Make your own free website on Tripod.com

Madhehebu kuwakutanisha wanasiasa

Na Charles Misango

VIONGOZI  wakuu wa dini kutoka  BAKWATA, CCT, TEC na Ofisi ya Mufti Zanzibar, wanatarajia kuwakutanisha wanasiasa nchini wakiwamo wenyeviti na makatibu wakuu wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu ili kujadili amani na Uchaguzi Mkuu ujao.

Habari za kuaminika zilizolifikia KIONGOZI, zimebainisha kuwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar,

katika mkutano wao uliofanyika Jumatano iliyopita kwenye Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam, waliazimia kufanya mkutano huo Juni 22, mwaka huu.

Habari hizo za kuaminika zilizothibitishwa na mmoja wa viongozi hao waliohudhuria mkutano, zimesema taasisi hizo zinafanya maandalizi maalumu ya mkutano huo ikiwa ni pamoja na kuwapa taarifa viongozi wa wa kisiasa ngazi ya kitaifa, wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mkutano huo pia utawahusisha  Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania na yule wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Msajili wa vyama vya siasa nchini.

Wengine ni Wenyeviti wa Tume za Uchaguzi za Zanzibar (ZEC) na ile ya Tanzania Bara (NEC) na wawakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Kiongozi Zanzibar.

Habari zimedai kuwa, mkutano wa viongozi hao waandamizi wa siasa na dini, una lengo la kuangalia mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na taifa ili kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais na Wabunge pamoja na ule wa Rais wa Zanzibar na Wawakilishi, unaendeshwa katika misingi ya haki, uhuru na amani.

Aidha, mkutano huo unatarajiwa kuzungumzia namna viongozi wote wa dini watakavyoweza kutumia nafasi zao kuchangia katika kufanikisha zoezi zima la uchaguzi.

Habari zimesema, uamuzi huo wa viongozi wa dini, umetokana na utaratibu wao wa kukutana na viongozi wa siasa kila mwaka na kwa namna ya pekee, mkutano huo wa mwaka huu utajadili mbinu bora za kuendesha na kufanikisha Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais na Wabunge wa mwaka 2005.

Historia inaonesha kuwa, kila baada ya chaguzi kunakuwa na manung'uniko na migogoro ndani ya vyama hali iliyofikia baadhi kufukuzana uanachanma na hata wakati mwingine, kufikishana mahakamani.

Imekuwa ikidaiwa pia kuwa, katika baadhi ya vyama vya siasa rushwa imekuwa ikitumika katika baadhi ya chaguzi ili kushinda.

Dosari nyingine ambayo imebainishwa wazi na wananchi wengi katika chaguzi zilizopita, ni baadhi ya wagombea kutumia ukabila, udini na hata ukanda kama kigezo cha kumpigia au kutompigia kura mgombea.

Uchunguzi zaidi wa Gazeti hili umebaini kuwa, hadi sasa baadhi ya vyama vya siasa havina uhusiano mzuri baina yao na pia, suala la uandikishwaji  wapiga kura, pia lina mchango wake katika kuleta matatizo.

Wakati taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu huu wa Tatu katika mfumo wa Siasa wa Vyama vingi nchini, vyama vingine vya siasa vimekuwa vikitumia lugha za vitisho na zinazohatarisha amani na usalama katika jamii.

 

 

Sheria ya Ugaidi ‘inasaliti’ Katiba’

Na Joseph Sabinus

 

Akitoa mada katika semina hiyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Kitivo cha Sheria, Dk. Sengodo Mvungi,  alisema sheria hiyo ambayo ni dhahiri imeundwa kwa shinikizo la Taifa la Marekani, ni hatari kwa jamii kwa kuwa inawapa mamlaka watawala na vyombo vya dola kukiuka haki za binadamu kama zinavyoelezwa katika Katiba.

Alisema miongoni mwa haki hizo, ni pamoja na uhuru wa kupokea na kutoa habari, haki ya kuheshimika na kuchukuliwa kutokuwa na hatia hadi sheria itakapomthibitisha mtu kuwa na hatia.

