Ahadi ya Brigedia Kirigiti isiwe 'danganya toto'

TUNAZIPONGEZA juhudi kubwa zinazofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) za kuhakikisha amani iliyopo nchini inadumu.

Hivi leo katika Ulimwengu uliojaa vita, bado Tanzania inaonekana ni miongoni mwa nchi chache zenye upendo, amani na umoja.

Kazi hii siyo ya mchezo, ni ngumu inayohitaji moyo wa pekee na bila kuwa na jeshi imara, bila shaka hata Tanzania ingekuwa  miongoni mwa nchi ambazo umwagaji damu kwao ni jambo la kawaida.

Pamoja na pongezi hizo, Jeshi hilo sasa linaonekana kuingiliwa na mdudu mbaya na hatua za haraka zisipochukuliwa, sifa zote hizo zitatoweka.

Tunasema hivyo kwani baadhi ya wanajeshi wa Jeshi  la Kujenga Taifa, kwa bahati mbaya sasa wamekuwa wakitumia jina la Jeshi lao kuwanyanyasa wananchi na jamii kwa jumla.

Tukio la hivi karibuni lililotokea jijini Dar es Salaam, ambapo wanajeshi  wa JKT wapatao 12 walilizingira eneo la Kariakoo na kuanza kuwashambulia Askari wa Jiji kwa madai kuwa askari hao wa Jiji walikuwa wamevaa sare zinazofanana na zao, ni la kushangaza.

Katika purukushani hizo, Wanajeshi hao  mbali na kuwachalaza bakora Askari wa Jiji, pia walimvua nguo mmoja wa askari wa Jiji na kumuacha na nguo yake ya ndani.

Swali tunalojiuliza ni kwamba, hivi kweli uongozi wa JKT ulishindwa nini kufanya mazungumzo na uongozi wa Jiji na kufikia muafaka juu ya sare ipi itumike baina ya pande zote mbili, badala ya askari hao kufanya mashambulizi ya aibu kiasi kile?

Wanajeshi hao walifahamu fika kuwa wanachokifanya ni kinyume cha sheria za nchi na ndiyo sababu waliamua kuharibu kamera ya mpiga picha wa kujitegemea ambaye alikuwa akifuatilia tukio hilo ili aujulishe umma.

Bila shaka waliona picha hizo zikionekana kwenye vyombo vya habari, jamii itajenga hisia mbaya dhidi ya JKT.

Kibaya zaidi wafanyabiashara wa eneo hilo la Kariakoo baada ya kushuhudia askari anavuliwa nguo, ilibidi waingilie kati. Wakachukua madaraka na sheria mikononi na kuungana na askari wa Jiji kuwashambulia wanajeshi hao.

Sisi tunasema, tabia hii iliyoanzishwa na askari hao wa JKT, ni hatari  na iliyo na harufu ya damu.

Ikumbukwe pia kuwa, askari wa Jiji ndio wanaohusika na suala zima la kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi ikiwa ni pamoja na kuhahikisha kuwa wafanyabiashara hao wanafanya shughuli zao katika maeneo waliyotengewa kufanyia biashara zao.

Kufuatia kitendo cha wafanyabiashara hao  kuungana na askari katika kupambana na wanajeshi, upo uwezekano mkubwa wa shughuli za kusimamia zoezi la usafi kukwama kwani tayari askari wa Jiji na wafanyabiashara  wameisha jenga ‘undugu’ hasa ikizingatiwa kuwa   akufaaye kwa dhiki, ndiye nduguyo.

Kuna usemi kwamba "Usipo ziba ufa, utajenga ukuta". Hivyo, ni vema uongozi unaohusika uchukue hatua za haraka kuwaadhibu Wanajeshi walihusika na tukio hilo la kusikitisha ili jamii iendelee kuwa na imani ambayo sasa, imeanza kufifia  dhidi ya jeshi lao lililo na dhamana ya usalama wao.

Pamoja na kauli nzuri iliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Ulinzi  na Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Jenerali Philimon Kirigiti kwa vyombo vya habari kuwa Wizara yake itawashughulia wahusika kwa kulizalilisha Jeshi la Kujenga Taifa, ni matumaini yetu kwamba kauli hiyo haitakuwa  ‘danganya toto’.

