Mwaka 2002 tupigane na ujinga wa kiroho na kimwili

DESEMBA 31, ni siku muhimu katika kumbukmbu kwani ndiyo inakamilisha ngwe ya kipindi cha mwaka 2001. Baada ya hapo, jamii itasherehekea kuanza kwa Mwaka Mpya yaani, Januari Mosi, 2002.

Tunamshukuru Mungu kwa ukarimu aliotujalia hadi kukifikia kipindi hiki. Tunaamini kuwa bahati ya kuuona mwaka mpya, haimaanishi kuwa sisi ni bora kuliko waliotangulia kaburini, la hasha! ni mpango maalumu wa Mungu.

Wakati tunaadhimisha siku hizi baada ya kuihitimisha vema Sikukuu ya Krismas, ni vema sasa kila mmoja kwa nafasi yake, ajiulize ni kwa namna gani anauvuka Mwaka 2001, na kuuingia Mwaka 2002.

Hapa pia tujiulize, je, kila mmoja amejichunguza kiasi cha kutosha ili malengo yake mema ambayo hakuyakamilisha katika mwaka huu, ayakamilishe kwa mwaka ujao?

Je, kila mmoja amechunguza madhambi yake yote na amenuia kuuanza vema mwaka hususan baada ya kuzaliwa upya na Yesu Kristo wakati wa Krismasi?

Sisi tunaamini kuwa mwaka mpya ujao utakuwa muafaka zaidi wa kuendeleza mapambano dhidi ya maadui wote wa kiroho na wa kimwili. Msisitizo tunauweka zaidi katika maadui wa kiroho kwa kuwa ndio chanzo cha masumbuko yote duniani.

Tunasema hivyo tukiamini kuwa lazima tukitumie kipindi hiki kipya kuunganisha nguvu zetu ili tushinde katika vita dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi.

Huu nii wakati wa kuitafuta na kuirudisha mikononi mwa Mungu, nafasi yote iliyokuwa imetekwa na shetani katika maisha yetu.

Tunasema 2002 uwe ni mwaka wa kutafuta maendeleo zaidi hivyo kila mmoja alipo ajiangalie kuwa katika kipindi kilichopita, amefanya nini kupambana na umaskini kwake mwenyewe, katika jamii na kwa taifa zima.

Kijana ajiulize kuwa ameutumia vipi muda wake na amevuna nini kitakachomfaa katika maisha kiroho na kimwili.

Kila mtu ajiulize kuwa, kwa kipindi kilichopita amekitumia vipi kundaa maisha yake ya baadaye kule mbinguni na hapa duniani.

Tunajua matatizo katika jamii yanatokana na ujinga wa kiroho na kimwili na ndio sababu tunashauri kila mmoja autumie mwaka mpya kupigana vita dhidi ya ujinga.

Tunasema ujinga kwa kuwa kutokana na ujinga, watu wengi huzama kuzama katika uasherati na uzinzi na hivyo kuingia katika janga la UKIMWI.

Wakati tukisherehekea Krismasi, tuliwasikia viongozi mbalimbali wa kiroho namna walivyolilia uhai tunaouangamiza kwa vitendo vyetu viovu.

Tuungane nao kuulilia uhai huo usizidi kungamizwa.

Walizungumzia pia suala la UKIMWI na hivyo, tunaamini kuwa tutayafanyia kazi waliyoyasema ili yasiwepo maambukizi zaidi ya UKIMWI katika jamii kwa kipindi tunachokianza.

Tunaamini kuwa mtu mwenye akili, hawezi kudanganywa kwa matumizi ya kondomu ili ajaribu kuchezea maisha yake kwa vitendo vya kipuuzi.

Tunahimizwa kupigana vita dhidi ya ujinga kwa kuwa ni kutokana na ujinga, watu huwapora wenzao uhai wao kwa mfano wazee wanaouawa kwa sababu za tuhuma za uchawi wakiwa na macho mekundu.

Tunasema ujinga kwa sababu ndio huwafanya wale wanaopata mimba kuua watoto ambao ama tayari wamezaliwa au hawajazaliwa. Huo ni unyama.

Kilio cha Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, Mhashamu Daminai Kyaruzi wakati wa Mkesha wa Krismas juu ya uhai, maadili na imani, tulikisikia. Ni vema tuungane naye kukemea na hatimaye kukomesha vitendo hivyo vinavyokwenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Ni dhahiri kama alivyosema kuwa hali hii, inatokana na udhaifu wa imani na mmomonyoko wa maadili. Ni wakati sasa wa kuanza upya na kumgeukia Mungu.

Bado tunasisitiza kuwa Mwaka 2002 uwe wa vita kali dhidi ya ujinga kwa kuwa ujinga ni chanzo cha umaskini.

Bado tunasisitiza kupambana na ujinga kwa sababu ni kutokana na ujinga huo, ndio maana wengi wanadanganywa na kuwa rahisi na kukubali, kujihusisha katika migogoro isiyo na maana ikiwamo vita vya kikabila, migogoro ya kisisasa na hata ile ya kidini.

Umefika wakati wa kuzinduka toka usingizini na kujua kuwa wote tu ndugu moja katika Mungu vita na mauaji hayana maana na wala havitamfikisha yeyote mbele za Mungu.

Tufungue upya maisha kwa kuziacha njia zote zinazotutenganisha na mapenzi ya Mungu na badala yake, tushirikiane kila mtu ili kuyatimiza.

KWA HERI MWAKA 2001, KARIBU MWAKA 2002.

