ILI KUWAKABILI IPASAVYO WAZIMBABWE...

Twiga Stars yalilia mechi za kirafiki

          Na Anthony Ngonyani

TIMU ya Soka ya Taifa  ya Wanawake nchini (Twiga Stars) imekitaka Chama cha Soka nchini (FAT), kuiandalia timu  michezo mbalimbali ya kirafiki ili iitumie kama mazoezi  na hivyo, kufanya vizuri katika pambano baina yake na timu  ya Zimbabwe.

Akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni mshambuliaji hatari wa timu hiyo, Ester Chabruma maarufu kwa jina la Lunyamila, alisema michezo ya kirafiki itawawezesha kufanya vizuri zaidi kwani itaiongezea ujuzi Twiga Stars.

Alisema timu ya Taifa ya Zimbabwe siyo timu inayotisha, hivyo ana uhakika wakipata mechi nyingi za kirafiki, watafanya vizuri na kuinua jina la Tanzania katika Soka ya wanawake.

“Hata kama inatisha sisi tuna uwezo mkubwa kuifunga timu hiyo, kinachotakiwa ni kufanyiwa maandalizi bora,”alisema.

Hata hivyo mchezaji huyo aliipongeza FAT kwa kuiweka mapema kambini timu hiyo.

Prisons yaitaka FAT kuwa makini na ratiba

Na Anthony Ngonyani.

TIMU ya soka ya Prisons imekilalamikia Chama cha Soka Tanzania (FAT), kuhusu kushindwa kupanga ratiba nzuri ya mzunguko wa awamu ya pili ya Ligi Kuu Hatua ya Nane Bora.

Malalamiko hayo yametolewa hivi karibuni na Meneja wa timu hiyo Bw. Hassani Mlilo wakati alipokuwa akizungumza na Gazeti hili jijini Dar-es-Salaam juu ya mashindano hayo.

Alisema ratiba  hiyo inaibana sana timu yake na kwamba inawezekana kuwa chanzo kikubwa cha timu hiyo kutofanya vizuri katika mashindano hayo.

Alisema timu ya Prisons italazimika kusafiri kila itakapocheza mchezo mmoja wa ligi hiyo ambayo ilianza kutimua vumbi wiki  iliyopita.

Aliongeza kuwa, kutokana na safari hizo zitakazomalizika pindi ligi hiyo itakapo malizika mapema mwezi ujao wachezaji wake watachoka na kushindwa kutafakari makosa yaliyojitokeza wakati timu hiyo ilipokuwa imeshuka dimbani na kukosa muda mazoezi.

Mlilo aliongeza kusema kuwa kutokana na mpango huo mbaya wa ratiba, kuna hatari kwa timu yake kutofanya vizuri  hasa ikizingatiwa kuwa  inao wachezaji wengi ambao ni majeruhi.

Alisema kuwa hakuna sababnu nyingine ambayo itakayopelekea timu hiyo kufanya vibaya zaidi ya hiyo, hivyo wanakitaka FAT kufanya wawezalo  ili kubadili ratiba.

Akasisitiza kuwa kufanya hivyo, kutaiokoa timu hiyo ambayo sasa iko katika wakati mgumu wa katika kufanya vizuri Ligi Kuu ya VodaCom.

Prisons ni moja kati ya timu ambazo ni tishio ambayo imeweka rekodi kwa kutoa dozi kwa timu kubwa ambazo ni Simba na Timu ya Yanga zote za jijini Dar es Salaam.

Imefanikiwa kujiweka katika nafasi nzuri ya kuweza kuingia Tabora na kuweza kushiriki Kombe la Muungano.

Tunajisikia vibaya timu za Taifa zinapofungwa-Wizara

l  Yaionya Twiga Stars isifuate mwenendo wa Taifa Stars

            Na Lilian Timbuka

SERIKALI imesema kuwa inajisikia vibaya pindi timu zilizofikia ngazi ya Taifa katika michezo mbalimbali, zinapofungwa na nchi nyingine.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana na Michezo, Mudhihir Mudhihir wakati alipotembelea kambi ya timu ya mpira wa miguu ya Wanawake ya Twiga Stars iliyoweka kambi katika hosteli za Jeshi la Wokovu Jijini Dar es Salaam.

“Tunajisikia vibaya sana sisi wote hapa ni viongozi, lakini taaluma yetu ni kufundisha soka, hivyo timu ikifungwa tunajisikia vibaya,” alisema Mudhihir. Alisema kufanya vizuri kwa timu hizo, ni sifa kwa Taifa ambapo alitoa  mfano wa timu hiyo ya Wanawake iliyoifunga timu kutoka Eritrea.

“Timu hii imeweza kufanya vizuri licha ya kukumbana na mazingira magumu katika kambi pindi ilipopambana na timu ya Eritrea,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Waziri aliwaasa akinadada hao wa Twiga Star kuwa na moyo wa ustahimilivu na kujituma wawapo kwenye mashindano makubwa kama hayo. “Kamwe msifuate mwendo wa kaka zenu wa Taifa Stars ambao mmekuwa timu ya  kufungwa kila siku,”alisema.

Mudhihir aliwaomba Watanzania ambao wana mapenzi na timu zao za Taifa kuichangia timu hiyo ambayo tayari imekwishafunguliwa Akaunti na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), na akasema tayari kwenye akaunti hiyo kuna kiasi cha sh.500,000 kwa ajili ya timu hiyo.

