Make your own free website on Tripod.com

Sio Lazima Afe Lakini...(5)

Kwa Wasomaji Wapya:Happyness Ndaro ameeleza bayana azima yake ya kutaka Mzee Ndaro auawe ili mali zinazodaiwa kuporwa kwa mama yake mzazi na kumsababishia mama huyo kifo, zimrudie yeye na kampani yake. Nini kitaendelea, fuatilia hadithi hii ya kusisimua.

Na Gerald Lwomile

Kabla Steve hajaongea lolote, Momo akiwa mbele mimi nikiwa nyuma, tuliingia ndani tukiwa tumielekeza midomo ya bastora zetu kwake. Moja katika kichwa, na nyingine katika kifua cha Steven.

"Hapo ulipo weka mikono juu!" Momo akaamuru nami nikaongezea, "Ukiwa hivyo hivyo toka juu ya kochi hilo na ukae chini. Ujue kuwa huna hiari yoyote maana uko chini ya ulinzi wetu."

Steven kijana mdogo mwenye umri upatao miaka 28 hivi, mwenye rangi na sura ya kuvutia kama ya kike-kike hivi, hakuwa na la kufanya. Akatekeleza.

Happyness naye akaitoa wazi ile bastora yake ambayo wakati huo ilikuwa kiunoni mwake alipoichomekeza katika suruali yake aina ya "jeans". Akaanza kumkaripia Steven. Hali hiyo ikaongeza mduao kwa kijana huyo.

"Haya wewe kuku wa kizungu, kuanzia sasa maisha yako yako mikononi mwetu. Inakubidi uwe makini sana katika kujibu maswali yote tutakayokuuliza. Kinyume na hapo, mauti kwa chuma cha mzungu ni halali yako," Happyness akasema kwa sauti inayoashiria asivyo na chembe ya huruma na wala asivyotambua undugu wala utu.

"Tumekuja hapa kuchukua pesa na wala hatuhitaji maelezo mengi; umesikia?" Nikamuuliza Steven huku nikimsukumiza kichwa chake kwa kutumia mdomo wa bastora iliyokuwa mkononi kwangu.

Akajibu, "Ndiyo".

"Haya tuambue pesa zote ulizo nazo ziko wapi. Na wala usijaribu kuficha au kudanganya kwa sababu tunajua kila kitu." "Ziko wenye droo ya kabati". "Kabati iko wapi?" "Iko chumbani kwangu." "Haya simama kama ulivyo; twende ukatuoneshe bila kutupotezea muda. Wakati ni mali," nikadhihaki.

Huku akiwa chini ya ulinzi wetu, Steve akatutanguliza hadi chumbani kwake anapotunzia ufunguo wa kabati lile muhimu kwa shughuli yetu.

Alipodunga ufunguo katika kitasa cha droo ya kabati lile na kuifungua, mapigo ya moyo yakanienda mbio. Fema sikuamini macho yangu. Nilidhani kile ninachokiona, ninakiona ndotoni tu na wala hakuna uhalisi wowote.

Kwa muda kadhaa nikapigwa na mduao nikistaajabia noti zile za shilingi elfu kumi- kumi, zilivyojipanga kwa mafungu ya utaratibu maalumu.

Kama ninayetumia umeme, Fema nikazipakua na kuzipakia pesa hizo ambazo hadi wakati ule niliamini kuwa hazipungui milioni 25 za Kitanzania pamoja na Dola kadhaa za Kimarekani. Kisha tukarudi sebuleni huku mateka wetu akishuhudia kile kilichobebwa, lakini aseme nini!

"Kaa chini," Happyness akamwambia Steven aliyezoeleka kama kaka yake. Akaongeza, "Pesa tumechukua sasa tunaomba roho yako ambayo ndilo hitaji letu la mwisho toka kwako."

"Eee! Dada Happy nimekukosea nini, pesa umechukua; naomnba roho yangu uniachie."

Happyness akajibu, "Mwenye makosa si wewe, lakini wewe pia unastahili adhabu kwa kuwa wewe pamoja na baba yako mlishirikiana kunitesa na ndio maana ninakuadhibu hata wewe."

Kisha kama utani vile, Happy akanyoosha mkono wake wenye bastora huku kidole kimoja kimeegeshwa sawia katika kiwambo. Akakiminya kuruhusu risasi zitoke kwa kasi na mtindo unaohitajika.

Ikawa hivyo. Risasi mbili mfululizo zikambusu Steven katikati ya kifua. Akanguka chini akigalagala huku damu zikimtoka. Akaenda; akafa.

Baada ya kuweka makusanyo yetu yote katika mfuko ulioonekana kama kifurushi muhimu na cha kawaida, tuliondoka katika nyumba hiyo tukimuacha steve anatumia mawasiliano ya kisasa kuzungumza na wafu waliotangulia kuzimu.

Tukaingia ndani ya NISSAN PATROL, na safari ya kurudi Moshi ikaanza.

Hadi kukamilika kwa shughuli hiyo, ilikuwa sasa yapata saa 8:27 hivi usiku huo.

NISSAN PATROL ilizidi kutambaa juu ya barabara hiyo ya lami na hata tulipofika sehemu ya tukio letu la kwanza, spidi ikawa kali zaidi.

Ilibidi mwendo uwe mkali kwa maana hakuna aliyejua hadi wakati huo nini kilikuwa kinaendelea. Kila mmoja wetu alijua kuwa huenda polisi wamepewa taarifa na sasa wanafuatilia nyendo zetu na hata kwamba wamekwenda kuwaokoa waathirika wa utekai wetu.

