Simba yapania zaidi kuichapa Nkana Red Devils

l Yasema itarudia historia ya mwaka 1976

l Yadai mabao 4-0 si lolote si chochote

Na Lilian Timbuka

Timu ya soka ya simba ya jiji Dar es Salaam imesema itumia historia ya mwaka 1976 kuifunga timu ya Nkana Red Devils ya Zambia katika marudiano ya Michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika katika mechi itakayofanyika nchini hivi karibuni.

Katibu Mkuu wa timu hiyo Kassim Dewji aliyasema hayo ofisini kwake jiji Dar es salaam kuwa wakati akizungumza na gazeti hili.

Alisema kufungwa mabao 4-0 si neno kwa klabu hiyo ya Msimbazi, isipokuwa kinachotakiwa hivi sasa ni kufanya mazoezi vya kutosha na kurekebisha makosa yaliyopelekea timu hiyo kufungwa idadi hiyo kubwa ya magoli na timu ya Nkana Red Devils ya Zambia.

"Tutahakikisha tunashinda inawezekana kwani ni simba pekee iliyowahi kuitoa Mufurila Wandarers mwaka 1976 pale walipotufunga nyumbani mabao 4-0 na sisi tukawafunga kwao mabao 5-0", alisema Dewji.

Alisema kwa kutumia historia kama hiyo wanamatumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano ambao utafanyika baada ya wiki mbili zijazo hapa nchini.

Dewji alisema uongozi wa simba utashirikiana kwa hali na mali kocha Mkuu wa simba Mkenya James Siang’a kuhakikisha inafanya vizuri katika mchezo huo ambao alikiri kuwa ni mgumu.

Naye Innocent Ndwewe, RCJ, anaripoti kuwa,

Washabiki wa timu ya simba wamejigamba kuibuka na ushindi katika mchezo wa marudiano na Nkana Red Davils ya Zambia katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika kutokana na sababu kwamba timu hiyo inacheza nyumbani.

Wakizungumza klabuni hapo kwa nyakati tofauti,washabiki hao walisema kuwa wao kama wapenzi wapo tayari kujitokeza kwa wingi na kuishangilia.

Mmoja wa washabiki hao Muustapha Ayoub alisema kuwa wanamatumaini na ushindi kwa sababu Simba ni moja ya timu yenye wachezaji wazuri na wenye uwezowa kufanya maajabu

Alisema uzoefu wa mechi za Kimataifa pia utachangia ushindi kwani wiki mbili zilizopita imetoka kulitwaa Kombe la Afrika Mashariki na Kati

Katika mchezo wa awali wa raundi ya kwanza uliofanyika mjini Kitwe Zambia, Simba ilichapwa mabao 4-0 na Nkana Red Devils ya Zambia.

Ili timu hiyo ya Simba iweze kusonga mbele katika michuano hiyo,inahitaji ushindi wa mabao 5-0 kazi ambayo itakuwa ngumu.

SUALA LA MADAI YA SIMBA DHIDI YA FAT

Wanachama watakiwa kutoa uamzi

Na Lilian Timbuka

UONGOZI wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam,umeliacha mikononi mwa wanachama wa klabu hiyo suala la madai ya milioni 30 ambazo inazidai kwa Chama cha Soka nchini (FAT)baada ya kunyakua Ubingwa wa Ligi ya Soka Bara.

Akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake katikati ya wiki, Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo Ramadhani Balozi alisema kwamba kutokana na uzito wa suala hilo uongozi umeona hauna uwezo wa kulitatua zaidi ya wanachama wenyewe kulitolea maamuzi.

Alisema sio busara kwa uongozi wa klabu hiyo kutoa maamuzi kuhusiana na fedha hizo pasipo kuwashirikisha wanachama.

Alisema kamati ya utendaji itakutana na kupanga siku ya kukutana na wanachama ili waamue la kufanya.

"Sisi kama uongozi hatuwezi kutoa uamzi juu ya suala hili bila kuwashirikisha wanachama ambao ndiyo wadau wakubwa kwani uamuzi kama huo una madhara makubwa ambayo tutashindwa kujitetea mbeleni tutakapokwama" alisema Balozi.

Kaimu Mwenyekiti huyo alisema wanafanya mpango mkutano huo ufanyike kabla ya Ligi Kuu ya soka ya VODACOM kuanza inayotarajiwa kuanza Aprili 13 mwaka huu.