Watanzania tumezoea kuambiwa na viongozi wetu kupitia vyombo vya habari kwamba watachukuwa hatua kwa watu ama vikundi vinavyo kwenda kinyume na sheria za nchi, lakini baada ya kutolewa tamko, hatua ama maendeleo ya adhabu hizo huwa hayatangazwi tena.

Hii ni sawa na watoto wanapo pigana na ikatokea mmoja akaenda kushtaki mwenzake kwa mzazi ama mlezi wake, halafu eti katika kumridhisha mtoto aliyeshitaki, basi mzazi huyo anamwambia mtoto mlalamikaji "Mwangu ndiyo kakupiga! Basi nyamaza akija nitampiga".

Sasa, mtoto kwa kuridhisha na kauli hiyo, mtoto huyo huondoka kwa furaha iliyojaa matumaini ya kutendewa haki.

Yetu sisi siyo matumaini ya ahadi tupu, tunategemea Brigedia Generali Kirigiti hapendi hao vijana wake wachache waharibu sifa nzuri ya JKT nzima.

Tafadhali, mapema, mapema, mchuzi huu unywewe; kabla haujachacha.

Kwaheri Baba Mwanyika, Karibu Baba Maluma

 

1.        Mpendwa Baba Mwanyika, tamko ulilitoa,

           Kustaafu kazini, umri umeshatimia,

           Hata sisi tunaona, muda umeshawadia,

           Kwaheri Baba Mwanyika, karibu Baba Maluma.

 

2.        Kustaafu sio tamati, bado tunakuhitaji,

           Njombe tunakushukuru, kazi ulofanya fiti,

           Hatuna cha kukulipa, Mungu atakubariki,

           Kwaheri Baba Mwanyika, karibu Baba Maluma.

 

3.        Kazi uliyoifanya, ilikuwa ni kabambe,

           Neno ulilihubiri, hapa Kanisani Njombe

           Mkate ulitulisha, na divai mu kikombe

           Kwaheri Baba Mwanyika, karibu baba Maluma.

 

4.        Mwanyika kafanya mengi, yasoweza lesabika,

           Kanisa kuliongoza, miongo mitatu sasa,

           Kanisa ulilijenga, tusipate taabika

           Kwaheri baba Mwanyika, karibu baba Maluma.

 

5.        Ulienda kotekote hata kusikofikika,

           Jimbo lote twakujua, kwa jina lako Mwanyika,

           Matembere wanakujua, Ikonda wewe Mwanyika

           Kwaheri baba Mwanyika, karibu baba Maluma.

 

6.        Milimani ulienda, mabondeni ukashuka,

           Wa sunji na wa Mundindi, uwemba hadi kisinga,

           Kipengere Lugarawa, Igwachanya na Usuka,

           Kwaheri baba Mwanyika, karibu baba Maluma.

 

7.        Mara ulipotangaza kustaafu hiyo kazi,

           Mungu akatupa macho kwa wake watenda kazi,

           Akamuona Maluma, anafiti hiyo kazi

           Kwaheri baba Mwanyika, karibu baba Maluma.

 

8.        Ndipo kamtuma Papa, atangaze hadharani,

           Naye hakulaza damu, akatoa redioni,

           Jina tukalisikia twamshukuru Manani,

           Karibu baba Maluma, kwaheri baba Mwanyika

 

9.        Atafuta nyayo zako, sisi tunamuamini,

           Elimu anayotosha, tena yeye ni makini,

           Mkufunzi si mdogo wa pale seminarini,

           Karibu baba Maluma, kwaheri baba Mwanyika.

 

10.     Papa ameona mbali, hata akamteua,

           Hata mimi namjua ndo mana nakupa shua,

           Maluma anatufaa, shetani kumbutua,

           Karibu baba Maluma, kwaheri baba Mwanyika.

 

11.     Maluma Karibu sana, Dayosisi yetu Njombe,

           Utufundishe kusali Mungu wetu tumwombe,

           Utufundishe ibada, sio kucheza likembe

           Karibu baba  Maluma, kwa heri baba Mwanyika.