“Nyingine ni haki ya kutembea, kuandamana, kukusanyika, kumiliki na hata haki ya mtu kutoingiliwa faragha,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 Kifungu cha 18, kila mtu ana uhuru wa kuwasiliana na watu wengine, kutembea, kuandamana na kukusanyika bila vipingamizi.

Dk. Mvungi alisema kuwa, kwa kurithi mfumo wa Utawala wa Uingereza, hivi sasa Dola inaichukulia Katiba ya nchi kama mali yake. “Hali hii inafanya hata Bunge lijione kuwa ndilo linalotunga Katiba na sio wananchi. Ndio maana sasa utaona wanatunga Katiba, wanatunga sheria,” alisema.

Katika mfano wake, Dk. Mvungi alisema Sheria hiyo ya Ugaidi katika Kifungu cha 9(1), inamzuia mwandishi wa habari kupokea wala kusambaza habari zozote za kigaidi.

Katika mada aliyoitoa kwenye semina hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, alisema Sheria ya Kuzuia Ugaidi ilipaswa kulinda haki za binadamu na utawala bora na kwamba, ina mapungufu makubwa kwa kuwa haielezi tafsiri ya ugaidi.

Balozi Ramia alisema badala yake, sheria inazungumzia vitendo vya kigaidi na kwamba, bila kuwapo kwa muafaka na tafsiri ya wazi, itakuwa vigumu kwa dunia kupambana na ugaidi.

Katika kuchangia, wajumbe walisema ukosefu wa tafsiri halisi ya ugaidi unasababishwa na ukweli kuwa, baadhi ya mataifa yanayoshinikiza vita na sheria dhidi ya ugaidi yakiongozwa na Marekani, yanashiriki kwa namna nyingi katika kufanikisha na kuendeleza ugaidi.

“Mara nyingine utata huo umesababisha ugaidi kufananishwa na upiganiaji wa uhuru,” alisema.

Katika semina hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Helen Kijo-Bisimba, alisema miongoni mwa mapungufu na ukiukwaji wa haki za binadamu uliopo katika sheria hiyo, ni kutotajwa kwa muda wa kumalizika kesi huku mtuhumiwa akiwa mikononi mwa dola.

“Sheria hii pia, haitaji kama kuna fidia yoyote endapo mtuhumiwa wa ugaidi atabainika kutokuwa na hatia,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Muungano wa Asasi zisizo za Kiserikali nchini Tanzania (TANGO), Marie Shaba, alisema wakati akifunga  semina hiyo kuwa,  jamii haina budi kuungana ili kupinga mambo yote yanayokwenda kinyume na haki za binadamu.

“Bila watu wote kuungana tangu makanisa, misikiti, wanaharakati na NGOs, tutafika mahali pabaya ambapo sasa sheria mbaya kama hii, zitamfanya mwandishi wa habari aogope kuripoti baadhi ya vitu kwa kuogopa kuitwa gaidi,” alisema.

Semina hiyo iliazimia kuendesha kampeni maalumu kuhakikisha kuwa, sheria hiyo inabadilika.

Maazimio mengine yaliyofikiwa ni juhudi za makusudi za kuwaelimisha Watanzania kuhusu sheria hiyo kwani watu wengi wakiwamo baadhi ya viongozi Serikali, vyama na dini hawaijui kwa kuwa hawakushirikishwa katika kuandaa muswada.

Chini ya Sheria ya Ugaidi, ni marufuku kusoma au kusambaza habari za kigaidi.

Sheria hii inazuia mtu anayedhaniwa kuwa gaidi, kuhutubia wala kusikilizwa akihutubia mkutano.

Katika Kifungu cha 29, Sheria inatoa nguvu zaidi za upekuzi kwa polisi. Chini ya Sheria hii, bila kulazimika kupata waranti, afisa wa polisi chini ya cheo cha Assistant Superintendent of Police, anaweza kuingia na kufanya upekuzi mahali popote.