Ligi hiyo itakuwa chini ya udhamini mpya wa kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom baada ya kuchukua nafasi ya wadhamini waliojitoa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) iliyokuwa ikidhamini michuano hiyo hapo awali kupitia bia yake ya Safari Lager.

Chama cha soka nchini FAT kupitia kwa uongozi wake uliopita waliahidi kutoa zawadi kwa timu zilizoshinda kama ilivyokuwa imeahidiwa na wadhamini wa awali TBL kabla hawajajitoa kudhamini ligi hiyo ikiwa ni pesa taslim zipatazo Shilingi milioni 30, kwa klabu ya Simba ambao walifanikiwa kutwaa ubingwa wa Bara kwa mwaka jana kitu ambacho hakijatekelezwa hadi sasa.

Lakini tangu kuingia madarakani kwa uongozi mpya wa Chama cha Soka nchini FAT kimekuwa kikishindwa kusema lolote kuhusiana na fedha hizo, na cha ajabu na kushangazaKatibu mkuu wa sasa Michael Wambura kila akiulizwa kuhusu sakata hilo huwa akikana kulizungumzia suala hilo ambalo kwa sasa ni kitendawili kilichokosa mteguzi, FAT au waziri Kapuya kupitia wizara yake ya Maendeleo ya Vijana na Michezo.

Doi Make wa Yanga aanza mazoezi

Na Anthony Ngonyani.

MLINDA mlango wa timu ya Yanga ya jijini Dar-es-salaam Doi Make ameanza mazoezi na timu yake baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuumia.

Akizungumza na gazeti hili kwenye eneo la uwanja wa Karume ambako timu hiyo inafanyia mazoezi,alisema tangu aumie kirefu kimepita amekuwa akihudumiwa na timu na ndio sababu iliyopelekea kurudi na kuendelea na timu hiyo.

Alisema ataichezea Yanga katika mechi zake mbali mbali zinazokuja na kabla ajajiunga na wenzake alikuwa akifanya mazoezi peke yake nyumbani kwake.

Alisema hivi sasa yupo fiti na ana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika mechi zake zijazo katika nafasi yake hiyo ya ulinda mlango.

Sina imani na FAT - Pape

lAdai uongozi hauna dira wala mwerekeo

Na Joseph Kiboga

MSHAURI wa ufundi wa Shirikisho la Soka ulimwenguni (FIFA) BukhardPape amedai kuwa hana imani na viongozi wa sasa wa Chama cha Soka nchini (FAT).

Akizungumza na KIONGOZI juzi,Pape alisema kuwa hadhani kama viongozi waliopo madarakani kwa sasa wana nia ya kweli ya kuendeleza mchezo wa soka.

Mshauri huyo ambaye FAT imesitisha mkataba wake,alisema kuwa uongozi wa sasa ambao upo chini ya Katibu Mkuu Michael Wambura hauna dira wala mwelekeo.

Alisema kuwa wiki mbili zilizopita aliwapelekea programu ya kuendeleza mchezo huo lakini alichoambulia ni taarifa ya kusitishwa kwa mkataba wake.

"Hawana mpango wowote wa kuendeleza soka hawa, afadhali FAT ya Rage" alisema Pape na kuongeza kuwa hana kahika iwapo Wambura alipata hata kucheza soka.

Alisema mtu ambaye ameshiriki soka kabla ya kuwa kiongozi ni lazima awe na programu lakini hivi sasa kitu kama hicho hakipo FAT.

Pape alisema huwa programu aliyowakabidhi FAT inahusu uendelezaji wa soka kwa vijana watoto na wanawake na amekitaka chama hicho kiitumie programu hiyo kama kina nia ya kweli ya kuendeleza mchezo.

Alisema amefikia hatua ya kuandaa programu hiyo baada ya kuona chama hicho kinakuwa bubu juu ya mikakati ya uendelezaji wa soka.

"Kila nilipokuwa nawauliza walikuwa wananijibu mara subiri kidogo,mara ooh... wiki ijayo na vitu kama hivyo,inasikitisha" alisema na kuongeza kuwa hasikitiki kukatishwa kwa mkataba wake ambao ulikuwa unamalizika miaka miwili ijayo.

Pape ambaye alidai kwamba anakidai chama hicho zaidi ya shilingi 500,000 ambazo ni pesa za mafuta ya gari, mshahara wa mlinzi na gharama zingine alisema kuwa katika kipindi ambacho amekuwepo amegundua kuwa kuna hazina ya wachezaji wenye vijapaji lakini viongozi ni wabovu ambao hawana nia ya kuendeleza mchezo wenyewe.