Ugonjwa wa sare wazua manung'uniko Simba

Na Lilian Timbuka

KLABU ya Soka ya Simba ya jijini Dar es Salaam, imegubikwa na jinamizi nene baada ya matumaini ya kutetea Ubingwa wa Tanzaania Bara kuwa finyu kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo uliotawaliwa na sare mfululizo.

Wanachama wa klabu hiyo wameulalamikia uongozi kwa kushindwa kubuni mikakati madhubuti ya ushindi ili kulibakisha tena taji hilo ililolitwaa mwaka jana baada ya kulikosa kwa miaka zaidi ya mitano mfulullizo.

Wakizungumza na Gazeti la KIONGOZI jijini Dar es Salaam, juma lililopita, wanachama hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walisema kwa pamoja kuwa “ugonjwa wa sare” uliotawala Simba katika mechi mfululizo umesababishwa na uzembe wa viongozi ambao wanajisahau na kutokuwa makini kutafuta mbinu mpya za ushindi tofauti na mwaka jana.

Ugonjwa wa sare umeikumba Simba katika Ligi ya VODACOM, Hatua ya Nane Bora inayoendelea nchini.

Walisema kitendo cha uongozi kushindwa kudhibiti nidhamu ya wachezaji, pia kimeonesha udhaifu katika uongozi na kimechangia kuporomoka kwa kiwango cha uchezaji na kuifanya timu ijikongoje kwa mfululizo wa sare.

“Tunajua kwamba Ligi ni ngumu,  uongozi nao umejisahau mno; umeshindwa kubuni mikakati ya ushindi na kudhibiti nidhamu,” alisema mmoja wa wanachama hao.

Akaongeza, “Wachezaji wetu sasa hawachezi kama ilivyokuwa mwaka jana au mwaka huu tulipotwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kule Zanzibar; viwango vyao vimeshuka mno.”

Walisema kushuka kwa viwango vya wachezaji, pia kumechangiwa na wachezaji kuendekeza starehe na kushindwa kuthamini nidhamu ya mazoezi.

Walisema hawana tatizo na Kocha wa Timu hiyo, James Siang’a kwani amejitahidi kurudisha hadhi ya Klabu ya Simba na hivyo, hawana budi kumshukuru.

 “Wa kulaumiwa hapa ni viongozi wenyewe wanaoyafahamu fika mazingira ya Tanzania na wachezaji wao walivyo,” alibanisha mwingine.

Nahodha wa Timu hiyo ya “Wekundu wa Msimbazi,” Selemani Matola, alijibu madongo hayo akisema alikiri kuwapo kwa tabia ya kuendekeza starehe miongoni mwa wachezaji hali inayowafanya baadhi wajisahau katika mazoezi.

Hata hivyo, alisema hiyo si sababu kubwa ya wao kutofanya vizuri katika Ligi hiyo.

Alisema Ligi ya mwaka huu, ni ngumu mno kwa kuwa timu nyingi za mikoani zikuja juu kiushindani.

"Tunachotakiwa ni kubuni mbinu mpya za ushindi badala ya kukaa na kuanza kutupiana lawama kwani hazitasaidia kuleta maendeleo ya timu," alisema.

Aidha, aliwaomba wanachama wa Klabu ya Simba kuwa na subira na wakati mwingine, wajaribu kukubali matokeo badala ya kuona kwamba timu yao ndiyo inayopaswa kuwa na ushindi katika kila mechi inayocheza.

Aliongeza kuwa, hata timu zingine ambazo zinazopambana na Simba, pia zinahitaji ushindi na sio kufungwa kama wanavyodhani wanachama hao.

Hadi juma lililopita, Timu hiyo ya Msimbazi ilikuwa ikishikaa nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi 15. Ilicheza mechi 10, ikashinda mechi 3 na kutoka sare katika mechi 6. Ilikuwa imefungwa katika mechi moja.

Hata hivyo Jumatano iliyopita katika pambano baina ya Simba na 82 Rangers ya Shinyanga lililofanyika katika Uwanja wa Taifa.jijini Dar es Salaam, Simba ilitoka uwanjani ikiwa kifua mbele baada ya kuilaza timu pinzani kwa bao 3-0.

Watani wa Jadi wa Timu hiyo, Yanga ya Dar es Salaam ndiyo inayoongoza katika Ligi hiyo kwa kujikusanyia Pointi 18 kutokana na michezo 10 iliyokwisha kucheza.

Hata hivyo, ili Wekundu hao wa Msimbazi waendelee kutetea ubingwa wao, itabidi washinde mechi zote zilizosalia na hilo likiwezekana, Simba itakuwa na jumla ya pointi 27.

Endapo timu za Mtibwa na Yanga zitapoteza michezo yao hata kama ni mmoja, basi hakuna timu nyingine itakayofikisha pointi hizo 27 na hivyo, kuwaachia Wekundu hao ubingwa kwa mara nyingine tena.