Bahati nzuri kwetu, hali ya barabara ilikuwa shwari.

Ilikuwa sasa yapata saa 9:00 hivi usiku huo. Gari letu lilifunga breki zake mbele ya nyumba ya Mzee Evance Waibe.

Huyu alikuwa na ushirika wa kibiashara na Mzee Ndaro. Yeye, alikuwa akiendesha duka moja kubwa sana hapo mjini Arusha. Shughuli hii iliyoendeshwa kwa niaba ya Mzee Ndaro, ilikuwa ikifanyika kwa siri kubwa. Hakuna aliyetaka uhusiano baina ya wazee hao ujulikane kwa mtu yeyote.

Safari hii hatukuona sababu ya kumtumia Happyness kama chambo chetu ili tufunguliwe. Mazingira ya mahali pale yalikuwa tofauti na yale tuliyokutana nayo pale nyumbani kwa Steven.

Safari hii badala ya kubisha hodi kama ilivyokuwa awali, tulitumia njia nyingine ambayo ni maarufu kwa ufunguaji milango kwa wageni wasio rasmi, inaitwa "FATUMA".

Tulilinyanyua jiwe lile lenye uzito upatao kilogramu 60 hivi, tukahesabiana kama harambee na tuliporidhika na momemtamu iliyopatikana, tukalibamiza mlangoni baada ya kuhesabiana, "Moja! Mbili!... Tatu!" Ndipo mlango ule uliokuwa katika mtindo wa kizamani licha ya kutunza mali za thamani kubwa ulipogawanyika na kuwa mithili ya vipande vya kuni.

Basi, tukaingia ndani huku silaha zetu zikiwa mikononi tayari kwa kupambana na tatizo au upinzani wowote utakaojitokeza dhidi yetu.

Mimi na Benny tulitembea kwa mwendo wa kunyatia kuelekea chumba kile iliposikika sauti iliyoashiria kuguswa kitasha mithili ya mtu kutaka kufungua mlango.

Benny alisimama upande wa kulia wa mlango na mimi nikajibana upande wa kushoto.

Mwanzoni, mlango ulifunguliwa kwa sehemu ndogo tu li kuchungulia. Baada ya kuridhika na ukimya na pia kuona kuwa haoni vizuri kinachoendelea, aliyeufungua mlango huo aliongeza upana wa uwazi wa mlango. Hali hiyo ilimruhusu kutoa kichwa na sehemu nyingine ya kiwiliwili chake nje ya chumbachake cha kulala.

Kama nilivyosema awali, Benson Momo ni mtu hatari sana awapo kazini na mara nyingi huwa hapendi kupoteza nafasi muhimu ili eti baadaye aijutie.

Kama chui aliyekosa mawindo na wala asipate cha kuhemea kwa siku tatu hivi, kisha akamuona swala ameinama kunywa maji mtoni, Momo alitumia spidi na staili ya aina yake aliporuka na kutua juu ya shingo ya Nzee Waibe kwa pigo la karate. Pasipo kujbu kitu, Waibe akadondoka chini.

Nilibaki kumchunga Mzee Waibe wakati Momo alipoingia chumbani kuona kama kuna mtu mwingine anayestahili suluba. Akamkuta mke wa Waibe. Mwanamke huyo alikuwa kesha teremka kitandani huku mkojo wa hofu ukimtiririka ovyo.

Momo akamshikilia mkono hadi sebuleni na kumkabidhi mikononi mwa Happyness Ndaro. Akarudi nilipokuwa.

"Haya beba huko tumpeleke kwa mke wake," Bensonmomo akaniambia nami bila ajizi, nikafanya kama alivyotaka.

Tulimbeba mzee huyo ambaye sasa fahamu zilianza kumrudia taratibu. Tukambwaga jirani kabisa na alikuwa mke wake.

"Wewe mwanamke ndiye utakayejibu maswali ya mumeo hadi hapo atakapozinduka. OK?" Nikamuungurumia mama huyo ambaye tayari uso wake ulibainisha wazi hali ya kukata tamaa kuwapo duniani.

"Ndiyo nimeelewa," Akajibu kwa hofu. "OK! Unamfahamu Mzee Ndaro?" Nikaanza swali la kwanza. "Ndiyo; ninamfahamu," Mke huyo wa Mzee Waibe akajibu harakaharaka. Nikaendelea na maswali, "Unamfahamu vipi?" "Ni rafiki wa mume wangu." "Urafiki wao ukoje; yani unahusu nini?" akajibu, "Unahuisu mambo ya kibiashara."

Nikamgeukia Happyness Ndaro na kumuangalia kwa ishara ya mafanikio. Nikaendelea kuuliza, "Ehee! Wanashirikiana vipi?" "Kwa kweli mimi sijui namna wanavyoshirikiana ila, kitu ninachofahamu ni kwamba kila Jumamosi mume wangu huniaga kuwa anakwenda Moshi kwa rafiki yake(Ndaro). Kinachokuwa kinaendeleahuko naapa kwa Mungu; sijui. ...Maana akirudi huwa hanielezi kitu hata kama nitamuuliza chochote juu ya safari yake."

Mama huyo akatulia kidogo kumeza mate. Akaendelea, "Kuhusu kuja kwake hapa, Mzee Ndaro huwa anakuja kila baada ya mwezi mmoja kupita. Akifika wanakaa kidogo halafu wanakwenda baa kwa mazungumzo yao ambayo huwa hawataki hata mimi niyajue."

"Unadhani huwa wanazungumzia kitu gani?" Itaendelea toleo lijalo