Make your own free website on Tripod.com

Miujiza Kisiwani (3)

 

         Na Peter Dominic

Siri hiyo iligundulika baada ya wazazi wa binti huyo kumtaka anywe dawa ili aiharibu mimba hiyo aepukane na adhabu ya kifo ambacho kingeliwaandama yeye na binamu yake baada ya kuvunja sheria.

Hata hivyo kwa mshangao wa wazazi wake binti huyo aliwakatalia katakata na aliahidi kuwa angaliweza kuilea mimba. Kinyume chake yupo tayari kupoteza maisha kuliko kuitoa mimba hiyo.

Walikuwa wamekubaliana na binamu yake kwamba kuliko kuitoa mimba basi bora wakabilianane na adhabu ya kupigwa mawe. Labda waliamua kupeana ahadi hiyo kwa vile walikuwa wadogo kiumri.

Ndiyo kwanzahuyo binti alikuwa akiitwa Nyamwiza alikuwa na umri wa miaka 15 na mwenzake alikuwa na umri wa miaka 17. Ni wazi kuwa adhabu ya kifo iliyoambatana na kupigwa mawe walikuwa wakiisikia kwa hadithi.

Awali wakati wazazi wa Nyamwiza wakimueleza yote katika nyumba yao ya msonge, ingawa ilikuwa usiku walikuwa wamekosea maana pembezoni mwa nyumba yao alikuwapo mpelelezi wa Mfalme akipeleleza kila kitu hivyo taarifa zilimfikia Mfalme siku ya pili yake.

Nyamwiza alikuwa mwepesi kutumwa na alikuwa makini tangu utotoni ndiyo maana alitokea kupendwa sana na wazazi wake.

Aliaminiwa na aliachwa huru kufanya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuruhusiwa kwenda kuteka maji peke yake na kuwatembelea majirani.

Lakini wakati yeye yuko hivi ilikuwa ni tofauti sana na binamu yake aliyekuja kumpa mimba ya aibu. Binamu yake Mugalula ni kujana ambaye alionekana kutokuwa natabia njema tangu kukua kwake.

Wazazi wake walijaribu kumuonya juu ya vitendo vyake lakini ilikuwa vigumu kubadilika.

Ni siku moja Nyamwiza alipokwenda kuteka maji umbali wa mita mia mbili kutoka nyumbani kwao. Hatua kidogo kabla ya kuufikia mto ule uliohudumia watu wa eneo hilo kwa maji,alijikuta mikononi mwa binamu yake ambaye alimbaka akamsababishia maumivu makali na kumuachia ujauzito.

Hata hivyo kutokana na ujasiri wa binti huyo pamoja na maumivu aliyoyapata hakuwahi kuwaeleza wazazi wake kilichopata hadi ilipogundulika kuwa tayari anao ujauzito wa miezi mitatu na wiki tatu.

Tabia yake ilibadilika ghafla, siku moja jioni bibi yake mzaa Baba alipomuhoji na kukagua tumbo lake kwa viganja vyake vilivyozeeka, alimkagua karibu kila sehemu ya mwili wake ndipo alipobaini kuwa alikuwa na ujauzito. 

Nyamwiza pia limweleza ukweli wa mambo bibi yake na kumuomba amfichie siri lakini bibi yake alimweleza kuwa anaweza kuficha vingine lakini siyo mimba.

Nyamwiza hakuelewa namna nyingine ya kuficha siri yake ilibidi kuwaeleza kila kitu kilichomkuta.  

Inagwa ilikuwa mwiko mzazi kumshauri binti yakle kufanya jaribio la kuharibu mimba lakini mapenzi ya wazazi wake, walimshauri anywe dawa za kuiharibu mimba ili anusurike kifo cha kupigwa mawe.

Nyamwiza alikubali mbele ya wazazi wake. Bibi yake akishirikiana na mama yake walitayarisha dawa za kumpatia ili  aanze  kuzitumia usiku ya pili

lakini mchana wa siku ile aliruhusiwa kwenda kisimani ali apate kuoga na kufua nguo zake.

Akiwa kiimani alikutana na binamu yake aliyekuwa akitumikia adhabu kali ya kuchota maji na kujaza mitungi kadhaaa kutokana na kitendo chake cha kumpachika mimba binamu yake. 

