FAT yasitisha pambano baina ya Yanga, Nkana Red Devil

Na Anthony Ngonyani

CHAMA cha Soka nchini (FAT) kimesitisha mchezo wa kimataifa ambao ulikuwa ufanywe kirafiki kati ya Timu ya Yanaga ya Tanzania na Nkana Red Devils toka nchini Zambia

Akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake mwishoni mwa juma, Katibu Mkuu wa FAT ,Michael Wambura alisema mchezo huo umesitishwa kutokana na sababu kwamba waandaaji wa mchezo huo wameshindwa kuwasiliana na FAT.

"Waandaaji wa mchezo huu walipaswa kuwasiliana na chama cha soka nchini ili kuweza kutoa taarifa kuhusu mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa" alisema Wambura.

Alisema FAT ilipata taarifa ya mchezo huo kupitia vyombo vya habari kuwa kuna mpambano mkali kati ya timu hizo mbili.

Mpambano huo kati ya Yanga na Nkana Red Devils ya Zambia uliokuwa umeandalia na Chama cha Soka cha Sinza ,ulipangwa kufanyika Jumapili ijayo katika uwanja wa taifa.

Wawekezaji watakiwa kuwekeza katika sekta ya utamaduni

Na Lilian Timbuka

WAWEKEZAJI nchini wametakiwa kuwekeza katika sekta ya utamaduni kwa kujenga kumbi na viwanja vya kisasa.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni nchini ,Daniel Ndagala wakati wa warsha ya siku moja iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

Ndagala alisema wawekezaji waione na kuitambua kazi ya utamaduni kwa kujenga kumbi na viwanja, ambapo watapata faida kwa kuweka ada, ambayo itakuwa kiingilio kwa watakaotumia.

"Zipo sanaa na utamaduni ambao kwa mazingira ya hapa kwetu hazistahili kabisa na zipo ambazo zinafaa hata mbele ya vijana na watoto wadogo", alisema Ndagala.

Pia alisema itabidi wawatumie wanasheria ili kuwapa mawazo wasanii ili wasiingie mikataba ovyo isiyokuwa na maslahi, ikiwemo kuwa na Bima, malipo baada ya kufariki na kuumia.

Naye Afisa Mtendaji wa Haki Miliki na Haki Shiriki (COSOTA), Steven Mtetewaunga aklisema wasanii wana haki ya kurekodi kazi zao, kuzitangaza, kuuza na kupata malipo kutokana na kazi zao.

Washa hiyo ilihudhuriwa na wasanii na wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi kutoka vituo vya polisi vya wilaya zote za Mkoa wa Dar es salaam, Katibu mkuu wa chama cha muziki wa dansi Tanzania hakuweza kuhudhuria washa hiyo.

LIGI DARAJA LA TATU KANDA YA DAR ES SALAAM

Abajalo yatembeza ‘bakuli’

Na Richard Timothy , RCJ

WAPENZI wa michezo nchini, wameomba kuisaidia kwa fedha na vifaa vya michezo,timu ya mpira wa miguu ya Abajalo iliyopo katika Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam,inayo jiandaa kushiriki mashindano ya Ligi Daraja la Tatu Kanda.

Mashindano hayo yatakayo zishirikisha timu sita za Manispaa za Kinondoni, Ilala na Temeke,yanatarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Ombi hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa timu hiyo,Novatus Damiani Chizani wakati akizungumza na gazeti hili ofisini kwake katikati ya juma.

Alisema licha ya ukatailiyonayo, timu yake ipo katika maandalizi makali chini ya kocha Stephine Wimbo ,mazoezi yanayoendelea kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mashujaa .

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, mashindano hayo yameandaliwa na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).

Katibu huyo amesema pia kwamba timu yake imeshwai kutoa wachezaji lukuki waliochuliwa na timu kubwa nchini ambapo alitaja baadhi yao kuwa ni pamoja na Kally Ongala (Yanga) ambaye sasa yupo Uingereza, Matokeo Lukas na Selemani Seif, Raymond Ndunguru na Aron Nyanda ambao wote wanachezea timu ya Yanga kwa sasa pamoja na George Ngasonwa [Lipuli] na Edward Kayoza (Simba).

Kwaya ya Moravian yaisubiri Pasaka kwa hamu

l Mlutheri ainoa zaidi

Na Mwandishi Wetu

WAIMBAJI wa Kikundi cha kwaya cha "Neema Choir" cha Kanisa la Moravian Tanzania, Ushirika wa Temeke, Dar es Salaam, wamo mbioni kukamilisha maandalizi na wamesema wanaisubiri Sikukuu ya Pasaka kwa shauku ili waoneshe vitu vyao.