 

…Wanaochanganya dini, siasa wavurugaji Zanzibar- Sheikh

Na Joachim Mushi

HALI ya machafuko ya amani yanayotokea Visiwani Zanzibar kila mara, inachangiwa kwa kiwango kikubwa na baadhi ya watu wanaochanganya dini na mambo ya siasa; Imesema Ofisi ya Mufti wa Zanzibar.

Mwakilishi kutoka Idara ya Mufti Zanzibar, Sheikh Said Nassoro Seif alisema hayo katika mahojiano na waandishi wa habari, nje ya ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam wiki iliyopita, wakati wa mkutano wa siku moja wa viongozi wakuu wa dini, uliojadili hali ya amani nchini.

Alisema mambo mengi yanayolalamikiwa na baadhi ya Waislamu Visiwani humo, yana mtazamo wa kisiasa zaidi kuliko wa kidini.

“Hali hiyo imeharibu sifa na heshima ya Uislamu katika macho ya watu wengine duniani,” alisema.

Sheikh Said alisema malalamiko juu ya Serikali kuingilia masuala yanayowagusa Waislamu moja kwa moja kama yanavyotolewa na baadhi yao, sio ya msingi kwa kuwa, sio jambo geni Visiwani humo.

Alisema awali, kulikuwa na vyombo kadhaa vilivyokuwa vinamilikiwa na Waislamu, huku vikisimamiwa na serikali, na hakukuwa na malalamiko yoyote kwa muda wote.

“Sasa iweje leo hii kuwepo na shutuma kali dhidi ya Serikali, wakati sio jambo geni?” alisema.

Akifafanua zaidi, Sheikh Said alisema, Chuo Kikuu cha Kiislamu Zanzibar na Mahakama Kuu ya Kiislamu ni baadhi ya taasisi nyeti zinazomilikiwa moja kwa moja na Waislamu, huku zikiongozwa kwa muda mrefu na Serikali bila matatizo.

“Hata mapendekezo ya majina ya watu wanaofaa kuwa Mufti wa Zanzibar, yanafanywa na Waislamu wenyewe na Rais wa Zanzibar anafanya kazi ndogo tu ya kutangaza. Sasa kosa liko wapi hadi mtu aseme kuwa Serikali inawaingilia Waislamu?” aliuliza kwa mshangao.

Alisema ingekuwa vyema kwa Waislamu wenye mapenzi ya siasa kuendesha shughuli hiyo bila kuhusisha upande wa pili wa dini. “Huwezi kutumikia watu wawili kwa wakati mmoja hata siku moja. Kama wewe utaamua kuingia kwenye siasa, basi uondoe udini ndani ya siasa au ukiingia kwenye dini, basi usiingize mambo ya kisiasa,” alisema.

Kauli ya Mwakilishi huyo wa Mufti inatokana na malalamiko ya siku nyingi, yanayotolewa na baadhi ya Waislamu Visiwani humo, wakidai kuingiliwa na vyombo vya Serikali katika masuala yanayaohusiana na Dini ya Kiislamu.

Katika Mkutano huo, Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Elinaza Sendero, alisema jamii haina budi kuunganisha nguvu zake pamoja ili kuwadhibiti watu wanaofanya majaribio ya kuvuruga amani nchini.

 

‘Tusikubali kuwa watumwa wa wafadhili’

Na Lilian Timbuka

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Valentino Mokiwa, amesema Umasikini ni mchezo wa utandawazi unaompumbaza mwananchi ajione mnyonge na asiyejiweza, ingawa baadhi ya viongozi wanaushabikia utandawazi huo.

Aliyasema hayo juma lililopita wakati akifungua warsha ya siku mbili iliyoandaliwa kwa pamoja na Jumuiya za Kikristo Tanzania (CCT), BAKWATA, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), na Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Kuondoa Umasikini.

