Make your own free website on Tripod.com

Askofu aichachamalia Serikali

l  Wawekezaji wanawanyanyapaa raia

l  Dola inakejeli Katiba;Utawala wa sheria ‘umekufa’

 

Na Josephine Nsolo

UVUNJAJI wa Sheria unaofanywa na baadhi ya watu dhidi ya raia wengine, ni kinyume na madai ya Serikali kuwa Tanzania inafuata misingi  ya utawala bora na sheria; amesema ASkofu Agustino Shao wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar. Aidha, Mhashamu  Shao, ameijia juu Serikali akidai vurugu katika chaguzi, unyanyasaji wa wawekezaji dhidi ya raia na uharibifu wa mimba ni matunda inayovuna Tanzania kwa kutowajibika viongozi wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyolifikia KIONGOZI, Mhashamu Shao aliyasema hayo katika maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi yaliyofanyika kitaifa Jimboni Zanzibar.

Alisema katika kipindi hiki sherehe hizo zimesongwa na wasiwasi kwani furaha iliyopo nchini na duniani kote ni tofauti na iliyotarajiwa kwa kuwa imesongwa na hofu ya vurugu na ukosefu wa amani.

Askofu Shao alisema kwa kuwa uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu, kila mmoja anawajibika kuulinda, kuuheshimu na kuuenzi ,“….Je, ni kwa namna gani tunauenzi na kuutunza Uhai ? Kitendo cha vyombo vya dola kusajili vituo vya kuharibu na kuondoa uhai kwa kisingizio cha UZAZI WA MAJIRA ,ni kinyume cha sherehe za leo,” alisema.

Akaongeza, “Nchini mwetu leo kuna utitiri wa vituo vya uzazi wa majira na shughuli kubwa za vituo hivi ni kuharibu Uhai. Sera ni kwamba, kadiri wanavyoweza kutoa dawa nyingi za kuharibu mimba au kusitisha mimba, ndivyo wanavyojipongeza na kuzawadiwa na wale walio watuma”.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alisema kuwa, kitendo cha Serikali kufumbia macho vitendo hivi ni kutowajibika na kufanya Katiba ya Nchi inayolinda uhai wa raia, kuwa kejeli.

“Enyi viongozi wetu, si kila linalofaa pale China, Amerika au Ulaya, linafaa pia Tanzania… Jueni kwamba, mamlaka yoyote ina uwezo wa kugeuza mabaya kuwa mazuri, lakini hamna ruhusa yakuyafanya mazuri kuwa mabaya,” alisisitiza ubaya wa vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya Uhai.

Aidha, Askofu Shao alisema inasikitisha kuona hivi sasa kipimo cha haki za raia si uraia wa mtu na ubinadamu wake, bali chama cha siasa, dini, kabila na uwezo wake kiuchumi hali aliyosema, ni hatari.

“Hata kitendo cha wana usalama kuingilia mahakama ni ashirio wazi la kutokuwa na utawala wa sheria,” alisema na kuongeza kuwa, mfano mzuri ni waamini Wakristo wa Kiuyo Pemba walionyimwa na vyombo vya dola, haki ya kusali katika kanisa lao baada ya Mahakama ya Mwanzo kuamua kinyume.

“Je, huo ndio utawala bora wa sheria? Ni zaidi ya miezi kumi sasa tangu ajali ya gari la skuli ya Tomondo kugongwa, hakuna kesi kwani aliye sababisha ajali hiyo ni mzito kiuchumi. Mnyonge akimbilie wapi? Na hali kama hii itaendelea hata lini?” Alihoji na kusisitiza kuwa, ni wajihu wa kila Mtanzania kulinda haki za wote wakiwamo wanyonge.

Akaongeza, “Mboni ya utawala wa sheria ni HAKI kwa wote na uwajibikaji wa vyombo vilivyopewa jukumu la kutekeleza hayo. Kutowajibika kwa vyombo dola athari zake ni kubwa na za hatari.”

