Make your own free website on Tripod.com

MICHUANO YA KUMTAFUTA MBABE WA MATAIFA

Cameroon kuendeleza historia?

Renatus Mgongo na Bernard Ndelema

SIKU tano kabla ya kindumbwendumbwe cha kumtafuta mbabe wa soka katika Mataifa ya Afrika, joto la michuano hiyo limeanza kupanda miongoni wa mashabiki wa soka jijini Dar Es Salaam.

Uchunguzi uliofanywa na KIONGOZI katika viwanja mbalimbali vya michezo jijini Dar Es Salaam, umebaini kuwa hivi sasa gumzo kuu kwa wapenzi wa michezo ni juu ya nani atamtwaa mwanamwali hapo Februari 10,mchezo utakaofanyika nchini Mali.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika kila mashabiki wa soka watano, wanne wanampa nafasi kubwa bingwa mtetezi Cameroon " Simba wa nyika" kutwaa kombe hilo; lakini waliionya timu hiyo kutozibeza timu chipukizi na zinazoitisha katika medani ya soka Afrika ,kama Senegal, Togo na Liberia.

"Naamini Cameroon bado ni timu imara kuweza kutetea ubingwa wake. Hata hivyo nina wasi wasi mkubwa na ‘vitimu’ kama Senegal na Togo ambavyo vinacheza soka la kujituma, la kisasa na lakuvutia", alisema Lucas Magoha mkazi wa Mburahati.

Hata hivyo mahasimu wakuu wa Cameroon, Nigeria, wamekuwa wakisemwa semwa sana na baadhi ya mashabiki kuwa wanaweza kuchukua Kombe hilo, ingawaje wengi wameonesha wasiwasi kuhusiana na tabia ya wachezaji wa timu hiyo kucheza kwa mzaha na kutokuwa wazalendo.

"Nawapenda sana ‘Super Eagles’ ila wananikatisha tamaaa kutokana na tabia yao ya kuringaringa na kutokuwa ‘serious’ wawapo dimbani", alisema Abdallah Mweri mkazi wa Sinza ambaye pia ni Waziri wa michezo na burudani katika serikali ya Wanafunzi wa Chuo Cha Uandishi wa habari Dar es salaam (DSJ).

Naye Thomas Mongi Mkazi wa Kariakoo alionya tabia yoyote ya kuwadharau Wanigeria akisema, jamaa hao bado nimwiba na wanaweza kuichoma timu yoyote.

Pia uchunguzi huo umeonyesha kuwa wapenzi wengi wa soka wanategemea kupata burudani safi na ya kuvutia ikizingatiwa, soka la nchi nyingi barani Afrika limepanda.

Michuano hiyo ya 23 kwa Mataifa ya Afrika inatarajiwa kutimua vumbi Jumamosi ijayo Januari 19; huku wenyeji Mali "Les Aiglons (Eagles)" wakikata utepe kwa kupambana na Liberia "lone Stars" katika uwanja wa Berema Bacoum mjini Mopti. Mabingwa watetezi Camerooun "Simba wa nyika" chini ya kocha wao Mjerumani Winfried Schafer watutupa karata yao ya kwanza jumapili Januari 20, wakikwaruzana na J K ya Kongo "Simba wa Kabila".

Jumla ya Mataifa 16 yatashiriki michuano hiyo inayoanza Januari 19 na kumalizika Februari 10 nchini Mali.Timu hizo zimegawanywa katika makundi manne (A,B,C na D) ambapo kila kundi lina timu nne.

Kundi A linatimu za Mali "Les Aiglons (Eagles)", Liberia "lone Stars", Algeria "Wapiganaji wa jangwani" na Nigeria " The Super Eagles".

Wakati kundi B linazipambanisha timu za Afrika Kusini " Vijana wa kazi", Burkina fasso "Mafarasi dume", Morroco "Simba wa Atlas" na Ghana "Black Stars".

Kundi C linawakutanisha Cameroon "Simba wa nyika" , J K ya Kongo "Simba wa Kabila", Ivory Cost "Tembo" na Togo "Mwewe".

Nalo kundi D linatimu za Misri "Mafarao", Zambia "Chipolopolo", Tunisia na Senegal.

