchini hawafahamu umuhimu wa haki ya kila mtu kuishi kwa jasho lake, lakini ni nani anayewahalalishia kwamba mwekezaji ana mahitaji zaidi ya mwenyeji anayemwezesha kuzalisha ?

Mishahara, marupurupu na faida wanayopata wawekezaji ikilinganishwa na wasomi na wahudumu Watanzania, ni kielelezo wazi cha ukoloni mambo leo na muundo endelevu wa matabaka ya watu!

Ili ulimwengu utambue Mungu tunaye msheherekea leo kuwa  ni Mungu wa wote, vyombo husika vidhibiti unyanyapaa wa raia wanaofanyiwa na wawekezaji.

Ndugu zangu, shangwe ya usiku huu na kipindi chote cha Krismas ni kwamba; Mungu anazungumza nasi kwa mara ya mwisho kwa njia ya mwiliisho-Mungu kuwa mwanadamu ni ukweli ambao hauwezi kuondolea kwani ni yeye mwenyewe amependa iwe hivyo.

Ni Mungu amejishusha ili aweze kutuinua kwa hali zote. Hiki ni kielelezo wazi kwamba anatupenda na yupo nasi. Yeye ni uhai wetu, muda wetu na anasafiri nasi katika yote.

Ni Mungu anayesema kwa maneno ya Nabii Isaya; “Kwa ajili ya Unguja na Pemba sitanyamaza, na kwa ajili ya Tanzania sitatulia, hata haki yangu itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wangu kama taa iwakayo.”

Tumwombe atembee nasi kipindi chote cha matayarisho ya Uchaguzi Mkuu wa 2005. Tumwombe hekima yake na tuweni wavumilivu na wenye subira katika kusikiliza sauti yake.

Mungu Immanuel abariki watu wa Tanzania, Mungu Immanuel abariki Afrika na Mungu Immanuel abariki jamii yote aliyopenda kuigawia upendo wake.  

Nawatakieni nyote kila Baraka na Amani ya Mungu Immanuel.

 

 

Familia takatifu chimbuko la utakatifu

l    Ndoa ni kazi ngumu, lakini muhimu

l          Kwanini wengine hawaoi au kuolewa ?

 

Na Furaha Nakulele

KWA kawaida, neno familia linaposikika, mara moja mtu hukumbuka BABA, MAMA na WATOTO. Yesu, Maria na Yosefu ni mfano bora wa Familia Takatifu ambayo kubwa zaidi, inaheshimu tunu ya UHAI.

Ni kwa mantiki hiyo, tunapozungumzia juu ya KRISMAS na kuisherehekea, tunazingatia kuwa, Maria na Yosefu walizingatia na kuuheshimu uumbaji wa Mungu hasa juu ya uhai, ndiyo maana kamwe, hawakufanya jaribio lolote la kumuuua Yesu, baada ya kuzaliwa, au hata KABLA YA KUZALIWA ; kwa njia ya utoaji mimba (ABORTION).

Ni kwa mamtiki hiyo, tunaposherehekea Krismas ya mwaka huu, wote hatuna budi kutambua, kuwa chanzo cha sherehe hizi ni wito wa ndoa ambao ndio asili ya miito yote na hivyo, kwamba ndoa inatarajiwa kuwa inayoleta FAMILIA TAKATIFU duniani, isiyo na magomvi, mauaji, masengenyo, UTOAJI MIMBA na vitu vingine vyovyote visivyoendana na mapenzi ya Mungu.

Ni kwa msingi huo, tuanze toleo hili kwa kuangalia NDOA hasa kwa mujibu wa Kanisa Katoliki.

Kwanza ijulikane kuwa, kuna aina tatu za ndoa ambazo ni Ndoa yaKimila, Ndoa ya Kiserikali na Ndoa Takatifu ya Kikristo.

NDOA YA KIKRISTO

Kwa maneno mengine, Ndoa ni agano linalowekwa kati ya mwanaume na mwanamke wabatizwa mbele ya Mungu ili wawe mke na mume.

Kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu, agano hili linawafanya wabatizwa wawe mwili mmoja wakishiriki haki zote za ki-ndoa pamoja na mafao ya kijamii yatokanayo na hali ya ndoa.

Ndoa humpa uwezo na mamlaka mwanamke na mwanamme kuishi pamoja wakishirikiana na kujengana na kutekeleza upendo wa ki-Mungu (Mwa. 2: 20b - 24).

Ndoa ina malengo makuu mawili yaani, kuwafanya wanandoa kushirikishana upendo unaowawezesha kuishi katika umoja, pamoja na kuendeleza tendo la uumbaji, yaani kuleta uhai mapya, yaani kuzaa watoto kama alivyozaliwa MTOTO YESU.  1Yoh. 1: 8-16, Mwa. 1: 22.

Mwasisi wa ndoa ni Mungu mwenyewe Mungu akishawaumba, mwanamme na mwanamke hupendana kati yao; huwa sura ya mapendo kamili na daima ambamo Mungu ampenda mtu.

Kwamba mwanamme na mwanamke waliumbwa mmoja kwa ajili ya mwingine, maandiko yanathibisha  (Mwa. 2:18, Mwa. 2:24, Mt 19:6)

Mwanzoni mwa maisha yake, Yesu alifanya ishara yake ya kwanza kwa ombi la mama yake wakati wa arusi ya Kana  (Yoh.2 : 1-11)

Hapo kanisa laona maana kubwa ya uwepo wa Yesu katika arusi ya Kana. Linaona uwepo uthibitisho wa uzuri wa ndoa na tangazo kwamba:- ndoa itakuwa ishara halisi ya uwepo wa Kristo.

Ruhusa iliyotolewa na Musa ya kumwacha mke ilikuwa ni kibali kilichosababishwa na ugumu wa moyo, (Mt. 19: 8). Kwa hakika yake umoja wa ndoa ya mume na mke hauvunjiki kwani Mungu mwenyewe aliunganisha. (Mt. 19:6). Kutengana kunakoeleweka ni kwa kufa mmoja.

Vitabu vya Ruthu na Thobiti vyatoa ushuhuda wa kusisimua wa maana ya ndoa iliyoinuliwa ya uaminifu na ya upole.

Yesu mwenyewe anatambua hilo. Ndio maana yeye mwenyewe anatoa nguvu ya neema kwa ajili ya kuishi ndoa kama mtazamo mpya wa ufalme wa Mungu. Kwa kumfuata Kristo, kwa kujikania wenyewe, na kwa kuchukua kila mmoja msalaba wake, watu wa ndoa wataweza kupokea maana ya asili ya ndoa na kuishi kwa msaada wa Kristo (Mt. 19:11)

Kama ndoa ina yote hayo mazuri kwa nini baadhi  hawaoi na hawaolewi, mfano Mapadre na Watawa?

Shirika la Kutetea Uhai (PRO-LIFE), Tanzania linasema, “Kristo ni kiini cha maisha yote ya Kikristo. Kifungo cha uhusiano naye, huchukua nafasi ya kwanza kabla ya vifungo vingine vyote, vya kifamilia au vya kijamii. (LK. 14 : 26, Mk. 10 : 28 - 31), Kristo mwenyewe amewaalika mapadri, watawa kumtafuta/kumfuata katika mtindo huu wa maisha ambamo yeye anabaki mfano.’ 

