Make your own free website on Tripod.com

Darasa la Saba wamemaliza; sasa kifuate ni nini ?

JUMATANO iliyopita wanafunzi takribani nusu milioni wa shule za msingi nchini, walifanya mitihani yao ya mwisho.

Hii ilikuwa kipimo cha mwisho cha nini kilichopandwa na kila mmoja katika shamba lake baada ya safari ya miaka saba ya elimu ya msingi.

Tunapenda kutumia nafasi hii kuwapongeza kwa kuvumilia na hatimaye kuikamilisha safari hiyo ndefu iliyowapitisha katika milima na mabonde mbalimbali.

Tunasema tunawapongeza kwani ni ujasiri mkubwa waliotumia kukamilisha safari hiyo licha ya vikwazo mbalimbali ambavyo kwa namna moja ama nyingine, wamekumbana navyo.

Bado tunasema tunawapongeza kwa kuwa ni wazi kuwa takribani asilimia 28 ya wanafunzi wenzao, hawakumaliza safari hiyo.

Wengine walilazimika kukatiza masomo yao kwa uzembe wa makusudi, wengine kwa kukatishwa tamaa na jambo hili ama lile na wengine, kwa shinikizo la jamii wanamoishi ikiwa ni pamoja na wazazi kuwanyima mahitaji ya shule na kuozwa kabla ya kukamilisha masomo yao.

Ni wazi kuwa wengine hawakuhitimu masomo yao kutokana na kupata ujauzito na hata matatizo mengine ya kifya.

Sisi tunawapongeza wazazi na Taifa kwa jumla ambao walikubali kubeba na kutimiza jukumu  sahihi la kuhakikisha kuwa vijana hao wanapata haki yao ya elimu, na malezi ya msingi kwa maisha yao.

Tunajua wazazi na walezi wamejinyima mengi na wengine walilala njaa huku wengine wakitembea hata nusu uchi ili mradi tu, wahakikishe watoto wao wanapata hazina hiyo ya elimu ambayo ni msingi na ufunguo bora katika maisha.

Serikali ilijua hilo na ndiyo maana pia ilijitahidi kutoa kipaumbele katika kupambana na maadui wale wakubwa wa Taifa ambao ni umaskini, ujinga na maradhi.

Katika kuimarisha vita dhidi ya ujinga hasa katika ngazi ya elimu ya msingi, ikaondoa vikwazo vyote vya michango kwa shule hizo na kuboresha mazingiza ya wanafunzi kujifunza vema.

Hii ilikuwa pamoja na kuongeza idadi ya walimu katika shule na kuchochea ongezeko la vyumba vya madarasa ili kutoa uwiano bora wa mwalimu na wanafunzi katika darasa.

Pamoja na pongezi hizo, bado tunawakumbusha wazazi, Taifa na jamii kwa jumla, usemi kuwa : Kulea mimba si kazi, kazi ni kulea mwana na pia, Kumvua numbi si kazi, kazi ni magawioni.

Tunasema hivyo kwa kuwa sasa vijana hao wametoka katika ulimwengu wa shule ya msingi, wameingia katika ulimwengu mpya ambao shetani anataka agawane na jamii adilifu ya kimungu ili nae apate fungu lake.

Hiki ni kipindi hatari sana kwa watoto wetu hasa ambao hawatapata bahati ya kujiunga na masomo ya sekondari.

Ni kipindi chenye vishawishi vingi vya hatari. Ni kipindi ambacho shetani anawaalika na kuwavuta vijana kumfuata kwa kujitumbukiza katika vitendo vya uhuni, ukiwamo ufuska, uvutaji bangi na ulevi wa ama pombe, au dawa za kulevya.

Ni kipindi ambacho vijana wanapenda kupata maisha mazuri bila kujua wala kufuata hatua muhimu za kuyafikia.

Pia, ni kipindi ambacho sasa, vijana wengi wanakuwa katika hatari ya kujifunza kuuza mayai, karanga na sigara mitaani na vilabuni ; ni kipindi ambacho shetani anawapa semina vijana juu ya kuwa majambazi na matapeli huku akiwaalika wengine kuwa vibaka na wachomozi wanaojificha katika  upigaji debe kwa kisingizio cha ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira.

Ni kipindi cha vijana hawa kuanza safari kuiendeleza 'Nchi ya ahadi' yaani miji yetu mikuu kama  Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na kwingineko. Wanaiendelea wakiwa wamejaa matumaini ya kupata ajira ya kiutu, na kuwa na maisha mazuri, na katika hali ya mshituko wanajikuta wakijiunga na jeshi la 'Machinga' wanaolazimika kusaga lami na kupokea makali ya jua lote siku nzima bila kula ili kuuza (tooth picks) njiti za kusafishia meno pale wale wanaokula wanapokuwa wameshiba.

Sisi tunasema, hiki ni kipindi  kigumu, lakini muhimu sana kwa wazazi, walezi, marafiki, asasi za kibinafsi na za Kiserikali, kuonesha upendo na kuwajali vijana hawa kwa kuwafanya kuwa raia wema na watumishi bora wa Mungu.

