Kamati ya Amani KKKT ilete amani

KWA takribani miaka sita, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limekuwa katika mgogoro, ambao siri, imewahuzunisha Wakristo wengi na Watanzania kwa jumla.

Asili ya mgogoro huu, ni baadhi ya waamini wa KKKT kutaka iundwe Dayosisi Mpya ya Mwanga, ambayo kwa mujibu wao, ilitakiwa kujimega toka kwenye Dayosisi ya Pare. Sisi hatujui ni kwani , lakini tunaamini wanasababu zao ama njema, au la!

Suala la mgogoro juu ya kuanzishwa kwa Dayosisi Mpya ya Mwanga, liliwahi kuchukua sura mpya hasa baada ya kuwahusisha baadhi ya watu waliowahi kushika nyadhifa nzito Serikali na pia, lilichukua sura nyingine mpya baada ya Chama Tawala mkoani Kilimanjaro kuingilia kati ili kupata suluhisho la amani.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani humo kwa wakati huo, Peter David, aliiomba KKKT kutumia busara zaidi katika kushughulikia mgogoro huo, badala ya ubabe, udanganyifu au unafiki wowote ili kurejesha amani na utulivu vilivyoanza kutishia kutoweka miongoni mwa jamii hiyo ya Mwanga.

Alisema, inawezekana kabisa mgogoro huo ukasuluhishwa na kupata muafaka wa kudumu ndani ya KKKT.

Sisi tunasema, hii ni kweli kwani mwenye nia njema anapokutana na mwenye nia njema, lazima jambo jema na la heri litapatikana.

Hivi karibuni,  uongozi wa juu wa Kanisa hilo akiwamo Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Samson Mushemba,  waliomba kusaidiwa kupata suluhisho la mgogoro huo kupitia Chama Tawala cha CCM.

Hatuna nia wala sababu ya kusema ni nani mkosefu, lakini tunahimiza na kuomba Mungu azidi kuwaongoza waamini wa ngazi zote wa KKKT, ili watumie hekima na busara zao kuchangia mawazo yatakayoleta mafanikio zaidi katika kufikia muafaka.

Tunasema hivi maana hivi karibuni kumekuwapo na tuhuma mbalimbali toka kwa viongozi wa juu wa KKKT kuwa, baadhi ya waamini wanahusika na kuwa chanzo au chachu ya mgogoro huo.

Sisi tunasema, chachu yoyote ya mgogoro katika jamii ni hatari kiroho na kimwili.

Waamini wa Mwanga wanaotuhumiwa kuwa chanzo kikubwa cha mgogoro huo kwa madai eti ndio wanaodai kuanzishwa kwa Dayosisi ya Mwanga nje ya utaratibu wa KKKT, waliwahi kutangazwa kutengwa na Kanisa hilo.

Uamuzi wa KKKT kutangaza kuwatenga wanaounga mkono kuanzishwa kwa Dayosisi ya Mwanga, ulikwenda sambamba na kutolewa tamko rasmi la kuvunjwa kwa iliyokuwa Kamati ya Usuluhishi, hapo Julai 18, mwaka huu, katika Mkutano Mkuu uliofanyika Morogoro.

Hata hivyo, bado jamii ya Watanzania inazidi kufarijika ikiamini kuwa suluhisho na amani ya kudumu, itapatikana ndani ya KKKT kwani Wakristo na Watanzania wote wenye mapenzi mema, wanawaombea heri.

Matumaini haya yanakuja hasa baada ya kuundwa kwa KAMATI YA AMANI MWANGA, yenye wajumbe 13 toka makundi yote mawili; linalounga mkono kuanzishwa kwa Dayosisi ya Mwanga, na lile linalopinga kunanzishwa kwa Dayosisi hiyo.

Sisi tunasema tunaiombea heri Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Elinaza Sendoro, Askofu Mstaafu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, ili izae matunda yaliyokomaa, yakaiva na sasa ni matamu; matunda ya upendo, uelewano na umoja.

Wakati sisi na Watanzania wengine tukiwaombea hilo, ni vema wana KKKT wakajua kuwa ndio wenye uwezo wa kuileta amani hiyo hivyo, wote tuiombee KAMATI YA AMANI YA MWANGA, ILETE AMANI.

Je, kujipamba Kanisani ni kosa?

Ndugu Mhariri,

 

Kwa kuyasoma Maandiko kwa kadiri Wakristo (au viongozi) fulani wanavyoyaelewa na kuyachukulia katika makanisa yao, kwa kipindi cha miaka mingi zilizuka hoja zilizoanzisha misimamo tofauti kati ya jamii ya Wakristo na hivyo, kuigawa jamii hiyo katika makundi kadhaa yenye mitazamo, misimamo, itikadi, na mafundisho yanayotofautiana au hata kupingana juu ya suala hilo.

