Kushamiri kwa UKIMWI sababu ni nini?

WATU wengi wakiwamo Watanzania, wanautambua UKIMWI kuwa ni ugonjwa gani, na hasara zake ni zipi. Kila siku katika vyombo karibu vyote vya habari, hatukosi kusikia juu ya ugonjwa huu mbaya unaosababisha vifo, umaskini na unaoongeza idadi ya mayatima na watoto wa mitaani.

Wengi wetu tumeshashuhudia jinsi ndugu zetu walivyopoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huu. Tunaweza kusema hakuna hata familia moja au mtu yeyote kati yetu watanzania anayeweza kusema kuwa hajaguswa na athari mbaya za UKIMWI, kama yupo, basi ni wa kutazamwa kwa mshangao usiopimika.

Ili kufahamu ubaya na hasara zitokanazo na UKIMWI na asiyefahamu wala kuamini kuwa UKIMWI una madhara mengi makubwa, basi huyo atembelee hospitali na makaburini.

Hatuna shaka kuwa tofauti na ilivyokuwa katika siku za nyuma, atakuta makaburi mengi mapya ambayo siyo siri, idadi yake inakua kwa kasi kutokana na UKIMWI usiochagua rangi, jinsia, umri, imani, cheo wala hadhi ya mtu katika jamii.

Hili ni jambo la kusikitisha. Waliokufa kwa ugonjwa huu, ni wengi ambao wangeweza kutoa michango mingine muhimu kwa maendeleo ya jamaa zao na taifa kwa jumla.

Wanaokufa kwa UKIMWI ni nguvu kazi ambayo inaondoka duniani huku mchango wao ukiwa bado unahitajika. Tunasema hivyo tukiamini kabisa kuwa wengi wa wanaokufa kwa UKIMWI kwa sasa ni wasomi, vijana na watu wenye nguvu motomoto katika kutenda.

Inatia moyo hasa kuona kuwa, viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali hadi kitaifa, wameivalia njuga vita dhidi ya UKIMWI na kuweka mikakati mbalimbali kupigana na ugonjwa huu.

Hata hivyo, bado inasikitisha kwani licha ya juhudi hizo zikiwamo za elimu ya mara kwa mara juu ya UKIMWI, bado ugonjwa huu hatari unazidi kushamiri.

Hata hivyo, yapo mambo mengi yatupasayo kufanya ili kuondokana na ugonjwa huu mbaya lakini kubwa zaidi, tukae chini tuulizane kuwa, KWANINI UKIMWI UNAZIDI KUSHAMIRI? SABABU HASA NI NINI, NASI TUNASHINDWA WAPI? SASA, KILA MMOJA AFANYE NINI?

Tunapenda kuungana na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Kanali Anatoli Tarimo aliyetamka wazi wazi kuhusu nyumba za kulala wageni zinazotoa mapumziko ya muda kwa watu.

Ama kwa hakika hiyo ni nafasi kubwa, mbaya na hatari sana katika kueneza UKIMWI. Mara nyingi nafasi hizi hutumiwa hata na watu wasiofahamiana kwa muda mrefu ambao huchukuana kiholela na kwenda huko kufanya uzinzi katika nyumba hizo.Nyumba nyingi za wageni zipo pamoja na baa za vinywaji mbalimbali kama bia na pombe za aina nyingi. Hapo ni vema kila mmoja akumbuke na kuzingatia kuwa, kwa asilimia kubwa uzinzi na ulevi ni marafiki wakubwa na ndiyo maana kila alipo bwana ulevi si rahisi kumkosa bwana uzinzi.

Hivyo, ni rahisi kwa mtu aliyelewa pombe kutamani kufanya mapenzi na mtu yeyote, bila kufikiria kwa makini, hata kama hamjui, bila woga kwa Mungu na bila aibu kwa watu. Huu ni ukweli ulio bayana.

Sisi tunasema, sababu moja wapo inayochangia kushamiri kwa UKIMWI ni kuruhusu kuwapo nyumba za kulala wageni zinazotoa huduma za muda kwa wageni ambao siyo wasafiri wala wapangaji. Kibaya zaidi, wahudumu wakijua kabisa kuwa wanaruhusu ili kitu gani kikafanyike.

