Miujiza Kisiwani (5)

         Na Peter Dominic

Alikaa kimya ili fisi wasimuone maana ulikuwa  usiku wa mbalamwezi.

Kitendo cha fisi kuilalua maiti ya binamu yake kilimuhakikishia kuwa kweli binamu yake alikuwa amekufa kitambo maana fisi hawezi kumla mtu aliye hai.

Alikumbuka maana bibi yake mzaa mama aliwahi kumsimulia alipomtembelea.

“Safari ya wawili imekwisha, niko peke yangu sijui nitakwenda wapi? Bora ningebaki nyumbani nikabiliane na kifo cha kupigwa mawe kuliko kulaliwa na fisi, binamu umeniponza lakini na kusamehe,” alilalama na kusononeka moyoni. Ndege walianza kupiga kelele kuashiria kuwa ni alfajiri.

Aliteremka kwenye mti na kushuhudia vipande vya nyama vya maiti ya binamu yake. Hata hivyo hakuwaza kurudi nyuma maana ilionekana alikotoka ni kubaya kuliko anakokwenda.

Jibu la haraka ilikuwa ni kufikiria namna ya kuvuka ule mto.

Alilikokota lile gogo na kulilaza kwenye maji, halikuzama kama lile alilolipanda yeye na binamu yake. Alichukua mti mrefu uliokuwa pembeni yake ambao aliutumia kama kasia. Alikuwa amepiga hatua na alikaribia kuuvuka mto. Waswahili husema, siku njema huonekana hasubuhi.

Mbele yake aliwashuhudia viboko waliokuwa wakigombana. Walifukuzana kwa kasi ya ajabu huku muungurumo wa viboko hao ukiufanya mwili wake ushikwe ganzi. Kiboko mmoja kati yao liyezidiwa na mwenzake andiye alisababisha maafa kwa upande wake.

Alimpita kando kwa kasi lakini aliliguza gogo alilolipanda na kusababisha gogo hilo kuyumba na kujirusha katika maji yenye kina kirefu. Kwa ujasiri alilishikilia gogo hilo bila kuliachia na kufanikiwa kuliweka sawa japo  kasi yake ilikuwa imepotea.

Kwa mara nyingine tumbo lilianza kumuuma. Upepo mkali uliokuwa ukivuma ulimuwezesha kufika upande wa pili wa mto huo na yeye aliweza kufika salama. Wakati akifikiria yote akiwa haamini kama ameweza kuuvuka mto huo, mluzi wa mvuvi aliyekuwa akilelekea kulowa samaki ulimtoa katika lindi la mawazo.

Aligeuka na uso wake uligongana uso kwa uso na mvuvi huyo. Bila kuuliza mvuvi aligundua kuwa msichana huyo amefikwa na janga kubwa. Alikuwa hatamaniki. Nguo zilikuwa zimechanika na mwili wake umedhoofu kwa kukosa chakula.

Sauti ilimkauka hata alipoulizwa hakuweza kusema kitu zaidi ya kujishika tumbo lililokuwa likimuuma kwa njaa na kiumbe kilichopo tumboni mwake.  Kwa vile alikuwa akitetemeka kwa hofu na njaa. Mvuvi alikoka mota halaka na kumulekeza apashe viganja vyake kwenye moto.

Kwenye kikapu chake alitoa kibakuli kidogo kilichohifadhi ugali wa muhogo na mboga ya samaki. Nyamwiza hakusubiri kunawa, aliufakamia ugali huo kisha aliomba maji ya kunywa, kisha alishukuru na sauti yake ilisikika vizuri.

Alimsimulia kila kitu mvuvi huyo na kwa huruma alisitisha shughuli yake ya uvuvi na kuamua kuongozana na binti huyo hadi nyumbani kwake mita chache kutoka katika mji mkubwa uliokuwa na watu wengi ambao walikuwa huru, chakula tele tofauti na kule alikotoka.

