Sio Lazima Afe Lakini...(2)

Katika toleo lililopita, tuliona Happyness Ndaro amewakusanya Benson Momo na Fema ili kuwapa siri ambayo ilikuwa sirini kwake na amewataka wawe jasiri ili waifaidi dunia hii. Benson Momo ambaye alikuwa mpenzi wake, pamoja na Fema wanakataa mpaka awambie wazi ndipo wakubali au wakatae "tenda" hiyo. Ni siri gani hiyo, Happyness anaanza kusimulia...

Na Gerald Lwomile

"Mimi mwenzenu nina tatizo ambalo sio siri ufumbuzi wake ni mgumu maana unahitaji ama kugharimu damu ya mtu au vinginevyo," akatulia kidogo.

Kisha akandelea, "Nyie wote natumaini mnamfahamu vema Mzee Ndaro; baba yangu..." "Ndiyo tunamfahamu," mimi na Benson Momo tukaitikia kwa pamoja.

"Ninasikitika kuwaambia rasmi kuwa utajiri ule alionao, ni dhuluma ambayo sio siri inanitia uchungu sana ninapomkumbuka marehemu mama yangu.

Ingawa siifahamu sura yake kutokana na kufariki mimi nikiwa mdogo, lakini ninaumia sana ninapozidi kupata ushahidi wa kutosha kuwa Mzee Ndaro ndiye aliyemua mama; eti ili arithi mali hiyo ambayo sasa amanaringa nayo," akatulia kidogo.

Akaendelea, " Mzee huyo niliyeambiwa nimwite baba ingawa kimsingi ninamtambua kuwa ni mjomba, kumbe baada ya kutumia mbinu zote bila mafanikio, aliona na kuamua kuwa njia yake nzuri itakayomfikisha katika jina la utajiri, ni kumuua mama; mama mzazi," Happyness akajipangusa machozi kwa kutumia upande wa nyuma wa kiganja chake cha mkono.

Akaendelea, "Kumbe kuna kipindi Mzee huyo alikuwa akimshawishi mama wafanye biashara naye, lakini mama akawa anakataa kwa kuhofu kuwa Mzee Ndaro angeweza kumdhulumu.

Hata hivyo, baada ya kukataa mama alikuwa akipokea barua mbalimbali za vitisho. Karibu zaidi ya mara sita nyumba ya mama ilikuwa ikivujwa na kuvamiwa kwa mbinu mbalimbali tofauti ingawa inashangaza kuwa ilikuwa bahati kwani mara zote hizo mama alikuwa safarini kwa vipindi tofauti na hivyo, majambazi hao walikuwa hawamkuti ndani.

Maskini kwa kuwa nia yao ilikuwa ni uhai wa mama, kila walipomkosa hawakujaribu kuiba wala kupora chochote; yaani dunia hii..." akatulia kumeza mate.

"Eheee; endelea tunakusikiliza," Nikasema huku nikimuonesha umakini katika kumsikiliza.

"Mauaji ya kutisha aliyofanyiwa mama yalinilazimisha kuanza kulikosa titi la mama nikiwa na umri wa mwaka na nusu.

Mzee Ndaro ambaye ni kaka wa mama ndiye aliyebeba jukumu la kunitunza ili kunipunguzia simanzi.

Sio siri, mimi nilizaliwa na mwanaume ambaye sijui ni kwanini hadi sasa simjui na badala yake, nikapandikizwa kwa mjomba (Mzee Ndaro) kuwa ndiye baba na mke wake eti ndiye mama yangu mzazi.

Hata hivyo, dunia hii haina siri maana mbona tayari nimeyajua yote namna yalivyokuwa."

Ninadhani labda pia walifanya hivyo (mjomba na mkewe)ili nikue nikijua kuwa nipo kwa wazazi wangu na mali zote ni zetu ili baadaye, nisianze kuhoji uhalali wa mjomba na familia yake kumiliki mali ambazo chimbuko lake, ni mama yangu," Happyness akatuangalia machoni na huku akiketi sawia pale kitandani na kuvuta pumzi alizozishusha taratibu.

" Duniani hakuna siri na ndiyo maana sasa the cat is now out of the bag (paka yuko nje ya gunia sasa); siri imefichuka na ukweli wote ninao.