Warsha hiyo ililenga kujadili Mkakati wa Pili wa Kuondoa Umasikini uliofanyika katika ukumbi wa mkutano TEC, jijini Dar es Salaam.

Alisema ingawa jamii inaendesha mijadala mingi juu ya suala la kuondoa umaskini, lakini haina matunda kwa kuwa wafadhili wa semina na warsha juu ya umaskini, hushinikiza wapate maazimio ambayo mataifa wahisani huyatumia kubuni mbinu nyingine za ukandamizaji wa wanyonge.

Askofu Mokiwa alisema vita dhidi ya umaskini haina budi kutoa kipaumbele pia katika kupambana na ujinga kwa kuwa matatizo haya, huambatana.

“Wakati mwingine utaona kuwa hizi semina zinazofadhiliwa na mataifa  ni mbinu za matajiri kuwatuma masikini wajadili hali zao, na kisha wawaambie wafikiri nini ili wajiondoe kwenye umasikini.”

Akaongeza kuwa,“Kwa kuwarudisha kule, basi hukaa na kusema, hivi ndivyo masikini wanavyozungumza; wamesema wanataka kufanya hivi, sasa sisi tunafanya hivi kuwadhibiti.”

Alidokeza kuwa ndio maana mara nyingi wafadhili hutaka ripoti za semina hizo, kabla nchi husika haijatoa maamuzi.

Askofu Mokiwa aliyalaumu mashirika ya fedha ya kimataifa, IMF na Benki ya Dunia akisema kuwa, yamekuwa yakitoa fedha kwa ajili ya kupanga mikakati ya kupambana na umasikini wakati huo huo yanazibana nchi masikini katika kuondokana na umasikini.

Alisema iwapo Mashirika hayo yana nia ya kuinua uchumi na utajiri kwa nchi masikini, basi yafute madeni yao yote inayozidai nchi masikini ikiwamo Tanzania, bila masharti.

 “Ninyi mjijue wazi kuwa ni sauti ya watu wasio na sauti, fanyeni juhudi mumkomboe mwananchi aliye kwenye mahangaiko,” alisisitiza.

Alisema Watanzania si masikini kwa kiasi kikubwa kama inavyodhaniwa, bali ni hali ya mazingira ndiyo yanawafanya wajione masikini.

Alibainisha kuwa, maono hafifu, sera za ubabaishaji za mdomoni na zisizotekeleza, zinachangia kwa kiasi kikubwa Mtanzania kujiona masikini.

Akitolea mfano wa mto Rufiji, Askofu Mokiwa alisema kuwa, mto huo umekuwa ukitiririsha maji mabilioni ya lita kwenda baharini kwa siku,  hali watu hawana maji ya kutumia.

“Tunasubiri Wahisani waje watujengee malambo ya kuhifadhi maji ya mto ule.”

Alisema katika nchi ya Tanzania watu wana utajiri mkubwa wa madini, ambayo hayawanufaishi Watanzania wenyewe, bali ni kwa faida ya wawekezaji.

Alisema hivi sasa utajiri wa nchi umekabidhiwa kwa wageni wenye mitaji mikubwa, huku Mtanzania akikejeliwa kuwa ni masikini na mtaji wake ni mdogo.

“Utajiri tumewakabidhi wageni ambao hivi sasa wanaondoka nao mpaka makontena ya mchanga, lakini hatuulizi wanapeleka wapi huo mchanga na una nini ndani yake,” alisema.

Akaongeza, “Iko haja hivi sasa, wakati mkakati wa kujadili mchakato wa kuondoa umasikini unavyoendelea, kutafuta na kuzibaini hali za umasikini tulizo nazo na kuzifanyia kazi kabla ya kuwapelekea hao wanaojiita wafadhili wa kuondoa umasikini.”

Akitoa mada juu ya Uhusiano wa Jinsia, Rasilimali na Ushiriki wa Wananchi katika PRSP, Bibi Mary Mwingira alisema kuwa, muktadha wa uchambuzi wa sera za umasikini wa Tanzania, usipoangaliwa nchi inaweza kujikuta iko ndani ya kisiwa kinachomilikiwa na wafadhiri.

