Daladala kutosimamisha abiria sawa, lakini...

MWISHONI mwa juma, Jeshi la Polisi, mkoani Dar es Salaam, lilitangaza uamuzi wake wa kupiga marufuku gari za abiria kusimamisha abiria.

Hatua hii ya Polisi, ilikuja baada ya Jeshi hilo kubaini kuwa, miongoni mwa sababu kuu zinazochangia ongezeko la ajali za barabarani, zinazoua watu wengi na kuwaacha wengine wakiwa na ulemavu, ni ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na wafanya biashara hao wa usafirishaji, kujaza abiria kuliko uwezo wa gari.

Sisi tunalipongeza Jeshi hilo nchini kwa kuwa makini juu ya suala la usalama wa raia. Hii, inatoa picha halisi kuwa kweli Jeshi la Polisi, ni Jeshi linaloshughulikia usalama wa raia na mali zao.

Tunafarijika zaidi kutokana na agizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Bw. Alfred Tibaigana, kuwaagiza askari wake kuzikamata daladala zote zitakazozidisha abiria, pamoja na gari ndogo na kubwa za mizigo zitakazobeba abiria nyuma.

Ni wazi kuwa amri hiyo, ina lengo zuri, na ni nia njema kabisa ya Jeshi hilo kupunguza idadi ya vifo na majeruhi pindi ajali zinapotokea.

Amri hiyo iliyoanza kutekelezwa Alhamisi, inawahusisha pia, polisi wa kawaida katika kusaidia kukamata magari yanayokiuka sheria za usalama barabarani, ikiwa ni pamoja na kubeba abiria wengi kupita idadi ya viti vilivyopo ndani ya daladala.

Kinachotutia moyo zaidi, ni ujasiri wa Jeshi hilo, kusisitiza kuwa sasa, gari litakalokamatwa na kufikishwa polisi, halitatozwa faini na kuruhusiwa kuondoka kama ilivyokuwa awali, bali litaendelea kushikiliwa na polisi katika kipindi chote cha kesi mahakamani.

Tunasema hiyo inatutia moyo kwani kabla ya agizo hilo, wengi wa wanajamii walifikia hatua wakaamini kuwa faini inayotolewa kwa wakiukaji wa sheria za usalama barabarani, hailengi kweli kupunguza ajali, bali inalenga kutunisha mfuko, au ni mradi wa kitengo fulani ndani ya polisi. Hayo ndiyo yalikuwa mawazo ya baadhi ya watu.

Walisema hivyo kwa kuwa, hali hiyo pia ilikuwa inatoa mwanya mkubwa na kishawishi cha kutosha kwa askari kudai na kupokea rushwa, hususan barabarani.

Katika kusimamia hilo bila mzaha, Polisi mkoani humo imewatahadharisha wananchi kutopanda magari yaliyojaza abiria, vinginevyo watateremshwa bila kujali kama wamelipa nauli, au la; na hakutakuwa na sharti lolote likiwamo la kurudishiwa nauli.

Kama tulivyotangulia kusema, tunaipongeza hatua hiyo ya Jesh la Polisi mkoani Dar es Salaa kwa kujali maisha ya watu.

Ni kwa mantiki hiyo, tunatoa wito kwa jamii kuunga mkono juhudi za Jeshi hilo katika kuimarisha usalama wa raia hususan katika sekta ya usafirishaji jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, licha ya pongezi hizo, bado tuna mashaka juu ya utekelezaji wa agizo hilo, kama utakuwa na manufaa kwa jamii, au utakuwa kero zaidi.

Pia, bado vichwa vinatugonga kwani tunajiuliza kuwa ndiyo, ni hatua nzuri katika kuimarisha usalama wa wananchi, lakini je, wazo au agizo hilo limekuja wakati muafaka na jamii imejiandaa kwa hilo?

Tunasema hivyo huku tukijiuliza kuwa, kama kabla ya agizo hilo, bado wafanyakazi na wanafunzi walikuwa wakichelewa kazini na shule na hata wakati wa kurudi nyumbani, kutokana na abiria kuwa wengi kuliko daladala, je sasa hali itakuwaje kama sasa hatasimama abiria hata mmoja?

Kinachozidi kugonga vichwa vyetu ni kutaka kujua, Serikali na Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam, wamechukua hatua gani kuona kwamba gari zinapatikana kwa kiasi cha kutosha ili kukidhi mahitaji ya jamii na kuepusha mwanya wa abiria kulazimika kusimama ndani ya daladala japo hawafurahii hali hiyo? Polisi jijini Dar es Salaam wanajua kabisa kuwa daladala haziruhusiwi kukatiza safari, Je, wanaoishi maeneo ya katikati  ya safari hizo, watasafiri?

