Mwaka 2002 uwe wa maendeleo zaidi

KABLA ya kufunga mwaka wa 2001, tulishauriwa kufanya tathmini ya utendaji wetu wa mwaka huo uliopita.

Wananchi wengi walihimizwa kujichunguza kuona ni wapi hawakufanya vizuri na wapi walifanya vizuri katika utendaji wao wa kila siku.

Wapo waliofanikiwa kukamilisha mipango yao kutokana na bidii yao katika utendaji. Pia, wapo ambao hawakuweza kukamilisha mipango yao kwa sababu mbalimbali.

Ili kuweza kupiga hatua mbele katika maendeleo, hatuna budi kuwa na mipango bora ya utendaji katika kazi zetu. Kwa hiyo basi tunalopaswa kufanya toka mwanzo kabisa wa mwaka ni kuwa na mipango kabambe ya utendaji wetu.

Kila mmoja wetu anapaswa kuwa na mipango maalumu ya kila siku, kwa kila mwezi, kwa mila miezi sitasita na hata kwa mwaka mzima.

Licha ya mipango hiyo ya mtu binafsi, inafaa pia kuwapo kwa mipango bora ya kifamilia kwa kuwa yapo mambo mengi wanayoweza kufanya ili kujiletea maendeleo katika familia zao.

Kwa vile binadamu tumepewa akili na Mwenyezi Mungu, hatuna budi kuzitumia akili hizo ili tuweze kuleta maendeleo. Tutatumia akili hasa kwa kuwa na mipango thabiti ya utendaji.

Watanzania wengi ni wavivu sana; wavivu katika kutumia akili zao, na pia wavivu katika kutumia nguvu zao.

Wananchi walio wengi hupoteza muda wao mwingi katika kuzungumza na katika mambo ya starehe kama vile kunywa pombe.

Wataalamu hutuambia kuwa muda wetu wa kuishi hapa duniani ni mfupi mno ukichukulia kuwa kwa miaka hiyo michache tunayopewa kuishi hapa duniani hutupasa kulala usingizi, kula, kusali na shughuli nyingine nyingi.

Hivyo, ukiangalia kwa makini utabaini kuwa muda unaosalia ni kidogo sana na inatupasa kuutumia vizuri ili kujipatia maendeleo ya kimwili na kiroho.

Ukiangalia hali ya nyumba zilivyo kule vijijini, hutisha sana. Nyingi ni zile zinazoitwa "mbavu za mbwa", yaani mtu anaweza akasimama nje na kuona kila kitu kilichopo na nini kinaendelea ndani.

Papo hapo hao wenye nyumba hawashituki, wako tu wakiendelea kupumzika bila kufanya chochote kile. Hivyo pia mazingira ni machafu sana ambayo huweza kukaribisha magonjwa mbalimbali.

Tatizo ni kwamba wananchi wengi hawana moyo wa kujituma ili kujiletea maendeleo. Lakini, wengi wameridhika sana na hivyo hakuna nguvu ya kujimudu ili kujiongezea kipato na kubadilisha hali zao za maisha.

Pamoja na kuwa na mipango, yatupasa kuwa na wivu wa kimaendeleo na papo hapo kuwa wabunifu na waaminifu. Binadamu ni kiumbe mwenye akili na hivyo, hana budi kutumia akili, yaani kuona watu wengine wanafanya nini, na papo hapo kuomba ushauri kwa wale ambao wako mbele katika kujitegemea na mwenye maendeleo.

Tunambiwa kuwa yatupasa kujifunza kila siku na kila mahali na kutoka kwa mtu ye yote yule mwenye maendeleo ya kweli. Wako binadamu ambao kutokana na kiburi cha maisha hawataki kujifunza lolote kutoka kwa wenzao. Hao wamejaa kiburi ambacho ni kizingiti kukubwa katika maendeleo.

Kwa hiyo, mwaka huu wa 2002 hatuna budi kupiga hatua mbele katika kujiendeleza na hasa katika kuwa na mipango binafsi na ya familia zetu.

Tusilale na kuamka bila kuwa na kitu madhubuti cha kufanya ili kutuongezea kipato chetu. Tuachane kabisa na uvivu ili tuweze kulisukuma gurudumu la maendeleo kwa kuweza kubadilisha hali zetu ili zizidi kuwa bora zaidi na zaidi.

Wale wataalamu wa Kirumi walikuwa na msemo wa maswali ya kujiuliza katika kujitafutia maendeleo ya mtu binafsi.

Walisema hivi: Ikiwa mtu mwanaume amefaulu, na ikiwa mtu mwanamke amefaulu kwa nini nami nisifanikiwe? Hivyo ndivyo nasi tunavyopaswa kujisemea kila siku tukitaka maendeleo.

Labda ni kuwa na nyumba, hapo tunaona kuna wanaume wengi waliofanikiwa kuwa na nyumba nzuri.