Alisema kuwa hivi sasa imeonesha kuwa, Watanzania walio wengi wana umasikini wa akili na kufikiri na si rasilimali kama inavyodhaniwa na wengi.

Bibi Mwingira alisema kuwa Mkakati wa kwanza wa uchambuzi wa umasikini unaonesha kuwa, upande wa uwekezaji umepiga hatua japo serikali na bunge wamekuwa wakitoa muongozo wa uwekezaji katika njia zisizo sahihi.

Hata hivyo Bibi Mwingira alibainisha kuwa, umasikini wa Mtanzania unalemazwa na utegemezi uliojengeka akili mwao, kwa kufikiri kila jambo watafanyiwa na wafadhili.

“Hebu tujiulize kwanza, kama hawa wafadhiri wasingekuwapo Tanzania ingekuwa wapi?” alihoji Bibi Mwingira.

Wakichangia mada washiriki wa warsha hiyo, waliwalaumu wafadhiri kwa njia zao wanazotumia kusamehe madeni ya nchi masikini, Tanzania ikiwa ni moja wapo ikiwa ni pamoja na masharti magumu.

Warsha hiyo ya siku mbili, iliwashirikisha washiriki kutoka Jumuiya za Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na BAKWATA.

 

Milioni 200/= zahitajika kujenga Kanisa Kimara

Na Joseph Chewale

JUMLA ya shilingi milioni 200 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa kubwa na la kisasa la Parokia mpya ya Kimara, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Paroko wa Parokia hiyo, Padre John Frances ameliambia KIONGOZI kwamba, fedha hizo zinategemewa kupatikana kutoka kwa waamini wa parokia hiyo ambao wamejizatiti kuhakikisha kuwa, wanafanikisha upatikanaji wa fedha hizo mapema iwezekanavyo.

Padre Frances amesema hadi sasa, parokia hiyo imekusanya shilingi milioni 30 na tayari michoro ya jengo la Kanisa hilo, imekamilika.

Alisema Kamati ya Ujenzi na Ardhi imeundwa kusimamia ujenzi wa Kanisahilo linalotazamiwa kuchukua waaini 1,500 kwa wakati mmoja.

Alisema kuwa, mbali na michango ya waamini parokiani hapo, waamini wengine na Watanzania wote wenye mapenzi mema, wanakaribishwa kutoa chochote kitakachosaidia katika ujenzi huo.

“Tunategemea kufanya michango na mbinu nyingine zitakazotusaidia kupata pesa. Lakini vilevile, tunawaomba waamini wengine na Watanzania wenzetu wenye mapenzi mema watusaidie,” alisema.

Waamini wa parokia hiyo wanaokadiriwa kufikia 5140 kwa sasa, wanatumia banda la miti wakati wa ibada kwa vile Kanisa lililojengwa likiwa kigango, ni dogo na linaloweza kuchukua waamini 200 tu.

Parokia hiyo iliyomegwa kutoka Parokia ya Ubungo Msewe, hadi sasa ina vigango viwili vya King’ong’o na Korogwe. Ni parokia inayokua kwa kasi kwa kuwa na ongezeko kubwa la waamini. Ikiwa na vyama tisa vya kitume, Parokia ya Kimara inazo Jumuiya Ndogondogo 49 zilizogawanywa katika kanda nane.

Wakati huo huo: Padre Frances ameiomba Serikali kuwasaidia wakazi wa Kimara, kuwaongezea shule za msingi badala ya mbili tu zilizopo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.                                                       

Amesema, shule za Mavurunza na Korongwe ndizo tu zilizopo katika parokia yake na kwamba hali hiyo, inawafanya watoto wengi kusoma shule za mbali. Amedai kuwa, watoto wengi wanapata taabu ya kusafiri umbali mrefu na kukabiliana na kero za daladala ambazo zingelikwisha tu, iwapo kungekuwa na shule nyingi zaidi katika eneo hilo.