Huko nyumbani wazazi wake walikata tamaa, matumaini ya kupatikana watoto wao wakiwa hai yalikwisha. Watu walizidi kuukimbia utawala wa Mfalme kitakwete, siku zilivyozidikwenda ndivyo hali ilizidi kuwa mbaya zaidi.

 Kitendawili kuhusu njaa iliyosumbua himaya ya mfalme hakikupata jibu. Baada ya kifo cha Lwamwasha  wa pili watabili  walikaa kimya wakihofia kuuawa.

  Baada ya maisha ya hapa na pale, huko ughaibuni Nyamwiza alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume.    

 Lakini hakuwahi kumueleza mwanae siri iliyojificha moyoni mwake licha ya udadisi wa mwanae.

 “Mhu….. mwanagu, usisumbuke sana kujua mambo ambayo yatakusumbua, ulimwengu huu una mambo mengi, ni bora tu umuheshimu kila mtu utakayekutana naye maana Baba zako na ndugu zako ni watu unaowaona humu.”

 Mara kwa mara alimweleza mtoto wake akimjengea heshima na busara za kuwaheshimu watu wote.

Kauli hiyo ilimjengea mazingira mazuri mwanae, alikuwa kijana mwenye heshima, pia Mungu alimjalia kipaji cha hali ya juu kwa kung‘amua mambo mapema.

 Wakiwa katika mji mkubwa na wenye watu wengi, tofauti na mazingira alimokulia mama yake, Alibalio Rweshabula  tayari alikuwa na majukumu makubwa ya kumtunza mama yake kama zilivyo mila nyingi za kiafrika. Baada ya mzazi kumlea mtoto, mtoto naye huwajibika kumle mama yake.

  Jioni moja  alimuaga mama yake  kuwa alikuwa akielekea katika moja ya migahawa mikubwa kubarizi upepo, baada ya   mazoezi yake ya viungo aliyoyafanya kila siku.

 Ndani ya Mgahawa wa Night Café uliofurika watu wengi siku hiyo. Rweshabula alivuta kiti na kukaa.

“Shikamoo”, alimsalimia mzee mmoja aliyeketi karibu yake.

 Hata hivyo mzee huyo hakujibu kitu zaidi ya kuedelea kula chakula ambacho hakika Alibalio hakukitambua kwa haraka.

 Aliagiza soda na kunywa huku akiangaza macho yake huku na kule, lakini hakuona mtu yoyote aliyefahamiana naye usiku huo, alijisikia upweke  kwakuwa hata rafiki zake aliowazoea  hawakutokea siku hiyo.

 Alibalio alijaribu kurusha macho yake walau kumtambua vizuri mzee yule, akitaka kujua hasa ni mtu wa namna gani aliyekuwa akila chakula kwa kutumia vijiti viwili alivyovishikilia kwa vidole vyake vya mkono wa kulia.

 “Nimezoea kuona watu wakila kwa kwa mikono na hata kwa vijiko inakuwaje huyu anakula kwa kutumia vijiti!” alijiuliza.

 Lingine lililomsumbua kijana huyo ni kutokana na mzee huyo kutofanana na mtu mwingine kati ya watu waliofika katika mgahawa huo, ni mweupe lakini si mzungu maana yeye ni mfupi zaidi na pua yake haikuwa ndefu kama ya wazungu.

 Kichwani mwake kulikuwa na unywele mmoja mmoja mweupe,  macho yake madogo madogo lakini makali mithili ya chui awapo mawindoni,  kutokana na udadisi wake  Alibalio alihitaji kuwa karibu naye apate kumtabua vizuri.

 “Ni Mzee hasa mwenye busara, lakini mbona hakunijibu niliposalimia, au haijui lugha yetu?” Alibalio alijisemea kimoyo moyo na kuamua kumsalimia kwa lugha ya kigeni “Good evening Sir.”akikumbuka kwa uchache maneno ya Lugha ya kiingereza aliyofundishwa na marafiki zake,  hata hivyo Babu huyo alitingisha kichwa hakusema kitu ila aliendelea  kula chakula chake akitumia vijiti.