Ubungo Shooting yaifanyia 'roho mbaya' Sanaa Sports

Na Msafiri Mdami, DSJ

TIMU ya Soka ya Ubungo Shooting Stars imeifanyia roho mbaya klabu ya soka ya Sanaa Sport zote za Dar es Salaam, kwa kuifunga mabao 3-0, katika mchezo wa kirafiki uliofanyika wiki iliyopita katika Uwanja wa UFI, Dar es Salaam.

Bao la kwanza la Ubungo Shooting Stars  lilipatikana kunako dakika ya 10 baada ya mchezaji Ally Issa kuwalamba chenga mabeki wawili wa Sanaa Sports na kisha kuachia mkwaju mkali uliotinga kimiani.

Dakika saba tangu kuanza kwa kipindi cha pili, mchezaji huyo machachali, aliiongezea timu yake bao la pili baada ya kuvunja mtego wa kuotea na hivyo, kufunga bao kwa urahisi.

Bao la tatu liliwekwa kimiani na mshambuliaji Hassan Mpemba katika dakika ya 70, baada ya kutokea piga nikupige katika lango la Sanaa Sports na hatimaye Mpemba kufumua shuti lililojaa wavuni.

Hata hivyo, Sanaa iliongeza ushambuliaji katika kipindi cha mchezo japo haikuambulia bao na hivyo, Ubungo Shooting kuondoka uwanjani kifua mbele kwa kufunga bao 3-0.

Wakati huo huo: Uongozi wa Nyagatwa Inn, iliyopo njia panda ya Uwanja wa Ndege, Dar es Salaam, umeanzisha klabu ya mchezo wa pool ikiwa njia moja wapo ya kuendeleza michezo nchini.

Mlezi wa Klabu hiyo hiyo, Bibi. Grace Chacha, alisema wameamua kuanzisha mchezo huo ili kuuinua na kuutangza kwani hadi sasa bado haujapata washiriki wengi.

Hivi sasa klabu hiyo ikiongozwa na Kapteni wake, Aldoph, inajindaa kwa ziara ya mechi za kirafiki wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Hadi sasa imekwisha cheza mechi tatu za kirafiki na kushinda katika michezo yote.

Waamuzi wa Tanzania si 'mabomu'- FRAT

l Yahoji:Mbona kuna wenye beji za FIFA?

l Wataka makocha waandae timu ipasavyo; waache lawama

 

Na Lilian Timbuka

 

CHAMA cha Waamuzi wa Soka nchini (FRAT), kimepinga vikali kauli iliyotolewa hivi karibuni na Kocha wa Timu ya Simba, James Siang’a kuwa waamuzi wa hapa nchini hawana uwezo wa kuchezesha mchezo huo.

Akizungumza na KIONGOZI jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Msaidizi wa FRAT, Lishie Liunda, alisema Tanzania ina waamuzi waliobobea katika kuchezesha kabumbu na kwamba, baadhi yao wapo wenye beji za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

“Sikubaliani na kauli ya Siang’a kwani  hapa Tanzania kuna waamuzi zaidi ya 700 ambao kati yao wapo wenye beji za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na wengine mmojawapo ni mimi tumeteuliwa kuchezesha Ligi ya Mabingwa Afrika. Inakuaje tena waseme waamuzi wabovu?” Alihoji Liunda.

Aliyataja majina ya waamuzi ambao wana beji za FIFA kuwa ni pamoja na Omar Abdulkadir, Emmanuel Chaula, Pascal Chiganga, Victor Mwandika na Fredeick Tibaijuka.

Waamuzi wengine ni David Nyandwi, Charles Mchau, Soud Abdi pamoja na yeye mwenyewe Liunda.

Alisema imekuwa ni tabia ya baadhi ya Watanzania hususan makocha wa timu, kuwalaumu waamuzi pindi timu zao zinapofungwa na kuwasifia pale wanapofunga.

Akitoa mfano wa kauli ya Kocha wa Yanga, Jack Chamangwana, Linda alisema kuwa, Chamangwana aliwahi kutamka kuwa waamuzi wa Tanzania hawafai kuchezesha mechi kubwa, bali wanafaa kuchezesha Ligi Daraja la Pili, lakini timu hiyo ilipopambana na Tukuyu Stars na kushinda kwa mabao mengi, aligeuka na kuanza kumsifia mwamuzi wa pambano hilo bila kukumbuka kuwa awali alisema kuwa hafai.

“Unajua timu zetu za Tanzania huwa daima zinapenda ushindi tu na pindi timu ikifungwa, basi lawama zote huwa zinakuja kwa waamuzi wa mchezo huo siku zote,” alisema Liunda.

Alisema kinachotakiwa ni makocha kuziandaa vema timu zao badala ya kujenga dhana potofu ya kuwalalamika waamuzi wa michezo yao ili kuficha udhaifu wa makocha hao.

Hivi karibuni, Kocha Siang’a alitoa kauli kuwa waamuzi wa Tanzanaia hawana uwezo wa kuchezesha mashindano mbalimbali yakiwemo ya Ligi Kuu, hivyo akapendekeza waletwe waamuzi kutoka nje ya nchi.