Hatuna maana kuwa sasa jamii ielekeze nguvu zake katika kuwapa chakula na pesa bure, la hasha ! Tunachosema, sasa vijana hawa waelekezwe kilicho bora kufanya ili kujipatia riziki halali.

Wahimizwe kushiriki kikamilifu katika vikundi na asasi za kidini ili kupata mafundisho mbalimbali yanayowajenga kiroho.

Wajengewe moyo wa kupenda kujiunga na kushiriki katika vikundi vya uzalishaji mali ili wajitegemee kwa manufaa ya familia zao, Kanisa, Taifa na hata kwa wao wenyewe.

Wazazi na jamii hawana budi kujua kuwa huu ndio wakati muafaka wa kuwajengea vijana hao maisha bora ya siku za usoni, au kuwabomolea.

Kila mzazi ajue kuwa uzembe wowote utakaofanywa na mzazi katika kipindi hiki, utakuwa ndio bei ya mauti ya mwanae na kilio kwa Taifa na hasa wakati huu ambao ulimwengu umegubikwa na janga la UKIMWI na uhalifu wa kila namna.

Tukumbuke usemi kuwa mtoto hakui kwa mzazi na kwamba, mchelea mwana kulia, hulia yeye. Hivyo, wazazi hawana mwanya wowote wa kukwepa majukumu ya kuwalea kimaadili vijana wao waliohitimu masomo na hata vijana hao waliohitimu, pia ni nafasi yao kujua kuwa wazazi, Taifa linategemea mchango wao wa hali na mali katika kulijenga.

Wajue pia kuwa macho ya jamii yote yanawatazama kwa matumaini.

Kila mmoja ajionee aibu kuwa tunda lenye sumu katika jamii na badala yake, awe tunda tamu lenye harufu na ladha tamu ya matumaini inayovutia jamii, Taifa, Kanisa na kikubwa zaidi, kwa Mungu.

Umaskini ni nini? Na maskini ni nani?

Ndugu Mhariri,

 

BILA shaka Watanzania walio wengi wanalifahamu sana, licha ya kuliishi neno hili “umasikini”.

Pengine wengi wamewahi kuitwa “maskini” na hata kutukanwa kwa maneno kama “mjinga wewe maskini tu.” Na mara nyingine watu huonesha masikitiko yao kwa tukio fulani baya ambalo limempata mwenzao wakisema, “maskini wa Mungu... !”.

Wanasiasa nao hasa katika majukwaa yao ya kunadi sera na propaganda za vyama vyao, husikika mara nyingi wakizungumza juu ya neno hilo umaskini hasa katika nchi zinazoendelea.

Wakristo nao katika ibada mbalimbali kama Ibada ya Misa Takatifu, husoma Maandiko Matakatifu ya Yesu Kristo akizungumuzia masuala mbalimbali juu ya “umaskini na maskini”

Nilijikuta katika tafakari inayoibua maswali mengi mno juu ya maana  na matumizi sahihi ya maneno hayo.

Hivyo, lengo la makala haya siyo tu kuelimisha jamii bali pia  kutafuta majibu kutoka kwa wasomaji na waandishi juu ya maswali umaskini ni nini? Na maskini ni nani?

Tafakari juu ya maswali hayo ilinirudisha nyuma mwaka mmoja tokea sasa. ninakumbuka nilipokuwa mkoani Kagera nikifanya utafiti juu ya chanzo na madhara ya uharibifu wa mazingira mkoani humo’. Matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa umasikini ni chanzo  kimojawapo kati ya vyanzo vingine vingi vya uhalibifu wa mazingira. Ilinibidi kutembelea wilaya na vijiji mbalimbali ili nijionee uhalisi wa mambo.

Nikiwa katika kijiji  cha Ruanda kilichopo tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, nilibahatika kuzungumza na baadhi ya wanakijiji juu ya maana ya umaskini.

Wao waliufafanua umaskini kwamba ni hali ya chini kimaisha ambapo mtu anakuwa hana uwezo wa kuwa na nyumba iliyoezekwa kwa bati, hana uwezo wa kumiliki baiskeli aina ya Phonex, hana kuku angalau watatu, hana shamba la migomba, hana uwezo wa kupata angalau mikungu mitatu ya ndizi kutoka kwenye shamba lake kwa wakati mmoja na pia, mtu huyo hawezi kumudu kula ndizi kila mlo.

Maelezo ya wanakijiji hao yalinifurahisha sana kwani yalinipa changamoto ya kuanza kujitathimini ili nifahamu niko upande upi kati ya walio maskini na wasio kuwa maskini.

Mwisho, nikajikuta ninaangukia kwenye kundi la wale watu ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za kula ndizi kwa kila mlo, pili hawana kuku hata mmoja na tatu hawana nyumba ya bati hivyo basi mimi ni maskini.

Baada ya tathimini hiyo fupi niliingiwa na hofu kubwa kwa kutoamini maelezo yao kwani yalipingana kabisa na fikra nilizokuwa nazo awali juu ya maana ya umaskini na maskini ni nani.

