Sio Lazima Afe Lakini...(4)

Happyness Ndaro ameeleza bayana azima yake ya kutaka Mzee Ndaro auawe ili mali zinazodaiwa kuporwa kwa mama yake mzazi na kumsababishia mama huyo kifo, zimrudie yeye na kamapani yake. Nini kitaendelea, fuatilia hadithi hii ya kusisimua.

Na Gerald Lwomile

Happyness Ndaro ni msichana ambaye kwa kipindi cha kujuana kwetu, tumefanya naye mambo mengi ikiwa ni pamoja na kwenda naye katika matukio ya hatari zaidi hivyo, naye alikuwa amekwisha ambukizwa sumu ya uhatari na amekwisha kuwa mzoefu wa kushudia mauaji na maasi kadha wa kadha yakifanyika.

Hakuwa mtoto mayai, bali ni mwanamke aliyepewa roho ya kiume. Endelea na hadithi hii ya kusisimua.

Toka Moshi, dereva alikanyanga mafuta hadi Arusha ambapo abiria wote waliteremka kuashiria kuwa huo ndio uliokuwa mwisho wa safari yao. Hali hiyo, iliwapa fursa abiria wengine kujipatia usafiri huo huo kwenda waendako.

Licha ya usumbufu mbalimbali tuliupata njiani wa hapa na pale ambao ni wa kawaida tu kwa wasafiri, bado tuna kila sababu ya kumpongeza dereva kwa kumudu kutufikisha salama tulikokutaka na tena, kwa wakati muafaka. Yalikuwa ni majira ya saa 1:30 jioni.

Mjini Arusha tulikaa kwa takribani nusu saa hivi kisha dereva akaanza "kuikodolea macho barabara" na karibia saa nzima na kitu, tulikuwa kimya ndani ya gari tukishuhudia namna alivyo na "usongo na mbio za kufukuzana na hewa".

Wote katika kikosi chetu tulikuwa makini kusubiri yeyote baina yetu atakayeona kuwa sasa umefika wakati muafaka wa kutimiza kusudio letu, atoe ishara na kazi ianze mara moja.

Hayawi hayawi, huwa na hatimaye kama yalivyo makubaliano yetu, Benson Momo alichomoa kiberiti chake cha gesi toka mfuko wa shati na kukiwasha kana kwamba alitaka kuvuta sigara.

Waliojua kuwa anataka kuvuta sigara yake aina ya Embassy, walijua hivyo, na hata wale waliojua vinginevyo, nao walijua wajuavyo mradi tu, sisi wenyewe tulijua tujuacho.

Nikisha uona mwanga, nilimsogelea dereva wa basi letu kama mtu niliyetaka kumuomba msaada ili asimamishe gari nikajisaidie haja ndogo.

Nikamuinamia huku naye ametegesha sikio kwa chati ili asikie kama ninajua kuomba kwa adabu, asimamishe gari na abiria wengine wenye shida kama yangu watumie nafasi hiyo muhimu kama ingetolewa.

"Bila jaribio lolote la ubishi wala upinzani, weka gari pembeni," niliamuru kwa sauti iliyoashiria kuwa hivi sasa roho yake imening’inizwa katika uzi mwembamba sana ambao unaweza kukatika wakati wowote akitaka hali hiyo itokee.

Akatii mara moja na kufuata. Ingewezekanaje asifanye hivyo wakati sasa hata aliyenifahamu kuwa ni Fema, alijua sio Fema Oroginal., anayemjua sasa angeweza kudhani ni Fema Photocopy?

Wakati huo, bastora yangu ilikuwa ikilinong’oneza sikio la dereva huyo juu ya taarifa za mauti yanayoweza kumfika wakati wowote endapo atafanya jaribio la kuleta jeuri.

Ni dhahiri kifo hakina rafiki na ndiyo maana hata anapofariki mtu, wanaolia wanalia sana na wengine kuzirai na kujigalagaza chini, lakini hakuna hata mmoja anayesema: marehemu tulikuwa tunapendana sana, sasa naomba tuzikwe pamoja nikiwa hai ili tuendeleze uhusiano wetu kaburini, hilo halipo.

Sauti ya risasi mbili zilizopigwa hewani ilisikika na kufuatiwa na sauti niliyoitambua kuwa ya Benson Momo.

"Haya! Abiria chini teremka chini, lala kifudifudi haraka. Mwenye ubishi ajue anaomba mauti ya ghafla". Momo akatulia.

