Make your own free website on Tripod.com

Sio Lazima Afe Lakini...(3)

Happyness Ndaro ameeleza bayana azima yake ya kutaka Mzee Ndaro auawe ili mali zinazodaiwa kuporwa kwa mama yake mzazi na kumsababishia mama huyo kifo, zimrudie yeye na kamapani yake. Nini kitaendelea, fuatilia hadithi hii ya kusisimua.

Ninasema hivi maana kwa jinsi ninavyohisi, shughuli hii ni kubwa, kwa hiyo malipo yatategemea wepesi au ugumu utakaoonekana katika kazi hii."

"Sijui kama nimekujibu shemeji ?" Akauliza huku akinitazama kwa macho ya msisitizo ili ama nikubaliane naye, au nikatae, ajue moja.

"sawa umeeleweka lakini, kwanini usitueleze bayana kuwa ni mtu gani huyo unayemhitaji na ni yupi usiyemhitaji ili wakati shughuli inaanza, ianze moja kwa moja," Benson Momo aliyekuwa kimya kwa muda mrefu," akasema.

"Mmhhh! Sina shaka kuwa hakuna yeyote kati yetu asiyekubaliana nami kuwa kitu muhimu tunachokihitaji hapa ni pesa. Sasa kama ni hivyo, lazima tuanzie penye uwezekano wa kupata nyingi halafu kwingineko kunafuatia," Happynes akasema.

Akaendelea, "Suala la ni nani ninayemhitaji na ni nisiyemhitaji, ni pesa kwanza. Kama kuna mtu ataonekana kuleta upinzani utakaotukosesha pesa, huyo ndiye ninayemhitaji ili naye atangulie Ahera. Amfuate Marehemu mama" happyness akasema kwa ghadhabu.

"OK. Tumekuelewa ila napenda nikushauri namna ya kuendesha shughuli nzima," Momo akatulia kidogo. Akatuangalia usoni ili kujua umakini wetu katika kumsikiliza. Akabaini kuwa upo wa kutosha.

Akaendelea, "Itabidi tupande moja ya mabasi yake, linaloondoka hapa Moshi sa 10:00 jioni. Tutakapofika porini, tutaliteka na kuwanyang'anya abiria wote kila kitu kinachoitwa pesa watakachokuwa nacho. Kisha, tutatokomea porini," Masikini bila hata kujali kuwa tunawakosea wanadamu wenzetu na kikubwa zaidi tunapanga mipango inayomkana Mungu na kuvunja Amri yake ya upendo, tukazidi kujadili.

Bwana Momo akaendelea, "Tutasogea mbele kidogo. happyness utasimamisha gari lolote bila kujali linatoka au linakwenda wapi.

Ninaamini dereva akikuona mwanamke porini, ataamini kuwa kuna masaibu yamekufika na sasa unahitaji msaada; atasimama tu.

Hilo ninaamini litakuwa hivyo," akatulia kidogo kututazama na tulitikisa vichwa ishara ya kukubaliana na maneno anayoyasema.

Akaridhika na kuendelea, "Sisi ambao wakati huo tutakuwa tumejificha, tutavamia ghafla na kufanya linalowezekana. hatutajali watakuwa vipi hao wenye gari, maana Waingereza wanasema, NO EASY TASK( yaani hakuna kazi rahisi)."

"Dereva itabidi aende, atangulie afe ili asitutilie usiku. sasa hilo gari lake ndilo tutakalotumia kwa shughuli zetu kwenda kote tunakohitaji," akasema.

"Kwa kuwa wakati huo utakuwa usiku, tutakwenda moja kwa moja hadi kule Arusha tuonane na huyo kijana wake (Steven) na kuchukua hizo pesa za duka la spea za magari.

Tutachukua kila alichonacho na bila kupoteza muda, tuatarudi moja kwa moja na kumpitia huyo rafiki yake mpakani Namanga.

Kama mambo yatakwenda kama tulivyopanga, mnamo saa 9:00 hivi usiku tayari tutakuwa sasa tupo ndani ya mji wa Moshi kumalizia zoezi na kumrudia Mzee Ndaro, au unasemaje Happy?" Benny akauliza.

"Lakini mimi kwa upande wangu, sioni sababu ya kumuua Mzee Ndaro , labda la msingi ni kwamba tukifanikiwa kupata hicho kitita, tuviteketeze hivyo vitumishi vyake vyote na kuiangamiza kabisa familia yake, bila kujali ni nani, na amekosa nini na yeye mwenyewe, tumkamate na kumhoji mzima mzima atueleze kwanini alifanya hivyo." Bila huruma wala kujua kuwa ninamkosea Mungu kwa ushauri huo, nikashauri huku nikimtazama happyynes usoni.

