Uhamiaji yamtaka Sirengo aondoke haraka nchini

Na Lilian Timbuka

IDARA ya Uhamiaji nchini imemtaka mshambuliaji wa Kimataifa Mark Sirengo kuondoka nchini mara moja kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hana kibali cha kufanyia kazi nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katikati ya juma, Afisa Uhusiano wa Uhamiaji, Ally Kileo alisema kuwa Sirengo aliyesajiliwa na Klabu ya Simba kwa ajili ya mechi za Kimataifa na Ligi Kuu msimu huu kutoka timu ya Mumias Sugar nchni Kenya,hadi sasa anaishi nchini kinyume cha sheria.

Kileo alisema kuwa licha ya uongozi wa Simba kupeleka fomu za kuomba kibali cha mchezaji huyo,fomu hizo hazikupokelewa kutoka na sababu kwamba baadhi ya vipengele vilikosewa.

"Tuliwaambia kuwa fomu hizo zijazwe upya halafu wazirudishe huko" alisema Afisa Uhusiano huyo.

Kileo alifafanua kuwa fomu za Sirengo zilipelekwa ofisi za uhamiaji na mtu aliyejitambulia kwa jina Josiah Jackson, lakini siku zilporudishwa alizifuata Abushir Kilungo, ambaye alipewa maelekezo ya nini cha kufanya kuhusiana na fomu hizo.

Alisema marekebisho yanayotakiwa ni kuhusu mkataba wake na Simba na kuna barua pamoja na kupeleka barua kutoka Chama cha Soka Tanzania (FAT)inayomtambua mchezaji huyo.

Uhamisho wa Sirengo kutoka Klabu yake ya Mumias Sugar ya Kenya kuja Simba ya Tanzania ulikuwa na mvutano uliosababisha mchezaji huyo kushindwa kucheza michuano ya Kimataifa kwa kile kilichodaiwa kuchelewa kupelekwa kwa kibali chake kwa shirikisho la soka la Afrika (CAF).

BMT yavitaka vyama vya michezo kuwasilisha kanuni zamashindano

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limevitaka vyama vya michezo nchini kuwasilisha kanuni za mashindano mbalimbali yanayoendeshwa na Vyama hivyo.

Kauli hiyo imetolewa katikati ya juma na Afisa Michezo Mwandamizi wa BMT, Mohamed Kiganja wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili kwenye ofisi zake zilizopo jijini Dar es Salaam.

Alisema ni vyama vichache vilivyo wasilisha kanuni hizo kikiwemo Chama cha Netiboli nchini (CHANETA) na Chama cha Mpira wa Kikapu .

Alisema BMT imeamua kuomba kanuni za mashindano mbalimbali ili kutoa ushauri kadri michuano hiyo itakavyokuwa ikiendelea lengo likiwa ni kuepusha migogoro ambayo imekuwa ikitokea mara kwa mara.

Aliongeza BMT imegundua kuwa migogoro mingi inyotokea katika mashindano mbalimbali,inatokana na kupuuzwa kwa kanuni za kuendesha mashindano huku kukiwa na upungufu katika kusimamia kanuni hizo.

"Wakileta kanuni za mashindano yao itakuwa rahisi kusuluhisha migogoro ambayo imekuwa ikitokea katika mashindano mbalimbali", alisema Kiganja.

Alisema kanuni hizo zinatakiwa kuwasilishwa kabla ya mwezi ujao ili zijadiliwe katika kikao cha BMT kitakachofanyika mwanzoni mwa Aprili.

Kikao hicho kitajadili pia kalenda za vyama zilizopelekwa BMT licha ya kwamba Cchama cha Soka nchini (FAT) hadi mwanzoni mwa wiki hii kilikuwa hakijapeleka kalenda yake.

"Vyama vingine vimeleta kalenda tu lakini FAT, tunashangaa wameshindwa kuleta hata kalenda na wamekuwa wakikiuka taratibu kila mwaka", alisema Kiganja.

Kwa mujibu wa Kiganja baada ya kikao hicho cha mwezi April mwaka huu, kutakuwa na kikao cha makatibu wakuu wa vyama vya michezo hiyo.

Kwaya za Wabaptist, Wamoravian zaunda umoja kuchangiana pesa

Na Mwandishi Wetu

WAIMBAJI wa Paradiso Baptist Choir ya kanisa la Kurasini Baptist Church, Dar es Salaam, wametumia Kanisa la Moravian Tanzania, Ushirika wa Keko, kujikusanyia pesa kwa ajili ya safari ya Arusha.

Jumapili iliyopita Wanakwaya wa Paradiso walilitembelea Kanisa la Moravian Ushirika wa Keko na kushiriki Ibada zote mbili wakiimba pamoja na Kwaya ya Vijana ya Moravian Keko kwa lengo la kuchangisha pesa.