Sote tunapaswa kubadili tabia zetu, lakini mtu atabadilishaje tabia yake pale anahimizwa wazi kuwa ipo "kinga ya nguvu"ya UKIMWI ambayo ni kondomu?

Na biashara ya kondomu inashamiri ikionesha msisitizo feki unaowasadikisha watu kuzitumia kama kinga sahihi ya UKIMWI hali sivyo?

Pengine mambo hayo yanaweza kuwa kama alivyofundisha mtaalamu mmoja wa kidini kwamba watu watende dhambi kwa nguvu sana, lakinii waamini kwa uthabiti mkubwa. Na hivyo ndivyo mambo yanavyokuwa katika jambo hilo la UKIMWI.

Kuhimiza matumizi ya kondomu ni sawa na kusema kuwa watu hawawezi kujishinda na hivyo, waendelee na tabia ya uzinzi kwani kutumia kondomu kwa haiwezekaniki kabisa kuepuka uzinzi. Yaani wawe na imani na kondomu ambayo ni kinga kamili ya ukimwi. Hoja hizi ni HATARI NA ZINALIANGAMIZA TAIFA NA WATU WAKE.

Sisi tunasema huko ni kujidanganya, na hivyo ugonjwa huo hautaondoka kamwe katika jamii yetu licha ya jitihada mbalimbali zinazofanyika kila siku na kila mahali.

Binadamu ni kiumbe mwenye akili na utashi, na hivyo akili yake ndiyo inayotawala mwili, lakini kama inatokea kuwa vionjo vya mwili ndivyo vinavyotawala akili basi huyo si binadamu tena aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mungu.

Kwa kadiri ya akili ya binadamu akiambiwa kuwa kuna hatari mahali fulani, hujiweka katika tahadhari ili hatari isimpate, lakini cha kushangaza ni katika ugonjwa huu. Ingawa elimu kadha zinatolewa dhidi yake, tunashuhudia namna wengi wetu wanavyoendelea kupuuzia jambo hilo.

Sote tunapaswa kujua kuwa huo ni ugonjwa ambao kwa kweli hauna tiba bali una kinga ambayo siyo hasa kondomu, bali ni utashi wake binadamu wa kujishinda katika kufanya vitendo vya ndoa nje au kabla ya ndoa.

Katika hatari mbalimbali ambazo binadamu hukumbana nazo, mara nyingine huona kimakosa kuwa kitu fulani ni kinga itakayomsaidia, kumbe sivyo.

Tunao ule msemo usemao, kufa kufaana. Hivyo, yawezekana kuwa hata katika janga la UKIMWI, kuna kufa kufaana, yaani kuna watu wanaofaidika kutokana na balaa hilo.

Tunapaswa kuwa waangalifu sana katika kupokea ushauri na hata hizo zinazodaiwa kuwa ni kinga za nguvu. Ni lazima tutambue kuwa hapo kuna vitu vya biashara pia licha ya kudaiwa kuwa ni misaada ya kutuonea huruma sisi wananchi.

Tumesikia kuwa kuna mikoa inayosifika kwa utumiaji wa kondomu, lakini bado hatujaambiwa kwamba hiyo mikoa imepunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI.

Wengi wetu tumekuwa tukisikia kwamba wenzetu wa Uganda wamefanikiwa kupunguza kasi ya UKIMWI siyo kwa sababu waligawiwa na kutumia kondomu, bali kwa sababu walikubali kubadili tabia zao.

Sisi tunasema, Kanuni yetu iwe ni ile ya wanausalama kwamba tusimwamini kila mtu na tumtilie mashaka kila mtu. Haifai kusema kuwa mtu huyu ni salama ama sivyo kwa mtazamo wa macho matupu.

Pia, tusijidanganye kwa kuwaamini wanaodai kupimwa na kuonekana salama siku hiyo kwani cheti hicho si cha kudumu.

Yawezekana kuwa aliyekuwa salama juzi, leo anaweza kuwekwa katika kundi la waathirika hivyo, kinachotakiwa ni kuwa imara katika kuilinda miili yetu.

Tujue kuwa UKIMWI, NI HATARI, UKIMWI UPO, UKIMWI UNAUA NA WOTE TUPAMBANE Nao. MUNGU IBARIKI TANZANIA.