Wakizungumza kwa pamoja na KIONGOZI ushirikani hapo, mwanzoni mwa juma lililopita, Katibu wa Kwaya, Bw. Peter Kipwanya; Mwenyekiti, Bw. Asajile Mwakasege; Makamu Mwenyekiti, Bibi Judith E. Asejile na Mwalimu wa muda wa Kwaya hiyo, Bw. Archbold Tesha, walisema maandalizi yote muhimu tayari yamekwisha kamilika na kilichobaki kwao, ni kuisubiri Sikukuu ya Pasaka itakayofanyika kitaifa ushirikani hapo, ili waoneshe umahiri wao katika kuinjilisha kwa njia ya nyimbo.

Bw. Tesha ambaye ni Mwalimu wa Kwaya ya Sayuni ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Kinondoni, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alisema hadi sasa Kwaya ya Neema imekwisha andaa nyimbo kadha ikiwa ni pamoja na "Damu ya Yesu" na "Amefufuka".

Alikataa kuzitaja nyimbo nyingine kwa madai kuwa si vema kumaliza uhondo wa nyimbo na hivyo, zitasikika siku ya siku.

"Tunaamini mambo sasa yataenda vizuri na siku hiyo mambo yatakuwa moto moto kwa kuwa mazoezi tuliyoyafanya, yanatia moyo na yanatufanya hata sisi viongozi tujiamini kuwa tutafanya tunaokusudia kufanya," alisema Tesha.

Naye Katibu wa Kwaya hiyo Bw. Kapwaya, alisema, "Waimbaji wameonesha ari ya hali ya juu na hii ni kwa kuwa wanajua wako katika uwanja wa nyumbani hivyo lazima waoneshe mambo kama watu ambao kweli ni wenyeji. Tuna uhakika tutafanya mambo ya kuvutia sana."

Naye Mchungaji wa Ushirika huo, Tuntufye Mkumbo, alisema tayari maandalizi ya kwaya yanaridhisha na sasa wanachosubiri, ni siku hiyo ya kuushangilia Ufufuko wa Kristo.

Alisema hata Kwaya ya Wazee wa Wilaya ya Mashariki, ipo katika mazoezi makali kwa ajili ya siku hiyo.

Aliwataka waamini kujiandaa vema kiroho ili wafufuke vema na Yesu Kristo wakati wa Pasaka na hivyo, kuleta maendeleo zaidi ya Kanisa kiroho na kimwili.

Kanisa la Ushirika wa Temeke limekuwa katika maandalizi makali kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka kitaifa ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa jengo la kanisa, usafi wa mazingira, nyimbo mbalimbali na maandalizi ya kiroho kwa waamini.

Sikukuu ya Pasaka mwaka huu itafanyika kitaifa katika Ushirika wa Temeke wa Kanisa la Moravian Tanzania, Wilaya ya Mashariki, Jimbo la Kusini, Jumapili ijayo.

Viongozi wengine wa Kwaya hiyo ya Neema yenye wasanii wapatao 35 ni Katibu Msaidizi, Jema James, Mweka Hazina, Kisa Asion na Msaidizi wake, Leah Andrew.

Wengine ni Mwalimu Mkuu, Butusyo Mwatebela na Mwalimu Msaidizi wa Kwaya, Lwaga Mwambande.

Rwanda yamtaka Masamaki

 

Na Joseph Kiboga

LICHA timu ya Simba kumweka pembeni mchezaji wake mchezaji John Tomas ‘Masamaki’Kocha wa zamani wa timu ya Tibwa Sugar ya Morogoro,Roul Shungu anamtafuta kwa udi na uvumba mchezaji huyo ili aende kusakata kambumbu nchini Rwanda.

Kwa mujibu wa habari zilizopatika jijini Dar es Salaam zinasema mchezaji huyo anatafutwa aende kujiunga na timu ya Rayon Sport, inayofindishwa na Shungu mwenyewe kwa sasa.

Habari hizo ambazo zimedhibitishwa na Masamaki mwenyewe zinazidi kusema kuwa Shungu alikuwa anamwania mchezaji huyo kabla hajaenda Kigali.

"Ni kweli Shungu alinifuata ili niende naye Rwanda lakini sikuwa tayari kwa vile leseni yangu ya uhamisho bado ilikuwa Simba" alisema Masamaki.

Awali Masamaki alitngazwa kuachwa na timu hiyo ya Simba lakini alirejeshwa kabla ya kuachwa tena.

Hata hivyo alisema hata baada ya kutangazwa kuachwa mara ya kwanza,Shungu alimtuma mtu kuja kumchukua lakini alishindwa kuondoka kwa kuwa mambo yake hayakuwa sawa.

Alipoulizwa kama atakuwa tayari kwenda endapo atafuatwa kwa kipindi hiki ,alikataa kulizungumzia hilo.