Linaongeza, ‘Sakramenti ya ndoa na ubikira (useja) kwa ajili ya ufalme wa Mungu yatoka kwa Bwana mwenyewe. Ni yeye anayeyapa maana yao kulingana na neema inayotakiwa, kuyaishi kulingana na matakwa yake na maana ya kikristo ya ndoa, haya mawili hayatengani na yanaimarishana.’

Ieleweke wazi kuwa, watendaji wakuu wa agano la ndoa ni mwanamme na mwanamke waliobatizwa, walio  huru kufanya mapatano ya ndoa na wanaonesha kwa hiari ukubaliano wao. 

Kama hivyo ndivyo, labda mtu anaweza kujiuliza kuwa, kuwa huru maana yake nini ? Ni kutokuwa chini ya shuruti na kutokuwa na kizuizi kutokana na sheria ya maumbile au Kanisa. (CIC, Can 1057  #1) NB. Kama uhuru unakosekana, ndoa ni batili.

FAMILIA

Familia hujengwa na Baba, Mama na Mtoto au Watoto. Kwa kawaida, familia takatifu ni fam,ilia ambao wadau wake wote, wanapendana, wanaheshimiana, wanasameheana, wanasali pamoja na wanashiriki shida na raha mpaka mwisho lakini, kikubwa zaidi, yote hayo wanayafanya ili kutimiza mapenzi ya Mungu.

Wazazi wana jukumu kubwa la kuwajenga mazingira mazuri ya familia yaani, malazi, mavazi, chakula, elimu  na mahitajin mengine.

PRO- LIFE, Tanzania inasema, ‘Familia kama hifadhi takatifu ya uhai, itambue kuwa zawadi kubwa sana na yenye thamani kubwa sana katika ndoa ni watoto. (LG &1, Zab. 128:3). Hii ndiyo maana ulimwengu sasa umepewa zawadi ya UKOMBOZI ; yaani KUZALIWA KWA YESU KRISTO.

Kristo  alipenda kuzaliwa na kukua katika Familia Takatifu ya Yosefu na Maria. Kanisa si kitu kingine ni “Familia ya Mungu “ ,”ni kanisa la nyumbani.”

Familia ni muhimu sana, kiasi kwamba nafasi yake katika kujenga utamaduni wa uhai haiwezi kuchukuliwa na kitu kingine.

Jukumu la malezi si la mtu mmoja ni la wote, ni la jamii nzima.

Kama kanisa la nyumbani, familia imeitwa kutangaza Injili ya Uhai.

Familia isali ili kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai.

Haki za familia zizingatiwe.

NDOA NA FAMILIA:

 “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba, mwanaume na mwanamke aliwaumba, Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia zaeni mkaongezeke…” (Mwa 1: 26-27).

 “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu. Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (Mwa 2: 23-24)

Msingi  wa familia unatokana na katika Maandiko Matakatifu yanayoibua dhana zifuatazo, mwanaume na mwanamke wanaounganika na kuunda familia, wameumbwa kwa mfano wa Mungu

Binadamu ni kiumbe kilichobarikiwa na Mungu, uzao ambao ndio tunda la mwunganiko wa mume na mke umebarikiwa

Watoto, yaani uzao ni baraka itokayo kwa Mungu, ni baraka inayoendeleza tendo la uumbaji ambalo binadamu anashiriki pamoja na Mungu

“Kutozaa kwa makusudi, au kuzuia kuzaa bila sababu yoyote ni kuzuia tendo la uumbaji ambalo binadamu amepewa na kubarikiwa na Mungu na kama lingefanyika katika familia ya Maria na Yosefu, ulimwengu huu usingepata Mkombozi na badala yake, ungeamia,” linasema Shirika hilo la kutetea uhai, tawi la Tanzania kupitia Mwenyekiti wake, Bw. Emil Hagam.

Linasema, Mke na mume huunda muunganiko usioweza kugawanyika; kila mmoja ni mali ya mwezake, na kwa ajili ya mwenzake. Hawa, huunda familia ya pekee nje ya wazazi wao wakishiriki agano lisiloweza kuvunjwa

Sasa, katika dunia hii yenye mkanganyiko wa mawazo, dhana ya familia inaweza kuelezwa kwa namna mbalimbali kutegemeana na mwelekeo wa taaluma na lengo la mfasiri.

Mwanamume na mwanamke walioungana katika ndoa, pamoja na watoto wao ndio wanaounda familia. Familia kama taasisi ipo hata kabla mamlaka za kijamii hazijaitambua na ambazo zina wajibu wa kuitambua. Hii ndiyo tafsiri ambayo kwayo tafsiri nyingine zozote zihusizo familia zitarejea.

Kwa kuumba mwanamume na mwanamke, Mungu alikusudia kuunda familia ya binadamu na kuitengenezea mazingira maridhawa ya makubaliano. Wanafamilia ni wale wanaokaa na kushirikiana kijamii pamoja, lakini kila mmoja akiwa na hadhi yake.

 

Silika ya familia ya Kikristo

Agano la ndoa:

Wakati wote familia imetambulika kama msingi na namna ya kueleza tabia ya kijamii ya binadamu. Familia kwa hiyo ni muunganiko wa watu ambao namna yao ya kuishi na kukaa pamoja ni kwa njia ya “Komunioni”- - muunganiko wa watu.

Ndoa ni agano ambalo kwalo mwanaume na wanamke kila mmoja hujitoa kwa mwenzake na kila mmoja anamkubali mwenzake kama mwenzi na mshirika wake wa maisha.

Mwuungano wa hiari wa mwanamume na mwanamke.

 

 

Ni binadamu tu mwenye uwezo wa kuamua kwa hiari juu ya kuunganika pamoja kwa msingi wa uchaguzi wa hiari. Katika ndoa mwanamume na mwanamke wanaungana kiasi cha kuwa mwili mmoja (Mwa. 2:24). Japo ni binadamu wawili walio tofauti wanao uwezo wa kuishi pamoja katika ukweli na upendo.

Uzao wa binadamu: 

Muunganiko unaotokana na ndoa huleta furaha na faraja ya uzao wa binadamu wapya. Kwa hiyo, kwa tendo hilo wazazi hushiriki na Mungu Muumbaji katika kuumba na kuzalisha kiumbe kipya. Mungu anashiriki katika ubaba wa mzazi wa kiume na umama wa mzazi wa kike katika kuleta uhai mpya.

Sifa za familia kwa kadiri ya barua ya Papa Yohane Paulo II:  Families of the World”.

Familia halisi ni taasisi ya msingi ya jamii, inayojengwa katika uhalisi wa binadamu, na yenye kujikita katika muunganiko wa hiari wa mwanamme na mwanamke katika agano la maisha ya ndoa kwa ajili ya Kushibisha hamu za moyo wa binadamu za kutoa na kupokea upendo, Kuwapokea na kuwalea watoto katika maendeleo yao ya mwili na akili  na Kushirikiana makazi ambayo huunda msingi wa maisha ya kijamii, kielimu, kiuchumi na kiroho.

Mengine ni Kujenga uhusiano na kupasisha kizazi kipya pamoja na Kutoa huduma kwa wahitaji mbalimbali.

Familia kama Fumbo la Kanisa

Familia ya Kikristo inajifunua wazi na kutambulika kama jumuiya na wanakanisa, na kwa msingi huu familia ni kanisa la (mwanzo) nyumbani. Hii ni jumuiya ya imani, matumaini na mapendo.