Abiria wote waliteremka na hata aliyetaka kujenga wazo la kutoroka baada ya kushuka, wazo lake liliyeyuka mithili ya barafu iliyowekwa kwenye jiko la umeme likiendelea kuwaka.

Kwanini lisiyeyuke hali Happyness alikuwa chini, amevaa unyama kuliko hata ule wa wanyama wenyewe wa mwituni?

Nasema hivyo maana ingawa Happyness katika mazingira ya kawaida ni msichana anayetazamika vema na kuvutia kila mmoja kuwa na urafiki naye lakini siku hiyo alikuwa "amechacha" mithili yamboga za juzi zisizochemshwa hata kidogo.

Alikuwa hatazamiki wala hajadili na mtu; kwake, hakuna mjadala, kongamano wala warsha. Alichojua na kukiri ni kwamba, kila abiria anayeteremka, analala chini tena kifudifudi.

Wapo wachache waliofanya jaribio la kumdharau kwa kuwa eti ni mwanamke; kawaulize yaliyowapata na kwamba ni wakati gani walipata fahamu na kuzinduka toka katika usingizi ule mzito wenye ndoto zinazoionesha dunia kujaa damu tupu.

Katika kipindi hicho, wote watatu tulikuwa tukifanya kazi mithili ya mchwa na nyuki, hakuna dakika hata moja ya kupoteza wala kuchezea.

Nilipanda juu ya keria na kuvimwaga vitu vyote vilivyokuwa katika begi lile kubwa.

Mimi na Happyness tulianza upekuzi wa kina kwa kila abiria huku wengine wakijisalimisha wenyewe kwa kutoa walivyo kuwa navyo na kwa mpango maalumu.

Bensom Momo alikuwa kasimama kando kwa makini akimsubiri mbishi ili "wajadiliane" kuwa ni nani mbishi zaidi kuliko mbishi mwingine.

Kila tulichokidhani kuwa ni pesa au chaweza kuwa na pesa taslimu au kimebeba bidhaa "inayolipa", tulipakia ndaki ya begi. Tayari lilikuwa limefikia robo tatu ya ujazo wake.

Nilimtupia jicho, Momo akaonesha ishara ya kutuambia tutokomee porini na kwamba naye angefuatia punde tu.

Mdomo wake ukasisitiza tena kama uliosema kwa sauti ya chini, "Kimbieni! Ishieni harakla nitafuata!"

Tuliishia porini tukimuacha na wale mateka wake kwa dakika kadhaa. Aliporidhika kuwa tumetokomea vya kutosha, pasi wao kujua huku wameendelea kulala kifudifudi, akawatoroka na kuwaacha wanaendelea kuuchapa usingizi huo usio rasmi. Akatufuata na tukaungana naye.

"Jamani kama tulivyosema siku ile, mambo sasa yamekwisha anza. Tukifanya mzaha wa aina yoyote, tumekwisha. Kwa hiyo wewe(Happyness), nenda barabarani. Utumie ujanja wowote unaobidi kutumika, lakini cha msingi tupate usafiri wa kutuondoa huku porini," Momo akasema huku akitweta kidogo na jasho kidogo la ukali na lile la umakini likimtoka.

Hakuna aliyeona kuwapo kwa sababu ya ubishi. Happyness akatekeleza kama alivyoambiwa na akatuacha sisi tukila ambushi pamoja na begi letu lenye kiasi tusichokijua cha kitita na baadhi ya vitu vya thamani. Begi lilikuwa mikononi mwangu.

Takribani dakika 22 hivi zilikuwa zimekwisha yoyoma huku sisi tukiwa walinzi wa pori hilo. Sasa nasi tulikuwa roho juu maana hatujui wale wahanga wa utekaji wetu watakuwa sasa wameamua na wanafanya nini dhidi yetu.

Mwanga mkali wa taa za gari ulionekana kulipasua anga lililokuwa limetawaliwa na giza totoro. Mwanga uliashiria gari dogo likija eneo lile likitoka tulikofanya amaasi yetu.

Happyness alikuwa na kila sababu nzuri ya kuhofu kuwa huenda hao ni askari polisi waliopewa taarifa kwa nia yoyote juu yetu na sasa wanafuatilia, lakini alijua dhahiri kuwa UKITAKA UZURI, SHARTI UDHURIKE hivyo, hakuwa na sababu yoyote ya kumfanya aogope kulisimamisha gari hilo.