Inaniuma sana maana wakati huo nikiwa mdogo walifanikiwa kunidanganya; sasa nina akili zangu ninajua wapi pa kuanzia na wapi pa kumalizia katika kufanya jema au baya.

Kwa maelezo hayo marefu, nawaombeni nyie wenzangu msiniangushe; tushirikiane ili mali ile irudi katika mikono yangu na sisi sote iwe zamu yetu kutanua maana kutesa ni kwa zamu.

Ile mali aliyo nayo Ndaro, ni mali ya marehemu mama na ni haki yangu lakini wamekwisha nipora; au mnasemaje?" Happyness akatulia kusubiri jibu.

Wakati wote huo mimi na Momo tulikuwa tukimsikiliza kwa makini licha ya bia tulizokunywa.

Sio siri kila mmoja wetu na kwa nafasi yake, usongo ulizidi kumjaa dhidi ya namna gani tutazitia mali hizo katika viganja vyetu na namna ya kuzimiliki zaidi.

Nikasema kwa matumaini ya ushindi, "Mambo ndiyo hayo maana the ball is now on the ground. It depends on how you will kick it (mpira sasa upo uwanjani na unategemea namna utakavyoucheza), nikasema huku nikimtazama Benson Momo usoni.

"Shemeji hapo tumekuelewa vema isipokuwa, hata wewe nadhani unajua ugumu na unyeti wa kazi hii. Kwanza, ni hatari hata kwetu wenyewe.

Sasa ninashindwa kujua umeandaa lipi juu yetu maana makubaliano juu ya jambo hili kabla ya utekelezaji wake, ni muhimu; hili ni jambo zito.

Pia, kabla hatujaanza kazi ni vema tujue mali yenyewe ni kiasi gani ili tusifanye biashara ya kuuza ng’ombe ili kufanya kesi ya kuku," nilisema kisha nikatulia kidogo kumeza mate.

Nikaendelea, "Maana yangu ni kwamba, tungependa kujua uamuzi wako juu ya huyo mjomba wako na kisha, tujue juu ya ujira wetu kwa ufupi. Kwa maana kwamba utuambie unatuahidi nini tukimaliza kazi," nikatuilia.

"Ila kabla hujasema, lazima uape juu ya uaminifu; kuwa hautatusaliti hata kama mambo yataharibika. Ninatahadharisha hivyo, maana sisi mtu wa namna hiyo, huwa tunamhukumu wenyewe kwa KIFO. Sijui kama umenielewa?"

"Mali za Mzee Ndaro ni nyingi ingawa yeye anatumia ujanja wa kuzitawanya kwa watu mbalimbali. Ukiachilia mbali mabasi haya mnayoyaona yameandikwa ubavuni "MPAJI NI MUNGU".

Pia, analo duka la spea za magari mjini Arusha linalosimamiwa na mwanaye mkubwa, anaitwa Steven. Kule Same, anacho kituo kikubwa cha mafuta ambacho mwangalizi wake ni binti yake wa pili, anaitwa Jenifa...

Pale eneo la mpakani Namanga, ana duka la jumla ambalo amemkabidhi rafiki yake ambaye humkabidhi mapato yote ya wiki na hufanya hivyo kwa siri kubwa.

Mara nyingi hukutana katika nyumba ya wageni iitwayo Bondeni pale mjini Arusha.

Kuhusu uamuzi wangu juu ya Mzee Ndaro, mimi Happyness Ndaro, kama watu walivyozoea kuniita, ninasema kama yeye alidiriki kumuuua mama yangu mzazi kwa ajili ya mali, na mimi sioni kwanini asife kama alivyo kufa mama; eti abaki anazidi kutanua kwa mali ya mama yangu mzazi, Aka!" akasema Happyness.

Hivyo ni lazima ayaonje mauti ili akamsimulie mama kilichosababisha amfuate," akatulia kidogo na kukohoa ili kusafisha koo.

Akaendelea, "Suala la nitawalipa kiasi gani, linategemea mafanikio katika kazi yenyewe.

Ninasema hivi maana kwa jinsi ninavyohisi, shughuli hii ni kubwa, kwa hiyo malipo yatategemea wepesi au ugumu utakaoonekana katika kazi hii."