Utitiri wa makocha Taifa Stars si suluhisho la matatizo – ZFA

      Na Lilian Timbuka

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Farouq Karimu amesema mlundikano wa Makocha katika kuinoa timu ya Taifa (Taifa Stars) siyo suluhisho kwa timu hiyo kufanya vizuri katika mechi zake za Kimataifa.

Akizungumza na KIONGOZI mapema wiki hii jijini Dar es Salaam, Karimu alisema mabadiliko pekee ambayo yataifanya timu hiyo ifanye vizuri ni kutimiza mambo mihimu kwa wachezaji.

Sioni kama kutakuwa na mabadiliko ya kiufundi ikiwa baadhi ya mambo muhimu yanayohitajika hayafiki kwa walengwaalisema.

Alisema hata kama chama cha soka kitaamua kuweka makocha kumi bado hali itakuwa ni mbaya tu “Unajua hata kama tutaamua kulundika makocha pasipokuwa na maandalizi mazuri kwa timu zetu za Taifa, basi tusitegemee miujiza kutoka kwa makocha hao”.

Alisema makocha pamoja na timu yenyewe kwa ujumla zinahitaji vitendea kazi kuweza kufanya vizuri.

 Sasa kama mahitaji muhimu hayafiki kwa walengwa tunatarajia nini kutoka kwa hawa makocha hata kama ni hamsini?Alihoji Karimu.

Aliongeza  makocha hawa nao pia wanahitaji nyenzo za kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwafanyia majaribio wachezaji wao kwa kuwapambanisha na timu za nchi nyingine ili waweze kujifunza zaidi”.

Alisema suala la kuongeza makocha ni kuwachanganya wachezaji na kuwafanya washindwe kuelewa kile watakachofundishwa na makocha hao kwa wakati mmoja japo kuwa FAT wao hilo bado hawajaliona.

Alipendekeza timu ibakie na Kocha Mkuu na Msaidizi wake pamoja na kutafuta nyenzo za kufanyia kazi kwa makocha hawa na wachezaji.

Mbali na hayo Karimu alisema Chama cha Soka Tanzania (FAT), kinapaswa kuitafutia timu hiyo mechi mbalimbali za Kimataifa za majaribio kwa kujiweka tayari kukabiliana na wapinzani.

Wiki iliyopita FAT ilitangaza kuwarejesha makocha waliotemwa na chama hicho pale Taifa Stars ilipopata kipigo cha mabao 5-0 na timu ya Harambee Stars ya Kenya mchezo uliyochezwa mjini Arusha na hatimaye timu hiyo kuvunjwa na kuundwa mpya ambayo nayo inaendelea kupata vipigo vizito katika mechi zake za Kimataifa.

Makocha waliorejeshwa ni Mshindo Msola na James Siang’aa, ambao wote kwa pamoja watasaidiana na Kocha Salum Madad na Hafidh Badru.

Maamuzi ya kuongeza makocha yalikuja baaa ya timu hiyo iliyokuwa chini ya Salum Madadi kuvurunda mechi mbili za Kimataifa ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Afrika, zitakazofanyika nchini Tunisia mwaka 2004.

Awali stars ilichabangwa mabao 4-0 na timu ya Benin kabla ya kubanjuliwa tena na timu ya taifa ya Sudan hapa hapa nyumbani kwenye uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kwa jumla ya mabo 2-1.

Licha ya utitiri wa makocha,Taifa Stars bado inaendelea kuvurunda na katika kinyang’anyiro cha kuwania Kombe la Castle,ilichabangwa kwa mabao 2-0 na timu ya Taifa ya Uganda,mchezo uliochezwa Oktoba 23 mwaka huu.

TBF yavitaka vilabu vya mikoani kukamilisha marekebisho ya katiba

Na Lilian Timbuka

SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) limevitaka vilabu vya mikoani ifikapo Novemba 30 mwaka huu,kuwa vimekamilisha kufanya marekebisho ya katiba zao kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu viongozi,utakao fanyika Desemba 10 mwaka huu mjini Dodoma.

Akizungumza mapema wiki hii ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TBF, Ahmed Simba alisema kuwa mkoa utakaochelewa hautaruhusiwa kupiga kura.

Kwa mujibu wa Simba, moja ya marekebisho hayo ni kugeuza mfumo ulio katika muundo wa chama na kupeleka katika mfumo wa shirikisho.

Kabla ya mabadiliko ya katiba, shirikisho hilo ambalo sasa linajulikana kama TBF, awali ilikuwa ikiendeshwa katika mfumo wa chama na kwa jina la BATA

Simba alisema kabla ya uchaguzi huo kutakuwa na mashindano ya Kombe la Taifa kwa mchezo huo ambayo yamepangwa kufanyika kwa siku nne,kuanzia Desemba 6 mwaka huu.

 Wakati huohuo, simba alisema kuwa semina ya waamuzi wa mchezo huo itafanyika Novemba 6 hadi 15, mkoani mbeya.

