‘Kutegemea pesa kwa maendeleo ya michezo ni ndoto’

Na Mwandishi Wetu

Mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa FAT, Luteni Kanali Idd Kipingu, amesema ni ndoto kutegemea pesa kuleta maendeleo ya michezo badala ya uongozi bora.

Kipingu aliyasema hayo mwishoni mwa juma wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema mnapokuwa na fedha nyingi lakini mkakosa uongozi bora, ni ndoto kufikia maendeleo na malengo yenu.

"Hata kama mna fedha nyingi, halafu hakuna uongozi bora, basi itakuwa ni ndoto kupata maendeleo ya michezo", alisema.

Alisema wakati huu ni muafaka kwa kuufanya mfumo wa michezo nchini hasa soka kuwa wa ajira.

"Soka sasa ni kazi, hivyo inabidi ilenge katika suala la ajira, kwani vijana hodari na wenye vipaji tunao hivyo wanahitaji uongozi bora wa kuiendeleza kwa manufaa," alisema.

Kipingu ambaye aliamua kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti badala ya Mwenyekiti kama ilivyotarajiwa na wapenzi wengi wa michezo, alisema alipenda mwenyewe na si kwa kumuogopa Muhidini Ndolanga.

"Sio kwamba nilimuogopa Ndolanga, bali niliona kupitia hapa, ninaweza kutoa mchango mkubwa kama nitapita niko tayari kushirikiana na Mwenyekiti atakayeshinda," alisema.

Kipingu ambaye pia ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Makongo ya jijini Dar es Salaam, aliwahimiza watakaofanikiwa kushinda katika uchaguzi huo, kuongeza vita ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI.

FRAT sasa kupata viongozi wapya

Na Peter Dominic

CHAMA cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT), Jumamosi hii kinafanya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mjini Arusha.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam, zinasema katika Uchaguzi huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), wagombea 33 wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali na wanafanyiwa usaili asubuhi ya Jumamosi hii.

Katibu Msaidizi wa FRAT, Leslie Liunda, alisema maandalizi yote yamekamilika.

Ijumaa usiku Kamati ya Utendaji inayomaliza muda wake ilitarajiwa kuwa na kikao. hakuna habari zaidi zilizopatikana juu ya kikao hicho.

Habari zinasema Mwenyekiti wa kamati ya Mwafaka ya FAT, Muhidin Ndolanga, anatarajiwa kufungua mkutano huo Mkuu wa FRAT ambao utafuatiwa na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi.

Kwa mujibu wa habari hizo, nafasi ya Mwenyekiti inao wagombea watatu ambao ni Dk. Kassim Mchatta Dk. Mohammed Kirumo na Methord Buberwa.

Mchatta ndiye Katibu Mkuu wa sasa wakati Kirumo anamaliza muda wake kama Makamu Mwenyekiti Mwenyekiti wa sasa Kassim Malele Chona, hawanii uongozi huo.

wanaogombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Kirumo Ally Lilanga, Abdallah Malipula, Alfred Lwiza, Lawrence Lubigili na Abdallah Mitole.

Nafasi ya Katibu Mkuu inawaniwa na Joseph Pembe na David Lugenge, wakati wanaowania nafasi ya Katibu Msaidizi ni Khalid Ruvu Kiwanga na Liunda. Nafasi ya Mweka Hazina inawaniwa na mgombea mmoja ambaye ni Joseph Magazi wakati ile ya Msaidizi wake inawaniwa na Kiwanga Massoro Mango na Paul Opiyo.

Gwaza Mapunda anawania kutetea nafasi yake ya mkutano mkuu wa FAT akichuana na Mwamuzi wa Kimataifa wa Tanzania Omar Abdulkadiri na Twalib Ngwenya.

Wanaowania nafasi saba za ujumbe ni Magazi Muna Kisuda, Hassan Kitumbuzi,Opiyo Meja Isara Chacha, Rajabu Kubiga, Adbulrahman Wengi, Hamis Msonga na Ahmed Wise.

Wengine ni Abdallah Kiyungi, Elizabeth Kalinga, Idelphonce Magali, King Rwechungura, Joseph Mapunda, Malipula na Charles Manyama.

Msiwashirikishe watoto katika sherehe za usiku

Na Maryam Salumu

JAMII imeshauriwa kutowashirikisha watoto katika sherehe za usiku kwa kuwa hali hiyo ni hatari na inaweza kuwaathiri vibaya kimwili na kiroho.

Msimamizi wa Idara ya Maendeleo na Watoto wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Buguruni katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bi. Matrida Mbwambo, aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam.

Aliyasema hayo kufuatia kuwepo kwa Kwaya ya Watoto wa Shule ya Jumapili kanisani hapo ambayo mara kadhaa hualikwa na waamini katika sherehe mbalimbali.

"Hivi sasa tuna kwaya nzuri ya watoto wetu ambayo imekuwa ikialikwa katika sherehe mbalimbali. Kwa hiyo, ninawaomba Wakristo kutowashirikisha watoto hawa katika sherehe za usiku," alisema.

Alisema inapotokea umuhimu wa pekee kuwashirikisha watoto hao katika sherehe, wazazi na waamini kwa jumla wajitahidi kuwarudisha kabla ya saa 12:00 jioni.

Alisema hali hiyo itawafanya wasiathirike kimaadili, kiafya na kisaikoljia. Hata hivyo, Bi. Mbwambo amewataka wazazi kujenga utamaduni wa kuwafanya watoto wao kurudi nyumbani mapema.

Alisema mzazi mwenye kuwajibika vema katika familia yake, hapaswi kusita kumhoji mwanaye anapochelewa kurudi nyumbani kwa kuwa hali hiyo ina hatari kimwili na kiroho.

Wakati huo huo: Bi. Mbwambo amekemea tabia ya baadhi ya waamini kuendelea kuvaa mavazi yasiyostahili ndani ya nyumba za ibada.

Alisema, inashangaza kuona kuwa uvumilivu umekosekana miongoni mwa jamii kiasi cha kuwafanya baadhi ya waamini kuacha kuvaa nguo zinazokiuka maadili ya jamii ambazo huvaliwa mitaani na wahuni.

"Inasikitisha kuona kuwa watu wamekosa hata uvumilivu katika mioyo yao kiasi kwamba wanashindwa kuacha nguo wanazovaa huko mitaani na sasa wanazivaa hata ndani ya nyumba ya Mungu bila kujali kuwa miili ya wanadamu ni mahekalu ya Mungu," alisema.