Sisi wenyewe tulimjua Happyness kama msichana mwenye "nyama nzuri ya ulimi" hivyo, hata kama wangekuwa kweli ni askari polisi wanaofuatilia nyendo zetu, Happyness hangekosa "kamba za kuwafunga japo ni karatasi, lakini zikafanya kazi bora kama kamba za waya".

Happyness alijianda kukaa mkao wa kula na kisha akalipungia mkono gari hilo ishara ya kuomba msaada. Dereva hakuwa na hiyana, akakanyanga breki na gari likaitikia wito wa kusimama ili kujua kulikoni msichana huyo awe katika mazingira yale na kwa kipindi kama hicho.

Sote tulikurupuka huku bastora zetu zikiwa zimemlenga dereva wa gari hilo aina ya NISSAN PATROL la rangi ya kijani iliyochanganyika na bluu na kizuri zaidi, gari hilo lilikuwa na kila sifa ya kuaminika kuwa ni jipya sana.

" Hatufanyi biashara ya kubembelezana wala kushauriana. Mjadala wetu ni kifo. Achia funguo na teremka haraka," Momo akasema huku akimvuta dereva huyo aliyekuwa peke ndani ya gari na hali hiyo, ikamfanya dereva huyo adondoke chini.

Hatua ya kumvuta dereva huyo ilitokana na jaribio la ubishi alilofaya dereva yule na hata kilichoendelea hatujui bali mimi ninachokumbuka tu ni kwamba, hadi tunaondoka pale dereva yule alikuwa amelala na wala asijitingishe. Hadi sasa sijui nini kiliendelea.

Momo alipanda gari hilo, "akalitekenya. Lilipokolea kicheko cha ghafla", akaliondoa kwa mwendo ambao sio siri, hata mimi nilikuwa nimeshikilia roho yangu mkononi.

Gari hilo lilizidi kutamba kwa kasi ya kutisha juu ya barabara iendayo Namanga na majira ya saa tano na nusu hivi usiku huo, tayari tulikuwa katika eneo tarajiwa la Mpakani- Namanga.

"Ehe! Namanga ndio hii, sasa tuambie huyo ndugu yako Steven anaishi maeneo gani tufanye kazi yetu sisi," Momo akaunguruma kumuuliza Happyness.

"Kule eneo la Mabondekuinama," Happyness akajibu. Toka hapo ikawa ni kulia na kushoto hadi tulipoifikia nyumba ya kaka yake Happyness (Steven).

Ingawa Steven alikuwa miongoni mwa watu wanaomiliki pesa na mali nyingi katika eneo lile, bado alikuwa miongoni mwa watu ambao jamii huwatania kuwa wakati wowote wanaweza "kufa kibudu" kwa maana kuwa, hawajashiriki sakramenti zile za msingi katika Kanisa ama Ubatizo, au Ndoa.

Alikuwa na mtumishi wa ndani ambaye alikuwa kijana wa kiume. Huyo, alikuwa akimsaidia shughuli mbalimbali za ndani ikiwa ni pamoja na mambo ya usafi wa nyumba na mavazi yake; kufua na kunyoosha nguo.

Hata hivyo, kwa kawaida kijana huyu mfanyakazi hakuwa akilala pale nyumbani kwa Steven na badala yake, kila baada ya saa za kazi alikuwa akikabidhi funguo katika nyumba moja ya jirani na kuisha yeye kuondoka.

Ilkuwa wazi kuwa kwa kuwa Steve na Happyness wanajuana dhahiri kama dada na kaka, hata kama ingekuwa usiku wa giza ambalo fisi anaogopa kutoka vichakani, Steven asingesikia sauti ya Happyness ikiomba kufunguliwa mlango, eti asifungue.

Basi tukahesabu kuwa kwa kiasi fulani, ushindi tunao mikononi mwetu. Tukaona ni vema Happyness atangulie yeye, na kisha baada ya mlango kufunguliwa, tutaingia wote kama wageni rasmi.

Sisi tulibaki tumejibanza ukutani. Happyness aliuendea mlango kwa hali ya kawaida na kubonyeza kengele ya mlangoni.

Baada ya dakika kadhaa na Steven alipokwisha baini ukweli kuwa alikuwa anaongea na nduguye, alifungua mlango na kumkaribisha Happy.

Wakakaa pale sebuleni huku akiwa na hamu ya kujua sababu za ujio wa Happyness usiku huo.

Kabla Steve hajaongea lolote, Momo akiwa mbele nami nyuma, tuliingia ndani tukiwa tumielekeza midomo ya bastora zetu moja katika kichwa, na nyingine katika kifua cha Steven.