Mintarafu matukio ya vifo yaliyotokea katika zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Tanzania Bara na uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu huko Kusini Pemba, ni matunda ya kutowajibika kwa waliokabidhiwa jukumu hilo.

“Kitendo cha kuwaweka raia katika vituo vya kupiga kura kwa muda kwa sababu za uzembe au ubinafsi, ni kinyume cha utawala wa sheria na demokrasia hivyo, Kanisa lina laani kwa hali zote, umwagaji damu uliotokea huko Pemba na Dar es Salaam na linaagiza wahusika wawajibishwe kisheria,” alisema.

Alionya dhidi ya propaganda za kuwagawanya Watanzania kwa nadharia za Uzanzibari na Uzanzibara na kusema kuwa, vitendo vya kutishia raia juu ya haki ya kujiandikisha kupiga kura ni kinyume cha Katiba ya Muungano hivyo, wahusika wawajibishwe.

Aidha, Kiongozi huyo wa kiroho alitahadhalisha kuwa hadi sasa bado nia ya mataifa

makubwa kuzitawala nchi masikini inatekelezwa kwa kasi chini ya mwavuli wa UTANDAWAZI  na UBINAFSISHAJI unaolenga kumiliki njia kuu za uchumi wa nchi.

“Je, nani asiyejua nguvu ya utawala ni uchumi wenye nguvu?…Si kweli kwamba wawekezaji nchini hawafahamu umuhimu wa haki ya kila kuishi kwa jasho lake. Lakini, ni nani anayewahalalishia kwamba mwekezaji ana mahitaji zaidi ya mwenyeji anayemwezesha?” alisema.

Akaongeza, “Mishahara, marupurupu na faida wanayopata wawekezaji ikilinganishwa na wasomi na wahudumu Watanzania, ni kielelezo wazi cha ukoloni mambo leo na muundo endelevu wa matabaka ya watu…..Ili ulimwengu utambue kuwa Mungu tunayemsherehekea leo ni wa wote, vyombo husika vidhibiti unyanyapaa wa raia wanaofanyiwa na wawekezaji,” alisema.     

 

Vyama ‘vyaishitaki’ Serikali kwa viongozi wa dini

l  ‘Mashabiki wanaviponza vyama;      hawaongozeki kama wanachama’

Na Joachim Mushi

VYAMA vya siasa “vimeishitaki” Serikali kwa viongozi wa dini, vikidai kuwa, ndiyo inayosababisha vurugu za kisiasa zinazotokea wakati wa chaguzi kwa kuwa inafanya mambo kinyume na makubaliano.

Katika Mkutano wa Juhudi za Kuimarisha Amani Nchini, kwa mkoa wa Dar es Salaam (Wilaya ya Ilala/Kinondoni) ulioandaliwa na kufanyika katika Hoteli ya Travertine jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa juma, viongozi hao wa vyama vya siasa walisema, Serikali ni chanzo cha uvunjaji wa amani kwa kukiuka taratibu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia dola kwa manufaa ya chama kimoja cha siasa (CCM).

Juhudi za Viongozi wa Dini Kuimarisha Amani nchini ni mpango unaoendeshwa kwa pamoja na   viongozi wa dini kutoka Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA), Jumuiya ya Kikristo Tanzani (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Juhudi hizi zilizoanza mwaka 2003, zinayo ofisi ya kitaifa na ofisi mbili za mikoa ya dar es Salaam na Pwani.

Katibu wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Bw. Hubert Joseph, aliwaambia viongozi hao wa dini kuwa, kuzembea na kushindwa kutekeleza baadhi ya maazimio baina yake na vyama vya siasa, Serikali imesababisha machafuko ya amani pamoja na migogoro iliyojitokeza hasa katika Uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi karibuni kwakushindwa kutekeleza na kutetea, sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa vitendo hususan katika chaguzi.