Familia hii ni muunganiko wa watu, ishara na mfano wa muunganiko wa Baba na Mwana katika Roho Mtakatifu. Katika uzazi wa watoto na kuwaelimisha tunarejeshwa kutambua uumbaji wa Mungu Baba. 

Kwa hiyo, familia inaalikwa kuishi maisha ya sala na ya sadaka ya Kristo. Sala za kila siku zinaimarisha upendo na hivyo kuwezesha kazi ya uinjilishaji na umisionari kufanyika.

Familia imepewa jukumu la kutoa huduma ya kujenga ufalme wa Mungu kama mshiriki katika maisha na umisionari wa kanisa. Katika familia matendo ya kikanisa ya uinjilishaji, ufundishaji na uelimishaji hufanyika.

Matendo hayo hufanyika mithili ya mama kanisa anavyowezesha kizazi kuendelea kufundisha na kujenga familia ya kikristu. Familia hutekeleza utume wake wa kikanisa ndani na nje ya kanisa.

Katika familia wanandoa wanaishi kisakramenti, na hivyo ndoa inayojenga msingi wa familia inaonekana kama sakramenti ya kutakatifuza na kama tendo la ibada au kuabudu.

Wajibu wa familia

Familia kama taasisi iliyo wazi na ya msingi ina wajibu mbalimbali miongoni kwa watu wanaoiunda.

Mwandishi wa Barua kwa Waefeso anatujulisha wajibu wa kila mmoja wa watu wanaounda familia, mume, mke na watoto.

Mwandishi anatukumbusha kuwa wajibu wa msingi ni ule wa uhusiano. “Kila mmoja amstahi wenzake kwa sababu ya kumcha Kristo”. (Efe. 5: 21). Huu ndio wajibu wa msingi kwani unatutambulisha na kutushirikisha maisha yetu na Kristo.

Baada ya kueleza wajibu huo wa msingi, mwandishi wa barua hiyo anafafanua wajibu wa mume, mke na watoto. Kimsingi wajibu zote zinaegemea tunu za upendo, utii na heshima.

Familia zinazojengeka katika misingi hiyo ndizo zinazodumu na kuwa imara. Wanafamilia katika familia za namna hiyo hukubaliana, huchukuana, hujengana, kila mmoja kwa manufaa ya mwenzake na kwa manufaa ya pamoja.

Wajibu wa familia kwa jamii unaelezwa vizuri kwa kutambua uhusiano asilia uliopo kati ya familia ambayo sehemu, na ndiyo inayouunda jamii kwa upande mmoja, na jamii ambayo hundwa na mkusanyiko wa familia moja moja kwa upande mwingine. Kwa hiyo bila familia hakuna jamii. Kwa upande mwingine familia inahitaji jamii kwa ajili ya ustawi wake.

 

 

KONA YA SHERIA

Raia anaweza kumfungulia rais kesi ya madai

Na Dotto Shashi

SHERIA inaruhusu mtu yeyote ambaye ana madai dhidi ya Rais wa nchi kufungua kesi ya madai hayo, ili aweze kupatiwa haki yake.

Ni wazi kuwa mtu anaweza kujiuliza je, inawezekana vipi kwa raia kumfungulia kesi ya madai Rais wake?

Jibu la swali hili limewekwa wazi katika Katiba  ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mbalimbali.

Kifungu cha 46 Ibara Ndogo ya Pili (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, kinaeleza kuhusu ufunguaji wa kesi ya madai dhidi ya Rais kwa jambo lolote alilofanya katika uwezo wake kama raia wa kawaida yaani, “Institution of Civil Case in respect as an ordinary citizen.”

Katiba  kinaelekeza suala zima la ruhusa ya kumshitaki Rais kwa kosa la madai, yaani “a civil wrong,” .

Katika sheria juu ya shughuli au mambo ya Rais, yaani, “Presidential Affairs Act, CAP9.” Taratibu zimewekwa kuhusu suala zima la kufungua kesi ya madai dhidi ya Rais wa nchi.

Mahakama ambayo inaruhusu kupokea mashitaka hayo ya madai, katika, Kifungu cha Tano (5) cha sheria hiyo kinaeleza kuwa hakuna kesi yoyote ya madai inayofunguliwa dhidi ya Rais itaruhusiwa katika mahakama yoyote isipokuwa mahakama kuu pekee yaani, “No Civil Proceedings which may be instituted against the President shall be instituted in any court other than the High Court.”

Hivyo endapo una madai dhidi ya Rais wako, basi mahakama inayotakiwa kufungua madai hayo ni Mahakama Kuu pekee.

Kifungu cha Sita (6), Kifungu Kidogo cha kwanza (1) cha sheria ya shughuli au mambo yanayomhusu Rais (Presidential Affairs Act), kinasema, mtu yeyote ambaye anakusudia kufungua kesi ya madai dhidi ya Rais ni lazima atoe notisi ya siku Thelathini (30) kwanza kabla ya kufungua kesi hiyo.

Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 46 Ibara ya (2) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika Kifungu Kidogo cha Kwanza (1) (9) cha Kifungu cha Sita (6),inaelezwa kuwa, notisi ya mashitaka ya madai dhidi ya Rais ni lazima iambatane na Hati ya madai. Yaani “Plaint”

(b) Notisi na hati hiyo ya madai itatumwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi au kwa Katibu wa Kudumu au binafsi wa Rais au Notisi na Hati hiyo itatumwa kwa Rejesta iliyolipiwa kabla, kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu kupitia njia ya posta.

Kifungu Kidogo cha Pili (2) kinaeleza kuwa, endapo mahakama itaridhika kuwa kesi dhidi ya Rais imefunguliwa na kwamba mdai, yaani “Plaintiff” ana haki dhidi ya Rais, Mahakama hiyo haitatoa hukumu au agizo dhidi ya Rais isipokuwa kwa kuarifu kwa njia ya maelezo ya kisheria kuwa kuna madai dhidi ya Rais yaliyothabiti, yaani “By way of declaratory order.”

Lengo la utaratibu huu ni kumfahamisha Rais, ili aweze kukidhi matakwa hayo na wala si kumwamrisha, kama inavyokuwa kwa watu wengine wanapofunguliwa kesi za madai.

Kwa upande wa amri ya kukamatwa (arrest), Kifungu cha Nane (8), Kifungu Kidogo cha Kwanza (1) kinaeleza kuwa, Rais ana kinga dhidi ya kukamatwa yaani, “The President shall be immune from arrest.”

Kifungu Kidogo cha Pili kinasema hakuna amri yoyote itakayo tolewa kwa Rais na mahakama yoyote au mtu au mamlaka yenye uwezo wa kutoa amri ya;-

(a). Kumtaka Rais au kumlazimisha kufika mahakamani iwe kwa uwezo wake kama Rais au hata katika uwezo wa kawaida.

(b). Kumtaka au kumlazimisha Rais kumleta mtu au kutoa kitu chochote mahakamani.

Kifungu Kidogo cha Tatu (3) kinasema  endapo upande katika kesi unaomba ruhusa ya kuitwa mahakamani kwa Rais kama shahidi katika kesi hiyo au kumtaka Rais amlete mtu au kitu chochote mahakamani hapo, mahakama itatakiwa kumfahamisha Rais juu ya maombi hayo, lakini mahakama hiyo haitatoa amri nyingine au kutoa wito juu ya maombi hayo.

