Miujiza Kisiwani (4)

         Na Peter Dominic

Mfalme aliitisha mkutano mkubwa wa kuwasaka vijana hao, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.Endelea  

Imani iliyokuwa imejengeka miongoni mwao kutokana na kisa cha watu kupotelea katika Kisiwa cha Miujiza ilihusishwa na kupotea kwa vijana hao, ilidhaniwa kuwa labda wale vijana ni miongoni mwa watu waliochukuliwa kimiujiza na kupelekwa katika Kisiwa cha Shoshwa.

Siku zilipita wazazi wa vijana hao walikuwa na imani kuwa watoto wao wako hai,  kila mara  walikifikiria namna ya kuwapata watoto wao.

Huko njiani akina Nyamwiza ambao walitoroka bila kuwa na chakula wala maji ya kunywa, walilazimika kula mizizi ya miti na kunywa maji yaliyotuama kwenye vijito.

Huko porini walikutana na hatari nyingi, lakini kwa utundu wa binamu yake, waliweza kupambana na kila jambo.

Usiku walilala kwenye miti ama kwenye mapango ambayo baada ya kuingia humo, waliziba milango kwa kutumia mawe.

Wakati mwingine binamu yake Nyamwiza alimfunga kwa kamba mwenzake ili asidondoke chini kwa vile mara kwa mara usiku walipita wanyama wakali wakiwamo Simba na Chui.

Walitembea kwa muda mrefu kikiwa ni takribani kipindi cha mwezi mzima. Mbele yao, waliona moshi mkubwa ukifuka upande wa pili uliotenganishwa na mto mkubwa.

 Matumaini yao  yalirejea kwani moshi uliashiria kuwapo kwa binadamu katika maeneo hayo.

Walijitahidi kutembea ingawaje miguu yao ilikuwa na majeraha mengi yaliyosababishwa na kuchomwa miba na majani yaliyochongoka. Kwa kipindi chote cha mwezi mzima hawakuwahi kuonja chakula kilichopikwa.

Moshi uliokuwa ukifuka kwa mbali uliwakumbusha chakula cha nyumbani kinachoandaliwa na mama.

Walitembea hadi walipoufikia mto mkubwa na mrefu usiokuwa na mwisho.

Binamu ndiye alikuwa tegemeo la safari nzima na hilo lilimpa faraja mwenzake.

Walifanya mashauriano kadhaa yaliyopelekea kupatikana kwa jibu kuwa watauvuka mto huo kwa kutumia gogo kubwa ambalo binamu angeweza kulitafuta kando ya mto huo.

Alipata gogo la kwanza lililokuwa kavu, lakini walipojaribisha kulipanda lilinyonya maji na kuzama, hivyo wakalazimika kurudi nyuma ili wasimezwe na maji. Wakarudi nchi kavu. Kitendo cha gogo kilipekea maumivu makali tumboni  mwa Nyamwiza. Alitoka jasho jingi huku akihema mfululizo hatimaye alipoteza fahamu.

Binamu yake aliikumbuka dawa ambayo  alipewa na bibi yake siku alipodondoka kutoka katika mti.

Bibi yake aliifikicha kisha alimnusisha mdomoni na yeye alipona bila kupelekwa hosptali.

Aliitafuta kandoni mwa mto kisha alirejea haraka, alimnusisha mwenzake, kutokana na ukali wa dawa hiyo, Nyamwiza alipiga chafya na kuzinduka.

Alipozinduka alimuita mama yake ambaye hakuwapo mahali hapo ili ampatie chakula. Yeye alisema anatamani ugali na majani ya kunde.

Binamu yake alijua mwenzake amechanganyikiwa na alianza kuangua kilio.

Kilio hicho kilimsaidia mwenzake, alifumbua macho  na kuanagalia sehemu waliyokuwapo ndipo akakumbuka kuwa walikuwa katika safari ndefu ambayo haijulikani mwisho wake.

Binamu yake alimbembeleza atulie na kuwa mvumilivu wakati yeye akishughulikia gogo la kuwavusha.