Hata hivyo, Padre huyo amesema wananchi pia wanaowajibu kutumia nguvu zao ili kuionesha Serikali kuwa, na nia ya maendeleo isipokuwa, wamekwama sehemu fulani.

Alisema huu ni wakati muafaka kutambua kuwa, ili kupata maendeleo ya kweli na ya haraka, kila mwanajamii hana budi kutambua kuwa anawajibika kuchangia upatikanaji wa maendeleo hayo na kuondoa kero mbalimbali.

 

Mabaharia wabadili jina kuondoa mfumo dume

Lilian Nyenza na Wema  Figao

CHAMA Cha  Mabaharia  Nchini  (TASU), kina  mpango wa  kubadili  jina la  chama hicho ili kuondokana na lile la sasa linaloashiria mfumo dume.

Katibu  Mkuu  wa  TASU  Taifa, Bw. Nicholas Mgaya, amesema wanachama wengi wanalalamikia jina la sasa la Tanzania Seamen Union (TASU), kuwa linaelekeza watu kuamini kuwa chama hicho ni cha mabaharia wanaume tu, wakati wapo wanawake wanaofanya kazi hiyo.

Amesema ili kuondoa dhana hiyo, chama hicho kitaitwa Tanzania  Seafarers Union, jina ambalo wanaamini litakuwa limekidhi na kubeba jinsia zote za wanachama wa chama chake.

Katibu Mkuu huyo amesema hadi sasa, chama chake kina mabaharia wanawake 40, kati ya 900 waliopo.

Tanzania inakisiwa kuwa na jumla ya mabaharia 10,000 wanaofanya kazi katika vyombo mbalimbali vya usafiri katika maziwa nchini na bahari.

Kuhusu mikakati  ya  chama chao, Bw. Mgaya  amesema wanatarajia  kufungua tawi lake katika mkoani Lindi na kuimarisha matawi yake ya Mwanza na Kigoma .

Hivi karibuni, chama hicho kilifanya uchaguzi wake kitaifa ambapo Bw. Abeid Sheremu alichaguliwa  kuwa Mwenyekiti mpya kwa kupata kura 21. Bw. Nicholas  Mgaya aliibuka kuwa Katibu Mkuu Taifa kwa kupata  kura 23 na kumbwaga mpinzani wake Ahmedi Chakoma aliyeambulia kura tisa.

Viongozi pambaneni kuiokoa jamii - Askofu

Charles Hililla, Kahama

VIONGOZI wa Kanisa nchini, wametakiwa kuwa makini, wavumilivu na shupavu katika kupambana na kasoro mbalimbali zinazovuruga mwenendo na mfumo bora wa maisha katika jamii.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Askofu Severine Niwemugizi wakati akitoa salaam za Baraza hilo, kwenye Maadhimisho ya Miaka 50 ya Upadre na 80 ya kuzaliwa kwa Askofu Mstaafu wa Jimbo la Kahama, Mathew Shija.

Mhashamu Niwemugizi ambaye ni Askofu wa Jimbo la Rulenge, alisema kumekuwapo na kasoro mbalimbali katika mfumo mzima wa maisha ya Watanzania ikiwa ni pamoja na rushwa, ambayo imekithiri kwa wakubwa wengi hapa nchini na vita dhidi ya tatizo hilo, imekuwa ikipigwa kwa wadogo.

Aliongeza kuwa, Serikali haina budi kuweka mkakati wa makusudi kupambana na rushwa kama ilivyoweka mkakati wa kupambana na UKIMWI.

Aidha, Mhashamu NiweMugizi alisema kuwa, kukithiri kwa vitendo hivyo vya rushwa hapa nchini, ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa taifa na jamii kuonekana masikini, kwa kukosa maendeleo.

Alisema vitendo hivyo kwa sasa vinajificha ndani ya kivuli cha uwekezaji, ambao unatafsiriwa na jamii kuwa ni unyang’anyi na wizi wa mchana unaofanywa na wakubwa, huku jamii ikikosa huduma muhimu.