Kifungu cha Tisa (9) kifungu kidogo cha kwanza kinasema kuwa, hati ya kuitwa shaurini (Summous) ni marufuku kupelekwa Ikulu, au nyumba za kupumzikia wageni au katika viwanja vya Ikulu au katika makazi mengine yoyote maalumu ya Rais, isipokuwa mpaka yatolewe maelekezo kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi juu ya utekelezaji wa utaratibu huo wa ki-mahakama.

Katika kifungu cha Saba (7) Kifungu Kidogo cha Kwanza (1) kuhusu utaratibu wa kisheria dhidi ya Rais anaposhitakiwa,  sheria inasema taratibu nyingine zote zielekezwe kwa Mwanasheria Mkuu yaani, “The Attorney General,”  isipokuwa kwa zile zilizoelekezwa katika Kifungu cha 46 cha Katiba Ibara ya Pili (2) kama tulivyoona hapo awali.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

SHERIA ZA KANISA

Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa(2)

Wanaokwenda vitani wanaweza kupewa Sakramenti ya Mpako?

KATIKA toleo lililopita, tuliishia katika kipengele kinachoelekeza namna ya kumpaka mafuta mgonjwa wakati wa kutoa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Katika toleo hili, tutaanza kuangalia wajibu kwa wagonjwa na kisha, tutaona kama askari wanaokwenda vitani au watu wanaokwenda kunyongwa wanaruhusiwa kupewa SAKRAMENTI YA MPAKO WA   WAGONJWA. Endelea.

Wajibu kwa wagonjwa: kan. 1001

Wenye wajibu wa kuhakikisha kuwa wagonjwa wanapata Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa katika muda unaofaa ‘tempore opportuno’ ni wale walio karibu na wagonjwa. Hao, ni pamoja na jamaa, marafiki, madaktari na wauguzi.

Wengine ni wachungaji wa kiroho kutokana na kazi yao ‘ex officio’. Wengine ni wagonjwa wenyewe ingawa kanuni hii haiwataji.

Lakini, ni wazi kwamba iwapo wenye wajibu huo wamepuuzia, wagonjwa wenyewe hawana budi kujishughulikia kwa kuomba sakramenti hiyo (RAnointing 13: DOL 3333).

Kanuni hii inashauri kuwa, wagonjwa wapokee Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa katika ‘muda unaofaa’, yaani, ‘tempore opportuno’.

Je, maana yake ni nini? Mtaguso II wa Vatikano unasema kuwa, mara tu muumini atakapoanza kuwa hatarini kwa sababu ya ugonjwa au uzee, ni muda unaofaa kupokea Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa (SC 73).

Kwa hiyo, ‘muda unaofaa’ ni pale ambapo hali ya mgonjwa au mzee inaanza kuwa mbaya. Ni juu ya mhudumu wa wagonjwa au mzee au mgonjwa mwenyewe kwa kutumia busara kuona kwamba, hali imeanza kuwa mbaya na kumwita mhudumu wa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa.

Mpako wa watu wengi: kan. 1002

Ingawa mara nyingi mpako unafanyika kwa mtu mmoja, pengine unaweza kufanyika kwa watu wengi, kama vile: wakati wa mahujaji, mkusanyiko wa wagonjwa wa jimbo au wa mji au wa parokia au wa jumuiya fulani au hospitalini (RAnointing 83-85).

Mfano mzuri ni adhimisho la sakramenti hiyo wakati wa mahujaji ya Lurdi ya mwaka 1969 ambapo Ibada ya namna hiyo iliruhusiwa (N6 (1970)13-33; CLD 7,687).

Kanuni ya 1002 inaeleza kuhusu hali ambapo watu wengi wanaweza kupakwa katika Ibada moja. Lakini, askofu wa jimbo hana budi kusimamia au kutoa mwongozo kuhusu adhimisho ambapo wagonjwa kutoka maparokiani au hospitalini au sehemu nyingine wanavyoweza kupokea sakramenti hiyo kwa pamoja (RAnointing 17: DOL 3337).

Huu ni wajibu wa Askofu kwa jimbo tu  kwa sababu ndiye mwenyekiti na mratibu wa shughuli zote za kiliturjia jimboni (kan. 835).

 

MHUDUMU WA SAKRAMENTI: Kan. 1003

Ingawa ni kanuni moja tu inayoeleza kuhusu mhudumu wa sakramenti hii, kanuni hii inatoa mwongozo muhimu kwa wahudumu wa Kanisa. Kadiri ya kanuni hii, ni padrI tu anayeweza kuadhimisha sakramenti kihalali.

Ikisisitiza utaratibu huu, kanuni inasema:”……Unctionem Infirmorum valide administrat……..Solus sacerdos”. Neno “sacerdos” linamaanisha askofu au padrI.

Utaratibu wa kuwa na padrI kama mhudumu wa sakramenti hii umekuwa msimamo wa Kanisa kwa muda mrefu (Conc. Tridentino, Sess. XIV,25 Nov. 1551, cap. 3 et can. 4:DZ 1697 et 1719).

Kanisa linafuata mwongozo wa Mtume Yakobo aliyesema, “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa Kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana,” (Yak 5:14). Mtaguso wa Trenti ulitishia kumtenga mtu yeyote atakayefundisha kinyume na mafundisho hayo.

Mapadri au maaskofu wenye haki na wajibu wa kuadhimisha sakramenti hii ni wale wenye ofisi za kichungaji katika jumuiya za waamini, kama vile, askofu katika jimbo lake, paroko na paroko msaidizi katika parokia yao na chapleni katika jumuiya ya waamini aliyokabidhiwa.

Chapleni anakabidhiwa hospitali au jumuiya ya watawa au jeshi au wakimbizi au mabaharia au shule. Mapadri wengine ni pamoja na gombera wa seminari (Kan. 262) na mkubwa wa shirika la kiklero la watawa.

Kwa hiyo, haki na wajibu huo hauwahusu mapadri na maaskofu wasiokuwa na ofisi za kichungaji katika jumuiya za waamini.

Lakini, padri yeyote au askofu anaweza kuhudumia mgonjwa kwa sababu kubwa na kwa idhini iliyodhaniwa, yaani ‘de consensu…… praesumpto’, kutoka kwa mhudumu halali. Sababu kubwa ni, kama vile, hatari ya kifo.

Anaombwa, kuwa baada ya kuadhimisha sakramenti hiyo, kutoa taarifa kwa mhudumu halali au wa kawaida, yaani mhudumu mwenye haki na wajibu ‘ex officio’.

Adhimisho la pamoja linaruhusiwa, yaani, mapadri wawili au zaidi kushiriki katika ibada moja.

Mmoja kati yao anaweza kusoma sala na kupaka mafuta wakati wengine wakishiriki sehemu nyingine, kama vile, ibada ya utangulizi, masomo, sala ya maombi na kuweka mikono juu ya mgonjwa (Ordo, 19; RAnointing 17-19; DOL 3337-3339).

Washiriki wote hawawezi kushiriki katika kupaka mafuta kwa sababu sehemu za kupaka mafuta zimepunguzwa sana (kan. 1000). Baadhi yao au wote wanaweza kushiriki katika kupaka mafuta iwapo idadi ya wagonjwa ni kubwa.