“Vyama vya siasa tunapokaa na Serikali na kutoa mapendekezo juu ya kipi kifanyike ili kulinda amani nchini, Serikali imekuwa ikikubali kwa mdomo tu, lakini haitekelezi, sasa kama hali hii itaendelea hivi, amani ya nchi yetu ni wazi itakuwa rehani,” alibainisha Joseph.

Naye Katibu wa NCCR-Mageuzi Wilaya ya Kinondoni, Rajabu Kazimoto alikilalamikia Chama Tawala (CCM) kwa madai kuwa, kinaenea uzushi kuwa vyama vya upinzani vinatishia kuvunjika kwa amani nchini.

Alisema dola ni chombo cha umma, hivyo haipaswi kukisaidia chama chochote kupiga kampeni au kukijengea mazingira ya kukiwezesha kushinda katika u wowote ukiwamo Uchaguzi Mkuu wa Wabunge na Rais, unaotarajiwa kufanyika Oktoba Mwaka huu.

Kwa upande wa Chama Tawala CCM, Naibu Katibu Msaidizi Wilaya ya Kinondoni Bw. Mwendwa Ikuu alisema lugha zinazotumiwa na baadhi ya wanasiasa hususan wa upinzani wawapo majukwaani, ndizo zinazosababisha migogoro baina ya vyama, na hatimaye kuzusha balaa na machafuko.

Ikuu alisema viongozi wa vyama vya siasa nchini hawana budi kuwa makini na lugha zao wanapokuwa wanapozungumza na wananchi katika mikutano mbalimbali ikiwamo ya hadhara.

“Lugha za matusi, kashfa na vitisho katika majukwaa ya siasa baina ya chama na chama, serikali na chama kama hazitoepukika, basi tutaendelea kuwa na migogoro na hata pengine kuvunjika kwa amani ya Tanzania pasipo kutegemea,” alisisitiza .

Katika Mkutano huo, Mwenyekiti wa Taasisi ya kuimarisha Amani Tanzania Wilaya ya Kinondoni, Alhaji Suleimani Mwenda, aliwataka Viongozi wa Vyama vya Siasa nchini, kutanguliza utaifa mbele ili kulinda amani nchini.

Alhaji Suleimani alisema, vyama vya siasa havina budi kufuata na kulinda taratibu na sheria za nchi kwa kuwa na wanachama sahihi na si washabiki wa chama.

Alisema kwa kiasi kikubwa, taratibu na maelekezo katika vyama vya siasa huvurugwa na kukiukwa na mashabiki na kwamba, ndio wanaosababisha vurugu na upotevu wa amani katika jamii hasa nyakati za kampeni na mikutano ya kisiasa.

“Chama kinapokuwa na washabiki wengi zaidi ya wanachama, msimamo wake huwa hafifu kutokana na washabiki kutokubali kutii amri za chama na viongozi wao. Mashabiki wapo katika chama ili kuchochea vurugu na kamwe huwezi kuwaongoza,” alisema Alihaji Mwenda.

Aidha, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwaelimisha wanachama umuhimu wa kuheshimu uanachama wao alioulinganisha na namna mtu anavyoabudu na kuitii dini yake.

 

Parokia yazitunuku kanda zilizoshinda uchangiaji

Na Josephine Nsolo

KANISA Katoliki Parokia ya Kimara, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, limewatunukia baadhi ya waamini wake hati maalum za shukrani kutokana na michango yao ya ujenzi wa Kanisa.

Hati hizo zilitolewa kwa waamini hao Jumapili iliyopita na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Fransis John, zilienda kwa waamni wa Kanda nne, kati ya nane zilizochanga kiwango kikubwa cha fedha kwa mwezi Desemba.

Kwa mujibu wa paroko huyo, kanda iliyoshika nafasi ya kwanza katika uchangiaji huo unaofanywa kila wiki kwa njia ya kuzishindanisha ni Kanda ya Stop- Over iliyochanga shilingi 6,750,000/- ikifuatiwa na Kanda ya Kanisani iliyotoa shilingi 592,000 huku Kanda ya Jeshini ikichukua nafasi ya tatu kwa kutoa shilingi 572,000. Kanda iliyoshika nafasi ya nne na kujipatia hati hiyo ni Tanesco iliyotoa  shilingi 540,000/-.

