Riwaya

Miujiza Kisiwani (5)

Na Peter Dominic

Alikaa kimya ili fisi wasimuone maana ulikuwa  usiku wa mbalamwezi.

Kitendo cha fisi kuilalua maiti ya binamu yake kilimuhakikishia kuwa kweli binamu yake alikuwa amekufa kitambo maana fisi hawezi kumla mtu aliye hai.

Alikumbuka maana bibi yake mzaa mama aliwahi kumsimulia alipomtembelea.

“Safari ya wawili imekwisha, niko peke yangu sijui nitakwenda wapi? Bora ningebaki nyumbani nikabiliane na kifo cha kupigwa mawe kuliko kulaliwa na fisi, binamu umeniponza lakini na kusamehe,” alilalama na kusononeka moyoni. Ndege walianza kupiga kelele kuashiria kuwa ni alfajiri.

Aliteremka kwenye mti na kushuhudia vipande vya nyama vya maiti ya binamu yake. Hata hivyo hakuwaza kurudi nyuma maana ilionekana alikotoka ni kubaya kuliko anakokwenda.

Jibu la haraka ilikuwa ni kufikiria namna ya kuvuka ule mto.

Alilikokota lile gogo na kulilaza kwenye maji, halikuzama kama lile alilolipanda yeye na binamu yake. Alichukua mti mrefu uliokuwa pembeni yake ambao aliutumia kama kasia. Alikuwa amepiga hatua na alikaribia kuuvuka mto. Waswahili husema, siku njema huonekana hasubuhi.

Mbele yake aliwashuhudia viboko waliokuwa wakigombana. Walifukuzana kwa kasi ya ajabu huku muungurumo wa viboko hao ukiufanya mwili wake ushikwe ganzi. Kiboko mmoja kati yao liyezidiwa na mwenzake andiye alisababisha maafa kwa upande wake.

Alimpita kando kwa kasi lakini aliliguza gogo alilolipanda na kusababisha gogo hilo kuyumba na kujirusha katika maji yenye kina kirefu. Kwa ujasiri alilishikilia gogo hilo bila kuliachia na kufanikiwa kuliweka sawa japo  kasi yake ilikuwa imepotea.

Kwa mara nyingine tumbo lilianza kumuuma. Upepo mkali uliokuwa ukivuma ulimuwezesha kufika upande wa pili wa mto huo na yeye aliweza kufika salama. Wakati akifikiria yote akiwa haamini kama ameweza kuuvuka mto huo, mluzi wa mvuvi aliyekuwa akilelekea kulowa samaki ulimtoa katika lindi la mawazo.

Aligeuka na uso wake uligongana uso kwa uso na mvuvi huyo. Bila kuuliza mvuvi aligundua kuwa msichana huyo amefikwa na janga kubwa. Alikuwa hatamaniki. Nguo zilikuwa zimechanika na mwili wake umedhoofu kwa kukosa chakula.

Sauti ilimkauka hata alipoulizwa hakuweza kusema kitu zaidi ya kujishika tumbo lililokuwa likimuuma kwa njaa na kiumbe kilichopo tumboni mwake.  Kwa vile alikuwa akitetemeka kwa hofu na njaa. Mvuvi alikoka mota halaka na kumulekeza apashe viganja vyake kwenye moto.

Kwenye kikapu chake alitoa kibakuli kidogo kilichohifadhi ugali wa muhogo na mboga ya samaki. Nyamwiza hakusubiri kunawa, aliufakamia ugali huo kisha aliomba maji ya kunywa, kisha alishukuru na sauti yake ilisikika vizuri.

Alimsimulia kila kitu mvuvi huyo na kwa huruma alisitisha shughuli yake ya uvuvi na kuamua kuongozana na binti huyo hadi nyumbani kwake mita chache kutoka katika mji mkubwa uliokuwa na watu wengi ambao walikuwa huru, chakula tele tofauti na kule alikotoka.

Huko nyumbani wazazi wake walikata tamaa, matumaini ya kupatikana watoto wao wakiwa hai yalikwisha. Watu walizidi kuukimbia utawala wa Mfalme kitakwete, siku zilivyozidikwenda ndivyo hali ilizidi kuwa mbaya zaidi.

 Kitendawili kuhusu njaa iliyosumbua himaya ya mfalme hakikupata jibu. Baada ya kifo cha Lwamwasha  wa pili watabili  walikaa kimya wakihofia kuuawa.

  Baada ya maisha ya hapa na pale, huko ughaibuni Nyamwiza alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume.    

 Lakini hakuwahi kumueleza mwanae siri iliyojificha moyoni mwake richa ya udadisi wa mwanae.

 “Mhu….. mwanagu, usisumbuke sana kujua mambo ambayo yatakusumbua, ulimwengu huu una mambo mengi, ni bora tu umuheshimu kila mtu utakayekutana naye maana Baba zako na ndugu zako ni watu unaowaona humu.”

 Mara kwa mara alimweleza mtoto wake akimjengea heshima na busara za kuwaheshimu watu wote.

Kauli hiyo ilimjengea mazingira mazuri mwanae, alikuwa kijana mwenye heshima, pia Mungu alimjalia kipaji cha hali ya juu kwa kung‘amua mambo mapema.