Sala inayosomwa na kuiongoza-ibada tu ni: “Kwa mpako huu mtakatifu na kwa pendo lake kuu, Bwana akujaze/awajaze na nguvu ya Roho Mtakatifu”.

Baada ya jibu la “Amina”, anaendelea kusema: “Akuondoe/awaondoe katika enzi ya dhambi, akuweke/awaweke huru.

Kwa wema wake akupe/awape nafuu katika mateso yako/yenu na kukujalia/kuwajalia neema”. Jibu ni: “Amina”.

Kuhusu utayari wa kuadhimisha sakramenti hii, kila padri ameruhusiwa kusafiri na mafuta matakatifu. Lengo ni kumwezesha kuadhimisha sakramenti hii wakati wowote wa ulazima (SC Rit, Decr., ‘Pientissima mater ecclesia’, Mar. 4,1965;AAS 57(1965),409;DOL 3314; SCC, general directory, ‘Peregrinans in terra’, Apr. 30,1969:AAS 61 (1969),3605; DOL 2616).

Chimbuko la mwongozo huu ni hati ‘Pientissima Mater Ecclesia’ ya mwaka 1965 iliyotolewa na Idara ya Kiti cha Kitume kuhusu Ibada.

Lakini, mwongozo huu umepoteza uzito wake kutokana na ruhusa iliyotolewa na kanuni ya 999 inayomruhusu padri yeyote kubariki mafuta ya mpako wakati wa adhimisho la Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Ruhusa imetolewa wakati wa ulazima, kama vile, hatari ya kifo.

WAPOKEAJI WA SAKRAMENTI: Kan. 1004-1007.

Sehemu hii ya sheria ya kanisa inazo kanuni 4. Kanuni ya 1004 inahusu adhimisho halali na marudio ya sakramenti. Kanuni ya 1005-1006 zinahusu kesi za mashaka na dhana katika adhimisho la sakramenti. Mwisho, kanuni ya 1007 inawataja wale wanaozuiliwa kupokea sakramenti hii.

Adhimisho halali: Kan. 1004

Kuhusu uhalali wa adhimisho la sakramenti, Sheria ya Kanisa imetaja masharti 5: ubatizo, umri wa mang’amuzi, nia ya mpokeaji (kan. 1006), ugonjwa mbaya au uzee na hali ya kiroho.

Kutokana na uwazi wa baadhi ya masharti hayo, nitajaribu kueleza baadhi tu ya masharti, kama vile, umri wa mang’amuzi na ugonjwa au uzee.

Kwa kuwa lengo la kwanza la adhimisho la sakramenti hii ni kuondoa dhambi na kukamilisha kitubio, kuongeza neema au kurudisha neema iliyopotea kwa sababu dhambi, mpokeaji hana budi kuwa na uwezo wa kutenda dhambi.

Kwa hiyo sakramenti hii haitolewi kwa watoto wachanga au watu waliozaliwa punguani (kan.99) kwa sababu hawana uwezo wa kutenda dhambi.

Hawajapoteza neema ya Mungu walioipata wakati wa ubatizo (DZ,3536). Badala yake sakramenti hii inatolewa kwa muumini aliyefikia umri wa mang’amuzi au zaidi.

Hata mtu mzima aliyebatizwa wakati wa hatari ya kifo na ameelezwa maana na umuhimu wa sakramenti hii katika maisha ya waumini, anaweza kupewa sakramenti hii.

Iwapo kuna mashaka kama muumini amekwishafikia umri wa mang’amuzi apewe sakramenti hii kwa masharti, ‘sub conditione’ (Kan. 1005).

Sharti la pili ni ugonjwa mbaya au mkubwa au uzee. Ndiyo maana Mtume Yakobo anasema, “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana”, (Yak. 5:14). Hayo, pia, ndiyo mafundisho na desturi ya kanisa (Dz,1698).

Kwa bahati mbaya, kanuni hii haielezi kuhusu hali ya ugonjwa au uzee ambapo muumini anapaswa kupokea sakramenti hii.

Inataja tu kuwa muumini apewe sakramenti hii pale ambapo hali yake inaanza kuwa hatarini kwa sababu ya ugonjwa au uzee, ….ob infirmitatem vel senium in periculo incipit versari”.

Kwa hiyo, kanuni hii inatoa nafasi kwa waamini (kan.1001) kutumia busara na hekima zao katika kuamua kuwa afya ya muumini fulani imeanza kuwa hatarini.

Aidha, kanuni haitaji aina ya ugonjwa, ndiyo maana, hata magonjwa ya akili yanahusishwa. Siku hizi magonjwa ya akili yameanza kuwa tatizo na tishio kubwa kwa wanadamu.

Kwa hiyo, waamini wenye magonjwa mabaya au makubwa ya akili wanahitaji kuimarishwa na Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa (Pastoral Care, 27, n. 53).

Mgonjwa anaweza kupakwa kabla ya kufanyiwa upasuaji hospitalini iwapo upasuaji unasababiswa na ugonjwa (Rituale Romanum, Ordo, 10).

Lakini, siyo maaskari wanaokwenda vitani au watu wakunyongwa kwa sababu hali hizo hazisababishwi na magonjwa au uzee. Maaskari walio vitani wanaweza kupakwa iwapo wamepata majeraha mabaya.

Kuhusu uzee, muumini  mzee anaweza kupakwa iwapo ameanza kuwa dhaifu ingawa uzee siyo ugonjwa (Rituale Romanum, Ordo unctionis infirmorum eorumqe pastoralis curae, vaticanis, 1972, n. 11).

 

Itaendelea

 

Kwanini Injili ya Barnaba haikuingizwa katika Biblia?

 

 

Padri Titus Amigu, Mkuu wa Seminari Kuu ya Peramiho iliyopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Songea, ambaye ni Mtaalamu wetu wa Biblia, anajibu swali la mmoja wa wasomaji wetu linalosema: Nasikia kwamba kulikuwa na Injili Barnaba. Je, hiyo ni kweli? Kama ilikuwepo, imekwenda wapi?

Jibu: Injili ya Barnaba ipo lakini haikuingia katika Biblia, iliachwa tangu mwanzo. Ifahamike kuwa, sio hiyo tu iliyoachwa, bali kuna Injili nyingine kama 22 juu yake zilizoachwa. Hazikuingia na hazikupata ruhusa ya kuingia katika Biblia.

Watu wengine wengi pia, hawana habari na Injili hizo. INJILI ZA APOCRIFA, ziliachwa na Kanisa katika Karne ya 4 na mpaka sasa zipo na zimechapwa katika vitabu husika.

Maktaba kubwa zote ni sharti ziwe na vitabu vya Apocrifa. Nami kwa bahati nzuri, ninazo huko niliko. Injili zingine zilizoachwa na Kanisa ni hizi zifuatazo; Injili ya Batholomeo, Injili ya Baslibosi, Injili ya Kuzaliwa Bikira Maria, Injili ya Waebioni, Injili ya Wamisri, Injili ya Eva, Injili ya Gamalika, Injili ya Waebrania, Injili ya Utoto wa Yesu na Injili ya Kiarabu ya Utoto wa Yesu.

