Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ni uhai wa Kanisa tuziimarishe

JULAI 14 hadi 28, mwaka huu, Umoja na Ushirikiano wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi za Mashariki mwa Afrika, utafanya Mkutano Mkuu hapa Tanzania (AMECEA-2002) sambamba na maadhimisho ya miaka 40 tangu kuzaliwa kwa umoja huo.

Ni ukweli ulio bayana kuwa mkutano huo ni heshima kubwa kwa Watanzania na una faida zake kwa Watanzania kiroho na kimwili. Mkutano huo utahudhuriwa na maaskofu zaidi ya 100 na wajumbe wengine zaidi ya 400.

Umoja wa AMECEA una maana na faida kubwa kwa waamini wa nchi wanachama lakini miongoni mwa makubwa yanayoonekana wazi na ambalo tunapenda kulizungumzia leo, ni Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo.

Wazo la AMECEA kuanzisha Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo, lilianza mwaka 1976. Chimbuko la Jumuiya hizi ni Jumuiya ya Kwanza ya Wakristo kama tunavyosoma katika Maandiko Mtakatifu, Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 2:42-47 ; 4:32 -37).

Fasili hii inasema: Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali. Kila mtu akaingiwa na hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume. Na wote walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia wote kama kila mtu alivyokuwa na haja.

Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.

Kifungu hiki pamoja na Matendo 4: 32-37, zinahimiza umuhimu wa Wakristo kujiunga katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo na kufanya kazi kwa ushirikiano.

Jumuiya hizi hujengwa na familia kadhaa zisizopungua tano (5 hadi 15) zilizo jirani. Familia hizi hushirikiana katika mambo yote ikiwa ni pamoja na kusali pamoja, kusoma na kushirikishana katika kutafakari Neno la Mungu, kufarijiana, kulea watoto, kusaidia wenye shida, kupanga maendeleo yao, na kuwa msingi wa uongozi wa Kanisa mahalia.

Hata katika masuala ya uongozi, viongozi wote walei hadi ngazi ya kitaifa lazima waanzie katika ngazi ya Jumuiya Ndodo Ndogo za Kikristo.

Sisi tunasema kuwa ni dhahiri jumuiya hizo zimekuwa chachu ya kujenga umoja na ushirikiano wa Kanisa kama familia moja.

Pia, zimekuwa nyenzo bora katika kuimarisha maisha ya Kanisa lote. Ni wazi kila mmoja wetu anaona namna zilivyochangia kukuza umoja, upendo, mshikamano na maendeleo ya watu katika nchi wanachama.

Kama hivyo ndivyo, basi ni wajibu wetu Wakristo Wakatoliki kuhakikisha kuwa wote tunashiriki kikamilifu kuzijenga, kuziimarisha na kuzitumia kwa manufaa ya kiroho na kimwili jumuiya hizo.

Tuzidi kuonesha umuhimu wake kwa kuzitumia kuwasaidia hata wenzetu ambao wameshindwa kusomesha watoto wao, tuzitumie katika kuwasaidia wenzetu wenye matatizo ya kiafya wanaohitaji huduma lakini wanashindwa kutokana na kukosekana kwa pesa.

Pia, tutumie jumuiya hizo kujengana kiroho kwa kurekebishana pale mmoja wetu anapoyumba kimaadili ama kulegalega kiimani.

Bado tunasisitiza kuwa, Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo tuzitumie kutatua matatizo yetu mbalimbali ikiwa ni pamoja na migogora baina ya wanandoa na hata zitusaidie kuwapata vijana wengi bora watakaokuwa watumishi bora wa kanisa kwa zama zijazo.

Waamini wote tukumbuke kuwa hatuna budi kuziimarisha jumuiya hizo kwani hata sasa, hakuna huduma yoyote anayoweza kupata muumini, bila kuanzia katika ngazi ya Jumuiya yake.

Kupitia jumuiya zetu, tuwafundishe vijana kusali nasi pia tusali, tuhimizane na tushirikiane katika kusoma Neno la Mungu kwa pamoja, kulitafakari na kikubwa zaidi, kuliishi.

Hata hivyo, tunasema kuwa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ni za waamini wote Wakatoliki, wanawake, wanaume, wazee, vijana na hata watoto.

Ni aibu kwa mwanaume anayejiita kuwa Mkatoliki lakini akapuuzia na kushindwa kushiriki katika jumuiya hizi kwa mlolongo wa visingizio kikiwamo cha muda na kazi.

Tunasema Jumuiya hizi ndio msingi wa Kanisa, tuziimarishe ili zituimarishe kiroho katika Kristo.

Maaskofu wa Tanzania wanatualika waamini wote kuimarisha imani, umoja, mapendo na maendeleo kwa sala hasa katika kuimarisha Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo.

