Simba, Mtibwa 'zapiga misele' kusaka wachezaji Uganda, Kenya

       Na Lilian Timbuka

BAADA ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Castle,hivi sasa vilabu vya soka nchini vimeingia katika hatua mpya ya kusaka wachezaji wa kusajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.

Akizungumza na Gazeti hili hivi karibuni jijini Dar es Salaam , Kocha Mkuu wa timu ya soka ya Mtibwa,Morogoro Twahir Muhiddin amesema amefanya mazungumzo na mchezaji wa timu ya Taifa ya Kenya (Harambee Stars) Mambo Robert kwa lengo la kumsajili katika timu yake.

Twahir anaifundisha Mtibwa kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya aliyekuwa Kocha wa timu hiyo,Roul Shungu kurejea kwenye timu yake ya zamani ya Rayon Sports ya Rwanda.

Twahir alisema japokuwa tayari mchezaji huyo amekwisha rejea nyumbani lakini amemuahidi kuwa wataendelea kuwasiliana ili kukamilisha mipango ya kumsajili.

“Sasa hivi tayari tumefanya mazungumzo ya awali na mchezaji mwenyewe ameonyesha nia ya kukubali kusajiliwa na timu yangu,kwa hiyo nasubiri tena niwasiliane naye katika hatua nyingine inayofuata”,alisema Twahir.

Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mchezaji huyo kabla hajaondoka kueleka nyumbani Kenya, naye alithibitisha kuwa ni kweli alifanya mazungumzo ya awali na kocha huyo na hivyo alimuahidi kuwa watawasiliana zaidi pindi akiwa kwao

“Twahir ni Kocha ninaye mfahamu vizuri na alikuwa akinipenda tangu tulipokuwa naye Kenya, na ni Kocha mzuri sana hivyo namuelewa vizuri kwa hiyo ombi lake nitalifanyia kazi huko nyumbani”, alisema Robert.

Mchezaji huyo kwa hivi sasa hana klabu anayoichezea nchini kwake zaidi ya timu ya Taifa baada ya kurejea nchini mwake hivi karibuni akitokea majuu ambako alikuwa akilisukuma gozi ,hivyo kwa hivi sasa ni mchezaji aliye huru.

Wakati huo huo wekundu wa Msimbazi,timu ya Simba ,imefanya juhudi za kufanya mazungumzo ya kumsajili mchezaji wa timu ya Taifa ya Uganda, Mubiru Hassan,lakini juhudi hizo zimegonga mwamba kufuatia mchezaji huyo kutaka dau kubwa.

Akizungumza katika ofisi za Klabu hiyo ya Simba zilizopo jijini Dar es Salaam,Katibu Msaidizi wa klabu hiyo,Marko Masanja alisema amesikitika kumkosa Mubiru ambaye ni mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Uganda na Sports Club Villa nchini humo kutokana na kutaka pesa nyingi ili asajiliwe.

Masanja alisema Mubiru anahitaji kiasi cha Shilingi za Kitanzania milioni 10 ili asajiliwe na timu hiyo ya simba kitu ambacho ni ndoto kwa klabu za Tanzania kusajili mchezaji kwa dau kubwa kiasi hicho.

Alisema alijitahidi kumuelewesha hali halisi lakini bado Mubiru hakubadilisha msimamo wake.

“Yeye binafsi alionyesha nia ya kujiunga na sisi lakini bado alikuwa na msimamo wake huo wa shilingi milioni 10”, alisema Masnja.

Masanja alisema kwa kuwa Mubiru ameng’ang’ana na kiwango hicho, wao Simba wameonelea ni bora kumuacha japo ni kwa shingo upande.

“Tungekuwa na pesa hiyo na uchumi mzuri katika klabu yetu tusingesita kumsajili lakini hali ndiyo haituruhusu, acha tushindwe sisi, kwani si unajua kisichoridhiki hakiliki” alisema Masanja.

Msanii atabiri ngoma za asili kupoteza maana halisi

Na Peter Dominic

PAMOJA na wasanii mbalimbali nchini kujitokeza kuimba nyimbo za asili,imeelezwa kuwa nyimbo hizo hususan za kikabila, huenda zikapoteza maana halisi kufuatia wahusika kutumia zana za kisasa katika uimbaji wao.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katikati ya juma, mmoja wa wasanii kutoka katika kikundi cha ngoma za asili cha Abateshweka chenye makao yake Manzese jijini Dar es Salaam,Ponsian Twiganaki alisema ili ngoma hizo zionekane za asili kikwelikweli,ni lazima upigaji wake utumie zana za asili.

“Utumiaji wa vyombo maalumu kama gitaa na vifaa vingine, vinafifisha ngoma za asili na huenda kizazi kijacho kikashindwa kujua kama kabila fulani lilikuwa na ngoma za asili”alisema.

Msanii huyo alitoa mfano wa wanamuziki chipukizi na machachari katika kuimba nyimbo za kiasili,Saida Kalori na Pracsida Lweyendela ambao wamekuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kabila ya Wahaya kwa kutumia vyombo vya kisasa baada ya kurekodi nyimbo zao katika studio.

“Msanii huyo pamoja na mambo mengine, alisema wasanii hao licha ya kuwa kazi yao ni nzuri lakini hawapigi ngoma zao pale wanapofanya maonesho badala yake hucheza shoo kutokana na muziki unaolia katika vyombo.”alisema.