Hadithi na Simulizi za Watoto

Jishi Kijana Shupavu alivyotwaa zawadi ya Mfalme

Na Anti Lilian 

HAPO zamani za kale palikuwapo na fundi seremala mmoja aliyekuwa bado ni kijana mdogo, licha ya umri mdogo aliokuwa nao kijana yule aliweza kufanya kazi yake vizuri na aliipenda jambo lililo wafanya watu wengi  wamsifu kwa hilo.

Siku moja akiwa anaendelea na kazi yake, aliishiwa mbao, hivyo aliamua kwenda kutafuta mbao msituni. Kwa kuwa safari ilikuwa ya muda mrefu alichukua mkate na maji ya kunywa.

Aliweza kusafiri kwa muda mrefu sana katika msitu mkubwa na mnene pasipokuonana na mtu yoyote yule. Hatimaye alifika katika mti mmoja na akaamua kupumzika chini ya ule mti mkubwa, lakini kutokana na uchovu aliokuwa nao alipitiwa na usingizi mzito pale kwenye ule mti.

Alipokuwa katika lindi la usingizi ghafla alishituka kutoka usingizini  kutokana na sauti nzito iliyomuamsha na ndipo alipokuta mbele yake kuna jitu kubwa lenye sura ya kutisha limesimama mbele yake.

Kijana huyo aliogopa sana kwani alishasikia habari za jitu kubwa liishilo msituni ambalo huuwa watu. Lile jitu lilimuuliza kijana unataka nini huku msituni? Akalijibu “ninatafuta mbao, mimi ni fundi seremala”.

Lile jitu lilicheka sana kisha likamwambia “kijana usilete mzaha, wewe unaweza kukata hata mti?” yule kijana akamwambia “ninaweza kwani mara kwa mara nimekuwa nikikata kwa ajili ya kupata mbao”.

Lile jitu lilicheka tena kicheko kikubwa cha kebehi likachukua udongo ardhini na kuuminya kwa mkono hadi majimaji yakatoka. Likamwambia “kama na wewe ni kiumbe shupavu fanya kama mimi”.

Yule kijana akatoa mkate kwenye mfuko wake na kuumiminia maji bila lile jitu kuona na kisha akamwambia angalia, akauminya ule mkate hadi ukatoa maji, lile jitu halikuridhika, likachukua udongo mwingine na kuurusha mbali sana na kumwambia kijana na wewe ni zamu yako sasa rusha na wewe tusione utakapoangukia.

Yule kijana akasema, siyo mbaya kwani nimeona udongo umeangukia ardhini lakini mimi hautauona kabisa, kumbe yule kijana alikuwa tayari amemuona ndege aliyekuwa ametua karibu yake hivyo alimdaka yule ndege bila lile jitu kuona na akaliambia lile jitu kuwa sasa ona na mimi ninarusha udongo wangu, yule kijana akamrusha yule ndege kwa nguvu zake zote na yule ndege akapaa kwenda juu bila kushuka chini na akapotelea angani.

Lile jitu lilishindwa kuelewa ni kwanini kijana mdogo kama yule anakuwa na nguvu kiasi kile, bali akabuni njia nyingine akamwambia yule kijana sasa nataka tubebe huu mti tuupeleke kule ng’ambo, kijana akasema sasa itabidi wewe utangulie mbele na mimi ntabeba kwa nyuma huu mti, lile jitu likakubali likatangulia na kunyanyua ule mti kwa mbele na yule kijana akabaki nyuma.

Lile jitu kwa kuwa lilikuwa limetangulia mbele halikuwaeza kumuona kijana kutokana na ule mti kuwa na matawi hivyo yule kijana alipanda kwenye tawi la mti kule nyuma na kuliacha lile jitu likiwa limebeba ule mti peke yake.

Itaendelea