Tuzingatie kuwa jumuiya hizi sio jukumu la wasichana, wavulana, wanawake, wanaume, wazee au vijana bali ni JUKUMU LETU SOTE. TUSHIRIKI KIKAMILIFU. Mwisho tunasema, AMECEA MZAZI WA JUMUIYA NDOGO NDOGO KARIBU TANZANIA.

Wanakwaya msibinafsishe Liturujia

Ndugu Mhariri,

Siku hizi ukipita katika kila Parokia na hata vigangoni utasikia kwaya karibu zote zinafanya mazoezi kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka. Ni matumaini yangu kuwa Wana Kwaya Wito wao ni " kumwimbia na Kumsifu Bwana" siyo vinginevyo kama vile kujiimbia wenyewe. Mimi ni mpenzi sana wa kuimba na kama mwanaliturujia wakati mwingine nimejiuliza hivi kweli hizo nyimbo ni za kumsifu Bwana au la. Liturujia ni ya Kanisa, na siyo ya kikundi kimoja. Huu ni mkusanyiko wa watu wa Mungu, na hivi basi ni Kanisa lipo katika sala kwa Mungu Baba , kwa njia ya kristo . Hivi basi wito wa kwaya ni kuwasaidia watu wa Mungu kusali vema, wito wa kwaya ni kuwahamasisha waamini wamwimbie Mungu kwa shangwe na kwa ibada. Kazi ya kwaya ni kuinjilisha kwa njia ya Nyimbo. Kama suala ni hilo basi kwaya lazima zifuate katiba na sheria zilizowekwa ili liturujia yetu ilete mnufaa katika kumsifu Mungu wetu.

Nyimbo za aina gani ziimbwe katika Liturujia ya kanisa? Wanakwaya lazima wajue kipindi cha Liturujia katika kanisa, kama ni wakati wa kawaida, au majilio, au mateso kanisa sasa, basi nyimbo ziendane na kipindi mwanana. Nyimbo zinazoimbwa ziwe rahisi kwa waamini kuzifuata. Mara nyingi utakuta wanakwaya wanaimba nyimbo ambazo waamini hata padre hawezi kuziimba, na mbaya zaidi kama wenyewe wanaimba kwa mashaka, inakuwa ni kioja na vichekesho.

Kama kuna nyimbo mpya hakikisheni kuwa walao kiitikio waamini wanafundishwa, ili wote washiriki katika Liturujia takatifu. Hii ni haki ya msingi kila muumini, kushiriki Liturujia kikamilifu. Ukisoma Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani katika hati ya Liturujia inasema "Tendo la liturujia ni tendo la watu wa Mungu na sio watu binafsi". Hivi basi natoa wito kwa wanakwaya kuondokana na dhana potofu kwamba wao ndiyo watendaji wakuu, na kwamba bila wao hakuna Misa Takatifu. Wanakwaya tuache au kutaifisha liturujia ya kanisa. Wanakwaya ni chombo mojawapo tu katika liturujia,

maana katika liturujia watu wengi wanahusika, kwanza ni Mungu Mwenyewe, halafu kuna padre ambaye ni Rais katika liturujia hiyo, kuna wasomaji, na pia kuna waamini wote. Kila mtu anawajibu wake, na hivi lazima kuwe na uhusiano wa pande zote, yaani uratibu au ukubaliano.

Nikiwa Padre nimepata mang’amuzi mengi kidogo kuhusiana na kwaya zetu. Kusema kweli ni chombo kizuri sana iwapo kitajaribu kufuata sheria za kanisa kuhusu kuimba nyimbo katika ibada. Mara chache nimejisikia kama nipo "Mbinguni" na hata kutokwa na mchozi kwa sababu ya kuguswa na ujumbe wa wimbo fulani. Hivi basi jueni kuwa wanakwaya mna wito wenu katika Liturujia, lakini siyo kweli kwamba bila nyie hakuna misa. Kuwa wanyenyekevu ni kitu muhimu sana katika kanisa. Mara nyingi nimeshuhudia magomvi, mitafaruku, chuki na machafuko katika ya mapadre na wanakwaya, sababu ni moja, kwamba wanakwaya wanataka kufanya wapendavyo au kama wanavyosema waswahili "kufanya vitu vyao". Katika liturujia hatufanyi vitu vyetu;tunaitwa kushiriki katika tendo la Yesu Kristo. Sisi tunaalikwa, hivi basi tusichukue nafasi yote . Tujue wajibu na mipaka yetu. Ni vema wanakwaya kila wakati kuongozwa na katiba kama ipo, kwa sababu kazi waliyonayo ni muhimu sana, hivi lazima daima kabaki katika lengo lile lile la kumwimbia Bwana na kuwashirikisha waamini, na siyo

Kujiimbia wenyewe kwa ajili ya kujipatia sifa na utukufu. Kwaya isifanye Shoo, isiwe taarabu.