Hatupendi kuona migogoro makanisani

Ndugu Mhariri,

NAOMBA Kulitumia gazeti lako la KIONGOZI kutolea ushauri wangu kwa baadhi ya vongozi wa kiroho ambao wanasababisha na kuendesha migogoro ya kidini katika makanisa.

Ninapenda kutoa kile nina chokijua mimi kuwa makanisani na sehemu nyingine za ibada ni mahala ambapo sisi waamini tunatarajia kwenda kulishwa Neno la Mungu na kunyweshwa Maji ya Uzima.

Ni sehemu tunayotarajia kwenda kufundishwa namna ya kuepuka tamaa, kuepuka ugomvi na namna ya kusaidiana na kuishi katika familia moja iliyojaa upendo wa Kimungu.

Sisi waamini tukiwa kama kondoo tulio chini ya uangalizi wa wachungaji wetu wa kiroho (Viongozi wa dini), tunatarajia kupata angalisho sahihi kutoka kwa walezi hao.

Angalisho na malezi hayo sahihi tunatajrajia yawe ya maneno na matendo sahihi. Hii ndiyo maana tunawatambua viongozi hao kama wazazi wetu wa kiroho.

Inakera na kukwaza inapotokea waamini katika makanisa na madhehebu mbalimbali, tukashuhudia migogoro ndani ya makanisa.

Tunakerwa zaidi tunapoona migogoro hiyo inawashirikisha viongozi na watu muhimu katika malezi ya kimwili na kiroho kwa jamii.

Ukichunguza chanzo, utagundua kuwa baadhi ya viongozi wa kiroho wanavua miito yao na kuiweka kando, wanatawaliwa na tamaa ya madaraka na mali, wanatawaliwa na kasumba ya masengenyo na unyanyasaji kwa wadogo wao.

Kibaya zaidi, baadhi ya viongozi wanahimiza upendo kwa maneno majukwaani huku wao wakionesha matendo ya chuki hadharani.

Sasa hapa waamini wajifunze nini toka kwa viongozi wa namna hiyo?

Ninapenda kuhitimisha barua hii fupi kwa kusisitiza kuwa, viongozi wa aina yoyote ama wa kiroho au kijamii, ni mfano bora wa kuigwa.

Viongozi wa kiroho mjue kuwa kosa mnalolifanya nyie hasa la makusudi, ni sawa kabisa na kuua mamilioni ya roho za watu hivyo tunaomba mtuongoze katika mema na siyo kwa mifano michafu.

Raphael Kimweko,

Makumbusho

S.L.P. 77709

DAR ES SALAAM.

Tumsaidie Makamba wanafunzi wasinyanyaswe

Ndugu Mhariri,

NAOMBA nipate nafasi katika gazeti lako ili na mimi niweze kueleza kile nilicho nacho moyoni kuhusiana na suala la usafiri wa wanafunzi wa jiji la Dar es Salaam.

Kwa kweli hili limekuwa ni tatizo la muda mrefu kwa wanafunzi ukiachilia mbali jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kulitatua.

Pamoja na jitihada hizo, bado Serikali haijafaulu kwa kiwango kinachostahili kwani mpaka sasa ukikutana na mwanafunzi wa jiji hili na ukapata nafasi kumuulizia moja kati ya matatizo makubwa anayokumbana nayo katika maisha yake kama mwanafunzi, hataacha kutaja suala la ugomvi wa kila siku kati yake na wahudumu wa daladala yaani madereva na makondakta.

Katika siku za hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Yusuph Makamba, alionesha kulivalia njunga tatizo hili kwa kujaribu hata kutoka ofisini kwake na kupambana na makondakta wanaowakorofisha wanafunzi.

Napenda kumpongeza Luteni Makamba kwa kazi hiyo aliyoifanya kwani ameamua kuonesha kwa vitendo kuwa wanafunzi ni moja kati ya kundi kubwa na muhimu kwa maendeleo ya taifa la kesho.

Ni kweli kuwa Makamba ameonesha wazi kutambua kwake kuwa mwanafunzi wa leo ndiyo viongozi wa kesho yaani rais, waziri, askari, daktari, mwalimu na afisa yeyote katika taifa la kesho.

Kwa kweli umefika wakati kwa wazazi na wale wasiojaliwa kupata watoto wasaidiane na Mzee Makamba katika kupambana na tatizo hili kwani linatuaibisha wakazi wa Dar es Salaam.

Unyanyasaji wa namna yoyote kwa wanafunmzi unaonesha wazi kuwa wanaofanya hivyo hawakusoma na hawajui maana ya elimu. Na wale wanaofanya hivyo wakijivuna kuwa nao walisoma, wajitambue kuwa wanaonesha wazi kuwa hawakusoma bali walipita shuleni tu.

Ninawashauri Wanadaresalam kuwa, tunapoona wanafunzi wakitendewa visivyo na hawa wahudumu wa daladala, tuwe wakali kwa kuwakaripia na kuwakemea ikiwezekana hata tuutumie muda wetu kuwafikisha watu hawa wakorofi mbele ya sheria ili wakafunzwe ustaarabu.

Ninasisitiza hivyo kwani tukimuachia Makamba peke yake suala hili au ofisi zingine ikiwemo ile ya Leseni za Usafirishaji Dar es Salaam chini ya Bw. David Mwaibula, tatizo hili halitaisha leo wala kesho.

Tukumbuke kwamba umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu bila kusahau kuwa kidole kimoja hakivunji chawa.

Hivyo tuunganishe nguvu zetu kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata elimu katika mazingira matulivu na sio ndani ya dhoruba la usafiri.

Gerome Ladslaus

P.O. Box 2958

Dar es Salaam