Pallsons yatamba kuinyuka Yanga

l Mziray asema 'Yanga ya sasa haitishi kama nilivyofundisha'

Na Lilian Timbuka

BAADA ya kuicharaza na kuitupa nje ya mashindano ya Kombe la Tusker kwa mabao 3-1 timu ya soka ya Pallson imetamba kuisambaratisha Yanga katika mashindano ya nusu fainali ya kundi A.

Kocha Mkuu wa klabu ya Pallsons ya Arusha Sleysaid Mziray alisema mwishoni mwa juma wakati akizungumza na KIONGOZI katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuwa timu yake atahakikisha kwa udi na uvumba inaisambaratisha Yanga katika mchezo unaofanyika jumamosi hii katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa kutamba kuwa anavyoifahamu Yanga anaamini haiwezi kuikwamisha timu yake kufuzu katika mashindano ya nusu fainali.

"Yanga ya mwaka huu haitishi kama Yanga niliyokuwa nikifundisha siku za nyuma" alisema.

Mziray aliongeza kuwa kwa hatua iliyofikiwa na timu yake hadi sasa Pallsons haioni sababu y a kutoingia fainali na timu yoyote itakayopatikana kutoka kundi B.

Hata hivyo alikiri kuwa katika kundi B kuna timu aliyoiita Kigogo ambayo ni watani wa jadi wa Yanga wekundu wa Msimbazi (Simba).

Alisema kwa sasa timu yake inao vijana machachari na wanaojituma wawapo uwanjani.

Aliongeza kuwa pia wachezaji wake wanaonesha ari ya ushindi. Aliwashauri viongozi wa Yanga kutokalia benchi la wachezaji wao siku hiyo kwani Yanga itakapofungwa na Pallsons itakuwa aibu kwa viongozi hao hivyo bora wakaed kwa washabiki wengine.

Mziray alisema timu yake haikuja Dar kutalii bali kulitwaa kombe la Tusker.

Hata hivyo alikataa kukitaja kikosi kitakacho jitupa uwanjani.

Yanga na Pallsons kwa pamoja zimefuzu kuingia nusu fainali ya kombe la Tusker katika kundi A zote zilishinda katika nafasi mbili za kwanza.

Mshindi katika mechi baina ya Yanga na Pallsons ndiye atakayemenyana na mshindi wa kundi B. Timu za kundi B ni pamoja na Simba, Prisons ya Mbeya na vijana wa Ilala.

Ni Mtibwa ama Ferrivialio ?

Na Anthony Ngonyani

TIMU ya Mtibwa ya Morogoro inatarajiwa kushuka dimbani Jumamosi kupambana na Ferrivialio ya Msumbiji katika raundi ya kwanza ya ya Michuano ya Kombe la CAF,mchezo utakaochezwa katika uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Mratibu wa timu hiyo Jamal Bayser aliliambia gazeti hili juma lililopita jijini Dar es Saalam kuwa timu hiyo inaendelea na mazoezi na wanauhakika wa kushinda.

Bayser aliongeza kusema kuwa mgeni rasmi katika mchezo huo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mussa Nkanga.

Alisema ushindi huo utakaopatikana utaiweka katika mazingira mazuri timu hiyo ya Tuliani mjini Morogoro katika mchezo wa marudiano utakaofanyika wiki mbili zijazo nchini Msumbiji.

Alisema timu yake ina matumaini ya kufanya vyema kutokana na kuwa na wachezaji tishio ambao wananolewa Kocha kutoka nchini Kenya.

Waziri Kapuya azitaka Mtibwa, Polisi Zanzibar kuiga mfano wa timu ya Simba

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, Professa Juma Kapuya amezitaka timu za Mtibwa Sugar ya Morogoro na Polisi Zanzibar, kufuata nyayo za timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam.

Waziri Kapuya aliyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari habari hizi ofisini kwake.

Huku akiimininia sifa kemkem, timu ya Simba kwa kutwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki Kati,Waziri Kapuya alisema kuwa timu hizo hazina budi kuiga mfano huo.

