TBL yakwepa kudhamini timu kupitia FAT

l Ni matokeo ya matumizi mabaya ya fedha za timu

 

      Na Lilian Timbuka

 

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), inayodhamini Michuano ya Kuwania Kombe la Castle, imesema sasa itapekleka mahitaji ya timu zinazoshiriki moja kwa moja bila kupitisha kwa Chama cha Mpira wa Miguu Nchini (FAT).

Hatua hiyo imekuja baada ya FAT  kuonesha mwenendo mbovu wa matumizi ya fedha za wadhamini kwa vilabu vya soka hapa nchini.

Meneja Uhusianao wa TBL, Aggrey Marealle, alisema jijini kuwa, Kampuni yake imeamua kufanya hivyo ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza kwa baadhi ya wajanja kutaka kutia ndani haki za timu shiriki.

Alisema lengo lingine ni kuhakikisha kuwa, timu zote zinashiriki mashindano hayo bila kupata usumbufu ili kulinda hadhi ya mchezo wa soka nchini.

Kama ni fedha ya chakula na malazi, italipwa moja kwa moja kutoka TBL na hata kama ni nauli, timu zitatumiwa moja kwa moja na sio kupitia sehemu yoyote. Tutahakikisha hakuna matatizo yanayojitokeza kwenye timu zitakazoshiriki,” alisema Marealle.

Timu zinazotarajiwa kushiriki kwenye michuano hiyo ya hivi karibuni ambayo huandaliwa na Kampuni ya Bia ya Afrika Kusini, kupitia Bia yake ya Castle, ni pamoja na Timu za Taifa za Kenya, Uganda, Afrika Kusini na wenyeji Tanzania.

Michuano inatarajiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu na itachezwa katika viwanja viwili hapa nchini.

Viwanja hivyo ni Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Karume, mkoani Arusha na katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa Bingwa Mtetezi wa Kombe hilo ni Tanzania ambayo ilifanikiwa kulitwaa mwishoni mwa mwaka jana, katika Uwanja wa CCM Kirumba kule jijini Mwanza baada ya Tanzania kuwabwaga wapinzani wao Timu ya Taifa ya Kenya Harambee Stars kwa jumla ya magoli 3-1.

Kampuni ya Bia Tanzania TBL ambayo ndiyo inatarajia kudhamini michuano hiyo ambayo itaanza hivi karibuni, imesema itahakikisha mahitaji ya timu zitakazoshiriki kombe la Castle yatawafikia walengwa moja kwa moja kutoka kwa waandaaji wa michuano hiyo.

 

Fainali za Ligi ya Muungano kuchezwa Zanzibar

    Na Tom Chilala

VYAMA vya Soka vya Tanzania na Zanzibar (FAT na ZFA), vimekubalina kuwa mechi  ya fainali  ya Ligi Kuu ya Muungano kuchezewa Zanzibar.

 Katibu Mkuu wa Chama cha Soka nchini (FAT) Michael Wambura aliiambia KIONGOZI ofisini kwake kuwa makubaliano hayo yalifikiwa katika mkutano uliowakutanisha viongozi wa vyama hivyo,uliofanyika  Zanzibarhivi karibuni.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa FAT,michuano hiyo itazishirikisha timu sita ambapo kila upande utatoa timu tatu.

Wambura aliongeza kusema kuwa timu zikazofanikiwa kuingia fainali zitachuana Novemba 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Zanzibar.

Kwa mujibu wa Wambura,atakaye patika kwenye fainali hiyo, ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Klabu Bingwa  Afrika ambapo  mshindi wa pili atacheza ataliwakilisha Taifa kwenye michuano ya Shirikisho la Soka  Afrika (CAF).

BASATA yataja sababu zinazo dumaza taaluma ya usanii

Na Victor Sinka

IMEELEZWA kuwa suala la kuweka  maslahi binafsi mbele na kutodumisha amani na upendo ni miongoni mwa mambo yanayochangia kudumaa kwa taaluma ya usanii nchini.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa juma na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA)), Shogholo Challi  wakati wa hafla ya utoaji wa vyeti kwa wahitimu 41 wa mafunzo ya sanaa katika Baraza hilo lililopo Ilala, Dar ea Salaam.

Kazi yoyote isiyokuwa na upendo na amani hukosa heshima wakati wa kuitumikia jamii,ongezezeni bidii katika kuwapika wasanii mbalimbali”alisema Bw. Shogholo.

Shoghoro alisema  ili kukuza kasi ya sanaa nchini,vyombo vya habari hasa Televisheni vinatakiwa kuonyesha michezo ya kizalendo zaidi ya asilimia 75 ili kulinda

na kujenga Sanaa ya Taifa.

Katibu mtendaji huyo amesema,  wasanii wanachukua nafasi kubwa ya kufanya kazi katika vyombo vya habari hapa nchini na kuwaomba watumie nafasi hiyo kwa kutengeneza vipindi na michezo inayoelimisha gonjwa hatari la UKIMWI.

Wananchi wamechoka kusikia habari za UKIMWI na sasa wanataka kuona kwa vitendo,huku akiwaasa wanachi kutunza uaminifu.

Shogholo, amewahimiza wahitimu hao kuvitumia vyeti vyao kwa vitendo badala ya kuviweka maofisini au majumbani kama urembo.

Pia amesema Serikali inampango wa kupeleka mafunzo ya muda mfupi vijijini, ili kuwarahisishia wale wenye nia ya kujiunga na taaluma hiyo.

Katibu huyo aliueleza umma uliofika mahali hapo kwamba BASATA ndiyo taasisi iliyopewa dhamana ya kufundisha na kuratibu shughuli zote zinazohusu  usanii nchini.