Make your own free website on Tripod.com

Miujiza Kisiwani (6)

         Na Peter Dominic

Alimaliza soda yake na kutoka nje ya mgahawa huo. Aliondoka nyumbani akipita ile njia ya miguu katika Mtaa wa Masikini mwendo wa robo saa hivi hadi kufika kwao.

 Dakika kama tano hivi zilizofuatia, akiwaza namna ya kukabiliana na mambo mengine ya maisha, kwa mbali alimuona mtu akikimbia nyuma yake, ulikuwa ni mwendo wa kawaida lakini ulimshtua kidogo, hata hivyo hakujali sana. Aliendelea na safari yake.

 Aligeuka tena kwa mara ya pili safari hii mtu aliyekuwa akikimbia tayari amesimama karibu upande wake kulia, aligeuka kumuangalia vizuri akatahamaki kuona mbio hizo zilikuwa zikitimuliwa na Babu aliyemuacha akila katika mgahawa wa Night Cafe.

 Bila shaka ilikuwa muda mzuri kwake kutimiza ndoto yake maana tangu awali alikuwa na shauku ya kuwasiliana naye ana kwa ana. Hata hivyo ukitegemea hili linaweza kuja lingine, “kibabu hiki hakivumiliki kukiangalia hata kwa macho!” alinungunika kimoyomoyo.

 “Nina hakika wewe pia ulihusika kumuangamiza mke wangu?” Sauti ya hasira ilitoka katika kinywa cha  Babu. “Mke wako yupi Babu!….Ni mara yangu ya kwanza kukuona, sijui unamzungumzia Mke wako yupi?” aliuliza.

 “Hata mke wangu mlimuua kikatili sikutegemea jibu la swali langu, nilijua na niliamini kuwa nyinyi ni wakorofi na wakatili, huu ndiyo mwisho wa ubabe wenu.” Kilitamba kizee hicho na wakati huo kikijiandaa kwa kujinyoosha viungo vyake mithili ya paka aliyekuwa usingizini.

 Akili ya Alibalio ilitambua mara moja kuwa hapa hapakuwa na mchezo tena. Kwani hata angemueleza vipi asingesadiki, alijiweka tayari kwa lolote. 

   Halikuwa tatizo sana  kwa kijana huyu maana hata hivyo alikuwa akijifunza mazoezi ya kujihami bila siraha.

Aliweza Barabara kuitumia mikono na miguu yake maana hata zilipotokea   vurugu katika sherehe ya rafiki yake Nicson aliwatuliza vijana  wa kihuni waliotaka kuharibu shughuli ya rafiki yake.

 Alibalio ni mwepesi na aliutambua vema mchezo wa karate, aliumudu kwa stahili ile ile yaTaikodo. Siku zote mcheza karate huhitaji kutumia muda wake mwingi kufikiri kabla ya kuamua, hupigana kwa makini akichunga vema adui yake.   Kwake halikuwa jambo la haraka kuamua kupigana na kikongwe hicho ambacho richa ya kukiheshimu alikidharau na alifikiria angeweza kukiua.

 Wakati akifikiria yote haya bila shaka alikuwa amechelewa, yupo chini anajizoazoa kujiweka sawa. Teke la pili lilitua balabala katika paji lake la uso, halikumpa nafasi ya kuona vizuri tena.

 Alirusha teke moja la (mawashi)  kubahatisha lakini kibabu hakikuwepo tena kama alivyokusudia, kimeruka juu kwa kutumia mtindo fulani wa sarakasi na kikijizungusha mara mbili kwa na kutua upande wa pili mbali na alipokuwa.

  Safari hii Alibalio akijipanga vizuri na kuweka sawa viungo vyake,  labda niseme kilikuwa kimbunga, dhoruba na upepo, kibabu kiliruka juu huku kuvurumisha mateke heweni mithili ya mbayuwayu  anayesherehekea kitoweo cha kumbikumbi. Mateke   yote yalitua barabara katika mwili wake.

 Sasa yuko chini anagaragara kwa maumivu hakuwa na uwezo tena wa kufanya lolote, kibabu kimekaa kitako pembeni huku kikichukua sigara iliyokuwa katika kijimkebe kidogo na kuiwasha kwa kutumia kiberiti cha gesi.

 Baada ya kuvuta pafu mbili na kutoa moshi mkubwa hewani kupitia katika pua zake na kuvuta hisia fulani, kilisimama na kumungalia kwa makini kijana huyu.   Rweshabula alikuwa chini akigaragara kwa maumivu makali, maana ilikuwa afadhari kupigwa kwa rungu la polisi kuliko kukumbana na teke la kibabu hichokwa jinsi miguu ilivyokomaa.

 “Ni afadhali kupigwa kwa mpini wa jembe la mkulima kuliko  kukumbana na teke la kizee hiki,”  Alibalio alijisemea kimoyomoyo. Hata hivyo alihisi lile zoezi la kukomaza mikono kwa kujipigapiga na fimbo fupi au kukalia miguu kwenye kokoto. Kwa   wacheza karate wanatambua hilo wawapo kwenye dojo.

