Make your own free website on Tripod.com

Simba, Yanga nani ataua mtu?

l Yanga yadai Simba inataka  kuhujumu mapato ya mechi

Na Lilian Timbuka

Wakati michuano ya Soka ya Ligi Kuu ya VODACOM, Hatua ya Nane Bora inatarajiwa kumalizika hivi karibuni, mechi kati ya wakongwe wa soka nchini inayochezwa Jumapili hii ndiyo itakayotoa mwanga wa nani bingwa wa mwaka huu.

Mechi hiyo ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa na washabiki wa soka nchini, inafanyika Jumapili hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam huku Timu ya Yanga ikiwa ni mwenyeji wa mechi hiyo

Yanga ambayo hadi mwanzoni mwa juma ilikuwa ikiongoza Ligi hiyo kwa kufikisha pointi 22, baada ya kutoka sare na timu ya maafande wa  Shinyanga; timu ya 82 Rangersilipolazimishwa kwenda sare ya bila goli. Hata hivyo, timu hiyo ilitolewa kileleni na timu ya Prisons ya Mbeya ambayo imefikisha pointi 23, baada ya kutoka sare na timu ya Mtimbwa, katika mechi iliyofanyika Jumatano iliyopita mjini Mbeya, kwa kwenda suluhu ya bila kufungana.

Kwa hali hiyo, timu ya Yanga katika msimamo wa ligi wa hivi sasa, iko nyuma ya Prisons ikiwa na pointi zake 22 huku Prisons ikiwa na pointi 23. Timu ya Simba imesukumwa kutoka katika nafasi ya tatu na kushuka hatua moja nyuma ya Mtibwa ambayo inashikilia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 21 ambazo ni sawa na timu ya Simba, lakini zikiwa zimezidiana magoli ya kufunga, Mtibwa ina magoli 18 ya kufunga na 11 ya kufungwa. Ikiwa Simba ina magoli 16 ya kufunga na kufungwa 8.

Kutokana na msimamo wa ligi hiyo ulivyo hivi sasa, upo uwezekano mkubwa kwa bingwa wa msimu huu kupatikana kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, ama timu tatu za kwanza kupishana kwa tofauti ya pointi chache

Licha ya pambano hilo la watani wa jadi kusubiliwa kwa hamu, bado kuna hali ya mkanganyo wa kufanyika kwa mpambano huo ambao timu ya Simba imesema haitatia mguu uwanjani siku Jumapili kwa madai kuwa mpango wa ratiba iliyotolewa na FAT hivi karibuni baada ya kuipangua ile ya kwanza unawatengenezea Yanga mazingira ya kuchukua Ubingwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ramadhani Balozi, kwa tamko alilolitoa kwa waandishi wa habari katikati ya wiki hii ni kuwa  uamuzi uliofikiwa na uongozi pamoja na wanachama wa klabu hiyo ni kutopeleka timu uwanjani siku hiyo.

 Alisema tayari klabu hiyo imekwisha kata Rufaa kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), kupinga kuchezwa kwa mechi hiyo.Akaongeza kuwa, rufaa yao inadai kuwa badala ya kucheza na Yanga, Timu ya Simba inatakiwa icheze na Timu ya Prisons ya Mbeya.

Alisema mechi ya Simba na Yanga haina budi iwe ya funga dimba, ili kuepusha upangaji wa matokeo kwa klabu ya Yanga.

Makamu Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wapenzi wa mpira wa miguu kutojisumbua kwenda uwanjani siku hiyo kwa vile hakutakuwa na pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki mbalimbali hapa nchini.

 Wakati huo huo: Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Yanga, Karigo Godson Karigo, amesema Simba iko kambini na inajiandaa na pambano hilo, “Sasa mimi nashangaa kama wao wanadai kutokuleta timu uwanjani siku hiyo sasa huko kambini Kibaha wanafanya nini, hiyo ni janja yao tu tumekwisha igundua sisi tutapeleka timu uwanjani na kitakachofuata tutakijua hapo uwanjanialisema Karigo.

Karigo alisema Simba wana dalili ya uoga na wanataka kueneza propaganda tu, ili watu washindwe kwenda uwanjani na nia kubwa ni kuhujumu mapato ya Yanga.