Simba kuingia kambini Januari 14

l Ligi Daraja latu Kindoni mbioni

Na Tom Chilala

MABINGWA wa soka Tanzania Simba Sport Club ya Dar es Salaam, Januari 14 mwaka huu wanatarajia kuingia kambini kujinoa kikamilifu kwa ajili ya michuano ya Kimataifa na Ligi Kuu msimu huu.

Akizungumza na KIONGOZI hivi kariubu ,Katibu Mkuu watimu hiyo,Kassim Dewji alisema kuwa timu hiyo itaingia kambini katika hoteli ya Ndege Beach ikiwa imekamilika na safu yake kali ya ushambuliaji iliyokuwa ikimendewa na mahasimu wao Yanga.

Dewji amesema wanatarajia kikosi cha wachezaji 25 ndicho kitakachoingia kambini baada ya kukamilisha kuwapunguza baadhi ya wachezaji kama Chama Cha Soka nchini (FAT), kilivyoagiza katika usajili wa timu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Michuano ya Ligi Kuu Bara imepangwa kuanza mwezi Machi mwaka huu ambapo usajili wa wachezaji watakaoshiriki ligi hiyo umepangwa kumalizika Januari 20.

Wakati huo huo:Fainali ya ligi ya soka ya Daraja la Tatu wilayani Kinondoni Dar es salaam inatarajiwa kuanza Januari 15 kwa kashiriksiha timu 16 kwenye viwanja vitatu tofauti.

Akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni Katibu Msaidizi wa chama cha soka wilayni humo (KIFA) Frank Mchaki amesema kuwa fainali hiyo itachezwa kwenye viwanja vya shule ya Msingi Mwananyamala B, Mwalimu Nyerere na CCM Msasani. Hata hivyo alisema kuwa ratiba ya mechi hizo itajulikana mara baada ya kupatikana washindi wawili katika ligi ya mtoano ya timu za upendeleo itayaomalizika Januari 11.

Nayo timu ya Mpira wa Kikapu ya Combine toka jijini Dar es Salaam, inatarajia kuingia kambini Januari 15 mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya majiji ya Africa Mashariki itakayofanyika wiki ijayo.

Katibu Mkuu wa chama cha Mpira wa Kikapu Dar es Salaam (DARBA) Mbamba Uswege amesema wachezaji wote waliomo katika vikosi vya timu za wanawake na wanaume wanatakiwa kuripoti kambini.

Uswege amesema kuwa mazoezi ya kujiandaa na michuano hiyo yatakuwa yakifanyika katika uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar-es Salaam.

Uchaguzi CHANETA kufanyika Morogoro Mei

Na Maryam Salumu

UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) unatarajia kufanyika mkoani Morogoro Mei mwaka huu.

Kaimu Katibu Mkuu wa CHANETA Josephine Mutahiwa alisema katika mazungumzo na gazeti hili hivi karibuni kuwa uchaguzi huo ni badala ya uliotakiwa kufanyika mwaka jana lakini ukakwama kutokana na ukosefu wa fedha.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es salaam Kaimu Katibu Mkuu huyo wa CHANETA alisema tatizo la kutokuwa na fedha ulichangiwa pia na baadhi ya mikoa kutolipa ada zao.

Aliitaja baadhi ya mikoa ambayo haijalipa ada kuwa ni pamoja na Tabora, Shinyanga, Lindi, Dodoma, Kigoma, Kagera, Ruvuma Mara na Kilimanjaro.

Mutahiwa alivitaka vyama ambavyo havijasajiliwa kulipa ada ya shilingi 20,000 mapema. Alisema chama ambacho hakijasajiliwa hakitashiriki michezo ya mwezi Mei. Kaimu Katimu Mkuu huyo alisema kuwa CHANETA ina mpango wa kuunda timu za vijana wenye umri wa chini ya miaka 21.

Alisema vijana hao ambao wengi wao wanatarajiwa kuwa wanafunzi wa shule za msingi watakuwa wanafanya mazoezi kila Jumamosi.

Aliongeza kuwa CHANETA wanampngo wa kuhamasisha vijana wa kiume kushiriki klabu bingwa ya mkoa hapo mwakani kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya.

Alivihimiza vyombo vya habari kuhamasisha mchezo huu ili ufanikiwe zaidi.