Alifafanua kuwa, hali hiyo kwa kiasi kikubwa inachangia kuwapo kwa tishio la kuvurugika kwa amani nchini.

 “Ni aibu kwa wananchi wa wilaya ya Kahama kukabiliwa na umaskini kwa kukosa huduma, wakati wilaya yao ina mgodi mkubwa wa dhahabu uliopo Bulyanhulu ambao hutoa madini, “ alisema  na kuongeza “… halafu madini hayo yanapitishwa mbele ya macho yao na kupelekwa kwa wakubwa ambao ndio wanaofaidi matunda yanayotokana na utajiri wao huku wao wanabakia masikini ndani ya ardhi iliyojaliwa utajiri.”

Alisema kuwa, viongozi wa Kanisa wanao wajibu mkubwa kushirikiana na viongozi wengine serikalini katika kupambana na changamoto za utandawazi wa kimaendeleo, ili kuondoa kasoro zinazojitokeza na watu wamtumikie Bwana kwa moyo safi.

Mhashamu NiweMugizi aliongeza kuwa, kinyume na hali ilivyo sasa, watu wengi wamekuwa wakitenda maovu kwa kisingizio cha hali mbaya ya maisha, huku UKIMWI nao ukichukua nafasi inayowaacha vijana wakikosa mwenendo mzuri wa kimaadili kwa kufundishwa masomo ya UKIMWI shuleni.

Alisema masomo hayo yanayofundishwa kwa kivuli cha stadi za maisha, yamekuwa yakiendeleza mmomonyoko wa maadili kwa jamii.

 

Kanisa Shinyanga kutafutia wakulima soko Ulaya, Asia

Na Peter Dominic

JIMBO Katoliki la Shinyanga lipo hatua za mwisho katika kukamilisha mpango wa kuwawezesha wakulima kuuza mazao yao katika nchi za Asia na Ulaya; Imefahamika.

Mkurugenzi wa Mpango wa Mradi wa Kilimo na Mifugo jimboni humo, Padre Zengo Mikomangwa, ameliambia KIONGOZI mwanzoni mwa juma lililopita kuwa, Jimbo hilo limefikia uamuzi huo ili kuwasaidia wakulima ambao wamekuwa na tatizo la ukosefu wa soko la mazao yao licha ya uzalishaji kuwa mzuri.

Alisema, tatizo la ukosefu wa soko la uhakika, limesababisha wakulima wa mazao mbalimbali walazimike kuuza, mazao yao kwa bei ya chini na hivyo, kuwasababishia hasara.

Alisema katika kutafuta njia sahihi ya kumsaidia mkulima ili auze mazao yake kwa faida, waliamua kufanya utafiti wa mazao yanayohimili ukame ambayo pia soko lake ni kubwa katika nchi za Ulaya na Asia.

Padre Mikomangwa alisema katika utafiti huo, wameshirikiana na Kituo cha Utafiti cha Ukiligulu na Shirika la Wakatoliki la Marekani na Shirika la Utafiti wa mazao ya mikunde na mazao yanayohimili ukame la International ICRISAT ambalo makao makuu yake yapo India na Nairobi kwa nchi za Afrika.

Wengine kwa mujibu wa Padre Mikomangwa, ni shirika moja linalojihusisha na utoaji wa huduma za kijamii (C.R.S).

Alisema utafiti huo uliochukua miaka mitatu, pia umehusisha wakulima wenyewe pamoja na halmashauri za wilaya ambapo mazao yaliyopewa kipaombele ni dengu, karanga, mbaazi na mazao mengine kama hayo ambayo yanavumilia ukame.

“Kilimo hiki kilikuwepo muda mrefu, sisi tunatafiti na kutafuta soko linahitaji mazao gani, Baada ya utafiti, tuliwapelekea wakulima mbegu tisa wakachagua nne, tuliamua kushirikiana na Shirika la  (Techno Serve). Hawa ni wataalamu wa masoko. Tumefanikiwa kupata soko katika nchi za India na Ulaya.” alisema.

