MIAKA 38 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

Historia ya umwagaji damu isijirudie

JUMAMOSI hii, Januari 12, Zanzibar inasherehekea miaka 38 ya Mapindizi.

Bila shaka Watanzania wote tutaungana katika kuadhimisha sherehe hizi bila kujali huyu ni Mtanzania kutoka bara na huyu ni Mzanzibari.

Kitu muhimu katika kusherehekea Mapinduzi haya ,ni kuzingatia suala la umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania wote kama walivyo sisitiza viongozi waasisi wa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani,hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hayati Sheikh Abeid Aman Karume kauli ambayo hadi sasa bado inasisitizwa na viongozi mbalimbali.

Tukirudi katika historia, kabla ya Mapinduzi,Wazanzibari walikuwa wananyanyasika sana kutokana na kile kilicho julikana kama Biashara ya Utumwa ambapo binadamu alikuwa akinunuliwa kama bidhaa nyingine sokoni.

Wananchi wengi walipoteza maisha yao huku wengine wakiendela kufanyishwa kazi ya utumwa ambapo kwa kuwatumikia mabwana hakuna mtwana au mjakazi ambaye alikuwa na sauti ama uhuru wa kujiamria mambo.

Hayati Sheikh Abeid Aman Karume ambaye ni Rais wa Kwanza wa Zanzibar kwa kushirikiana kwa karibu na hayati Mwalimu Nyerere na viongozi wengine enzi hizo,walijitahidi kwa hali na mali hadi wakawakomboa wananchi kutoka katika hali hiyo ya unyanyaswaji.

Baada ya hapo Zanzibar ilipata kuwa nchi ya amani huku ikishirikiana kwa karibu na Tanzania Bara ushirikiano uliokuja kuzaa Muungano.

Kutokana na hali hiyo,hali ya utulivu na amani vimekuwa ndiyo nguzo kuu ya Zanzibar.

Hali ilikuja kubadilika kidogo baada ya kuingia mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ambapo kila mwananchi alipata nafasi ya kujiunga na chama anacho kitaka.

Kutokana na hali hii ,taratibu vurugu zilianza kutokea ambapo uliibuka mvutano mkubwa baina ya vyama viwili vya CCM na CUF ambayo vinaoneka kuwa na nguvu visiwani humo.

Katika tukio la kusikitisha visiwani humo,ni lile la umwagaji damu lililotokea Januari mwaka jana baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge Katika tukio hili watu zaidi ya ishirini walipoteza maisha yao kufuatia mapigano baina ya askari na wananchi wa visiwa hivyo kwa kile kilichodaiwa kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki.

Vile vile maelfu ya Wazanzibari walikimbilia nchini Kenya kama wakimbizi walio kimbia mapigano.

Mungu ashukuriwe; kwani mapigano hayo bado hayajajirudia tena kutokana na viongozi wa vyama husika kwa kushirikiana na wale waasasi mbalimbali zikiwemo za kidini na serikali,kuingilia suala hilo.

Hadi sasa Zanzibar kuna hali ya utulivu na amani,Mataifa mbalimbali yamekubali kurudisha misaada nchini humo na watalii wanaendelea kutembelea eneo hilo.

Kufuatia hali hiyo,wananchi wa visiwa hivyo hawana budi kudumisha amani hiyo,wasikubali tena kudanganyika hadi kurudia tena mapigano.

Wakae kwa upendo,umoja na amani bila kujali tofauti zao za kidini,kisiasa na rangi za ngozi zao.Ni matumaini yetu kwamba yaliyo jitokeza Januari mwaka jana, hayatajirudia tena.

Simu za nini Kanisani?

Ndugu Mhariri,

NAPENDA kuchukua nafasi hii kutoa dukuduku langu ambalo limekuwa linanikera kwa muda mrefu.