Nyingine ni Injili ya Kiarmenia ya Utoto wa Yesu, Injili ya Kiapocrifa ya Yohane, Injili ya Malkion, Injili ya Maria, Injili ya Wanaseni, Injili ya Wanazareni, Injili ya Nekodemo, Injili ya Petro, Injili ya Filipo, Injili ya Thomasi, Injili ya Mapokeo ya Matia na Injili ya Ukweli.

Injili zote hizo zipo. Ilitokeaje tukio hili, hiyondiyo kazi tunayofanya sasa hivi. Kumbuka ndugu msomaji tukio la Yesu kuzaliwa kama binadamu na Mungu hapa duniani, lilikuwa tukio kabambe sana. Tukio la ajabu sana. Tukio lililowatingisha wote. Wayahudi na hata jirani zao Waarabu.

Basi, matokeo yake ikawa watu wengi sana wakaamua kuandika habari hiyo. Hilo unasoma katika utangulizi wa Injili ya Luka1:1-4 kwamba, Watu wengi sana wakati ule, waliandika habari za Yesu. Na yeye Luka pia akaamua kuandika habari za Yesu; hizo hizo. Ila baada ya kuzifanyia uchunguzi kamili.

Alichunguza huko na huko ili andike habari kamilifu. Basi ndugu msomaji, kwa vile watu walikuwa wengi walioamua kuandika, Injili zilikuwa nyingi sana kwa kadiri ya maweza ya waandishi.

Wengine waliandika habari za Yesu kwa mbwembwe na madoido na hata kutilia chumvi mambo mengi.

Ndipo wakubwa wa Kanisa letu katika karne zile za mwanzo, walipoamua kuitengeneza Biblia katika kukusanya mambo hayo rasmi yanayo muhusu Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu, wakazichukua Injili nne tu, zilizomo kwenye Biblia yetu.

Kwa maana hizo zilikidhi vigezo vifuatavyo bila shida; Kigezo cha kwanza kilikuwa ni muunganisho wa maandiko yale, na kigezo cha pili kilikuwa kuwa na asili ya kitume, yaani kuhusika kwa mitume katika kuziandika.

Kigezo cha tatu kukubalika kwa maandishi yale na jumuiya za awali za Kikrito; na kigezo cha nne, kuwa na hadhi ya kuchochea imani na mapendo. Kigezo cha jumla, kilikuwa ni Uongozi wa Roho Mtakatifu mwenyewe.

Basi Injili zote za mbwembwe na zile zilizojaa madoido mengi zilizokuwa haziwezi kuchochea imani wala mapendo ya mtu yeyote, na wala hazikuwa na muunganiko wa mafundisho na wala hazikukubaliana na jumuiya ya awali za Kikrito, hizo ziliachwa kwa maana zilikuwa wazi kwamba, hazikuandikwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Si Injili tu zilizoachwa kwa sababu hizo, bali vipo pia vitabu vingi vingine vya Apokrifa kama vile vitabu vya Matendo ya Andrea, Matendo ya Yohane, Matendo ya Paulo, Matendo ya Thomasi, Barua ya Lentulusi, Barua kwa Waledesia, Alexandria na Ufunuo wa Petro, Ufunuo wa Paulo na Ufunuo wa Thomasi na vitabu vingi vingine.

Jambo hili la kuacha vitabu kama hivyo na kutoviruhusu vitabu kuingia katika Biblia, lisiwe ni kikwazo. Jambo hilo ni alama ya wazi ya kukomaa na alama ya wazi ya uadilifu wa imani yetu ya Kikristo.

Hii ni imani makini yenye lengo la kuwaokoa watu, na sio kuwaongopea na kuwapoteza, au kuwayumbisha. Basi, vitabu vilivyo kwenye Biblia, ni SAFI na vyenye kuchochea na mapendo kati ya watu.

Vimewekwa rasmi vimekubalika na watu, vimetokana na Roho Mtakatifu. Havina mbwembwe, havina madoido, havina chumvi, neno wala jambo la ziada.

Ninamalizia kwa kuonesha uhalali wa kitendo hiki cha kuacha vitabu visivyowafaa watu safi kuingia katika Biblia. Tuikumbuke tukio lile maarufu dhidi ya Idd Amin wa Ugada, tangu 1978, mwishoni mwishoni kidogo hadi 1979.

Wakati wa vita au miaka ya mbele kidogo, watu wengi sana waliamua kuandika juu ya vita, wengine waliandika vitabu, wengine mashairi, wengine insha na hata wengine walifanya katuni na kadhalika.

Kumbe maandishi yote hayo yalitofautiana. Wengine walitia mbwembwe, wengine walitilia chumvi, wengine waliongeza mambo ya kwao na hivyo basi, kutofautiana kukawa ni jambo la kweli.

Basi ikiwa sisi leo tunataka kuchukua maandishi kwa ajili ya kufuindishia watoto wetu, historia halisi ya Tanzania na matendo yake, ni lazima jopo la wanahistoria liyachambue maandishi hayo.

Yaani wachukue vitabu au maandishi yaliyo makini na si yale yanayotiliwa mbwembwe, madoido na chumvi nyingi. Watu hao watayaacha yale mashairi yanayo mwita Idd Amin, NDULI, au JOKA KUKU na PAKA SHUME. Mashairi na vitabu vya namna hiyo, havitavifaa vizazi vya jamii vijavyo; ni lazima viwekwe kando.

Kufanya jivyo itakuwa ni ishara ya uadilifu wa taifa letu na ukweli wa wanahistoria. Ndivyo basi ilivyotokea kwa Injili ya Barnaba. Injili hii ipo na ukitaka unaweza kuiona na kuisoma.

Nenda kwenye maktaba kubwa na uliza vitabu vinavyoitwa APOKRIFA za Agano Jipya kwa maana vipo pia vitabu vya Agano la Kale ambavyo ni Apokrifa vilevile kama vile KUPALIZWA KWA MUSA  KITABU CHA ADAM NA EWA.

Ukiona utakubali kuwa kwa kweli, haikupasa kuchukuliwa na kufanywa kama kitabu cha makini maana mambo yake, hayakiri imani, wala hayachochei mapendo. Hata Wakristo wa mwanzo hawa kubali hayo mambo. 

 

Haki za watoto zisihusishwe na siasa; zilindwe

Na Tiganya Vicent, MAELEZO.

PAMOJA na jitihada za Serikali ya Tanzania, Shirika la Kazi Duniani (ILO) na wadau wengine, kupambana na utumikishwaji watoto katika kazi za hatari, baadhi ya wanasiasa wilayani Iramba, wamekuwa wanapotosha wananchi kwa kudai kuwa hizo ni kampeni za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, katika kuelekea uchaguzi Mkuu hapo mwakani.

Hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa kudidimiza maendeleo ya kampeni ya mapambano dhidi ya tatizo hilo linalowakabili watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

Kwa mujibu wa maelezo ya viongozi wa vikundi vya sanaa vinavyojihusisha na uhamasishaji wa mapambano dhidi ya utumikishwaji watoto wilayani Iramba, wamekuwa wakikabiliana na vikwazo kutoka kwa wanasiasa wanaodiriki kuwadanganya wananchi kwa kusema kuwa, zoezi la kuwaondoa watoto katika utumikishwaji katika kazi hatari ni sehemu ya kampeni za kisiasa za chama tawala.

Hali hiyo imekuwa ikichangia kuwakatisha tamaa wasanii wanaojitolea kuelimisha jamii dhidi ya mapambano ya tatizo hilo ambalo limeenea kwa kiasi kikubwa wilayani humo.