Tatizo hili limewaathiri Wakristo wengi wazuri kabisa inapotokea Mkristo kuhamia Kanisa lililo na mafundisho tofauti na alivyofundishwa kuhusiana na suala hilo. Suala hili kwa sehemu kubwa lina waathiri wanawake Wakristo kuliko Wakristo wanaume.

Katika ukweli ulio wazi kwa kila mtu, wanawake ndio wenye msukumo mkubwa wa kujipamba unao tokana na asili yao ya uumbwaji waliopewa na Mungu katika hisia za maumbile yao maalum yanayoweza kuchukuliwa kama kipawa..

Wapo wanawake wengi wa rika mbalimbali, wanaoshindwa ama kuacha wokovu muda mfupi tu baada ya kuokoka, kwa sababu aidha walitazamwa na wanawake wenzao waliotangulia kuokoka, kwa kubezwa au kubaguliwa kisirisiri au hata kwa kusengenywa pembeni, au kusemwa hadharani katika mtindo wa kuaibishwa au kudhalilishwa hadharani eti kwa sababu walionekana wakiwa wamejipamba.

Inaweza kuwa tendo hili lilitendeka kanisani na kiongozi fulani alikuwa madhabahuni akihubiri au kufundisha na kwa kukazia ujumbe wake, akaamua kumtolea mfano, Mkristo fulani aliyeonekana kuwa tofauti na msimamo na mtazamo wa kiongozi huyo.

Nimewahi kuliona tendo hili kwa macho yangu mimi mwenyewe likitendeka katika Kanisa fulani jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya mara moja, nikiacha matukio mengine ya jinsi hiyo hiyo yaliyotendeka hapo mimi bila kuwepo hapo kanisani na kuwaathiri vibaya sana baadhi ya akinamama wasiopungua wanne.

Taarifa za jinsi hii zimesikika karibia kila sehemu ya Tanzania na idadi ya wanawake Wakristo wanaoathirika imezidi kuongezeka sana.

Ni kwa sababu  ya vilio vya akinamama wa jinsi hii nimeonelea vyema kuiamsha jamii ya Wakristo hususan, Wakristo wa Tanzania, tulizungumzie kwa kina kinachostahili kupitia mwanga wa Maandiko Matakatifu na ninatoa wito kwa viongozi wa makanisa ya Kiroho, waliosomea Biblia katika viwango mbalimbali vya elimu kutoa mchango wao kuhusu fundisho sahihi kama kujipamba ni dhambi au siyo dhambi au Mkristo binafsi anaweza kuamua kwa kufuata dhamiri ya moyo wake mwenyewe juu ya jambo hilo ?

Kabla sijatoa mchango wangu juu ya hoja hii, ningependa kutoa ushauri kwanza kwa Wakristo au viongozi wa makanisa hasa wale ambao wanakosa subira au hekima katika kufuata kanuni sahihi ya kuwasaidia Wakristo au wanawake wale wanaoonekana kwenda kinyume na utaratubu wa Kanisa “lao hilo” katika suala la kujipamba au hata vinginevyo kuwa  wasiwakosoe kwa kuwafedhehesha mbele ya wenzao. Huu sio utaratibu wa Kikristo wa kumsahihisha  Mkristo mwenzako.

NI vizuri kwa kiongozi wa Kanisa kujua kuwa mtu aliyekwisha kutubu na tukaamini kwamba Mungu amemsamehe kabisa dhambi zake zote, tendo hilo la “toba na kusamehewa” na Mungu, ni muujiza mkubwa kabisa wenye nguvu inayoendelea kumbadirisha mtu huyo tukijua kwamba tatizo lake lililokuwa kubwa na la hatari Bwana ameliondoa. Na yaliyosalia kwa nje ni madogo mno, ikiwa ni pamoja na hilo la kujipamba.

Kinachotakiwa sana ni kumtia moyo Mkristo huyo na kumfundisha Neno la Mungu kwa upole na upendo bila kumkatisha tamaa kana kwamba hatua aliyokwishafikia bado haina maana eti kwa kuwa kasuka nywele saluni au kusuka “rasta”.