 Wakiwa katika mji mkubwa na wenye watu wengi, tofauti na mazingira alimokulia mama yake, Alibalio Rweshabula  tayari alikuwa na majukumu makubwa ya kumtunza mama yake kama zilivyo mila nyingi za kiafrika. Baada ya mzazi kumlea mtoto, mtoto naye huwajibika kumle mama yake.

  Jioni moja  alimuaga mama yake  kuwa alikuwa akielekea katika moja ya migahawa mikubwa kubarizi upepo, baada ya   mazoezi yake ya viungo aliyoyafanya kila siku.

 Ndani ya Mgahawa wa Night Café uliofurika watu wengi siku hiyo. Rweshabula alivuta kiti na kukaa.

“Shikamoo”, alimsalimia mzee mmoja aliyeketi karibu yake.

 Hata hivyo mzee huyo hakujibu kitu zaidi ya kuedelea kula chakula ambacho hakika Alibalio hakukitambua kwa haraka.

 Aliagiza soda na kunywa huku akiangaza macho yake huku na kule, lakini hakuona mtu yoyote aliyefahamiana naye usiku huo, alijisikia upweke  kwakuwa hata rafiki zake aliowazoea  hawakutokea siku hiyo.

 Alibalio alijaribu kurusha macho yake walau kumtambua vizuri mzee yule, akitaka kujua hasa ni mtu wa namna gani aliyekuwa akila chakula kwa kutumia vijiti viwili alivyovishikilia kwa vidole vyake vya mkono wa kulia.

Hadithi na Simulizi za Watoto

Kisa cha Kadidi Kuumwa Nyuki (2)

Na Anko Peter 

Akauliza,  “…kwani tukiangua sasa hivi anatuona nani?” Mwenzake akakaa kimya huku akimuona mwenzake mtu mkaidi.

Kadidi hakusikia. Akauendea ule mwembe.

Akakwea juu na kuanza kuangua maembe yaliyokuwa yameiva vizuri.

Aliangua embe la kwanza na kulishambulia kwa meno. Akaangua embe la pili na kuliweka mfukoni.

Aliedelea kufanya hivyo hadi alipoona mifuko yote imejaa. Sasa akajiandaa kuteremka toka mtini.

Kumbe masikini ule mwembe ulikuwa umetegeshewa mizinga ya nyuki, nyuki walianza kumshambulia.

Wengine walimng’ata kwenye macho masikioni hadi akawa haoni hatimaye akaanguka na kugaragara chini na kupiga kelele za maumivu.

Mwenye shamba aliyeitwa Mzee Mande, alikuja mbio na kumkuta Kadidi anagaragara chini huku huku nyuki wakiendelea kumshambulia na kuanza kurundikana juu ya mwili wake hasa katika mdomo, masikio, mapua na mcho.

Rafiki yake alisimama mbali. Ingawa aliogopa, ajabu ni kwamba nyuki wale hawakumshambulia wala kumgusa.

 Rafiki huyo kipenzi wa Kadidi alikuwa akilia kwa uchungu kwani alikuwa nashuhudia rafiki yake anakufa kwa nyuki mbele ya macho yake.

Ghafla, Mzee Mande akafika huku akiwa na nyasi kavu zilizowashwa moto.

Akaanza kuwababua nyuki walewaliokuwa wanazidi kumgeuza kadidi kuwa kama mzinga mpya.

Hali ya Kadidi ilikuwa mbaya hadi akapelekwa katika hospitali ya Mji wa Mawe.

Akalazwa hadi siku ya nne aliporuhusiwa kutoka kurudi nyumbani.

Ndugu wote walimsikitikia kadidi ingawa hata rafiki zake walikuwa hawakosi kwenda kumjulia hali.

Kisha, wazazi pale kijijini kwao walikaa pamoja na watoo wao. Wakamtaka Kididi aeleze ilivyokuwa hadi akaumwa na nyuki.

Kwa kuwa alikuwa mtoto mkweli, akaeleza kila kitu. Huku akilia, akasema, “Baba na mama nisameheni kwa kuvunja mliyoniambia. Na wewe baba mwenye maembe nisamehe naomba radhi sitarudia.

Naomba mnisamehe na mniombee msamaha kwa Mungu.”

Mzee yule mwenye shamba akasema, “Wewe ni mtoto mwizi utakufa wewe… shamba langu lote nimeweka mizinga ya nyuki, mtu yoyote akitaka kuiba mazao yangu nyuki watamshambulia. Umeona sasa yaliyokukuta!” akasema.

Kisha akaongeza,” lakini kwa kuwa wewe ni mtoto mzuri ambaye umeomba msamaha na kuahidi kutorudia, nimekusamehe na hata wazazi wako watakusamehe, lakini usirudie tena maana unaona umebaki na makovu, ungekufa wewe.”

Wakiwa nyumbani, uso wa kadidi ulikuwa ukizidi kupungua uvimbe na Kadidi akabadilika na kuwa mtoto mzuri aliyewakataza hata wenzake wasipuuze maneno ya wazazi wao.

Kila mmoja wa rafiki zake, Kadidi alimwambia kuwa, “Mimi nimejifunza kuwa asiyesikia la mkuu, huvunjika guu na kwamba, siku za mwizi ni arobainI. Akawambia wenzake .

Kuweni waaminifu ili na nyie msiumwe na nyuki na kuwa kama nilivyo sasa maana daktari amesema uso wangu hautaisha uvimbe huu uliobaki.”

MWISHO