Mratibu wa Programu ya Muda Maalum wa Kupambana na Ajira mbaya Wilayani Iramba, Bw. Hezron Msule, alisema kuwa, watu hao ni sawa na wauaji, kwani hawana huruma hata kidogo kwa maelfu ya watoto wilayani humo ambao wanapata mateso ya kutumikishwa katika ajira za hatari.

Alisema kuwa, watu hao si wema kwani wanapenda watoto hao waendelee kuwa watumwa wa wenzao wakati watoto wa sehemu nyingine wanapatiwa haki za msingi kama elimu na muda wa kuendeleza vipaji vyao.

Bw. Msule alisema kuwa, kuendelea kuachia tatizo la utumikishwaji kwa watoto, ni sawa na kuendelea kukubali madhara yanayotokana na tatizo hilo kama vile kupata maambukizo ya janga la UKIMWI.

Ni vema wanasiasa hao wakafahamu kuwa, watoto zaidi ya milioni nne nchini, wanatumikishwa katika kazi za hatari zikiwamo biashara ya mapenzi, kazi za nyumbani, mashamba na katika migodi.

Watoto hao wote wako katika hatari ya kuathirika na kudumaza vipaji vyao kwa kukosa elimu na hivyo, kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.

Aidha, watoto wengi walioko katika kazi za hatari, hufanyishwa kazi ambazo hazilingani na umri wao na kukosa muda wa kupumzika, kucheza, kukosa mapenzi ya wazazi au walezi na mara nyingine, unyanyaswaji wawapo kazini.

Mara nyingi watoto wanaotumikishwa, wamekuwa wakipata madhara mbalimbali kama vile kupata mimba katika umri mdogo ambazo huwasababishia matatizo wakati wa kujifungua, kupatwa na magonjwa ya zinaa ikiwemo UKIMWI, kutumia dawa za kulevya, kukua katika hali isiyo ya maadili, kuathirika kisaikolojia na kukosa heshima katika jamii.

Kufuatia hatari hiyo inayowakabili watoto wanaotumikishwa nchini, Serikali ya Tanzania chini ya Chama Tawala cha Mapinduzi, iliamua kuridhia mikataba mbalimbali duniani ya kupambana na ukatili dhidi ya watoto na siyo siasa kama baadhi ya wanasiasa hao wa Iramba wanavyodai.

Ni vema wanasiasa hao pia wakaelezwa na kuelewa kuwa, Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) na imeridhia mikataba miwili ya ILO.

Mikataba hiyo ni pamoja na ule wa Namba138 unaomtaja mtu mtoto kuwa ni yule mwenye umri chini ya miaka 18 na Mkataba Namba 182, unaofafanua kuwa, mtoto wa umri huo hapaswi kuajiriwa katika kazi ngumu na hatari.

Kufuatia utafiti uliofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na ILO, Wilaya ya Iramba ni miongoni mwa wilaya zenye matatizo makubwa ya usafirishaji na utumikishwaji watoto katika biashara ya mapenzi na kazi za ndani.

Katika kutambua ukubwa wa tatizo hilo, Serikali ya Tanzania kwa msaada wa Shirika la kazi Duniani imekuwa ikitumia mikakati mbalimbali kuwaelimisha wanajamii kuunga mkono mapambano dhidi ya biashara zote zinazohusu utumikishwaji watoto.

Mikakati hiyo ni pamoja na uundaji wa vikundi vya hamasa ambavyo vina jukumu la kutumia sanaa kuelimisha jamii madhara ya utumikishwaji watoto na faida za kuwaondoa katika utumwa huo.

Vikundi hivyo vilivyoanzishwa na Idara ya Habari Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), vimeshafanya kazi kubwa ya kuhamasisha jamii katika wilaya 11 ambapo kwa wastani, kila wilaya ina vikundi 14.

Vikundi hivi vimekuwa vinatumia kazi mbalimbali za sanaa kuelimisha jamii madhara ya mtoto kufanyishwa kazi ambazo ni nzito ikilinganishwa na umri wake.

Matokeo ya kazi za sanaa yameanza kuonekana ambapo baadhi ya wazazi wameapa kutowaruhusu watoto wao kuondoka nyumbani kwao kwenda mijini kufanya kazi wanapomaliza elimu ya msingi.

Siyo hivyo tu, Serikali pia inatumia waandishi wa habari kuielimisha jamii na kuhabarisha jamii. Kwa hiyo, kiongozi yeyote anayesimama bila aibu na kusema kuwa vikundi vinatumika katika jamii kuelimisha juu ya mapambano dhidi ya utumikishwaji huo vipo kwa lengo la kupiga kampeini, ni hatari na vinastahili kuogopwa kama ukoma.

Kiongozi kama huyo ni wazi kuwa atakuwa hafai mbele ya jamii ya Watanzania. Kwani tayari anaonesha udhaifu wake wa kiutendaji na hana utu kwa binadamu wenzake, kwa kuwa anaonesha kufurahia utumwa wanaofanyiwa watoto hao katika nchi yao na wengine, waendelee kupata magonjwa mbalimbali kwa tatizo la wajinga wachache.

Mkakati mwingine ambao Serikali imeshachukua ni pamoja na kutunga sheria inayowabana waajiri wa watoto, ambao Rais Benjamin William Mkapa hivi karibuni alitia saini sheria hiyo.

Sheria hiyo imekusudia kukomesha vitendo vyote vya kuwashurutisha watoto kufanya kazi ngumu na za hatari kwao. Hatua nyingine, ni pamoja na kuunda kamati za vijiji za kupambana na tatizo hilo.

Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu duniani, zinazotekeleza programu ya muda maalum ya kuwaondoa watoto katika utumikishwaji wa kazi za hatari, nchi nyingine ni Nepal na ELSalvador.

Programu hiyo inafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambapo kwa upande wake, Serikali ya Tanzania inakusudia kwamba hadi kufikia mwaka 2010, watoto wote wawe wameondolewa katika utumikishwaji nchini.

Programu hiyo ni moja ya shughuli za serikali zisizohusika na siasa bali zenye lengo la kuokoa maisha ya watoto. Hivyo, ni vema wanasiasa wakaacha kuchanganya siasa na shughuli za maendeleo ya jamii, kwani wanawapotosha wapiga kura wao katika mambo ambayo yana manufaa sio kwa watoto, bali kwa Watanzania wote.

Watoto hao walioko katika utumikishwaji ndio hao wanaotarajiwa kuwa wanachama wa siku za baadaye na viongozi wa vyama hivyo. Hivyo, siyo vizuri kuwaacha waangamie kwa utashi wa watu wanaojifunza siasa.

Ni vema pia wakasema ukweli juu ya mazuri yanayoridhiwa na serikali kwa manufaa ya nchi na wanachama wake. Upinzani sio ubishi wa kupinga kila kitu, bali ni ukosoaji unaolenga kujenga na sio kubomoa.

Ni ukweli usiofichika kuwa, vita dhidi ya utumikishwaji watoto ni miongoni mwa juhudi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu. Lakini, ni vema wanasiasa wanaoubeza mpango huo wakaelewa kuwa watoto hao wanaotumikishwa si wanachama wa CCM.