Kinyume na matarajio yake binamu yake alipiga magoti na kumuomba msamaha huku machozi yakimtiririka.

Nyamwiza  ambaye alisimama na kumuangalia asijue la kumfanya alimshika mkono na kumuinua. “Mimi nimekusamahe, lakini ni vipi tutakavyopigwa mawe hadi kufa!” alisema na kuanza kububujikwa na machozi.

“Mimi nimesabababisha haya yote, sina budi kukutetea na kufanya kila linalowezekana ili ikibidi basi tunusuru maisha ya mtoto aliyepo tumboni.” binamu yake alimpa moyo.

“Nimesikia Liwali mmoja akimweleza Mfalme kuwa katika ukoo wenu kuna watu waliopeana mimba! Mfalme aliamulu uchunguzi wa kina ufanyike ikibidi wahusika wafikishwe kwake kukabiliana na adhabu ya kifo.” Ni kauli iliyoka kwa kijakazi wa Mfalme pindi alipokutana na Nyamwiza.

Baada ya kusema hivyo Nyamwiza na binamu yake wote waliuliza kwa hamaki “ ni kweli wewe dada?”

Kisha yeye aliendelea kusema. “Ni kweli, hivi ni nani huko kwenu?

Lakini nimesikia wanasema ni binti mdogo na kijana mdogo au ni ninyi!?, aliuliza kwa mshangao.

Baada ya kusema hivyo Nyamwiza aliangua kilio na mwenzake alianza kumbembeleza. “Mimi nimewaabieni  msije mkanisema wataniua. Naomba msinisema kwenu jamani” aliwaarifu yule mfanyakazi kisha alitoweka kuelekea alikotumwa.

Binamu yake Nyamwiza alimbebeleza mwenzake kisha walikaa na kupanga namna ya kufanya ili kuhepukana na kifo cha kupigwa mawe ama adhabu ya kukatwa kichwa.

Wote kwa pamoja waliafikiana watoroke kabla habari sahihi hazijamfikia Mfalme. Suala hilo halikuhitaji kupoteza muda, “Hizi ni habari mbaya kwetu tukiendelea kukaa hapa, tutapoteza maisha tutoroke tuelekee Mashariki. Nadhani tutaweza kufikia vijiji vingine ambavyo watu wanaishi, nadhani watatupokea” alisema binamu yake Nyamwiza.

“Lakini itakuwaje tukifika huko!…ina maana watatatupokea na wakitupokea tutawaambije? sisi ni nani?… Wewe  ni nani wangu na huu ujauzito nilionao je?” aliuliza Nyamwiza.

Mwenzake alimpa matumaini kuwa hilo lisingelikuwa tatizo. Waliafikiana na kutokomea msituni kuelekea Mashariki ya mbali.     

Nyumbani kwa akina Nyamwiza na  kwa  binamu yake mambo hayakuwa shwari. Wapelelezi wa Mfalme waliwasili muda mfupi ili waweze kuwakamata Nyamwiza na binamu yake wafikishwe mbele ya Baraza kujibu tuhuma za kupeana mimba kabla ya kufunga ndoa na ikithibitika basi wakabiliwe na adhabu ya kupigwa mawe hadi kufa au kukatwa vichwa.

Wazazi wao ambao walikuwa katika hekaheka za kuwatafuta, walijikuta mikononi mwa nguvu za dola la Mfalme Kitakwete.  Kwakuwa vijana wao ndiyo hasa watuhumiwa, wao walikamwatwa na kufikishwa mbele ya Baraza la wazee.

Walihojiwa kwa masaa kadhaa lakini baadae waliachiwa. Kuachiwa kwao kulitokana na wao kukataa kuhusika na tuhuma hizo. Waliishinda kesi hiyo kwakuwa hakukuwa na ushahidi wa yote yaliyosemwa kwakuwa watuhumiwa hawakuwepo mahali hapo.

 

 

It is prepared by Miss. Christina Nyambo. Authorised and run by Rev. Fr. Revocatus Makonge, Exec. Sec. of the Communications Department of TEC.

 

Please visit the TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE WEB SITE