" Sawa maana hata asipokufa yeye, lakini ataonja machungu ya kufiwa ndugu na wapendwa wake kwa wakati mmoja yaani awe na misiba misibani.

na lazima ajue kuwa haya ndiyo madhara ya kuwa na uroho wa mali badala ya kutafuta kwa njia halali na kutumi a nguvu na akili alizojaliwa mtu na Mungu."

"...Kila atakapowakumbuka, nafsi yake itamsuta kwa kuwa ni yeye na uroho wake ndio wamesababisha roho hizo za awapendao ziteketee namna hiyo akasema huku uso wake ukionekana kupauka kidogo kutokana na umakini na huzuni aliokuwa nao katika mazungumzo hayo.

"sawa," nikasema huku nikisimama na kujinyoosha ishara ya kuondoa uchovu uliotokana na kukaa muda mrefu bila kunyanyuka. Nikaongeza,

Nadhani kila kitu kimeeleweka labda tu, tupange siku ya kuanza shughuli,"

"Leo mabasi mengi hayapo; yanategemewa kurudi kesho.

Kwa hiyo mimi napendekeza shughuli hii ifanyike keshokutwa. Mipango yote ya safari nitaiandaa mimi na nitawajulisha ikishakamilika" Happy akamaliza nami nikaaga na kuondoka nikiwaacha Benny na Happyness mle chumbani.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Ilikuwa Jumanne majira ya saa 9:45 hivi, alasiri.

happyness alikuwa tayari amekwisha kata tikiti za basi hilo liendalo Arusha.

Tikiti ya Benson Momo ilimruhusu kukalia kiti namba 32 na yangu ilikuwa namba 3. happyness alikaa karibu kabisa na mlango wa abiria.

Kila mmoja wetu alikuwa makini kuzikumbuka na kuzitumia ishara zote tulizokubaliana kuzitumia kwa mawasiliano baina yetu.Kila mmoja wetu alikuwa makini asipoteze nafasi na jukumu lake kama tulivyokabidhiana.

Basi, kila mtu kwa wakati wake, aliingia ndani ya basi hilo lilokuwa limeegeshwa kwenye egesho lake maalumu.

Baada ya muda si mrefu, dereva aliingia ndani ya basi na kukalia kiti chake. happyness alikuwa akiendelea kununua vopochopocho vidogo vidogo dirishani vikiwamo biskuti, juisi na, samaki wa kukaanga na karanga.

kama ilivyo kwa abiria wengi wanavyopendana mithili ya wavuta sigara wasionyimana hata kama ikibidi kugawana sigara, happyness anaye aliwagawia baadhi ya abiria vile alivyonunua.

Kwa mara nyingine nilimtupia jicho na kumshuhudia akiwa amembeba mtoto wa abiria mwingine waliyekuwa ameketi kiti cha jirani kidogo.

Alikuwa mtoto wa miezi takribani minane hivi. Mnene, mwenye nywele nusu kichwa na aliyevutia kila abiria kumbeba kuokana na afya yake na unadhifu hata wa mavazi aliokuwa nao.

Dereva alilitekenya gari hilo na kuanza kuondoka taratibu. Kila mmoja wetu alifanya kila awezalo ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu hata mmoja anayebaini mpango wala uhusiano wetu wala hatukutaka kwa namna yoyote, yeyote kati yetu aonekane tofauti.

xxxxxxxxxxxxxxx

Kabla ya kujihusisha na shuhuli hizi haramu, kwa siku za nyuma, Benson Momo alikuwa miongoni mwa askari wa jeshi la Ulinzi wa Wananchi (JWTZ).

Alikuwa na uzoefu wa mambo mengi ya hatari na pia, alikuwa mwepesi kutokana na mazoezi mbalimbali aliyokuwa akifanya.

Alikuwa na uwezo wa kupanga hata chupa kwa umbali wa mita hamsini na kisha akaanza kulenga mifuniko yake na kuipiga bila kupiga chupa zenyewe kwa mawe.

Mimi sikuwa na makuu zaidi ukiachilia mbali kale kauzoefu nilikopata wakati nikiwa JKT miaka kadhaa iliyopita na kaujanja ujanja nilikokuwa nako ka kuzaliwa nako.

Hivyo, basi katika maswala kama haya, sikuwa na wasiwasi wowote. labda kikubwa zaidi cha kuongezea ni kwamba tangu tuungane na Momo katika mambo haya, utaalamu na ukatili wangu katika maisha haya yanayokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu, umekuwa ukiongezeka siku hadi siku.

xxxxxxxxxxxxx

happyness Ndaro ni msichana ambaye kwa kipindi cha kujuana kwetu, tumefanya naye mambo mengi ikiwa ni pamoja na kwenda naye katika matukio ya hatari zaidi hivyo, naye alikuwa amekwisha ambukizwa sumu ya uhatari na amekwisha kuwa mzoefu wa kushudia mauaji kadha maasi kadhaa yakifanyika.