Twiga Star inatarajia kupambana na timu ya wanawake kutoka nchini Zimbabwe Septemba 21, mwaka huu mchezo utakaofanyika jijini Dar es Salaam.

Endapo itafanikiwa kuitoa Zimbabwe basi itakwenda moja kwa moja kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zilizopangwa kufanyika Desemba mwaka huu mjini Lagos Nigeria.

Tarimba ailaumu FAT

Na Lilian Timbuka

Kufuatia kipigo kikubwa kilichoipata timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) huko Benin, baadhi ya wapenda kandanda nchini wamezidi kukilaumu Chama cha Soka nchini (FAT), kwa kutoiandaa vema timu hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa Klabu ya Soka ya Yanga ya Dar es Salaam, Abas Tarimba alisema FAT inastahili kubebeshwa mzigo wa lawama dhidi ya kipigo hicho cha aibu cha timu ya Taifa kufungwa mabao 4-0 dhidi ya timu ya Taifa ya Benin.

Alisema endapo FAT imeshindwa kuongoza soka nchini ni vema iwaachie wadau wengine wenye uchungu na timu za nchi hii, “Sijui ni kwanini wanang’ang’ania hii aibu ambayo timu yetu imekuwa ikifedhehesha kila mwaka na kubakia kulalamikia waamuzi wa kila mchezo wanaochezesha mechi za Stars,” alinung’unika Tarimba.

Alisema Stars iliyokwenda Benin ilikuwa ni mbovu kuliko ile iliyovunjwa mara baada ya kupata kipigo cha magoli 5-0 dhidi ya Harambee Stars ya Kenya.

Alihoji, “Uliona wapi timu inayojiandaa na mashindano makubwa ikafanya mazoezi kwa mechi za majaribio na timu za ligi ya soka ya Daraja la kwanza nchini kwake badala ya kuitafutia timu mechi kubwa za kimataifa?”

Alisema yeye binafsi hakuona sababu ya FAT kuivunja ile timu ya kwanza, “FAT wangetafuta namna ya kukosoa makosa ambayo yalionyeshwa na timu ile, sasa wamefanya nini wavunje basi na hii iliyofungwa mabao 4”, alisema Tarimba.

Hata hivyo alisema kwa ushauri tu, anakishauri FAT kujaribu kuziandaa timu zake za Taifa kwa kuzitafutia mechi za kirafiki za kimataifa na si kama wanavyofanya hivi sasa.

Timu ya Taifa ambayo inashiriki Mashindano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, hivi karibuni ilipata kipigo cha kufedhehesha kutoka kwa mwenyeji wao timu ya Taifa ya Benin baada ya kufungwa magoli 4-0 kwenye mchezo uliofanyika katika mji wa Cotonou, Benin.

 Mtambo wa Gongo aapa kuua mtu

Na Steven Charles

BINGWA wa ndondi wa IBF, barani Afrika katika uzani wa Kati, Maneno Oswald (Mtambo wa Gongo), amesema washabiki wa Bondia Francis Cheka, wajiandae kubeba maiti kwani atamdunda vibaya katika pambano lao litakalofanyika Septemba 29, mwaka huu.

Bondia Maneno aliyezungumza na KIONGOZI katikati ya juma jijini Dar es Salaam, atapanda ulingoni katika Ukumbi wa Friends Corner uliopo Manzese, Dar es Salaam, Septemba 29, mwaka huu akijindaa kupambana na Rashid Matumla.

Mwezi Julai, mwaka huu, Bondia Maneno alipambana na Bondia Cheka, ambapo Maneno alitolewa katika raundi ya nane huko Morogoro.

Alisema, endapo Cheka atamdunda katika pambano hilo, atajiuzuru mchezo huo kwa kuwa Bondia huyo sio saizi yake.

“…Ushindi wake siukubali kwa sababu halikuwa pambano… yale yalikuwa mazoezi tu; lingekuwa pambano ningesaini mkataba kabla ya mwezi na nikajua nachezea shilingi ngapi, lakini sikujua,” alisema Maneno.

Akaongeza, “Kama alinipiga kweli, tutaona sasa… najua walimpa ushindi katika mazoezi hayo wanayoita mechi kwa sababu wanataka kumnyanyua kupitia mazoezi hayo tuliyochezea kwenye mchanga.”

Akisisitiza azima yake ya kumdunda Cheka, Maneno alisema, ”Washabiki watakaokuwapo uwanjani wajiandae kubeba maiti kurudisha Morogoro. Hawezi kunipiga kwa sababu hana mkanda wowote. Hawezi kunipiga kwanza yeye sio saizi yangu na mimi ninacheza naye kama mazoezi tu, ili kujiandaa kucheza na Rashid. Huyo (Matumla) na akina Joseph Marwa na wengine kutoka nje ya nchi, ndio saizi yangu”.

Mwaka juzi Bondia Rashid Matumla na Maneno Oswald, walipambana katika Ukumbi wa PTA Dar es Salaam ambapo Matumla aliibuka mshindi kwa KO katika raundi ya tisa.

Maneno Oswald anadai ana usonga wa kuthibitisha kuwa yeye ni mbabe dhidi ya Matumla na kwamba, pambano baina yake na matumla linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni, ndilo litalithibitisha ubabe wake.