Hata hivyo alisema, kabla ya kufikia uamuzi ya kutafuta masoko, Jimbo hilo lilianza kuwahamasisha wakulima wawe na vikundi vya uzalishaji, Produce Marketing Gruop (PMG).

“Mpango huu umewezesha kuundwa kwa vikundi vinane na vinne kati yao, vimekamilisha usajiri.” alisema.

Padre Mikomangwa alisema, vikundi hivyo vilivyopo katika Wilaya za Shinyanga na Maswa vimeanza uzalishaji na huenda vikaanza kuuza mazao yake katika soko la nje mwaka huu.

Mradi hiyo inafadhiriwa na Catholic Relies Services (CRS) “Lengo la Jimbo ni kuwasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa bei nzuri.” aisema.

 

Hospitali binafsi zabeza gharama za Muhimbili

Na Kizitto Joseph

BAADHI ya wagonjwa waliokuwa wakipata matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wamekimbilia katika hospitali binafsi za jijini Dar es Salaam katika kile kinachoonekana kama kukwepa gharama za matibabu zilizoanza kutozwa na hospitali hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na KIONGOZI, madaktari wa hospitali za Hindu Mandal, Regent na Aga Khan zote za jijini, walisema kuwa hospitali zao zimeanza kupokea wagonjwa wengi waliokuwa wakipata matibabu kutoka Hospitali ya Muhimbili tangu ilipoongeza gharama za matibabu.

“Watu wameanza kufurika katika hospitali za watu binafsi. Mtanzania gani ataweza kumudu gharama za Muhimbili,” alihoji Dk. Sharrif Patel wa Hospitali ya Hindu Mandal.

Alisema wengi wa wagonjwa waliokuwa wanaitumia Hospitali ya Muhimbili, wameanza kubadili mwelekeo kutokana na kushindwa kumudu gharama hiyo mpya kwa sababu za kiuchumi.

Pamoja na kufurahia kuongezeka kwa wagonjwa katika hospitali yake, Dk. Patel alisema uamuzi wa kuongeza gharama za matibabu katika hospitali hiyo ya serikali, haukuwa wa busara kwa kuwa hakujali kipato cha mtu wa kawaida.

“Yeyote aliyeshinikiza uamuzi huo (mabadiliko hayo) hakuwa na takwimu ya umaskini wa wananchi. Hakuna Mtanzania mwenye kipato cha kawaida anayeweza kutumia shilingi 10,000 kwa matibabu ya siku moja,” alisema.

Mmoja wa maafisa wa Utawala wa Hospitali ya Regent ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa, ongezeko la gharama za matibabu katika Hospitali ya Muhimbili ni mzigo usiobebeka kwa Mtanzania wa kawaida.

Aliishauri serikali kutumia kodi inayokusanywa toka vyanzo mbalimbali vya mapato, kugharamia matibabu ya wananchi wake badala ya kuwaachia gharama hiyo ambayo kwa hali yoyote ile hawawezi kuimudu.

“Huwezi kuongeza gharama za matibabu kabla ya kuongeza kipato cha mtu. Wagonjwa wengi wameanza kukimbilia hospitali za watu binafsi kuogopa gharama za Muhimbili,” alisema,

Akaongeza kuwa, katika hospitali yake na zile anazozifahamu, kumekuwa na wagonjwa wengi zaidi ikilinganishwa na siku za nyuma na utafiti walioufanya, umeonesha kuwa ni kutokana na ongezeko la gharama za matibabu katika Hospitali ya Muhimbili.

Hivi karibuni katika uamuzi uliolalamikiwa mno na Watanzania, Uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, uliongeza gharama za matibabu kutoka shilingi 500/= hadi 10,000/= kwa ugonjwa wa kawaida na shilingi 50,000/=  kwa upasuaji mdogo.