“Nyamwiza usiwe na wasiwasi, nina imani tutafika tunakokwenda moto ule unaouona upande wa pili ni watu wale,  tukifika watatusaidia, lakini tukifika huko tuwe wakarimu” .

Aliondoka kutafuta gogo. Baada ya kulipata alikokota kuelekea alikokuwa mwenzake, lakini kabla hajamfikia, nyoka mrefu mweusi mwenye sumu kali aliyesimama kwa kutumia mkia wake alimgonga kichwani na kutoweka kabisa.

Mugalula   Binamu yake Nyamwiza, alidondoka chini na gogo likampiga kichwani.

Nyamwiza aliyekuwa mbali kidogo alijikokota ili apate kumpa msaada. “Nina kiu kali naomba maji nisaidie nakufa.” Sauti ya huzuni ilisikika toka kinywani mwa binamu, alikuwa hoi baada ya sumu ya nyoka kupanda kichwani.

Nyamwiza alisahahu maumivu ya tumbo yaliyomkabili, alikimbia kuelekea mtoni. Alivua kipande cha nguo alichojifunga kiunoni kisha alikilowanisha kwa maji na kumkimbilia binamu yake.

 Alinyoosha miguu na kukiweka kichwa cha binamu yake kwenye miguu.

Alimuita ili apate kumkamulia matone ya maji kinywani mwake lakini siku ya kufa miti yote huteleza.

Juhudi za Nyamwiza hazikuzaa matunda, binamu yake alikuwa amefumba macho kabisa na hakuweza kutoa sauti wala kujitingisha.

“Amka maji haya hapa fumbua kinywa chako nikamue maji unywe,” Nyamwiza alimsihi mwenzake. 

Alimuweka chini na kuyaendea yale majani ambayo binamu yake alimtibu nayo baada ya kuzimia.

 Aliyafikicha majani kisha akamnusisha. Hata hivyo mwenzake hakuweza kupiga chafya wala kujitingisha.

Wakati huu binamu alikuwa haelewi chochote kinachoendelea, alikuwa amekata roho kitambo. Baada ya kuangaika kwa siku nzima bila kuona mafanikio yoyote, alihisi kuwa mwenzake amepoteza maisha.

Alilia kwa kwikwi, lakini hakujua amlilie nani, alikuwa peke yake mwituni na hakukua na mtu mwingine wa kumsaidia. Alimvuta na kumuweka kando ya mti mkubwa wenye matawi yaliyosambaa.

Roho ya ujasili iliutawala mwili wake, hivyo aliondoa woga wote na kujiandaa kwa lolote litakalomkuta. Aligundua kuwa eneo hilo si salama, majani yalianza kupata umande hali iliyoashiria kuwa ni majira ya jioni.

Alipanda juu ya mti huku maiti ya binamu yake ikiwa chini yake, lakini akiwa na matumaini kuwa labda mwenzake atazinduka usingizini. 

Alijituliza vizuri juu ya mti na kila mara alitizama mwenzake kuhakikisha yuko salama.

Kelele za fisi zilimzindua usingizini. Alipochungilia alishuhudia fisi wakigawana miguu na mikono ya maiti ya binamu yake.

Alikaa kimya ili fisi wasimuone maana ulikuwa  usiku wa mbalamwezi.

Kitendo cha fisi kuilalua maiti ya binamu yake kilimuhakikishia kuwa kweli binamu yake alikuwa amekufa kitambo maana fisi hawezi kumla mtu aliye hai.

Alikumbuka maana bibi yake mzaa mama aliwahi kumsimulia alipomtembelea.

“Safari ya wawili imekwisha, niko peke yangu sijui nitakwenda wapi? Bora ningebaki nyumbani nikabiliane na kifo cha kupigwa mawe kuliko kulaliwa na fisi, binamu umeniponza lakini na kusamehe,” alilalama na kusononeka moyoni. Ndege walianza kupiga kelele kuashiria kuwa ni alfajiri.

Aliteremka kwenye mti na kushuhudia vipande vya nyama vya maiti ya binamu yake. Hata hivyo hakuwaza kurudi nyuma maana ilionekana alikotoka ni kubaya kuliko anakokwenda.

