Make your own free website on Tripod.com

Chuki dhidi ya wayahudi yaongezeka duniani

 

WASHINGTON, D.C. Marekani

 

KUONGEZEKA kwa idadi ya Waislamu katika nchi za Magharibi mwa Ulaya, wengi wao wakiwa maskini na wasio na elimu, kumetajwa kuchangia kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi katika maeneo hayo.

Ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliyotolewa kwa Bunge la Congress imesema kuwa, makundi yenye mrengo wa kulia bado yanachangia kiwango kikubwa cha mashambulizi dhidi ya Wayahudi pamoja na mali zao, ilisema ripoti hiyo.

Katika mashariki mwa Ulaya, makundi mengi yenye itikadi kali pamoja na wanachama wengine wa matawi ya kisiasa yanawajibika kwa matukio mengi ya kuwashambulia Wayahudi, ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Associated Press.

Nchini Urusi, Belarus na katika nchi nyingine zilizokuwa chini ya Umoja wa Soviet, chuki dhidi ya Wayahudi imebaki kuwa tatizo kubwa, pamoja na matukio ya hivi karibuni yaliyotekelezwa na makundi ya itikadi kali, kwa mujibu wa taarifa.

“Utambulisho wa Wayahudi kama wavurugaji wa uchumi wa ulimwengu, unaendelea kutoa sababu nzuri za kuchochea chuki dhidi ya Wayahudi,” ilisema ripoti hiyo.

Mjumbe Tom Lantos, wa chama cha Democratic kutoka California ambaye alishinikiza kutolewa kwa ripoti za kila mwaka kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na ufuatiliaji wa karibu kupitia kwa ofisi mpya, alikaribisha ripoti hiyo ya kidunia juu ya chuki dhidi ya Wayahudi.

“Ni mwanzo tu,” alisema Lantos, kiongozi mkuu wa Democrat katika kamati ya Baraza la Wawakilishi la Marekani. “Wizara ni lazima ichukue hatua haraka kuteua wakili wa kiwango cha juu na mzoefu ili kuratibu juhudi za serikali yetu kukabiliana na mlipuko wa kisasa wa vurugu za chuki dhidi ya Wayahudi.”

Ripoti hiyo ambayo ilizungumzia kipindi kati ya Julai 2003 mpaka Disemba 2004, haikutoa takwimu za ulimwengu mzima, lakini pia ilijumuisha takwimu zilizotolewa na baadhi ya nchi.

“Kuna idadi ndogo ya Wayahudi katika maeneo ya Kaskazini mwa Afrika na Mashariki ya Kati, isipokuwa Israel na kuna matukio machache yanayohusisha Wayahudi kwa kuhusisha walio katika maeneo hayo. Lakini Syria inapuuza na kuunga mkono chuki kubwa dhidi ya Wayahudi kwa vile vyombo vya habari vinavyoungwa mkono na serikali vinaionesha Israel na viongozi wake kama mashetani,” iliongeza kusema ripoti hiyo.

Nje ya Ulaya na Mashariki ya Kati, pia kuna maelezo na maneno ya kutisha ya chuki dhidi ya Wayahudi.

Nchini Pakistan, ambapo hakuna jumuia ya Kiyahudi, chuki dhidi ya Wayahudi inayoshinikizwa na makala nyingi katika vyombo vya habari, imeanza katika siku za hivi karibuni.

Barani Ulaya ambapo mamilioni ya Wayahudi waliuawa katika Maangamizi (Holocaust), vitendo vya chuki dhidi ya Wayahudi vimeongezeka katika ukubwa na mtapakao tangu mwaka 2000 imeonesha ripoti hiyo.

Aidha ripoti hiyo ya serikali ya Marekani, imesema hali ya usalama na ulinzi kwa jumuia za Kiyahudi imevurugwa.

Ilisema jambo linalochangia sana katika mwelekeo huo ni kuongezeka kwa idadi ya Waislamu wenye chuki ya muda mrefu katika taifa la Israel na Wayahudi pamoja na maendeleo ya hali ya mambo nchini Israel hasa katika maeneo yanayokaliwa na Iraq.

Barani Ulaya na katika maeneo mengine ya ulimwengu, serikali nyingi zimeendelea kutambua chuki dhidi ya Wayahudi na zimeongea kupinga suala hilo.

Nchi kama Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani, zimechukua hatua mwafaka kupinga chuki dhidi ya Wayahudi na zimeongeza ulinzi kwa jumuia za Kiyahudi pamoja na mali zao, ilisema ripoti.

Mkurugenzi wa kitaifa wa Umoja wa Kupinga Udhalilishaji, Abraham H. Foxman alisema, Marekani inapaswa kupongezwa kwa uongozi wake katika kutambua ukweli kuhusu tatizo hilo, ambalo aliliita chuki ya zamani ya Wayahudi na itikadi kali mpya za Waislamu zinazolilia chuki kwa Wayahudi.

“Ni wazi katika kutambua hali inayobadilika ya asili na kitisho ya chuki dhidi ya Wayahudi, uhusiano wake, na kuonesha Israel na Wayahudi kama mashetani,” alisema Foxman katika taarifa.

Alisema Marekani iko moja kwa moja zaidi katika kuhusianisha chuki dhidi ya Wayahudi na kuongezeka kwa wanaharakati wa Kiislamu barani Ulaya na sio mgogoro kati ya Waarabu na Israel.

 

 

Baba Mtakatifu aombea wahanga wa Tsunami

 

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alifunga mwaka 2004, akimshukuru Mungu kwa baraka za mwaka na kuadhimisha misa ya mkesha kwa kuombea walioathiriwa na janga la mawimbi ya Tsunami na tetemeko la ardhi barani Asia.

Katika mahubiri mafupi baada ya kuimba “Te Deum,” ambayo kidesturi huimbwa mwisho wa mwaka, Baba Mtakatifu alisema, “Mwaka mwingine unafikia mwisho. Tukitambua namna muda unavyokwisha kwa haraka, tumekusanyika hapa jioni ya leo kumshukuru Mungu kwa baraka na faida zote ambazo ametujalia katika mwaka huu 2004.”

“Kwa pamoja tumshukuru Mungu kwa kutuonesha wema na huruma zake ambazo kwazo ameisindikiza safari ya mji wetu katika miezi hii,” alisema Baba Mtakatifu katika ibada ya mwisho wa mwaka katika Kanisa Kuu la Mt. Petro na kuongeza, “Ninamwomba alete ukamilifuwa  kila juhudi za kitume na kila kazi njema tuzitendazo.”

Katika ibada hiyo, Baba Mtakatifu aliongea kwa sauti yenye nguvu na inayosikika vizuri zaidi ya siku zilizotangulia. Alihitimisha kwa kumwomba Mungu kwa maombezi ya Bikira Maria, aijalie  dunia kipawa cha amani.

Saa chache baadae, usiku wa manane Baba Mtakatifu aliadhmisha Misa katika kikanisa chake binafsi kwa ajili ya wahanga wa mawimbi ya Tsunami yaliyotokea Kusini Mashariki mwa Asia, hiyo ni kwa mujibu wa msemaji wa Vatican, Dk. Joaquín Navarro Valls.

Alisema Baba Mtakatifu aliziombea familia zote za waathiriwa na wale wote wanaoteseka kwa matokeo ya maafa haya pamoja na wale wote wanaojitahidi kuondoa mateso makubwa ya watu walioathirika.