 Alisema waamuzi watakaoshiriki semina hiyo ni kutoka mikoa ya Iringa na Mbeya na itakuwa chini ya wakufunzi Saleh Zonga na Martini Kemwaga kutoka Dar es Salaam.

Nchi tano kushiri mashindano ya mpira wa wavu Ufukweni

Na Modest Msangi

JUMLA ya nchi tano zinatarajiwa kushiriki mashindano ya Mpira wa Wavu katika maeneo ya Ufukweni mwa Bahari,yanayotarajiwa kuanza Oktoba 27 mwaka huu katika Ufuko wa Coco jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni jijini Dar es Salaam,Mwenyekiti wa Kamati ya wa Kamati ya Mpira wa Wavu wa Ufukweni (Beach Volleyball) nchini,Erenest Mlinda alisema kuwa mashindano hayo yatahayo dhaminiwa na Pamuni ya Ok Plastic yatakuwa ya awamu nne.

Alisema awamu ya kwanza itawashirikisha wachezaji wa jijini Dar es Salaam ambapo awamu ya apili itawashirikisha wale wa Dar es Salaam na Pwani wakati awamu ya tatu washiriki watakuwa ni timu kutoka Mikoa ya Tanga, Lindi, Mtwara,Pwani  na Dar es Salaam.

Alisema awamu ya mwisho ndiyo itakayoshirikisha timu za Kimataifa ambazo alizitaja kuwa ni Kenya, Afrika Kusini, Msumbiji, Namibia na Tanzania yenyewe.

Alisema Mkataba baina ya Kamati yake na Kampuni ya OK Plastic yanajumuisha unajumuisha vifaa vya mchezo huo wa Wavu ambavyo ni sawa na nyavu za kuchezea na  mipira.

Mkataba huo pia utawanufaisha wachezaji wote ambao watashiriki kwa kupatiwa usafiri wa kwenda na kurudi ".

Amesema lengo la mashindano hayo ni  kuandaa timu ya Taifa ya Mpira wa Wavu wa Ufukweni itakayo shiriki mashindano ya Olimpiki mwaka 2008.

Katika mkataba huo chama cha Mpira wa Wavu nchini (TAVA) kitapatiwa asilimia 20 ya uzamini mzima wa OK Plastic ili kusaidia uendeshaji wa chama hicho.

TAVA ni miongoni mwa vyama ambavyo havina mapato yoyote yatokanayo na mchezo huo isipokuwa kwa kuzaminiwa.

Mlinda alisema wakati umefika kwa wafanyabiashara na makampuni kuzamini mpira wa Wavu ili kuendeleza mchezo huo.      

Kufyatua kanda ya nyimbo kusiwafanye mbweteke - Wanakwaya waonywa

Na Brown  SunzaCHANGAMOTO imetolewa kwa waimbaji wa kwaya katika madhehebu mbalimbali ya kidini nchini,kuacha kubweteka baada ya kutoa kanda moja ya nyimbo,badala yake wazidishe  bidii ili kuweza kutengeza  kanda nyingine zaidi.

Changamoto hiyo ilitolewa katikati ya juma na Mzee wa Kanisa la Evangelical Tanzaniani Assemblies of God,Kigamboni,Kapteni Wilson Magese wakati akizungumza na KIONGOZI jijini Dar es Salaam.

Kapteni Magese ambaye alikuwa ni miongoni mwa wageni waalikwa katika uzinduzi wa kanda  ya nyimbo iliyoandaliwa na kwaya ya  Amani  ya Kanisa la Anglikana,Usharika wa Tungi  Kigamboni  ,Dayosisi ya Dar es  Salaam, alisema baadhi ya kwaya zimekuwa na hali ya kujiona zimefika mbali baada ya kufyatua  kanda moja ya nyimbo.

Alisema kufanya hivyo hakutasaidia lolote zaidi ya  kuididimiza kwaya

Wakisha rekodi kanda moja ya nyimbo na kuanza kuuza kanda hizo,basi hujiona sasa wamefika mbali,hilo si sahihi kinachotakiwa ni kuzidisha nguvu katika uimbaji ili waweze kutoa kanda zaidi na zaidi”alisema Mzee huyo wa kanisa.

Naye Mwenyekiti wa Kwaya hiyo ya Amani, Emmanuel  Ndahani  aliliambia Gazeti hili kuwa  kanda hiyo waliyoizindua Jumapili iliyopita ni ya kwanza tangu waanzishe kwaya hiyo mwaka 2000.

Alisema  lengo la uzinduzi wa kanda hiyo  pamoja na  kutunisha mfuko wa kwaya,lakini pia ni kukata kuiinjislisha jamii kupitia nyimbo.

Kwaya ya amani  ilianzishwa  mwaka 2000 ikiwa na wanakwaya 13  na  hadi kufikia hivi sasa, inajumla ya wanakwaya 28  na kanda hiyo iliyozinduliwa  ina jumla  ya nyimbo 12 ambapo kila upande una  nyimbo sita.