Michuano ya Ligi Daraja la Tatu Ilala kuendelea wiki ijayo

Na Ester Masangula

MICHUANO ya Ligi Daraja la Tatu wilayani Ilala katika hatua ya Nane Bora,itaendela wiki ijayo,imefahamika.

Taarifa kutoka kwa uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu wilayani humo (IDFA),zinasema kuwa kimesema ligi daraja la tatu inaendelea wiki ijayo katika hatua ya kumi na nane bora.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katikati ya juma katika ofisi za Chama cha Mpira wa Miguu wilayani humo (IDFA) ,Afisa Mtendaji wa chama hicho ,Daudi Kanuti alisema timu hizo kumi na nane zimegawanyika katika makundi matatu na kila kundi linatoa timu mbili.

Katika timu hizo timu sita zitawakilisha wilaya hiyo katika ligi ya Kanda ya Dar es Salaam.

Alizitaja timu zilizopo kundi A kuwa ni Jiji Star, Black Pool, Kibasila, Wachache (Ndanda Manyema), Gold Lion wakati Kundi B zitakuwa ni Mungu, Kariakoo United, Mogo, Eleven fighter, Yetu Afrika na timu ya sita itatangazwa hapo baadaye.

Kwamujibu wa Katibu huyo Mtendaji kundi la tatu litakuwa Pascho, Black People, Livertorn, Mzambarauni, Ashant na Dar newala.

Afisa mtendaji huyo amesema lengo la michezo hiyo ni kukuza kipaji cha michezo kwa vijana.

Wape nafasi viongozi wapya FAT wafanye kazi-Mudhihir

Na Anthony Ngonyani .

NAIBU Waziri wa Kazi Maendeleo ya Vijana na Michezo, Mudhihir Mudhihir amewataka wanamichezo nchini kuwapa nafasi viongozi wapya wa chama cha soka Tanzania (FAT) ili waweze kufanya kazi yao ipasavyo.

Uongozi huo ulichaguliwa Desemba 31 mwaka jana mjini Arusha uliomba upewe muda ili uwezekufanya kazi zake vizuri.

Akizungumza na KIONGOZI hivi karibuni Mudhihir alisema kuwa anaamini kuwa viongozi hao watapata muda zaidi wa kufanya kazi zao.

Alisema wakipata nafasi hiyo, ni hakika Tanzania itakuwa na sura ya pekee katika medani ya soka ya kimataifa.

Alisema viongozi waliochaguliwa wameonyesha nia yao ya kulibadilisha soka la Tanzania na kufikia kiwango cha juu hali ambayo haitafikiwa kama wataendesha chama hicho kwa kusakamwa na migongano ya hapa na pale.

Alisema kuwa amefarijika sana kukutana na viongozi hao na kufanya nao mkutano kwani ni mara yake ya kwanza na vile vile ni mara ya kwanza kwa viongozi wa FAT kufanya mkutano na Wizara.

Bado nipo ya Yanga-Maadhi

Na Mwandishi Wetu

KIUNGO wa kutumainiwa wa klabu ya Yanga Waziri Mahadhi ambaye alikuwa anadaiwa kufuatwa na timu ya Simba amesema tayari ameisha saini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea timu yake ya awali ya Yanga.

Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam,Mahadhi alisema kuwa pamoja na Simba kumfuata lakini ataendelea kuichezea timu yake ya Yanga kwa kipindi kingine cha miaka miwili.

Wiki ilyopita uongozi wa simba ulikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari ukidai kuwa utajibu mapigo ya Yanga kwa kutaka kumsajili mshambuliaji wao hatari Joseph Kaniki kwa kumsajili kiungo huyo.

Mahadhi alisema simba wamemfuata nyumbani kwake kwa ajili ya kutaka kumsainisha fomu zao lakini alilazimika kuwaeleza ukweli kuwa tayari ameisha saini mkataba wa kuichezea timu yake ya Yanga kwa kipindi kingine cha miaka miwili .

Alisema kuwa hawezi kufanya makosa kama wanavyofanya wachezaji wengine kusajiajili timu mbili na matokeo yakeBado nipo ya Yanga-Maadhi wanaishia kufungiwa.

Mahadhi alisisitiza kuwa anaomba aeleweke kuwa ni mchezaji halari wa timu ya Yanga na si vinginevyo.