 Msimamo wa Ligi hiyo hadi Jumapili hii ni kama ifuatavyo;

 

                                                        P       W      D      L         GF    GA           PTS

 

Prisons                                            13        6       5       2        14       7         23

Yanga                                                           12        6       4       2        16       9         22

Mtibwa                                                          13        6       3       4        18      11         21

Simba                                                          12        5       6       1        16       8         21

Tukuyu Stars                                    14        5       1       8        10      17        16

82 Rangers                                       13        4       3       6        14      18        15

Reli                                                              14        4       2       8        17      22        14

Moro United                                                 13        3       2       8        10      19        11

 

 

Matola aipasulia FAT ukweli

Na Lilian Timbuka

MCHEZAJI wa timu ya soka ya Taifa, Seleman Matola, amekishauri Chama cha Soka Tanzania (FAT), kuelekeza nguvu zake katika maandalizi ya timu ya Soka ya Vijana chini ya umri wa miaka 17.

Matola aliyasema hayo katikati ya juma jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na Gazeti hili juu ya soka nchini.

Alisema pamoja na FAT kuiweka kambini timu hiyo mapema, lakini FAT inatakiwa kuisaidia timu hiyo kwa hali na mali ili ifanye vizuri katika mashindano yake ya kimataifa ya vijana chini ya miaka 17.

Alisema, kuisaidia timu hiyo kuandaa nafasi nzuri ya kushinda mechi yake dhidi ya Ethiopia mapema mwezi ujao.

Matola alifafanua kuwa muda uliopo kwa sasa unatosha kwa kujiandaa na mashindano hayo muhimu.

“Ni vizuri FAT na Serikali kwa jumla, wakawekeza nguvu za ziada ili kufanikisha timu hiyo kusonga mbelealisema mchezaji huyo ambaye ni kiungo wa Wekundu wa Msimbazi, Timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, FAT ina kila sababu ya kuelekeza nguvu hizo katika kikosi hicho baada ya timu nyingine ikiwemo ya Taifa Stars kupoteza matumaini ya kusonga mbele kwenye mashindano ya kimataifa.

Timu hiyo inayojulikanaa kama Serengeti Boys, ilifanikiwa kuingia hatua ya pili baada ya kuwaondoa timu ya Taifa ya Botswana kwa mabao 4-2

Katika mechi yao ya awali iliyofanyika nchini Botswana, Serengeti Boys iliwalaza Wabotswana hao kwa bao 1-0, kabla ya kuwapiga tena bao 3-2 katika mechi ya marudiano iliyofanyikia hapa nchini katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Karume mjini Arusha.

Timu hiyo iko chini ya makocha wa  Simba kwa nyakati tofauti, Abdallah Kibaden na Ronny Mitjens.

Alicante yaifanyia 'mtimanyonyongo' Valencia

MADRID, Hispania

 

TIMU ya Alicante imeifanyia roho mbaya Timu ya Valencia kwa kuifunga mabao 5-4  kwa penalti na kukata ngebe za kutwaa Kombe la Mfalme, Hispania mwaka huu.

Wiki iliyopita ilikuwambaya pia kwa timu nyingine za Athletic Bil- Bao iliyofungwa mabao 2-1.

Timu ya Real Union de Irun ya  Daraja la Tatu na Malaga iitolewa na timu inayoongoza msimamo Daraja la Pili, Xerez kwa mabao 2-0.

Baada ya kumalizika dakika 90 za kawaida kwa sare ya bao 1-1, vijana wa kocha Rafa Benitez, walibadilika na kusukuma mashambulizi ya nguvu na kufanikiwa kupata mabao kupitia kwa Juan Sanchez.

Bao la kwanza  lilitokana na pasi ya Miguel Angel Angulo, na jingine kupitia kwa Mista.

Valencia ilikuwa imejiweka vema kuweza kutoka nje na ushindi, lakini Alicante iliyo katika Daraja la Tatu, ilijibu kwa nguvu na kujipatia mabao mawili ya haraka haraka kupitia kwa Juli na Toni Garcia, na hivyo kuwa sare na ndipo ikipigwa mikwaju ya penalti.

Wakati Valencia iliishia raundi ya pili, Real Madrid haikuwa na matatizo makubwa, kwani iliitwanga bila huruma timu ya daraja la pili ya Real Oviedo mabao 4-0.

Kikosi hicho cha Kocha Vicente del Bosque kiliingia uwanjani bila ya nyota wake  10 walioachwa nyumbani.

Baadhi ya nyota hao ni Ronaldo, Roberto Carlos, Zinedine Zidane, Raul na Luis Figo.

pamoja na kutumia kikosi cha pili bado miamba hiyo ya soka barani Ulaya ilifanikiwa kuibuka na ushindi huo kwa mabao yaliyofungwa na Tote na Javier Portillo; kila mmoja alifunga mawili.