Jambo ambalo linaniudhi na ambalo linaleta karaha ni hawa wenzetu wenye simu za mikononi. Hivi jamani huwezi kuicha hiyo simu nyumbani kwa muda wa saa kadhaa au kuifunga tu na kusikiliza neno la Mungu kwa saa kadhaa?.

Nasema hivyo kwa kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanakwenda kanisani na simu zao za mkononi wakiwa hawajazifunga. Sasa nashindwa kuelewa kama wanakuwa wanasahau kuzima au wanafanya makusudi au ndio tuseme kuwa wao huwa wana simu za maana zaidi kuliko kumwabudu Mungu?

Hili limekuwa ni jambo la kawaida japokuwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya kidini wamekuwa wakiyakemea masuala haya ya kutokubali kuzima simu zao pindi wanapokuwa makanisani.

Katika tukio la hivi karibuni ni lile lililotokea katika kanisa moja ambalo nisingependa kulitaja.Katika tukio hilo simu ya muumini mmoja ilianza kuita kwa sauti ya juu kabisa wakati ikisomwa Injili.

Kitu cha kushangaza ni kwamba yule muumini hakupata mshtuko hata kidogo badala yake alijifanya yupo makini kusikiliza neno la Injili hadi hapo waamini wengine walipomgeukia kwa hasira, ndipo alipo jifanya kushtuka na kuipokea simu hiyo.

Kilichozidi kuwaumiza waamini ni kile kitendo cha mtu huyo kuanza kuongea na simu hiyo ndani ya kanisa bila kujali kwamba kipindi hicho kilikuwa ni cha Misa Takatifu.

Kutokana na hali hiyo ilibidi baadhi ya waamini waamke na kumfuata mtu huyo alipokuwa amekaa ambapo walimwamru atoke nje, naye bila aibu alifanya hivyo huku akiwa ameshikilia simu yake mkononi!.

Sasa sielewi mtu huyo ambaye kweli ni mtu wa makamo kabisa, sijui niseme kuwa alisahau kuzima simu au aliamua tu kuacha kwa makusudi.

Kwa kweli hii inadhihirisha ni kwa jinsi gani watu wanavyomdharau Mungu Muumini huyo hanabudi kujiuliza kuwa bila ya kumuomba Mungu hiyo simu angeweza kuipata kweli?

Kwani nini mtu usimpe Mungu shukrani zake badala yake unakuwa unakwenda kanisani kama msindikizaji au kutimiza wajibu kwa kuwa tunatakiwa kwenda kanisani.

Huu sio ustarabu hata kidogo. Kama unajua una simu ya maana kwanini hiyo simu usiiache nyumbani au ifunge kabisa; Misa ikiisha wakati wa kurudi nyumbani ndipo uitoe na huyo mtu kama anashida nawe atakupigia tu. Kwanini tunashindwa kuwa wastarabu jamani.

Nadhani hili suala la watu kwenda na simu kanisani mimi si wa kwanza kulizungumzia katika gazeti hili; kuna wengine wameshasema tukadhani yakuwa wahusika wakiisoma na wengine wote watajirekebisha.

Watu wasiwe wanageuza kanisani kuwa sehemu ya starehe ambapo kuna kila aina ya milio ya simu ambapo kila mmoja yupo bize na ulevi.

Kama unajijua unakuja kanisani kutimiza wajibu, tafadhali, ni heri usije kabisa ili kuondokana na hiyo kero maana kuna watu wanahamu ya kuja kanisani kumshukuru Mungu; lakini wanaposikia milio ya simu,wanakosa utulivu hivyo wewe unakuwa umewakwaza.

Mimi napendekeza kuwa viongozi wa kanisa walivalie njuga suala hili maana ikiendelea namna hii itafikia wakati kila mmoja atakuwa huru hata akiamua kupiga simu atapiga tu akiwa kanisani.

Ni matumaini yangu wenye tabia kama hii wataicha mara moja

Ngambakhia Damas,

P.O. Box 6202

Dar-Es-Salaam