 Ni kibabu hasa kimezeeka lakini shughuli yake ni pevu, Rweshabula alikuwa amelala chini na uso wake ulianza kuumuka, jicho lake la kushoto lilikuwa halioni vizuri baada ya kuvimba na kufumba kabisa, alilazimika kutumia jicho moja la kulia.

 Alijizoazoa na kukaa kitako,  alimuangalia vizuri yule Babu, akili yake ilimtuma kuomba msamaha na ikibidi akili kosa ingawa yeye hakuhusika na tuhuma za mauaji ya mke wa kibabu hicho.

 Wakati akijieleza kibabu kilipanda mzuka ghafla, kilisimama na kuanza kurusha mateke kadhaa hewani kwa kasi ya ajabu, mateke hayo hakika yaliambatana na upepo mkali na Rweshabula alikuwa akishuhudia kila kitu. Alitafakari haraka na kutambua kuwa hii ilikuwa nafasi yake ya mwisho kujitete vinginevyo angeungana na marehemu waliomtangulia.

 Wakati kijana huyu akijaribu kujitetea walau kuhepa kipigo cha Babu. Tayari mzuka wa Kibabu ulianza kupoa, kilichukua  sigara yake na kuvuta, ilikuwa ikitoa harufu kali iliyomfanya Alibalio kupiga chafya zilizoambatana na muwasho wa koo. 

 Kikongwe huyu alisogea na kutoa kijimkebe kingine katika kijimkoba chake cha ngozi ya simba kilichochakaa alimungalia Alibalio ambaye jicho lake lilikuwa taabani. Alitoa viungaunga fulani ambavyo hata hivyo Rweshabula hakuweza kuvitambua mara moja.

 Alivichukua vile vidawa na kuanza kulifikicha jicho lake kwa kutumia kipande kidogo cha kitambaa. dawa hiyo ilikuwa kali na chungu katika jicho hilo lililopata mkog‘oto,  ilikuwa inauma sana lakini hakuwa na budi kuivumilia kwani licha ya kipigo sasa alihitaji kupona.

 Alipata  nafuu hivyo waliondoka kuelekea sehemu ambayo Alibalio hakuifanamu, jua lilikuwa limezama na nuru iliruhusu giza kuchukua nafasi yake.

Hadithi na Simulizi za Watoto

Jishi Kijana Shupavu alivyotwaa zawadi ya Mfalme(2)

Na Anti Lilian 

Baada ya kitambo kidogo lile jitu lilisema nimechoka tupumzike hapa kidogo, yule kijana kwa haraka alishuka kwenye lile tawi la mti na kisha akaliambia lile jitu kuwa kumbe wewe huna nguvu yaani umechoka mara hii?.

Lile jitu halikuwa na la kujibu bali lilibaki likimuangalia yule kijana ambae hakuonekana kuchoka.

Lile jitu likamwambia yule kijana, twende mbele kuna mti una matunda mazuri sana, walipofika katika ule mti lile jitu likapanda juu ya ule mti kutokana na uzito wake basi matawi ya ule mti yote yakashuka na yule kijana akawaamepata urahisi wa kuchuma matunda mengi sana.

Baadae lile jitu lilishuka na kitendo cha kushuka tu matawi yote yakaenda juu, lile jitu likamwambia yule kijana kuwa, yaani wewe huwezi hata kushikilia tawi hata moja, yule kijana akasema ninao uwezo, lakini pia huwa nafanya mazoezi ya kuruka juu kwa urefu mkubwa je wewe unaweza, lile jitu likajibu kuwa ndio naweza.

Basi yule kijana akaliambia lile jitu liruke juu na likafanya hivyo lakini  wakati likirudi chini mguu wake mmoja ulinasa kwenye tawi kubwa la mti na hivyo lilianguka vibaya sana.

Hapo Mfalme na watumishi wake ambao walikuwa wanapita wakaona lile jitu linaanguka. Mfalme akauliza kuna nini? Ni swali ambalo alimuuliza yule kijana aliyekuwa karibu na ule mti ambao lilikuwapo lile jitu.

Yule kijana akamwambia Mfalme “nimelikamata hili jitu lililokuwa likitishia katika himaya yako Mtukufu Mfalme”.

Mfalme aliposikia hivyo alifurahi sana kwani lile jitu lilikuwa tishio kwa watu waliokuwa wakiishi katika nchi yake akawaamuru watumishi walifunge minyororo na kuliburuza na kisha wachimbe shimo kubwa walichome moto na majivu yake wayafukie.

Baada ya saa kadhaa habari za ushupavu wa yule kijana zilienea katika mji wote kwamba kijana mdogo amelikamata lile jitu hatari na kuliua.

Mfalme alimfanyia sherehe na kumzawadia zawadi ya kiboksi kilichojaa dhahabu ndani yake na tangu hapo yule kijana aliachana na kazi ya useremala na akawa na maisha mazuri na aliweza kuishi na wazazi wake raha mstarehe.