Jibu la haraka ilikuwa ni kufikiria namna ya kuvuka ule mto.

Alilikokota lile gogo na kulilaza kwenye maji, halikuzama kama lile alilolipanda yeye na binamu yake. Alichukua mti mrefu uliokuwa pembeni yake ambao aliutumia kama kasia. Alikuwa amepiga hatua na alikaribia kuuvuka mto. Waswahili husema, siku njema huonekana hasubuhi.

Mbele yake aliwashuhudia viboko waliokuwa wakigombana. Walifukuzana kwa kasi ya ajabu huku muungurumo wa viboko hao ukiufanya mwili wake ushikwe ganzi. Kiboko mmoja kati yao liyezidiwa na mwenzake andiye alisababisha maafa kwa upande wake.

Alimpita kando kwa kasi lakini aliliguza gogo alilolipanda na kusababisha gogo hilo kuyumba na kujirusha katika maji yenye kina kirefu. Kwa ujasiri alilishikilia gogo hilo bila kuliachia na kufanikiwa kuliweka sawa japo  kasi yake ilikuwa imepotea.

Kwa mara nyingine tumbo lilianza kumuuma. Upepo mkali uliokuwa ukivuma ulimuwezesha kufika upande wa pili wa mto huo na yeye aliweza kufika salama. Wakati akifikiria yote akiwa haamini kama ameweza kuuvuka mto huo, mluzi wa mvuvi aliyekuwa akilelekea kulowa samaki ulimtoa katika lindi la mawazo.

Itaendelea toleo lijalo

 

Hadithi na Simulizi za Watoto

Kisa cha Kadidi Kuumwa Nyuki

Na Anko Peter 

KADIDI na Mpipi walikuwa marafiki waliopendana sana kiasi kwamba mtu asiyejua angeweza kuwaita mapacha ingawa hawafanani kwa sura.. Wote wawili walikuwa wanasoma Darasa la Tatu katika Shule ya Msingi ya Msokwe, iliyopo katika Mji wa Mawe.

Urafiki wao ulitokana na wazazi wao ambao pia wanapendana na kushirikiana kwa kila jambo.

Siku moja Kadidi aliweza kuruhusiwa kwenda kumtembelea rafiki yake na wakati mwingine angeweza kumaliza hata siku mbili huko yake na rafiki yake alifanya hivyo pia.

Wazazi wao waliwafundisha tabia njema na walikuwa wakiwaheshimu watu wote hata walimu walikuwa wakiwatolea mfano marafiki hao kwa wanafunzi wengine ili waige tabia zao.

Kama Kadidi angekuwa wa kwanza, rafiki yake angekuwa wa pili katika mtihani, hivyo walimu waliwapenda sana na kuwapa zawadi mbalimbali. Hata wazazi wao, pia walifanya hivyo.

Siku moja Kadidi aliomba ruhusa kwa wazazi wake ili akamsalimie Babu yake aliyekuwa akiishi kijiji cha jirani. Wazazi wake walimruhusu kwa sababu ulikuwa wakati wa likizo.

Kadidi alifurahi, lakini hakupenda kumuacha rafiki yake, hivyo alimuomba Mama yake akamuombee ruhusa ili afuatane na rafiki yake.

Wote wawili waliruhusiwa wakapewa  kibuyu cha maji ili wasipate kiu njiani, lakini hawakupewa chakula kwa vile safari ilikuwa fupi mno kiasi cha saa moja tu, kufika alipoishi babu yao.

Njiani Kadidi alipatwana njaa kali. Akamwambia mwenzake, “Rafiki yangu, twende tukaangue maembe ili tule. Mimi nasikia njaa sana.

Mpipi akamkubusha namna wazazi wao walivyowakataza kuchukuia au kupewa vitu vya watu ambavyo hawakupewa.

Akamshauri kuwa, waende katika nyumba zile za jirani ili waombe maembe kuliko kuiba.

Kwa bahati mbaya, siku hiyo Kadidi akamuona rafiki yake kama mtu mjinga na muoga.

Itaendelea