UJUMBE WA BABA MTAKATIFU YOHANE PAULO II KWA AJILI YA
KUADHIMISHA SIKU YA AMANI DUNIANI JANUARI 1, 2004
MSISHINDWE NA UOVU BALI
MUUSHINDE UOVU KWA WEMA
1. MWANZONI mwa
Mwaka Mpya, kwa mara nyingine tena nawahutubia viongozi wa mataifa na watu wote
waume kwa wake wenye mapenzi mema, ambao wanatambua haja ya kujenga amani
duniani. Kwa ajili ya Siku ya Amani Duniani ya mwaka huu 2005 nimechagua maneno
ya Mtakatifu Paulo kwa Waroma: “Msishindwe na uovu, bali muushinde uovu kwa
wema” (12:21). Kamwe uovu haushindwi kwa uovu; mara njia ya namna hiyo
inapofuatwa, badala ya kuushinda uovu, mtu atajikuta badala yake anashindwa
na uovu.
Mtume
mkuu anafichua ukweli wa msingi: amani ni matokeo ya mapambano ya muda mrefu na
magumu ambayo ushindi unapatikana tu pale uovu unaposhindwa kwa wema. Iwapo
tutashangaa matukio ya vurugu na migogoro katika sehemu mbalimbali za
ulimwengu, na matukio yasiyosemeka ya mateso na ukosefu wa haki ambayo
yamesababishwa na migogoro hiyo, chaguo pekee la kweli na lenye kujenga ni,
kama Mtakatifu Paulo anavyopendekeza, kukimbia kile kilicho kiovu na
kushikilia kwa nguvu kile kilicho chema (rej. Rom 12:9).
Amani
ni wema ambao unapaswa kukuzwa kwa wema: ni
wema kwa watu binafsi, familia, kwa mataifa na kwa watu wote; hata hivyo ni ule
unaohitaji kutunzwa na kuendelezwa kwa maamuzi na matendo yanayosukumwa na
wema. Tunaweza kushukuru kwa ajili ya ukweli wa msemo mwingine wa Mtakatifu
Paulo: “Msilipe uovu na uovu kwa mtu yeyote” (Rom 12:17). Njia
moja ya kutoka kwenye mduara wa maovu wa kulipa uovu kwa uovu ni kukubali
maneno ya Mtume: “Msishindwe na uovu, bali muushinde uovu kwa wema” (Rom
12:21).
Uovu, wema na upendo
2. Kutoka mwanzoni, binadamu wamejua hatari za
uovu na wamepambana kujua mizizi yake na kueleza sababu zake. Uovu sio baadhi
ya nguvu zisizo za kirafiki na zilizopangiliwa zinazotenda kazi ulimwenguni. Ni
matokeo ya uhuru wa binadamu. Uhuru, ambao unatofautisha wanadamu na kila
kiumbe kingine duniani, uko daima katika moyo wa mchezo wa uovu. Uovu daima
una jina na sura: jina na sura za wale wale wanaume na wanawake ambao kwa
uhuru kabisa uuchagua. Maandiko Matakatifu yanafundisha kwamba katika
mapambazuko ya historia Adamu na Eva waliasi dhidi ya Mungu, na Abeli aliauawa
na Kaini, kaka yake (rejea Mwa 3-4). Haya yalikuwa machaguo mabaya
mawili ya mwanzo, ambayo yalifuatiwa na mengine mengi katika karne
zilizofuatia. Kila moja la haya machaguo yana kipimo cha ndani cha
kimaadili, kikihusisha wajibu maalumu wa watu binafsi na uhusiano mhimu wa
kila mtu na Mungu, na watu wengine na uumbaji wote.
Katika
hatua ya kina kabisa, uovu ni kukataa matakwa ya upendo.1 Kwa upande
mwingine, wema wa kimaadili, unazaliwa na upendo, hujionesha wenyewe kama
upendo na unaelekezwa kwenye upendo. Haya yote hasa yako wazi kwa Wakristo,
ambao wanajua kwamba uanachama wao katika Mwili-fumbo mmoja wa Kristo
yanawaweka katika uhusiano maalumu sio tu na Bwana bali pia na kaka na dada
zao. Mantiki ya ndani ya upendo wa Kikristo, ambayo katika Injili ni chanzo hai
cha wema wa kimaadili, inaongoza hata kwa upendo wa maadui wa mtu: “Iwapo
adui yako ana njaa, mlishe; iwapo ana njaa, mpe kitu cha kunywa” (Rom
12: 20).