Bado tuna wasiwasi kuwa wafanya biashara kama walivyo, hiyo haitakuwa nafasi yao nzuri kupandisha nauli ovyo ovyo na kuwanyanyasa wanafunzi?

Sisi tunasema, ingawa hatua hiyo ni nzuri na ina nia njema, lakini, Jeshi la Polisi lina kazi kubwa kuhakikisha utekelezaji wake hauleti madhara mengine kwa jamii, yakiwamo madhara ya kiuchumi.

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

KIONGOZI sasa mnaturidhisha

Ndugu Mhariri,

 

NAOMBA Unipe nafasi katika Gazeti lako la KIONGOZI ili nilitumie hilohilo kutoa yaliyonishinda kuzuia moyoni mwangu.

 Kwa siku za hivi karibuni, inaonekana mmefanya mabadiliko makubwa katika Gazeti hili la Wananchi.

 Ninasema hivyo kwa sababu sasa ninaona mnatuwekea vitu ambavyo hata mtu anapolinunua, anaona pesa yake imekwenda kihalali kwa kuwa hata makala mnazoandika sasa ni zile zinazoeleza mada kwa undani, zilizochunguzwa na kufanyiwa utafiti na pia, zinajenga kiroho.

 Mfano mzuri ni makala juu ya namba katika Biblia, wengi tulikuwa hatujui zina maana gani, pia, ujumbe anaoutoa Baba Askofu Kilaini( Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam) yenye kichwa cha habari; Uamsho ni Ulokole katika Ukatoliki?

 Ninapenda kuwambia kuwa, kwa muda mfupi tu, mlioamua kufanya mabadiliko hayo ya namna ya kuandika makala zenu, tayari sasa mtu anajisikia hasara kubwa asiposoma KIONGOZI kwa sababu sasa watu hawataki kukosa makala mnazoandika.

Ushahidi mzuri ni kwamba siku hizi mtu asipowahi kununua Gazeti hilo, akachelewa kidogo, atakuta yamekwisha na yapo haya mengine ambayo mnashindana nayo.

Hongera kwa kazi nzuri mnayoifanya na muongeze bidii.

Mungu awazidishie nguvu na moyo wa kazi, mshirikiane ili kuriboresha zaidi.

                                            Keraryo Christopher,

MABATINI

Mwanza.

Pongezi Watanzania Kazi mmeimaliza

1.             Mhariri shikamoo, nakuamkia kwanza,

                Shairi niloandika, nalileta hapa kwanza,

                Lipokee kwa mikono, ukalichapisha kwanza,

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

2.             Kazi mmeimaliza, kama mlivyoianza,

                Walo bara na mlima, wote ninawapongeza,

                Hamkufanya ajizi, katu Sensa kupuuza,

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

3.             Watanzania hakika, kielimu ni wa kwanza,

                Kujibu dodosa zote, kama walivyotangaza,

                Maswali mloulizwa, yote yote mmeweza,

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

4.             Nawasifu kwa kutii, yote waliyoagiza,

                Wa Iringa na wa Pwani, Pemba sitowabakiza,

                Ruvuma na Zanzibari, pokeeni sifa kwanza,

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

5.             Tanga hamna utani, sensa mlitanguliza,

                Mbeya kule kwa watani, sensa hawakuibeza

                Ikiwa Dar walitii, nani angelikataza ?

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

6.             Kilimanjaro Shinyanga, Lindi hadi kule Mwanza,

                One two, three kuhesabiwa, siyo kesi si baraza,

                Morogoro na Singida, walifanya hilo kwanza,

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

7.             Tabora asante sana, Rukwa ninawapongeza,

                Mara Mtwara Kigoma, majina mlicharaza,

                Kagera hadi Manyara, sensa hamkufukuza,

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

8.             Arusha nako Dodoma, kwenu ndiko tulianza,

                Kisha Tanzania nzima, madodoso yakaanza,

                Twahitaji pongezana, kazi tumeimaliza

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

9.             Beti tisa nastop, sina nilichokisaza,

                Naenda kuchinja mbuzi, niwape zawadi kwanza,

                Watanzania ni top kumbe mambo mnaweza

                Pongezi Watanzania, kazi mmeimaliza.

 

 

Sr. Ephraim J. Sanga (Babu Filo)

S.L.P 206

NJOMBE

TAFAKARI YA WIKI

"Wakati watu kwa maelfu mengi walikuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, "Jihadharini na chachu ya Wafarisayo, yaani unafiki. Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila siri itajulikana. Kwa hiyo, kila mlichosema gizani, watu watakisikia katika mwanga, kila mlichonong'ona faraghani, milango imefungwa, kitatangazwa juu ya nyumba."                                                                      (Luka 12: 1-3)