Miujiza Kisiwani

         Na Peter Dominic

WANAKIJIJI wote walikuwa wamepatwa na mshangao mkubwa baada ya watu  kupotea katika mazingira yasiyo eleweka.

Kila mmoja alikuwa hajui chanzo cha kupotea kwa watu hao  ambapo wapo wengine waliodhani kutoweka huko kulitokana na nguvu za giza.

Ukweli ni kwamba upotevu huo ulichangiwa na suala la njaa kali katika eneo hilo na sehemu pekee ambayo ingekuwa kimbilio ni katika kisiwa cha Shoshwa.

Tangu enzi za mababu,ilisadikika  kisiwa hiki  kuwa kina vyakula vingi. Lakini hajabu ni kwamba watu waliokwenda kisiwani humo,hawakurudi!

Wazee vikongwe walikusanyika pamoja katika mkutano ulioitishwa na mtawala wao, Mfalme Bwile Kitakwete, ambaye kwa upande mwingine alitawala kitabaka.   

Mazungumzo kati yao yaliendelea kutafuta muafaka wa suala lililokuwa likiwasumbua muda mrefu. Agenda katika mkutano huo ilikuwa ni kwanini watu wote waliokwenda katika kisiwa cha Shoshwa kilichokuwa Kasikazini mwa kijiji hicho cha Mategula.

Waliojiita waganga wa kienyeji na wapigaramli walizishika tunguli zao na kuanza kuagua kinachowamaliza ndugu zao, kwa amri ya mfalme huyo yeyote ambaye angefanikiwa kupata jibu la kitendawili katika kisiwa hicho, angepewa robo ya mali ya Mfalme huyo.

Waganga walizipiga tunguli zao usiku na mchana, watabiri walitoa maelezo yao lakini hakuna aliyebahatika kutegua ama kufanikisha kwa namna yoyote siri iliyojificha katika kijiji hicho.

Ilikuwa ni jambo la kawaida ufikapo katika kijiji hicho kuambiwa kuwa waedao Shoshwa hawarudi kamwe. Hivyo ilikuwa ni jambo la kawaida mtu kukutishia kuwa atakupeleka katika kisiwa hicho endapo ungemfanyia jambo lolote lisilompedeza.

Mkutano wa siku moja haukutosha kumaliza tatizo hilo, mara kwa mara ilifanyika mikutano mikubwa ikiwemo ya hadhara na ile ya kawaida acha vile vikao vya kila familia juu ya muujiza huo wa hatari.

Kadri vikao vilivyozidi kushamiri ndivyo hali ilivyozidi kuwa mbaya katika himaya ya Mfalme  Kitakwete.

Siku moja baada ya kumaliza mkutano, mtoto wa  kwanza wa Mfalme aitwaye  Lwiza aliyekuwa akitarajiwa kuwa mrithi wa kiti baba yake, hakuonekana   katika nyumba yake ya msonge iliyokuwa pembezoni mwa jumba la Mfalme Kitakwete.

Hofu kubwa   ilitanda, amri ilitolewa Ikulu ya Mfalme huyo kuwa haiwezekani mwanae akauawa na wanakijiji wakakaa kimya, aliamuru ipigwe ngoma  watu wakusanyike na waanze msako hadi mwanae apatikane, awe hai ama amekufa.

Msako uliingia katika wiki ya nne lakini hakuna lolote la maana lilopatikana zaidi wa kijana mmoja na mzee wa makamo kuraluliwa na mamba mara walipokuwa wakimtafuta Lwiza kwenye Mto Ngono.

Vifo havikuwakumba hao peke yao,pia wanaukoo wengine wa Mfalme wapatao watatu nao walipoteza maisha katika msako huo wa mtoto wa Mfalme.

Baada ya kuona watu wanazidi kuuwawa bila mafanikio ya Lwiza kupatikana,msako ulisitishwa, na amri  ilitolewa kwamba mtu wa aina yoyote asithubutu kwa namna yoyote kutumia maji ya kisiwa hicho  wala kujishughulisha na uvuvi kwa namna yoyote ile.

Tangu hapo samaki walikuwa hadimu, watu waliishia kuvua samaki wa mito.  

Hata hivyo  ilikuwa ni marufuku kuingia katika nyumba ya Mfalme.

Watu wengi walimlalamikia  Mfalme wao wakidai kwamba huenda kuna mambo hakuyatimiza ndiyo maana wamekumbwa na mabalaa hayo.

Hakukuwa na amani tena kwa Mfalme, maelfu ya watu walikuwa wamepoteza maisha yao.

Wengi walipotea katika kipindi cha njaa kali iliyoikumba himaya ya Mfalme.