“Muundo” wa sheria ya maadili ya mahali pote
3. Tukiangalia hali
ya sasa ya ulimwengu, hatuwezi kusaidia isipokuwa kugundua msambao mbaya wa mambo
kadhaa ya kijamii na kisiasa yanayodhihirisha kuwepo kwa uovu: kuanzia
ugomvi hadi vurugu za kijamii na vita, kutoka ukosefu wa haki hadi vitendo vya
vurugu na mauaji. Kuongoza njia kati ya madai yanayokwaruzana ya wema na uovu,
familia ya kibinadamu inahitaji utunzaji na heshima ambayo usimamizi wa
pamoja wa tunu za maadili uliotolewa na Mungu mwenyewe. Kwa sababu hii,
Mtakatifu Paulo anawahamasisha ambao wamedhamiria kuushinda uovu kwa wema kuwa
watu wa haki na kujihusisha katika kukuza ukarimu na amani (rej. Rom
12:17-21).
Miaka
kumi iliyopita, katika kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa juu ya haja ya
dhamira ya pamoja kwa ajili ya huduma ya amani, niligusia “muundo” wa sheria
maadili ya kila mahali,2 ambao juu ya huo Kanisa hutoa mwito katika
matangazo yake kadhaa kwenye eneo hili. Kwa kuvuvia tunu na kanuni za pamoja,
sheria hii huunganisha watu, licha ya tamaduni zao tofauti, na yenyewe
haibadiliki: “inahimili ndani ya mjongeo wa mawazo na mila na husaidia
maendeleo yake … Hata wakati inapokataliwa katika kanuni zake hasa, haiwezi
kuharibiwa au kuondolewa kutoka kwenye moyo wa mtu. Daima huibuka tena katika
maisha ya watu binafsi na jamii”.3
4. Muundo
huu wa pamoja wa sheria ya maadili daima huhitaji dhamira na wajibu mkubwa
katika kuhakikisha kwamba uhai wa watu bifasi na ya mataifa unaheshimiwa na
kuendelezwa. Katika mtazamo huu, maovu yenye asili ya kijamii na kisiasa ambayo
huiathiri dunia, hasa wale watu wanaochokozwa na milipuko ya vurugu,
inalaaniwa kwa nguvu. Mara moja ninalifikiria bara pendwa la Afrika,
mahali ambapo migogoro ambayo tayari imegharimu mamilioni ya wahanga na bado
inaendelea. Au hali ya hatari ya Palestina, Nchi ya Yesu, mahali ambapo
msingi wa maelewano ya pamoja, yaliyoraruliwa na mgogoro ambao kila siku
unalishwa na vitendo vya vurugu na kisasi, haiwezi tena kurekebishwa katika
haki na ukweli. Na vipi kuhusiana na matukio ya kutisha ya vurugu za kigaidi,
ambazo zinaonekana kuwa nguvu inayousukuma ulimwengu wote kuelekea hali ya
baadae ya hofu na mateso? Mwisho ni kwa vipi hatuwezi kufikiria kwa masikitiko
makubwa kuhusu hali inayojiri nchini Iraq, ambayo ambayo imesababisha
hali mbaya za ukosefu wa uhakika na usalama kwa wote?
Ili
kupata wema wa amani ni lazima kuwepo kukiri kwa wazi na kwa kutambua kwamba
matumizi ya nguvu ni uovu usiokubalika na kwa hayatatui matatizo. “Matumizi ya
nguvu ni uongo, kwa vile unakwenda kinyume na ukweli wa imani yetu, ukweli wa
ubinadamu. Matumizi ya nguvu yanaharibu kile yanadai kukitetea: heshima, uhai,
uhuru wa binadamu”.4 Kinachotakiwa ni juhudi kubwa za kulea dhamiri na
kuelimisha kizazi cha vijana kuhusu wema kwa kushikilia kwamba ubinadamu
mzima na wa kidugu ambao Kanisa linautangaza na kuuendelea. Huu ni msingi
kwa ajili ya utaratibu wa kijamii, kiuchumi na kisiasa unaoheshimu thamani,
uhuru na haki za msingi za kila mtu binafsi.