 

12.     Wino umemalizika, kalamu naweka chini,

           Nami sasa nakitoa, nenda zangu kanisani,

           Mhariri nashukuru, kuniweka gazetini

           Karibu baba Maluma, kwa heri baba Mwanyika

 

 

 

 

 

Na Sir, Ephraim J. Sanga (Baba Filo)

Silver Tailoring centre

P.O. Box 206

NJOMBE

 

Maisha  ya kiroho na Kondomu haviendani

 

1.             Tafuteni mtapata, ombeni mtapewa,

                Popote mkiniita, kwangu mtafunguliwa,

                Njia mtakayopita, sana mtasumbuliwa,

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

2.             Kuna mambo mengi bora, hapa nchini duniani,

                Na mengine yaso bora, naomba tuyaacheni,

                Akili ni kitu bora, kuliko mali jamani

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

3.             Tusisome kwa papara, tena kwa kurukaruka,

                Tulia tafuta sara, Mungu peke katanka,

                Utii ni kitubora, kuliko mali jamani.

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

4.             Musa toka mlimani, Alitufanyia kazi,

                Na kweli ndugu zanguni, ya nne twasoma wazi

                Kwa maisha ya mbinguni tuwaheshimu wazazi

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

5.             Tuwaheshimu wazazi kwa maisha ya mbinguni

                Tukawatii wazazi kwa dhati na kwa makini,

                Wao ni yetu mizizi kwa chakula cha mbinguni

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

6.             Wametuzaa wazazi, nakutupa tunzo bora,

                Juu chini ya wazazi, Twapata kipaimara,

                Ni kwa haki bila wizi, leo waumini bora,

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

7.             Matunda yao wazazi, Tayaona kwa wanao,

                Mifano huweka wazi, Watoto wafate  yao,

                Katika kundi la mbuzi, mwanawe awe kondoo

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

8.             Mungu wetu tumwamini, Neno lake hekaluni

                Asema tumwabuduni, na chochote hafanani

                Asema usizini hata kama ni moyoni

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

9.             Tungo yangu akisoma, inamisha kichwa chini

                Kwa busara na hekima, utafakari moyoni,

                Kwa kutumia salama twampongeza shetani

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

10.          Tamaa tuziacheni,  jamani tafadhalini,

                Mndoa wako nyumbani, ni mzuri kama nini

                Ukiranda mitaani, utaingia wimbini

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

11.          Eti maparokiani tuzitangaze salama,

                Hatuna haya usoni, kukaribisha kiyama

                Kwa dhati tukiamini kwa Yesu yote salama

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

12.          Wala sioni msala, kukuonyesha pengine,

                Fungua chuo cha sala, kurasa sabini na nane,

                Pale tumepewa sal, ni namba kumi na nane

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

13.          Wapendwa ndugu zanguni, tuangalie nyakati

                Uwapo majaribuni, Mwombe Mungu uthabiti

                Utamshinda shetani, ukikemea kwa dhati

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

14.          Hebu ndugu fikiria, Mchele umepembua,

                Mawe yote umetoa, na chuya umeondoa,

                Mwingine anatokea, mchanga anamwagia

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

15.          Watu wote Tanzania, Janga hili twalijua,

                Mikakati twaandaa, kwa sala kuliondoa

                Hatujalimalizia, Kondomu zinaingia

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

16.          Kwa dhati mnatambua, kila mtu ana dini,

                Kama Mungu twamjua, kondom sisi zanini?

                Naomba kuwaambia, zisitawanywe nchini

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

17.          Hebu kwanza fikiria, uzinzi pia ni dhambi

                Kondomu wazitumia, umeisahau dhambi,

                Eti umepata njia yakukwepa hili wimbi

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

18.          Ilitakiwa kwa Mungu si baa, aweza kuliondoa,

                Ndugu yangu na jamaa, ujumbe wangu pokea,

                Yeye tukimlilia kweli atatusikia

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

19.          Mvua isipotua, Sala tunakimbilia,

                Na kweli hutusikia wanawe kutuokoa,

                Jamani na hili baa hawezi kutukataa,

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

20.          Usiku huu wa manane nimerishiwa mawazo,

                Rudia beti ya nane, tena kwa msisitizo

                Hekaluni tuonane, kuzianza sala hizo

                Kama kweli muumini leo kondom zanini?

 

 

Na Simon A. Nsekella,

C/O Ally Kissiwa,

S.L.P

IRINGA