Wimbo wa 'mgumba' wawatoa machozi wapenzi wa African Revolution

Na Anthony ngonyani

WAPENZI wa bendi ya African Revolution ,TamTam, Jumanne iliyopita walishindwa kuyamudu machozi yao kufuatia wimbo mpya wa bendi hiyo unaozungumzia mateso anayoyapata mwanamke ambaye hajazaa mtoto yaani, mgumba.

Tukio hilo katika ukumbi wa Mango Garden wakati bendi hiyo ilipokuwa ikitumbuiza katika sherehe za mwaka mpya.

Katika wimbo huo Muumini Mwinyijuma anambembeleza kwa hisia nzito mwimbaji wa kike wa bendi hiyo Amina Ngaruma anayelalamika kuwa mumewe anamtesa na hatimaye kumfukuza kwa kukosa uzazi.

Kuolewa ni sheria lakini kuzaa ni majaliwa usilie Amina ni baadhi ya maneno yaliyopo katika wimbo huo mpya ambao unagusa mioyo ya watu wengi .

KIONGOZI lilishuhudia watu mbalimbali waliokuwepo ukumbini hapo wakiwemo akinamama ,wakijifuta machozi kutokana na kuguswa na mashairi yaliyomo ndani ya wimbo huo utunzi wake Muumini.

Hata hivyo baadhi ya wapenzi wa bendi hiyo walisema wimbo huo unahitajika kufanyiwa marekebisho kabla haujarekodiwa ambapo unastahili kuitwa kilio cha mwanamke tasa badala ya mgumba.

"Mgumba ni mwanaume lakini mwanamke huitwa tasa , wimbo huo ni mzuri lakini naomba urekebishwe hapo ili ulete maana halisi" alisema Mwanahamisi Halfani ambaye ni mmoja wa mashabiki wa TamTam.

TAFCA yaunda kamati ya kuratibu Uchaguzi Mkuu

Na Getrude Madembwe

CHAMA cha makocha wa Soka Tanzania (TAFCA) kimeunda kamati ya watu watano kwa kwaajili ya kuratibu shughuli za uchaguzi wake mkuu utakao fanyika mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa juma,Katibu Mkuu wa chama hicho Idd Machupa alisema kuwa wajume wa kamati hiyo wanatarajiwa kuwa na kikao cha kwanza kwenye ofisi za chama hicho zilizopo Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam hapo Januari 13 mwaka huu.

Aliwataja wajumbe hao kuwa ni Erenesti Mokake ambaye ameteuliwa kuwa mwenyekiti na Sunday Kayuni ambaye ameteuliwa kuwa katibu wake.

Wengine ni Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA),Mwina Kaduguda ,Jogn Charles pamoja na yeye Mwenyewe.

Machupa alisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa ufanyike kabla ya uchaguzi wa FAT,lakini ilishindikana kutokana na ukosefu wa fedha ambazo kiutaratibu hutolewa na FAT yenyewe.

Alisema kutokana na kuchewa kufanya uchaguzi huo, chama chake kilishindwa kushiriki uchaguzi Mkuu wa FAT uliofanyika Desemba 31 mwaka jana mkoani Arusha kutokana na ratiba ya FAT.

LIGI DARAJA LA TATU KINONDONI

Timu nne zashuka daraja

Na Benjamin Mwakibinga

LIGI ya soka ya Daraja la Tatu wilayani Kinondoni imemaliza hatua yake ya awali huku ikiziacha timu nne zikiteremka daraja baada ya kushika nafasi za chini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na KIFA timu hizo zilizo telemka daraja ni Day Black FC, Mfano FC, Kichangani FC pamoja na timu ya Rungwe FC.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa timu hizo zitacheza ligi daraja la nne katika msimu ujao wa ligi katika wilaya hiyo.

Timu za Sinza Express, Kagera Rangers Sifa united pamoja na ile ya jeshi la 94 KJ ndizo zilizofanikiwa kuendelea na ligi hiyo kwa hatua itakayofuata.

Timu hizo zitaungana na timu za Care Boys FC, Huduma FC, Polisi Ostabay Kawe Rangers, Maskani FC, Mwenge Shooting Stars, Tambaza FC, Kambangwa FC,Ukwamani FC pamoja na timu nyingine ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ya Chui FC.

Aidha taarifa hiyo imesema kuwa timu hizo zilitakiwa ziwe zimeanza kucheza hatua ya pili mwanzoni mwa Januari lakini kutokana na ugumu uliopo katika upangaji wa Ratiba ya michezo hiyo.Lidi hiyo inatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Simba yasema haiko tayari kugombea wachezaji

Na Mwandishi Wetu

KLABU Simba imesema kuwa haiko tayari kumgombea mchezaji yoyote atakaye sajiliwa na timu hiyo na baadaye kujisajili timu nyingine,ili itakacho kifanya ni kumfisha kwenye vyombo vya dola mchezaji huyo.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa klabu hiyo,Azim Dewji katika mazungumzo na gazeti hili jijini Dar es Salaam.

Alisema kwa mjibu wa sheria za usajili ,mchezaji lazima aichezee klabu yake kwa misimu miwili.

Hivi sasa Mshambulia machachari wa timu hiyo, Joseph Kaniki amejisajili katika timu mbili ikiwemo Simba yenyewe na mpinzani wake Yanga.

Hata hivyo imekuwa ni kitu cha kawaida kwa Simba na Yanga kugombea wachezaji kila kinapofika kipindi cha usajili.

Mwaka juizi mahasimu hao waliingia kwenye vita ya kuwagombea Ephrahimu Makoye na Steven Mapunda.