Wema wa amani na mafao ya pamoja
5. Kuendeleza amani kwa kuushinda uovu kwa
wema unahitaji tafakari makini juu ya mafao ya pamoja5 na juu ya maana yake ya
kijamii na kisiasa. Pale mafao ya pamoja yanapoendelezwa katika kila ngazi,
amani inakuzwa. Je mtu binafsi anaweza kupata utimilifu kamili bila kutimiza
asili yake ya kijamii, yaani kuwepo kwake “pamoja na” na “kwa ajili ya”
wengine? Kwa karibu mafao ya pamoja yanamhusu yeye. Kwa karibu yanahusu kila
kila maelezo ya asili yake ya kijamii: familia, mikoa (kanda), madola, jumuia
ya watu na mataifa. Kila mtu, kwa namna fulani, anaitwa kufanya kazi kwa ajili
ya mafao ya pamoja, kuendelea kutazama nje kwa ajili ya mambo mema ya watu
wengine kana kwamba yangekuwa yake mwenyewe. Wajibu huu kwa namna ya pekee ni
wa viongozi wa kisiasa katika kila ngazi, kwa kuwa wanaitwa kutengeneza ule
muhtasari wa masharti ya kijamii ambayo yanaruhusu na kukuza katika watu
maendeleo mazima ya nafsi zao.6
Kwa
hiyo mafao ya pamoja yanahitaji heshima na maendeleo mazima ya mtu na haki zake
za msingi pamona na heshima na uendelezaji wa haki za mataifa katika kila
mahali. Kwa maana hii, Mtaguso wa Pili wa Vatican ulisema “kuendelea kwa hali
ya kutegemeana kwa karibu ambayo polepole inajumuisha ulimwengu mzima
kunasababisha kuongezeka mafao ya pamoja ya kila mahali… na hii inahusisha haki
na wajibu pamoja na heshima kwa jamii yote ya binadamu. Kila kundi la kijamii
ni lazima lazingatie mahitaji na jitihada halali za makundi mengine na mafao ya
pamoja ya familia nzima ya binadamu”.7 Wema wa binadamu kwa jumla, ikijumuisha
vizazi vijavyo, unatoa mwito kwa ajili ya ushirikiano wa kweli wa kimataifa,
ambao kila nchi ni lazima itoa mchango kwa ajili yake.8
Baadhi
ya mitazamo-punguzi ya binadamu inajaribu kuonesha mafao ya pamoja kama hali
ya mafanikio ya kijamii na kiuchumi ikiwa inakosa lengo madhubuti, na hivyo
kuyaondolea maana yake ya kina kabisa. Hata hivyo bado mafao ya pamoja yana
kipengele madhubuti, kwa kuwa Mungu ni mwisho kamili wa viumbe wake wote.9
Wakristo wanajua kwamba Yesu ameangaza nuru kamili juu ya namna mafao ya kweli
ya pamoja kwa ajili ya binadamu yanavyopaswa kufikiwa. Historia inasafiri
kumwelekea Kristo na katika yeye inapata kilele: kwa sababu ya Kristo, kwa njia
ya Kristo na kwa ajili ya Kristo, kila ukweli wa kibinadamu unaweza kuelekezwa
kwenye ukamilifu kamili katika Mungu.
Wema wa amani na
matumizi ya mema ya dunia
6. Kwa kuwa wema wa amani umeunganika
maendeleo ya watu wote kwa karibu, matakwa ya kimaadili kwa ajili ya matumizi
ya mema ya nchi ni lazima daima yazingatiwe. Mtaguso wa Pili wa Vatican kwa
usahihi kabisa ulikumbuka kwamba “Mungu alikusudia ulimwengu na vyote vilivyomo
ndani yake kwa ajili ya matumizi ya kila mmoja na watu wote; ili mambo mema ya
uumbaji vipatikane kwa wote kwa usawa, kwa haki kama mwongozo na upendo katika
uwepo.”10
Kama
mwanafamilia ya binadamu, kila mtu anakuwa raia wa dunia, kama
ilivyokuwa kwa wajibu na haki mfuatano, kwa kuwa binadamu wote wanaunganishwa
na mwanzo mmoja na mwisho mmoja ulio kamili. Kwa kule kuchukuliwa mimba
tu, mtoto ana haki na kustahili matunzo na uangalifu; na mtu fulani ana haki ya
kutoa vitu hivi. Kulaani ubaguzi, ulinzi wa watoto, utoaji wa misaada kwa watu
waliokimbia makazi yao na wakimbizi, na uhamasihaji wa mshikamano wa kimaifa
kwa ajili ya wahitaji wote ni kitu kingine zaidi ya matumizi kamili ya kanuni
za uraia wa dunia.