Kanda nyingine zilizoshiriki ingawa hazikupewa hati ni Korogwe A, Korogwe B, Bonyokwa na Kigango cha King’ongo.

Padri Francis alisema kuwa, Uongozi umetoa hati hizo kama ishara ya shukrani kwa waamini hao na kuwatia moyo katika kazi ya ujenzi wa kanisa hilo linalojengwa kwa nguvu za waamini.

“Tumefarijika na moyo wa waamini wetu kwa kubuni mbinu kamambe za uhamasishaji wa kila wiki uliotusaidia kukusanya wastani wa shilingi 800,000/= kila wiki, tofauti na shilingi 70,000 hadi 100,000/= zilizokuwa zikikusanywa hapo awali,” alisema.

Paroko alisema Uongozi wa Kanisa hilo uliwashirikisha waamini waliogawanywa katika kanda nane, kuchangia angalao shilingi 1,000/=  kila wiki ili kusukuma zaidi upatikanaji wa fedha za ujenzi.

“… Wapo waamini ambao wamejitoa kikamilifu na huchangia hadi shilingi 70,000/= kila wiki na wengine ingawa uwezo wao mdogo, lakini wanajitolea kwa kile kidogo walichonacho,” alisema.

Hata hivyo, alisema baadhi ya waamini bado ni wagumu na kutoa michango yao. “Lakini hatuwezi kukata tamaa, tutaendelea kuwahamasisha,” alisema.

‘Yesu Kristo sio Nabii Issa bin Mariamu’

Na Mwandishi Wetu

WAKRISTO wametakiwa kuielewa vizuri imani yao pamoja na imani za dini nyingine zinazoonekana au kusemekana kuwa na uhusiano na Ukristo.

Wito huo uliotolewa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kristo Mfalme Tabata, Padri Gabriel alipokuwa akihubiri katika misa ya tatu katika sikukuu ya Noeli (Krismasi).

Wito huo wa Padri Gabriel umekuja kutokana na mchanganyiko kuhusu kufanana au kutofautiana kati ya Bwana Yesu Kristo katika Biblia na Nabii Issa bin Mariamu katika Kurani.

Katika mahubiri hayo yaliyogeuka kuwa darasa na kuvuta usikivu na umakini wa waamini, kiongozi huyo wa dini alisema kuwa Bwana Yesu Kristo na Nabii Issa ni wawili tofauti kabisa kutokana na vigezo kadhaa.

“Tulipoambiwa kwamba Yesu Kristo ndiye Nabii Issa sisi tukakubali tu. Hapo tulikuwa tumepotoka. Unakuta Mkristo anaambiwa kwamba nyie mnasherekea Issa ambaye sio Mungu anakasirika na kutaka kupigana, kumbe sio kweli ni ukosefu wa elimu tu,” alisema.

Alivitaja vigezo hivyo kuwa ni ukoo, utume, mahali na namna walivyozaliwa, maana ya majina yao pamoja na ukoo wa Mariamu ambavyo kila kimoja kinaonekana kuwa tofauti kabisa.

Juu ya kigezo cha ukoo, Padri Gabriel alisema kuwa wakati Biblia Takatifu inaonesha kuwa Yesu alizaliwa kutokana na ukoo wa Mfalme Daudi ambaye alitokana na mmoja wa watoto kumi na wawili wa Israel (Yakobo) aliyeitwa Yuda, Kurani kwa upande wake inaonesha kuwa Nabii Issa bin Mariamu alitokana na ukoo wa Haruni ndugu yake Musa.