Njia nyingine waliyotumia wanakwaya hao wa Kurasini Baptist Church, ni kuchezesha "Wimbo Niupendao" ambapo jumla ya shilingi 67, 450/= zilipatikana ushirikani hapo.

Wakizungumza kwa pamoja na gazeti hili, katika ushirika huo, Mwenyekiti wa Kwaya ya Paradiso, Bw. Fred Lameck na Katibu wa Kwaya, Bw. Jacob Makyasa, walisema kuwa lengo la safari hiyo kwenda Arusha ni kufanya uinjilishaji kwa njia ya nyimbo na na nyumba kwa nyumba.

Walisema katika safari hiyo ya Machi 30, mwaka huu, waimbaji hao 26 watafikia katika Kanisa la Baptist Ngarenalo, Arusha ambapo kila jioni watafanya semina kwa watu mbalimbali hadi Aprili 2, watakaporudi jijini Dar es Salaam.

Lameck alisema shilingi 500,000/=zilihitajika kwa safari nzima, lakini hadi siku hiyo, walikuwa na zaidi ya nusu ya kiasi hicho.

Alipoulizwa sababu za kuchagua Ushirika wa Keko pekee kwa ajili ya mchango huo, Lameck alisema, "Hawa ni ndugu zetu wa karibu na mara nyingi tumekuwa tukitembeleana na kushirikiana kwa mahitaji mbalimbali."

Naye Naibu Katibu wa Kwaya ya Vijana ya Ushirika wa Keko wa Kanisa la Moravian, Bw. Otto Tenge, alisema shilingi 67,000/= zilizopatikana hazikuwaridhisha wenyeji hao kwani walitarajia kuwachangia Wabaptisti kiasi kikubwa zaidi ya hicho.

Hata hivyo, alisema hali hiyo imetokana na sababu mbalimbali ambazo zilikuwa nje ya uwezo wa Wamoravian. Waimbaji wa Paradiso Baptist Choir wanaoshiriki safari hiyo ni Mhazini wa Kwaya, Olita Hezron na Msaidizi wake Aneth Mwaipola.

Wengine ni Mwenyekiti wa Uinjilisti, Bahati Mwakambonja; Katibu wa Unjilisti, Joram Mwakansope; Mwenyekiti wa Nidhamu, Asukile Mwakyusa, Mwenyekiti wa Miradi, Ester Kapangala na Mjumbe wa Miradi, Emi Luoga.

Wengine ni Happyness Gaudensi, Pancrasia Thomas, Serafina Hamis, Glori Aswile na Angela Ngogo.

Waimbaji wengine ni Anna Hassan, Neema Mwaitulo, Mariam Vitalis, Debora Masika, Teddy Kapangala na Agnes Mwamloso.

Wengine ni Sadoki Wilson, Robert Kapangala, Machimu Abasi, Simon Mwakubali na Dickson Ndumile.

Ni Ndoto soka la Tanzania kukua-FAT

lKufungwa kwa uwanja wa Taifa ni uzembe wa jeshi la polisi

lYasema uzembe wa polisi umesababishwa kufungwa kwa uwanja wa Taifa

Na Anthony Ngonyani.

IMEELEZWA kuwa ni ndoto kwa soka la Tanzania kukua kutokana kile kilichodaiwa kuwa waamuzi wengi hawana elimu ya kutosha ya kuweza kuchezesha mechi kwa muda wa dakika 90.

Kauli hiyo iletolewa juma lililopita jijini Dar-es-salaam na Mjumbe wa kudumu wa chama cha Soka nchini (FAT) Said AL-Maamry wakati akizungumza na gazeti hili.

Alisema kuwa kutokana na waamuzi hao kukosa elimu yakutosha ,Tanzania itaendelea kushindwa kufanya vizuri katika michezo ya Kimataifa.

Alisema waamuzi licha ya kwambawanajua fika kwamba timu zimekuwa zikitumia muda mwingi kwa ajili ya kujiandaa na michezo hiyo ya Kimataifa,lakini wamekuwa wakichzeesha vibaya bila kujali hilo.

Said aliongeza kusema kuwa ili kuepukana na tatizo hilo, ni bora FAT na Chama cha Waamuzi Nchini (FRAT) viwasomeshe waaamuzi hao ili kuinua viwango vyao vya kuchezesha mechi.

Alisema bila kufanya hivyo Tanzania itaendelea kuwa wasindikizaji katika mchezo huo wa soka licha ya kupendwa na wananchi wengi.

Kuhusu kufungiwa uwanja wa taifa Mjumbe huyo wa FAT alisema kazi ya ulinzi nchini inafanywa na Jeshi la Polisi hivyo uzembe wa polisi ndio waliosababisha mpaka uwanja huo umefungiwa na Chama cha Soka Afrika (CAF).

Alisema polisi wanapokwenda uwanjani wao pia huwa watanzamaji badala ya kufanya kazi kubwa iliyowapeleka hapo ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wa wachezaji na watazamaji na mali zao.