Isijitenge na jumuia nzima, inakuwa kama imekodiwa sijui na nani? Lazima wawe sehemu ya waamini na siyo kujiona watu wa pekee au maalumu.

Nyimbo mpya hazikataliwi bali kuwa na nyimbo mpya kila jumapili si kitu sahihi, kwa vile waamini watashindwa kwenda sambamba na mabadiliko hayo. Kama kuna wimbo mpya ni vema kuwafundisha waamini kiitikio namna nyingine kwaya inajikuta inaimba yenyewe tu, halafu mapato yake ni waamini kujikuta wasikilizaji na watazamaji mithili ya kwenda kwenye ukumbi wa Sinema. Uzuri wa kwaya yoyote ile unapimwa na kiasi gani inawashirikisha waamini wote kuimba na kushiriki liturujia kikamilifu.

Uzuri wa kwaya kamwe haupimwi na uzuri wa kwaya kwamba wanaimba kama malaika au malaila huko Zambia.

Wakati huu wa maandalizi ya sikukuu ya Pasaka ni wakati wa kujiuliza tunatawashirikisha vipi waammi katika liturujia nzima? Je, kama tuna nyimbo mpya tutafanyaje ili waumini waweze kushiriki? Hata hivyo ni wajibu wa mapadre kuona kwamba Liturujia ya kanisa inabaki ya kanisa na siyo ya kikundi binafsi. Mara nyingi mapadre tunapuuzia sana hii idara na basi wanakwaya wanajifanyia vitu vyao. Kwa vile " Liturujia ni kiini cha maisha ya Kikristo" kama inavyosema Hati ya Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani, ni vema mapadre kujihusisha na utendaji mzima wa kwaya. Ni kweli inachukua muda.

Pia ni muhimu kuwaelimisha juu ya suala nzima la Liturujia, na hasa kwa njia ya washa na semina au Matamasha. Wakati mwingine wanakwaya hawajui wajibu wao na mipaka yao kwa vile hawaambiwi. Hivi ni wito wangu kwa mapadre wenzako kutafuta muda wa kukaa chini na wanakwaya na kuweza kubadilishana mawazo, mbinu na kuelimishana.

Maadili mema yanatakiwa sana kwa wanakwaya kwa vile wao pia ni viongozi katika kanisa wa aina moja au nyingine. Ni kweli sisi ni binadamu na siyo malaika, hivi basi tunaweza kuwa dhaifu katika hili na lile. Lakini lazima tuangalie kuwa udhaifu wetu usiwe kikwazo kwa wengine.

Mara chache nimeshuhudia kwaya iliyokwaza waamini, na basi viongozi wa kanisa, mapadre, Maaskofu, au Baraza la Walei, wanapochukua hatua ya kurekebisha na kukaripia tabia hizo mbaya za utovu wa nidhamu, kumejitokeza uhasama, uadui, naomba tuwe wanyenyekevu na watiifu.

Na wengine wamediriki kusema sisi" tunaingia" msituni, je, unajiandaa na mapambano gani? Hali hii inaweza kusambaza sumu mbaya sana katika Jumuiya nzima ya parokia au kigango kwa vile inaleta utengano. Wanakwaya kazi zetu ni kuunganisha jumuiya ya kikristu na siyo kutenganisha.

Kama hali hii inatokea basi jueni kuwa hamna " ROHO MTAKATIFU" bali mnatawaliwa na "roho mtakavitu". Mkifikia hali hii mjue mko hatarini) ombeni msaada na ushauri kwa wakubwa wa kanisa.

Mwisho namaliza kwa kuserna, kwamba fani ya kuimba ni kipaji cha Mungu, basi tukitumie ipasavyo, hakuna sababu ya kudeka na kuwa na majivuno, ahaaaa!!! Mimi wameniudhi sasa bila mimi hii sauti ya pili imechemsha, sifiki kwenye mazoezi basi.

Hayo ni majiganibo yasiyokuwa na maana. Wanakwaya inatupasa kuwa ma maadili ya hali ya juu, sababu tunamwimbia Mungu na siyo mtu hata awe na cheo gani? Mungu anahitaji sauti zetu nyororo, zisizo na majivuno, wala vinyongo na hasira, roho zetu zilizotakaswa na maneno na matendo yetu. Hakika tukifanya kazi kwa kufuata mapenzi ya Mungu, na tukipendana kati yetu hakika Baba yetu aliye mbinguni atatukuzwa. Wanakwaya nawatakieni uimbaji mwema na ushirikishaji mzuri.

NAWATAKIENI PASAKA NJEMA NA BARAKA TELE!! YESU AMEFUFUKA ALELUYA, ALELUYA!

Padre Mapunda Tunda la Kanisa

P. O. Box

Dar es Salaam.