“Utume wao sasa, wakati Bwana Yesu Kristo alikuja kutafuta na kuokoa kilichopotea (kuokoa watu na dhambi zao), Issa bin Marimu alikuja kufundisha watu namna ya kumwabudu Mungu na kuamini torati na baadaye, akateremshiwa Kurani; yaani alikuja kuwafundisha watu dini,” alisisitiza.

Kwa upande wa namna walivyozaliwa, Biblia inasema kuwa Bwana Yesu Kristo alizaliwa katika mji wa Bethlehem nchini Israel, wakati wa usiku na katika zizi la ng’ombe; huku Kurani ikisema kuwa, Issa bin Mariamu alizaliwa chini ya mti wa mtende wakati wa mchana nchi na mahali alipozaliwa havijulikani.

Kuhusu maana ya majina yao, Padri Gabriel alisema kuwa jina Yesu linatokana na neno la Kiebrani ‘Yehosua’ lenye maana ya mwokozi au mkombozi; wakati Issa ni neno la Kiarabu lenye maana ya wekundu uliochanganyika na weupe yaani zeruzeru au albino.

Alisema katika Biblia zilizoandikwa kwa Kiarabu jina Yesu linajulikana kama ‘Yasu’ na sio Issa kama Waislamu wanavyodai na kama Wakristo walivyoaminishwa kwa muda mrefu.

Alisema katika Kurani, jina Yasu lipo lakini huwa hawasemi kama lipo bali wanasisitiza Issa tu, ambaye whana uhusiano wowote na imani ya Kikristo.

“Ndugu zangu ni muhimu kuyaelewa mambo haya vizuri ili tuheshimu imani na dini za wenzetu ili nao waheshimu imani zetu. Wao wana haki ya kuheshimu imani yao na sisi pita tunapaswa kuwaheshimu,” alisema.

Wito huo wa Padri Gabriel ulikuja siku chache baada ya kuripotiwa habari kwamba baadhi ya waamini wa dini za Kiislamu na Kikristo walishambuliana na kupigana baada ya kudaiwa kukashifiana huko Tabata Kimanga na kuvunja hali ya amani.

Wanasiasa wanageuza siasa biashara - Mbunge

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk. George Nangare, amesema miongoni mwa matatizo yanayoikabili Tanzania, ni baadhi ya wanasiasa kuigeuza siasa kuwa biashara huku wengine, wakiwamo wa Chama Tawala, kudhani bado wako katika mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Dk. Nangare aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari,  Ilala Dar es Salaam juu ya hali ya kisiasa wakati huu ambao Tanzania inaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, Oktoba 2005 .

Alisema kutokana na baadh ya wanasiasa kubweteka mawazo yao katika mfumo wa siasa wa chama kimoja ambao Tanzania iliupa mgongo mwaka 1992, ipo haja kwa jamii kupewa elimu zaidi ya uraia kuanzia ndani ya vyama vya siasa na katika sehe mu mbalimbali.

“Hata hizi vurugu zinazotokea katika chaguzi; tatizo ni kwamba kuna watu hata ndani ya CCM ambao bado mawazo yao yanaamini one party system mpaka sasa… Na wanasiasa wengine wanageuza siasa kuwa biashara badala ya utumishi wa umma,” alisema katika mazungumzo hayo baada ya mahafari ya hivi karibuni chuoni DSJ.

Hata hivyo alisema kuwa, vurugu zinazojitokeza katika masuala ya kisiasa hususan wakati wa uchaguzi, zinatokana na uchanga wa kidemokrasia uliopo miongoni mwa jamii hivyo, akashauri Watanzania kubadilika na kukomaa kisiasa ili kwenda na wakati.

“Demokrasia ni changa sehemu nyingi duniani na hii ndiyo maana hakuna uchaguzi kamili duniani, lakini kwetu Watanzania lazima tujitahidi kuonesha ukomavu wetu. Inapotokea kutoelewana, watu wazungumze na kupata suluhisho kwa amani,” alisema Dk. Nagare.

Aidha, katika mazungumzo hayo Dk. Nangare alisisitiza kuwa, jukumu la kuzisaidia taasisi mbalimbali nchini ni la umma mzima, lakini lazimaSerikali iongoze hali hiyo.