7. Wema
wa amani unapaswa kuonekana leo kama unahusiana kwa karibu na mambo mema
ambayo ni mapya yanayotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Haya
pia, katika matumizi ya kanuni ya hatima kuu ya mema ya dunia, inahitajika kuwekwa
katika huduma ya mahitaji ya msingi ya binadamu. Juhudi zifaazo katika
ngazi ya kimataifa zinaweza kutoa utekelezaji kamili wa kivitendo kwa kanuni za
hatima kuu ya mema kwa kutoa uhakikisho kwa wote – watu binafsi na mataifa –
masharti ya msingi kwa ajili kushirikishana katika maendeleo. Hii inawezekana
pale vizuizi na ukiritimba vinavyoweka watu pembezoni vinapoondolewa.11
Amani
kama wema itahakikishwa vizuri zaidi iwapo jumuia ya kimataifa itachukua wajibu
mkubwa kwa ajili ya mambo ambayo kwa pamoja yanaitwa mema ya umma. Haya
ni mema ambayo raia wote wanafaidika nayo moja kwa moja, bila kuyachagua au
kuyachangia kwa namna yoyote. Kwa mfano, suala la namna hiyo katika ngazi ya
taifa, ikiwa na mema kama mfumo wa mahakama, mfumo wa ulinzi na mtandao wa
barabara na reli. Katika ulimwengu wetu suala la utandawazi alioongezeka lina
maana kwamba mema ya umma zaidi na zaidi yanachukua tabia ya ulimwengu mzima,
na matokeo yake maslahi ya pamoja yanaongezeka siku kwa siku. Tunahitaji
kufikiria vita dhidi ya umaskini, ukuzaji wa amani na usalama, kushughulikia
mabadiliko ya hali ya hewa na udhibiti wa magonjwa. Jumuia ya kimataifa
inatakiwa kuitikia maslahi haya kwa mtandao mpana mwafaka wa mahakama wenye
lengo la kusimamia matumizi ya mema ya umma na kumotishwa na kanuni kuu
za haki na mshikamano.
8. Kanuni
ya hatima kuu ya wema inaweza pia kufanya makabala fanisi zaidi uwezekane ili
kukabiliana na changamoto ya umaskini, hasa pale tunapofikiria umaskini
mkubwa sana ambamo mamilioni ya watu bado yanaishi. Mwanzoni mwa milenia mpya,
jumuia ya kimataifa iliweka kipaumbele cha kupunguza umaskini kwa nusu mpaka
kufikia mwaka 2015. Kanisa linaunga mkono na kutia moyo dhamira hii na
kuwaalika wote wanaomwamini Kristo kuonesha, upendo mpendelevu kwa maskini12,
kwa vitendo na katika kila sekta.
Janga
la umaskini linabakia kuunganika kwa karibu na suala la deni la kigeni kwa
nchi maskini. Licha ya maendeleo muhimu katika eneo hili, tatizo bado
halijatatuliwa vya kutosha. Miaka kumi na mitano iliyopita nilitoa wito kwa
umma kutazama suala la deni hilo la nchi maskini kwamba “linahusiana kwa karibu
na mfululizo wa matatizo mengine kama vile uwekezaji wa kigeni, utendaji kazi
mzuri wa asasi kubwa za kimataifa, bei ya mali ghafi na mengine.”13 Hatua za hivi
karibuni kutaka deni lipunguzwe, zikiwa zimejikita kwenye mahitaji ya maskini,
kwa hakika zimeboresha ukuaji wa uchumi. Hata hivyo, kwa sababu ya mambo
kadhaa kiwango hiki cha ukuaji wa uchumi bado hakitoshi, hasa kuhusiana na
malengo ya milenia kwa ajili ya maendeleo. Nchi maskini bado zimebaki zikiwa
zimenasa katika mduara wa uovu: kipato kidogo na ukuaji hafifu wa uchumi
unazuia uwekaji akiba, na hivyo uwekezaji hafifu na matumizi yasiyotosha ya
akiba hayasaidii ukuaji wa uchumi.