Msanii huyo aliendelea kusema kuwa pamoja na kuwepo kwa vikundi vingi vinavyoimba vyimbo za asili lakini vimeshindwa kabisa kupiga ngoma za kimakabila kwakuwa havina wapigaji wa ngoma hizo.

Vilabu 45 kushiriki Ligi ya Watoto Temeke

Na Meryna Chillonji

 

JUMLA ya vilabu 45 vilivyopo chini ya Chama cha Michezo kwa Vijana Wadogo wilayani Temeke (TEDIYOSA) vinatarajiwa kushiriki  katika Ligi ya Watoto inayotaarajiwa kuanza November 25 mwaka huu.

Akizungumza na Kiongozi hivi karibuni kwenye ofisi za Chama cha Mpira wa Miguu wilayani humo (TEFA) zilizopo Tandika jijini Dar es salaam Katibu Msaidizi wa TEDIYOSA ,Nassoro Mwamba alisema kuwa  vilabu hivyo vitapangwa katika makundi matatu.

Mwaamba alisema ligi hiyo ambayo huchezwa kila mwaka, ina lengo la kuinua,kukuza na kuendeleza vipaji vya watoto wadogo ambao wanahitaji msaada wa kuendelezwa kimichezo na watu wenye mapenzi mema.

Hata hivyo Mwamba anavisisitizia vilabu vyote vilivyo katika Ligi Daraja la Tatu na la Nne ambavyo vinahitaji kushiriki katika ligi hii hiyo,vifike katika ofisi za TEFA  kuchukua kadi na fomu kwaajili ya maandalizi ya ligi hiyo.

Alisema hadi sasa vilabu vipatavyo kumi tayari vimekwisha chukuwa fomu za kujiunga na ligi hiyo inayotarajiwa kutimua vumbi katika viwanja vitatu wilayani humo.

Katibu Msaidizi huyo wa TEDIYOSA alivitaja vilabu hivyo vilivyokwisa chukua fomu kuwa ni Good Hope Kids,Big Fish Kids,Charaambe Sports,Nurykimi Kids,Mchikichini Kids na Serengeti Boys.

Vingine ni Vitukaa Boys,Polisi Balax Kids,Nia Kids na Buza Rangers,vyote vya Manispaa hiyo ya Temeke.

Sambamba na hayo,Katibu Msaidizi huyo ametoa ombi kwa  wafadhili na wahisani popote walipo wajitokeze kusaidia michezo hii kwani kujitokeza kwao kutasaidia kujenga mhimili wa maendeleo ya michezo nchini.

Makocha wanne Taifa Stars hawatoshi-Dewji aikejeli FAT

Dalphina Rubyema

UONGOZI wa Chama cha Soka nchini (FAT) umekejeliwa kuwa makocha wanne walioteuliwa kuifundisha timu ya Taifa (Taifa Stars),hawatoshi na badala yake waongezwe wanne wengine ili kazi ya kuwanoa wachezaji hao ifanyike barabara.

Kejeli hiyo imetolewa hivi karibuni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kuendeleza timu ya Taifa (Taifa Stars),Khasim Dewji wakati akizungumza na Gazeti hili jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Dewji alisema haoni sababu uongozi wa FAT kuweka namba kubwa ya makocha kwa ajili ya kuinoa Taifa Stars kwani hakuna cha maana kilichokwisha fanyika tangu makocha hao wateuliwe.

“Sioni kama kuna mabadiliko yoyote. Kama namba kubwa ya makocha inaweza kubadilisha sura ya mchezo basi waongezwe makocha wengine wanne na kufikia nane”alisema Dewji.

Dewji ambaye pia ni mfadhili wa zamani wa timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam,alisema FAT inachopaswa kufanya ni kutimiza mahitaji halisi ya kuboresha kiwango cha timu hiyo ya Taifa.

Alitaja moja ya mambo hayo muhimu kuwa ni pamoja na kutafuta fedha za kuweza kumlipa kocha wa kigeni mwenye upeo wa juu pamoja na kupata nafasi kuichezesha timu hiyo mechi za majaribio dhidi ya timu zenye uwezo kisoka.

Katika kinyang’anyiro cha kuwania Kombe la Mataifa Afrika ,Taifa Stars ilifungwa na timu ya Taifa ya Benin kwa mabao 4-0 kabla ya kufungwa tena na timu ya Taifa ya Sudan kwa mabao 2-1.

Kufuatia matokeo hayo,FAT iliteuwa makocha wanne kwa ajili ya kuinoa timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Castle.

Makocha hao ni pamoja na Mshindo Msolwa,Salum Madadi ,Hafidh Badru na James Siang’a.

Hata hivyo pamoja na utitiri wa makocha hao,Taifa Stars bado imeendelea kufanya vibaya katika michuano hiyo ya Kombe la Castle ambapo katika mechi ya kufuta mshindi wa tatu katika kombe hilo,ilifungwa  mabao 4-3 na timu ya Taifa ya Afrika ya Kusini(Bafana Bafana).

Hata hivyo katika mchezo huo uliofanyika Jumamosi iliyopita kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,ushindi wa Bafana Bafana ulipatikana kwa penati baada ya dakika za mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Timu ya Taifa ya Kenya ndiyo iliyoibuka mshindi wa Kombe hilo la Castle baada ya kuibamisa timu za Taifa ya Uganda kwa bao 5-3.