Vita dhidi ya utumikishwaji isichanganywe na siasa. Ni vema wanasiasa hao wakaviacha vikundi hivyo vya sanaa vifanye kazi waliyotumwa na jamii ili watoto waje kufurahia maisha yao hapo baadaye.

Ni vema viongozi hao wa vyama vya siasa wilayani Iramba, wakaelewa kuwa ziko wilaya nyingine kama vile Ilala, Kinondoni, Temeke, Kondoa, Urambo, Arusha, Simanjiro,Arumeru, Mufindi na Iringa Vijijini, ambapo wananchi wa huko wameshaliona tatizo linalowakabili watoto, ni la jamii na wala siyo la chama fulani, na hivyo wameungana katika mapambano hayo.

 

COLLETA; Shule ya msingi iliyozingatia elimu kwa wote

l        KAPTENI KOMBA: Marehemu                         alituusia kuwajali yatima

Na Lilian Nyenza.

MATOKEO ya mtihani wa darasa la saba yaliyotangazwa Desemba 2004, yameifanya shule binafsi ya msingi ya Kumbukumbu ya Colleta ya jijini Dar es Salaam, kuingia katika kitabu cha maajabu baada ya wanafunzi wake wote kufaulu kuingia sekondari isipokuwa mmoja tu.

Shule hiyo, pamoja na ile ya sekondari ya Bakili Muluzi inayomilikiwa na msanii maarufu na mwanasiasa wa siku nyingi, Kapteni Mstaafu John Komba, imeshika nafasi ya sita kwa Wilaya ya Kinondoni na 11 kwa mkoa wa Dar es Salaam katika matokeo hayo.

Wanafunzi hao waliofaulu ni wa kwanza tangu kufunguliwa kwa shule hiyo, iliyoko Mbweni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na ni mara ya kwanza pia kuwa na wanafunzi wa darasa la saba.

Matokeo hayo ndiyo yamewafanya wazazi na wananchi kujiuliza kuwa, chanzo kikubwa cha mafanikio ya haraka ya shule hiyo ni nini.

Shule ya Kumbukumbu ya Colleta inamilikiwa na Kapteni Komba kupitia taasisi ya Educate Girls ambayo pia inamiliki shule ya awali na Sekondari iliyoanzishwa rasmi mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi hivi karibuni na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bw. Frederick Sumaye.

Lengo kuu lilikuwa kuwaelimisha watoto wa kike ambao hapo nyuma, waliwekwa pembezoni katika usawa wa elimu.

Mkurugenzi huyo anasema, msukumo wa kuanzisha shule hizo ulitokana na wosia wa Marehemu Mama Colleta ambaye alikuwa mama mkwe wake ambaye kabla hajafa, aliwaagiza kuwatunza na kuwasaidia watoto yatima.

“Wakati wa uhai wake Mama Colleta aliwapenda sana watoto hasa waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu akiwahudumia kwa hali na mali, hali iliyosababisha kutuachia wosia kwamba, tuendelee kuwatunzwa na kuwapenda watoto yatima,” alisema Kapteni Komba na kuongeza kuwa, mama huyo alifariki dunia mwaka1995.

Aidha, Mkurugenzi huyo alisema mbali na wosia wa mama huyo, alipata nguvu baada ya kupewa wazo la kuanzisha shule hizo na aliyekuwa Rais  wa  Malawi Dk. Bakili Muluzi ambaye pia alitoa msaada wa hali na mali katika ujenzi wa shule hizo.

“ Ametoa karibu theluthi mbili ya gharama za ujenzi wa shule hizi,” anasema Kapteni Komba.

Kutokana na changamoto hizo, taasisi hiyo ilijiwekea malengo makubwa manne ambayo yalikuwa ni kuanzisha shule ya chekechea, msingi, sekondari na chuo cha ualimu.

 “Matatu kati ya hayo tumeweza kuyatimiza katika miaka saba ya uhai. Tumefanikiwa kuanzisha shule za chekechea, shule ya msingi pamoja na sekondari. Mipango ipo njiani ili kuhakikisha tunaanzisha chuo cha ualimu,” anasema.

Anasema ujenzi wa shule ya msingi umekamilika na tayari mwaka huu umeanza kutoa zao la kwanza la darasa la saba, wakati ujenzi wa shule ya sekondari iliyopewa jina la Bakili Muluzi kwa heshima ya Rais wa zamani wa Malawi, ikiwa imefanikiwa kupata wanafunzi wa kidato cha pili.

Kwa sasa, shule hizo zina jumla ya wanafunzi 23 wa chekechea, shule ya msingi wanafunzi 91na shule ya sekondari  wanafunzi 50,” Kati ya wanafunzi hao, tunao wale ambao ni yatima na wamefiwa wazazi wao kutokana na ugonjwa wa UKIMWI.

Kwa mujibu wa Kapteni Komba, idadi ya wanafunzi hao yatima ni 30, kati yao 20 wakiwa wasichana. “ Tunawapatia watoto hawa huduma zote kuanzia ada, chakula, usafiri pamoja na vifaa vya shule pasipo malipo yoyote,” anasema.

Pamoja na kujengwa nje kidogo na mji na wanakotoka watoto wengi wanaosoma katika shule hiyo, uongozi umetafuta usafiri ambao huwachukuwa na kuwarudisha wanafunzi kutoka nyumbani kila siku za masomo, wakati mipango ikifanywa ili shule hizo ziwe za bweni.

Ili kutimiza haja hiyo, ujenzi wa hosteli umeanza ambapo benki ya CRDB imeahidi kuwapa mkopo ili ifikapo Aprili, 2005 huduma ya kuwalaza wanafunzi shuleni hapo iweze kuanza.

Uongozi wa shule hizo una mpango wa kujenga zahanati itakayotoa huduma za afya kwa wanafunzi, baada ya kuahidiwa na Kanisa Katoliki Jimboni Dar es Salaam msaada wa wafanyakazi wa afya wakiwemo masista.

Hata hivyo, Kapteni Komba alisema pamoja na mafanikio hayo, shule inakabiliwa na matatizo kadhaa yakiwemo kukosekana kwa hali ya usalama ambapo watu wanaohisiwa kuwa majambazi, wamewahi kuvunja na kuiba vifaa kadhaa vya shule vikiwemo televisheni tatu na kompyuta  tano.

Kutokana na tatizo hilo, uongozi wa shule hiyo umeiomba Serikali  kuwaruhusu kujenga kituo kidogo cha polisi kwa gharama za shule na iwapatie askari wa kulinda usalama wa eneo hilo kwa nyakati zote. Aliwaomba wafadhili kuisaidia shule kujenga uzio {ukuta} kuzunguka shule zao.

Shule hizo bado zinakabiliwa na uhaba wa chakula, vitabu, viwanja vya michezo na vifaa vyake na kuomba wafadhili wajitokeze na kuwasaidia kutatua tatizo hilo.

“Tatizo sugu ni maji ambayo hatuyapati na tunaiomba Serikali iliangalie tatizo hilo,” alisema.

Katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu Fredrick Sumaye alikubali ombi la kuwa mlezi wa shule hizo na kuongeza kwamba, yeye kama mkereketwa mkuu wa elimu haoni sababu za kusita kuwa mlezi.

Bw. Sumaye aliahidi kufuatilia kwa karibu matatizo ambayo yanakikabili kituo na kuyapatia ufumbuzi wa haraka.