9. Kama
Papa Paulo wa Sita alivyosema na kama mimi mwenyewe nilivyosisitiza tena, njia
pekee za kuwezesha Mataifa kushughulikia tatizo kubwa la umaskini ni kuyapa
rasilimali muhimu kwa njia ya misaada ya kigeni ya kifedha – ya umma na
binafsi – iliyotolewa chini ya masharti mazuri, ndani ya wigo wa uhusiano wa
biashara ya kimataifa unaosimamiwa kwa haki.14 Kinachotakiwa kwa haraka ni
uhamasishaji wa kimaadili na kiuchumi, ambao unaheshimu makubaliano ambayo
tayari yamefanyika kwa ajili ya kuzisaidia nchi maskini, na wakati huohuo uko
tayari kupitia upya makubaliano hayo ambayo yameonekana kuwa mzigo kwa baadhi
ya nchi. Kwa maana hiyo, msukumo mpya unapaswa kutolewa kwa Msaada wa Umma
kwa ajli ya Maendeleo, aina mpya za kutoa fedha kwa ajili ya maendeleo
zinapaswa kuchunguzwa, bila kujali ugumu wowote wa kazi hiyo.15 Baadhi ya
serikali tayari zinatazama kwa uangalifu mbinu za matumaini kwa ajili ya
kufanikisha suala hili; juhudi hizi muhimu zinapaswa kuchukuliwa katika roho ya
ushirikishanaji wa kweli, kwa kuheshimu kanuni ya ukamilishanaji.
Usimamizi wa rasilimali za fedha unaolenga maendeleo ya nchi maskini unapaswa
pia kuhusisha uangalifu makini, kwa upaned wa wote wafadhili na wapokeaji wa
misaada, kwa hatua muhimu za kiutawala. Kanisa linatia moyo na kuchangia
jitihada. Mtu anahitaji tu kutaja mchango muhimu uliotolewa na asasi nyingi za
Kikatoliki zinazoshughulikia misaada na maendeleo.
10. Mwishoni
mwa Jubilei Kuu ya mwaka 2000, katika Barua yangu ya Kitume Novo Millennio
Ineunte, nilizungumzia juu ya haja ya haraka ya creativity
katika upendo,16 ili kueneza Injili ya matumaini duniani. Haja hii
inaonekana wazi pale tunapofikiria matatizo mengi magumu yaliyopo kwenye
njia ya maendeleo barani Afrika: migogoro mingi ya silaha, majanga ya
magonjwa yanayochochewa na umaskini wa kupindukia, udhaifu wa kisiasa
unasababisha ukosefu mkubwa wa usalama. Hizi ni hali za kutisha ambazo
zinatahitaji mwelekeo mpya kabisa kwa ajili ya Afrika: ipo haja ya kubuni
aina mpya za mshikamano, katika kiwango cha upande mmoja na pande nyingi,
kupitia kwa wajibu muhimu kwa upande wa wote, kwa imani kamili kwamba mafaniko
ya watu wa Afrika ni sharti muhimu kwa ajili ya ufikiaji wa mafao ya watu wote
kila mahali duniani.
Watu
wengi wa Afrika wanakuwa wahusika wakuu wa mustakabali wao wenyewe na maendeleo
yao ya kiutamaduni, kiraia, kijamii na kiuchumi! Ni maombi yangu kwamba Afrika
itakoma kuwa mpokeaji tu wa misaada, na kuwa mpatanishi anayewajibika wa
ushirikishanaji wa matumaini na wenye kuzaa matunda! Ufikiwaji wa lengo hili
unadai utamaduni mpya wa kisiasa, hasa katika eneo la ushirikiano wa kimataifa.
Kwa mara nyingine tena ningependa kutamka kwamba kushindwa kuheshimu ahadi
zinazojirudia za Misaada wa Umma kwa ajili ya Maendeleo, swali ambalo
bado halijatatuliwa la deni kubwa la kigeni la nchi za Afrika na kushindwa
kuzifikiria nchi hizo kwa namna ya pekee mahusiano ya biashara ya kimataifa,
kunawakilisha kizingiti kikubwa kwa amani ambacho kinhitaji kushughulikiwa na
kutanzuliwa kwa haraka kabisa. Leo zaidi ya wakati wowote ule, sharti muhimu kwa
ajili ya kuleta amani kwa ulimwengu kukiri hali ya kutegemeana kati ya nchi
tajiri na maskini, kiasi kwamba “maendeleo ama yanakuwa ya kushirikishana kwa
pamoja na kila sehemu ya ulimwengu au yanapitia mchakato wa kurudia nyuma
kimaendeleo hata yale maeneo yenye maendeleo imara.”17
Mtapakao wa uovu
na matumaini ya Kikristo
11. Mkabala
na hali nyingi za hatari zilizomo ulimwenguni, Wakristo wanakiri kwa tumaini
nyenyekevu kwamba Mungu pekee anaweza kuwapa uwezo watu binafsi na mataifa
kushinda uovu na kupata wema. Kwa kifo na ufufuko wake , Kristo ametukomboa na
kutununua “kwa bei” (1 Kor 6:20; 7:23), na kuleta wokovu kwa ajili ya
wote. Kwa msaada wake, kila mmoja anaweza kushinda uovu kwa wema.