Pia wapo akina mama wengi ambao wamefanikiwa kuwa na nyumba nzuri, na kwa nini wewe usifanikiwe?

Labda ni kulima, hapo pamekuwa na wakulima wengi, ambao wamefanikiwa katika kazi hiyo kutokana na juhudi zao. Je, kwa nini wewe usifanikiwe

Kwa hiyo tusijione wanyonge na hivyo tukakata tamaa ya na kuacha kujitafutia maendeleo. Tukiwa na nia, tutafanya mwaka huu wa 2002 kuwa ni kweli mwaka wa maendeleo na mabadiliko katika hali zetu za maisha.

Hayo yote yawezekana tu ikiwa tutatimiza wajibu wetu ipasavyo. Tuache uvivu na uzembe na badala yake tuwe na ule wivu wa kimaendeleo ili tuutumie mwaka 2002 kujiltea maendeleo ya kweli.

KIONGOZI wekeni picha za Ubatizo na Harusi

Ndugu Mhariri,

NAOMBA unipe nafasi katika gazeti lako la KIONGOZI ili nikiwa miongoni mwa wasomaji na wapenzi wa gazeti hili, nitoe maoni yangu.

Kwanza kabisa, ninawapongeza kwa kuwa siku hadi siku, ninaona namna mnavyojitahidi kuliboresha gazeti na hata makosa madogo madogo yasiyo ya lazima, sasa yanazidi kupotea kabisa.

Pia, ninawapongeza kwa kuwa sasa hata habari na makala mnazotupatia, zinatujenga kimwili na kiroho na hivyo mjitahidi kuboresha zaidi hali hiyo.

Hata hivyo, licha ya kuamua wazi kuwapa pongezi hizo, ninaomba nitumie nafasi hii kutoa ushauri wangu.

Kwa kuwa gazeti hili ni gazeti la kidini, tungeomba mtoe nafasi maalumu kwa ajili ya kuweka picha za matukio malumu ya kidini yakiwamo ya sherehe za sakaramenti mbalimbali kama Ubatizo, Kipaimara, Ndoa pamoja na matukio mengine yakiwamo kumbukmbu za siku maalumu za kuzaliwa (birth day).

Ninaomba picha hizo ziwe za sherehe za kanisani na hata za tafrija zinafanyika baada ya sherehe hasa zinayofanyika kanisani.

Nimeamua kutoa ushauri ama ombi hilo kwa sababu matukio ya kupokea sakramenti hizo ni muhimu kwa Kanisa na kwetu sisi wafuasi wa Yesu Kristona hivyo, tunapenda kuyakuta kwa wingi katika chombo cha Kanisa kama gazeti hili la KIONGOZI.

Binafsi, ninaamini kuwa wasomaji wengi wataniunga mkono katika hoja hii ili pia tupate hata nafasi ya kutumiana salamu na pongezi kupitia gazeti hili litolewalo kwa wiki.

Ndugu Mhariri, haya ni maoni yangu binafsi labda na mwingine yeyote anayeona yanafa.

Hivyo, ninaomba kwa niaba ya wengine kama utakubaliana nayo na hali ikikuruhusu, utuwekee nafasi hiyo. Ninaamini kwa kufanya hivyo, utazidi kutunufaisha sisi wasomaji wako.

Revocatus Makara,

P.O.BOX 3014.

MOSHI.

Kwa kuwa gazeti la KIONGOZI linaheshimu na kupenda maoni na maombi ya wasomaji wake, tunapenda kuwakaribisha wasomaji wetu kututumia picha zao za matukio mbalimbali na salamu ili tuzichapishe gazetini.

-Picha zinazoonekana vizuri zitakapotufikia, tutazichapisha bila gharama wala upendeleo wowote.

- Asante kwa ushauri wako na karibuni wasomaji wetu

-MHARIRI-

NANI ZAIDI ichanganye nyimbo za asili

Mhariri KIONGOZI,

NAOMBA unipe japo nafasi finyu tu, ili nitoe ushauri wangu kwa waandalizi wa RADIO ONE FM STERIO ya jijini Dar Es Salaam, hasa kipindi cha "NANI ZAIDI" kinachosikika kila Jumapili kuanzia saa 8:mchana kikiwapambananisha wanamuziki wa mahadhi yanayofafana ili kupata maoni ya wasikilizaji kuwa ni mwanamuziki gani au bendi gani kati ya zinazopambanishwa ni bora zaidi.

Ninaomba kama inawezekana, kipindi hiki kivishirikishe kwa mpambanao, wanamuziki au vikundi vya muziki wa asili . (Nina maanisha muziki au ngoma za makabila mbalimbali nchini)

Ninasema hivi kwa kuwa ninaona kipindi hiki kimeegemea zaidi katika muziki wa dansi.

Ninaamini kwa kufanya hivyo, watu watazijua na kuzithamini zaidi ngoma za asili za hapa nchini,

Bw. George Kibago,

CHAMWINO,

DODOMA.