Roho ya mtu ikishakombolewa hayo mengine hupukutika yenyewe moja baada ya jingine bila hata haja ya kumshurutisha. Kanisa zima limuoneshe upendo wa dhati na hata ajione kuwa anathaminiwa, baada ya muda yeye mwenyewe ataona kuwa hakuna mwanamke mwingine anayejitengeneza kwa jinsi yake, hivyo inawezekana ile hali ya kujiona tofauti peke yake katika Kanisa  zima, itaunda ushawishi moyoni mwake na kuhiyari kujirekebisha. Kikubwa ni “ basi sasa inadumu Imani, tumaini, upendo…na katika hayo lililo kuu ni UPENDO.” (1kor.13:13).

Upendo unapokutawala, unatuendesha katika mpango wa Mungu tunapotafuta kumsaidia mwenzetu: “ndugu zangu,mtu akighafilika katika kosa lolote, ninyi mlio wa Roho mrejesheni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe “ (Gal 6:1)

Na baada ya hayo machache , ninaingia katika mada yenyewe ya swali letu - “MAPAMBO” “AU UREMBO”.

Je, Kujipamba ni kosa; na Biblia inaliambia Kanisa liseme nini juu ya wanawake Wakristo wanaojipamba?

Utata na mabishano kuhusu kujipamba kuwa ni dhambi au sio dhambi katika jamii ya Kikristo unatokana hasa na Maandiko hayo mawili hapo juu.

“…..Wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” kwa kuwa hakutuma ushahidi wa Maandiko kama Paulo na Petro walihamasishana kuandika maono hayo.

Wakristo na viongozi wa makanisa wajue jambo jingine kuwa, suala hili la kujipamba lilikuwa katika baadhi ya vikundi vya Kikristo vilivyokuwa Asia tu na siyo katika makanisa mengine yaliyokuwa nje ya Jimbo la Asia Ndogo.

Mtume Paulo akiwa ndiye Mtume pekee aliyeandika nyaraka nyingi kwa makanisa na kwa watu binasfsi, hatuoni maonyo haya ya “kujipamba” katika nyaraka nyingine alizotuma kwingineko tofauti na ule wa Efeso; Hali kadhalika na Petro pia.

Swali ?

Je waraka wa Paulo kwa Timotheo huko Efeso na Waraka wa Petro kwa Wakristo hao hao wa Asia, maonyo yao yalimaanisha kuwa Mungu aliwakataza wanawake wao kujipamba kwa kuwa ni dhambi, au kulikuwa na tatizo lingine lililowakilishwa na hayo yaliyosemwa?

Kama tukikubaliana kuwa ni kweli Mungu aliwavuvia Paulo na Petro kuandika maonyo hayo kwa kuwa aliona kufanya hivyo ni dhambi, je wanawake Wakristo wengine katika sehemu nyingine duniani, ni kweli tuna ushahidi wa Maandiko unaothibitisha kuwa hawakujipamba?

Kabla hatujahukumu na kuwatenga au kuwafukuza wenzetu wanaojipamba Je, tunaweza kuthibitisha kuwa Mungu mwenyewe na kazi zake tangu uumbaji hadi katika ushirikiano wake wa huduma na watumishi wake tangu Agano la Kale na Jipya, hajihusishi au kuwahi kuhusika na mapambo kabisa ?

Kabla hatujahukumu na kuwatenga au kuwafukuza wenzetu wanaojipamba Je, tunaweza kuthibitisha kuwa Mungu mwenyewe na kazi zake tangu Uumbaji hadi katika ushirikiano wake wa huduma na watumishi wake tangu Agano la kale na Jipya, haji husishi au kuwahi kuhusika na mapambo ?

Maswali haya manne yanaweza kuwa rahisi sana kwa baadhi, ambapo wengine huenda wakayaona ni magumu.

Kutokana na mzigo wa uchungu moyoni mwangu, nikiwa ni mchungaji ninayewajibika kuchunga kondoo wa Bwana na kutoa ufafanuzi juu ya yale yanayowasumbua kondoo hawa; Ninajua kuwa wachungaji wenzangu wataniunga mkono kutafuta jawabu sahihi la Kibiblia, na sio hisia au kubahatisha tu kama wachungaji wengi walivyofanya kwa miaka mingi hata sasa, na kuacha athari kubwa katika mwili wa Kristo, ambacho ndicho kiini cha uchungu wa moyo wangu, uliopelekea kuandika makala hii.

Nimechagua kuuliza maswali haya  ili yatusaidie katika utafiti wetu wa kugundua utamaduni wa kujipamba  asili yake ni Mungu au Shetani? Utamaduni huu ulianza lini? Kabla ya torati? Wakati wa Torati? Baada ya Torati au katika kipindi cha Kanisa la Agano Jipya ?

 

Mchungaji Moses Kashakali,

P.O. Box

Dar Es Salaam

                TAFAKARI YA WIKI

Waefeso 6:7-9