Ili kuhakikisha ukweli wa maelezo hayo, niliamua kutembelea Wilaya ya Karagwe. Wilaya hii ipo mpakani kabisa mwa Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Uganda.

Nikiwa kule, nilibahatika kukutana na jamii ya wafugaji ambao wana mifugo yao ndani na kandokando ya Msitu wa Kimisi.

Wafugaji hao walieleza kuwa umasikini  ni hali fulani ya taabu na dhiki na wakafafanua kwamba, maskini ni yule mtu ambaye hana uwezo wa kumiliki anglau ng’ombe mia tatu, na hawezi kukamua ebyanzi  (chombo rasmi mfano wa chupa ya chai kinachotumiwa kukamlia maziwa) hamsini kwa wakati mmoja.

Nilipo muuliza mmoja kati yao swali kuhusu uwezo wa kuwa na nyumba ya bati na uwezo pia wa kula ndizi kwa kila mlo, alinishangaa na kunidharau kwani aliniambia kuwa nyumba za bati hupiga kelele sana wakati wa mvua na hasa wakati wa usiku ambapo huwa ni wakati wa kupumzika na kulala pono.

“Mvua zikinyesha huwezi kustahimili makelele ya bati unalazimika kuamka,” alieleza.

Kuhusu uwezo wa kumudu gharama za kula ndizi kwa kila mlo, alinidharau pia, akasema ndizi ni chakula cha watoto ambacho mtu maskini asiye na maziwa, nyama na mihogo hushindia.

Sasa nikazidi kuchanganyikiwa zaidi kwani maelezo yao yalitofautiana kabisa na kugongana na yangu na hata kushindwa kuoanisha maelezo ya wilaya ya kwanza na hii niliyopo sasa.

Nilipoivinjali maktaba ya Mkoa huo wa Kagera, kamusi na maandishi ya waandishi mbalimbali yalitafsiri umasikini kama hali ya ufukara, udhaifu, unyonge, uhoehae, hali ya kuwa na dhiki, upungufu, ukosefu na uhitaji.

Nao wataalam wa uchumi na maendeleo wao wanasema kwamba umasikini ni hali ile ambapo mtu anakuwa hana uwezo wa kupata mahitaji yake ya msingi kama malazi, chakula na mavazi.

Tafakari yangu juu  ya “umasikini ni nini?” “Na masikini ni nani?” haishii tu katika kusimulia yaliyotokea wakati nilipokuwa ninafanya utafiti  mwaka mmoja uliopita, bali hata leo hii ambapo mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa inafanyika ili kutafuta mbinu na mikakati ya pamoja ya kuuondoa umasikini duniani.

Ukienda kanisani utasikia maneno haya yaani umaskini na maskini, yakitamkwa ama katika Injili au katika mahubiri.

Ebu tujiulize tena “umasikini ni nini?” “Na masikini ni nani?”

Wakati mikakati na mbinu ya kuondoa umaskini inaendelea Yesu Kristo katika Maandiko Matakatifu kupitia waandishi Luka, Mathayo, Marko na Yohana, anaonekana kuipenda na kuifurahia hali ya umasikini akionesha sababu kwamba hali ya umasikini itamfanya binadamu kuufikia na kuupata ufalme wa mbinguni.

Mfano katika Injili ya Luka, inaeleza “Heri ninyi mlio maskini kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu”. (Lk 6: 20).

Katika Injili hiyo hiyo ya Luka tunaelezwa habari za Lazaro, mtu aliye kuwa maskini, alivyoupata ufalme wa Mungu (Lk 16:19-31)

Maneno hayo ya Yesu Kristo yananitia raha na matumaini katika roho yangu.

Wengi wetu tunaitwa maskini na nchi yetu imetengwa kwenye kundi la nchi zilizo maskini.

‘Heri ninyi mlio maskini kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.”Huenda Watanzania wakafarijika sana na matamshi haya.

Lakini; kwa maana hiyo mikakati na mbinu za kuondoa umaskini  kwa mtazamo huu huenda ukatuingiza mahala pengine na sio kwenye njia ya kutuelekeza katika ufalme wa Mungu?

Na je, tuufurahie na kuuenzi umaskini kwa sababu Yesu Kristo ameubariki? Au tufanye kila tuwezalo ili tuondoe huu umasikini wetu wakati huo tukijua kabisa kwamba kufanya hivyo kutapelekea sisi kuikosa nafasi  ya kuingia katika ufalme Mungu? Maana imeandikwa heri maskini?

Je, kuna sababu ya kuhangaika na mambo ya mbinguni wakati ya hapa duniani yanatushinda?

Hivi ni kweli kwamba umaskini aliouongelewa Yesu Kristo hauna tofauti na unaongelewa sasa? Je, matajiri wao hawana nafasi ya kuingia katika ufalme wa Mungu?

 Pamoja na maelezo na fafanuzi zote hizo, bado ninauliza na nina hamu ya kujua “umaskini ni nini?” “Na maskini ni nani?”

Ninakaribisha maoni au majibu kupitia Gazeti hili

 

Edward Mujungi,

S.L.P. 2133,

DAR ES SALAAM.