Alikuwa akijibu swali lililotaka maoni yake kuhusu taasisi mbalimbali kuichangia Timu ya Soka ya Serengeti Boys ili ishiriki michuano ya kimataifa.

Alisema kwa mantiki hiyo, si kwamba kila kitu Serikali ifanye peke yake, bali Watanzania wajue wana haki, hiari na wajibu kuziunga mkono taasisi zinazowawakilisha kitaifa na kimataifa.

Dk. Nangare alisema, “Mwendo huu ni mzuri, lakini Serikali iweke mipango mizuri ili isiwe kwamba kila taasisi inajiamria kufanya inavyotaka bila kontroo.”

Alisema, Serikali kupitia wizara zake, itenge bajeti kwa vikundi vyote muhimu ili kuepuka tabia ya wawakilishi wa nchi kupitisha bakuri kuomba misaada eti kwa kuwa Serikali haikutenga bajeti.”

 

Papa ampa Umonsinyori Padri Mutabazi

Na Mwandishi Wetu, Rulenge

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amempa Padri Emmanuel Mutabazi wa Jimbo Katoliki la Rulenge, heshima ya Umonsinyori.

Kwa mujibu wa taarifa toka kwa Askofu wa Jimbo hilo Mhashamu Severine NiweMugizi, Baba Mtakatifu alimpa Padri Mutabazi heshima hiyo Mwezi Novemba, mwaka jana nchini Italia.

Mhashamu NiweMugizi amesema, hadi anapata heshima hiyo, Padri Mutabazi (kwa sasa ni Monsinyori), alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Nchi za Mashariki mwa Afrika (CUEA) kilichopo Nairobi, Kenya.

Akielezea historia yake, Askofu NiweMugizi alisema, Monsinyori huyo mpya alizaliwa Julai 15, 1944 huko Runazi- Biharamulo. Baba yake ni Bw. Buswage na Mama ni Bibi Kabengo.

Monsinyori Mutabazi alibatizwa Desemba 24, 1944. Alipata Daraja ya Ushemasi Desemba 12, 1969 na Upadrisho Septemba 13, 1970.

Alipata masomo ya Theolojia katika Seminari Kuu ya Kipapala tangu mwaka 1967 hadi 1970, kisha akaenda katika Chuo cha Urbaniano  Roma kwa masomo ya Theolojia tangu mwaka 1971 hadi 1972. Pia, alipata masomo ya Biblia huko Roma tangu 1972 hadi 1975.

Mwaka 1970, aliteuliwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Nyaishozi na mwaka 1971, akatumikia wadhifa huo parokiani Ntungamo. Januari 1976 hadi Agosti mwaka huohuo, alikuwa Paroko Msaidizi katika Parokia ya Rulenge na kisha, akaendelea na wadhifa huo katika Parokia ya Nyakahura tangu mwaka 1976-1977.

Alikuwa Mwalimu wa Biblia katika Seminari Kuu ya Kipalapala tangu mwaka 1978 na mwaka 1979 hadi 1980, alikuwa akifundisha Biblia katika Seminari Kuu ya Segerea.

Alikuwa Mkuu wa Seminari (Rekta) ya Kibosho tangu mwaka 1981 hadi 1983 na akaendelea na wadhifa huo katika Seminari ya Ntungamo tangu mwaka 1984 hadi 1986.

 Januari 1987 hadi Septemba 1994 alikuwa Mwalimu katika Seminari Kuu ya Segerea na tangu 1994 hadi 1997, alifanya kazi katika Parokia ya Buziku akiwa Paroko, Mkurugenzi wa Utume wa Biblia na Katibu wa Ekumene.

Septemba 1997 hadi Agosti 1998, alikuwa Mlezi katika Nyumba ya Malezi ya Chabalisa, Msimamizi wa Utume wa Biblia na Katibu wa Ekumene.