Alisema "ushindi wa Simba ni fahari kwa Tanzania. Kwakweli wanastahili pongezi sana,timu nyingine akina Mtibwa na Polisi Zanzibar waige mfano huo"alisema Profesa Kapuya. Hata hivyo aliitaka timu hiyo ya Simba isibweteke kwa ushindi kwa ushindi huo na badala yake iendeleze ubabe huo ili iweze kunyakua ushindi mwingine wa Michuano ya Kimataifa. Mheshimiwa kapuya aliongeza kusema kuwa wakati umefika kwa wanachama na wapenzi wa timu hiyo kuacha tofauti zao na kuwa na umoja, mshikamano wa dhati kwani bila kuzingatia hayo mafanikio hayaji.

Alisema serikali itaendelea kuipa ushirikiano Simba katika michuano inayoendelea ya Klabu Bingwa Afrika ili iweze kuiwakilisha vyema Tanzania

Wakati timu ya Polisi ya Zanzibar inaiwakilisha Tanzania katika michuano Kombe la Washindi barani Afrika , timu ya Mtibwa Sugar ianawakilisha Tanzania katika Kombe la CAF.

Simba kumuadhibu Macho

Na Mwandishi Wetu

KLABU ya soka ya Simba imesema italazimika kumuadhibu mchezaji wake Yusufu Macho kwa kuchelewa treni Zambia kwa madai kuwa, kuchelewa ni kosa na ni utovu wa nidhamu.

Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa juma, zimemkariri Katibu Mkuu wa Simba, Kassim Dewji, akisema kuwa, Kamati ya Utendaji ya Klabu hiyo itakaa kujadili suala la mchezaji huyo.

Jumanne iliyopita mchezaji huyo (Macho), alishindwa kuondoka pamoja na wachezaji wa timu yake kwenda nchini Zambia katika mashindano Ligi ya Mabingwa wa Afrika.

Habari zinasema Macho alichelewa treni ya TAZARA iliyoondoka na wachezaji wenzake baada ya kumpeleka hospitali mkewe ambaye alikuwa mgonjwa.

Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Ramadhani Balozi, alikiri kuwa Macho alimpeleka mkewe hospitali. Kuhusu kuchelewa kwa Macho, Dewji alisema, "Kuchelewa ni utovu wa nidhamu... lazima tumuadhibu kwa kumnyima posho..."

Hata hivyo, habari zinasema Macho alikuwa na mpango wa kuwafuata wachezaji wenzake nchini Zambia, kwa ndege Ijuma iliyopita, akiongozana na na Meneja wa timu hiyo, Innocent Njovu

Jumamosi hii Simba inakung’utana na klabu ya soka ya Nkana FC.

Simba ambao ni majogoo katika kabumbu la Afrika Mashariki na Kati, imevuka hatua ya kwanza ya mashindano hayo baada ya kuikwanyua Red Star ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 4-1.

KINYANG’ANYIRO CHA KOMBE LA KLABU BINGWA AFRIKA:

Tanzania kuimba kidedea Zambia?

Na Joseph Kiboga

HADI hivi sasa bado ni kitendawili kwa wapenzi na mashabiki wa soka nchini, juu ya nani atakuwa mkali kati timu ya Simba na Nkana Red Devil ya Zambia, katika kinyang’anyiro cha Kombe la Klabu Bingwa Afrika.

Wengi wa mashabiki na wapenzi wa soka kama baadhi yao kama walivyo hojiwa na gazeti hili,wanadai kuwa ni lazima Simba ambao ni mwakilishi wa Tanzania, itaendeleza ubabe wake kwa kuibuka mshindi.

Shaaban Maalim mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam alisema kuwa hana wasiwasi na timu ya Simba juu ya mchezo wake dhidi ya timu ya Nkana Red Devil kutoka nchini Zambia.

"Ni matumaini yangu kwamba huko Zambia, Simba itapeperusha Bendera ya Tanzania,sina wasiwasi kabisa" alisema Maalim.

Naye shabiki Badru Mawadhi wa Keko wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, alisema kuwa ukali wa timu ya Simba umejidhihirisha baada ya kunyakua ushindi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.

Alisema pamabano hilo litakuwa nila kukata na shoka kwani anaimani kwamba Simba itacheza bila wasiwasi kwani hivi sasa wachezaji wake bado wana pesa za kutosha walizopata baada ya kunyakua kombe hilo la Kagame.

Timu ya Simba imekwisha ondoka nchini kwenda Zambia tayari kwa kuvaana na timu ya Nkada Red Devil,mchezo utakaofanyika Jumamosi hii nchini humo.