Kwa
msingi wa uhakika kwamba uovu hautashinda, Wakristo wanakuza matumaini
yasiyoshindwa ambayo yanaendeleza jitihada zao za kukuza haki na amani.
Licha ya dhambi za binafsi na za kijamii ambazo zinazosheneza shughuli zote za
binadamu, matumaini daima hutoa msukumo mpya wa kushughulika haki na amani,
pamoja na hali thabiti ya kujiamini katika uwezekano wa kujenga ulimwengu
ulio bora.
Ingawa
“fumbo la uchafu” (2 Thes 2:7) lipo na liko hai ulimwenguni, tunapaswa
tusisahau kwamba binadamu waliokombolewa wanaweza kuupinga uovu. Kila mwamini,
aliyeumbwa kwa sura ya Mungu na kukombolewa na Kristo, “ambaye kwa njia fulani
amejiunganisha na kila mwanadamu,”18 anaweza kushiriki katika ushindi wa wema.
Kazi ya “Roho wa Bwana anaijaza dunia” (rej. Hek 1:7). Wakristo, hasa
waamini walei, “hawapaswi, baadae, kuficha matumaini yao katika kina cha mioyo
yao, bali kuyaeleza kwa njia ya maisha yao ya kiraia katika uongofu na vita
endelevu ‘dhidi ya wakuu giza hili katika ulimwengu, dhidi ya nguvu za uchafu
wa kiroho’ (Efe 6:12).”19
, 12. Hakuna
mwanamume au mwanamke mwenye mapenzi mema anayeweza kuachana na vita ili
kuushinda uovu kwa wema. Vita hivi vinaweza kupiganwa ipasavyo kwa kutumia
silaha mwafaka za upendo tu. Pale wema unapoushinda uovu, upendo
unatamalaki, na hapo amani inatamalaki pia. Haya ndiyo mafundisho ya
Injili, yaliyosisitizwa tena na Mtaguso wa Pili wa Vatican: “sheria ya msingi
ya ukamilifu wa binadamu, na vivyo hivyo ya mabadiliko ya ulimwengu, ni amri
mpya ya upendo.”20
Jambo
kama hilo pia ni kweli katika mazingira ya kijamii na kisiasa. Kuhusiana na
hili Papa Leo wa 13 aliandika kwamba wale wenye madaraka ya kutunza amani
kwenye uhusiano kati ya mataifa wanapaswa kukuza ndani yao na kuwasha wengine
kwa “upendo, mama na malkia wa fadhila zote.”21 Wakristo ni lazima wawe
mashahidi waamini wa ukweli huu. Wanapaswa waoneshe kwa maisha yao kwamba
upendo ni nguvu pekee inayoweza kuleta ukamilifu kwa watu na jamii mbalimbali,
nguvu pekee ya kuongoza mwendo wa historia katika njia ya wema na amani.
Wakati
wa mwaka huu uliotolewa kwa Ekaristi, ninaomba wana na mabinti wa Kanisa
wapate katika sakramenti kuu ya upendo chemchemi ya umoja wote wa
kiroho: umoja pamoja na Yesu Mkombozi na, katika yeye, pamoja na kila binadamu.
Kwa kuzaliwa na kifo cha Kristo, ukweli unaokuwa halisi katika kila adhimisho
la Ekaristi, tumeokolewa kutoka katika uovu na kuwezeshwa kutenda wema. Kwa
njia ya maisha mapya ambayo Kristo ametupatia, tunaweza kutambuana kama kaka na
dada, licha ya kila tofauti za lugha, utaifa na utamaduni. Katika neno, kwa
kushirikishana katika mkate mmoja na kikombe kimoja, tunakuja kugundua kwamba
sisi ni “familia ya Mungu” na kwamba kwa pamoja tunaweza kutoa mchango wetu
fanisi wa kujenga ulimwengu wenye misingi ya tunu za haki, uhuru na amani.
Kutoka Vatican, 8 Desemba 2004.
Yoannes Paulus II