Make your own free website on Tripod.com

Wakristo tumieni Kwaresima kuonesha uungawana wenu

UUNGWANA ni hali ya kufanya mambo kama yanavyostahili ikiwa ni pamoja na uwezo wa kuyaelewa mambo mazuri na mabaya na kisha, kuamua kuyafuata yale mazuri na kuepuka kabisa kuyaruhusu mabaya kufanyika.

Uungwana huhusisha pia vitendo vya kusaidiana, kushauriana vema, kusameheana, kuhurumiana,na kupeana upendo wa kimungu; upendo unaozingatia faida ya mwingine.

Uungwana unajidhihirisha wazi hasa mtu anapotenda kosa, akalitambua kosa hilo, akalijutia na kisha kuliombea msamaha akiwa na azimio la kutokusudia kulifanya tena.

Uungwana unazidi kudhihirika pale mtu anapotimiza wajibu wake bila kusubiri kusukumwa wala kusubiri kusimamiwa na wenye madaraka ya juu yake. Labda kwa lugha nyingine, uungwana unaweza kuelezwa kuwa ni pamoja na nidhamu isiyo ya woga.

Kwa kifupi tunasema, daima mtu muungwana huwajibika bila kusukumwa, hutenda haki kwa wenzie kama anavyopenda yeye kutendewa haki, na daima mtu muungwana hutenda mambo sio kwa kuwafurahisha watu duniani, bali kwa kutimiza mapenzi ya Mungu.

Hii ina maana kuwa muungwana haoni sababu ya kuongopa, haoni sababu ya kuiba, kuhujumu, kusaliti, kuudhi, kuua kwa visingizio mbalimbali; wala muungwana haoni sababu ya kukwepa wajibu wake kwa visingizo mbalimbali na pia, muungwana haoni sabubu ya kuwa na wivu na kupiga majungu. Daima mtu muungwana hutumia muda wake mwingi katika kushughulikia mambo yenye faida kwake na kwa watu wengine ikiwa ni pamoja na maombi na sala.

Pamoja na kusema hivyo, tunapenda kukumbuka namna watu walivyokuwa wamefurika katika makanisa mbalimbali ya kikatoliki huku wakiwa wameifungua mioyo yao kwa ajili ya kuuanza Mfungo wa Kwaresima baada ya kupakwa majivu katika Ibada ya Jumatano ya Majivu.

Mfungo huu wa Kwaresima ambao mwaka huu umeanza Jumatano iliyopita( Februari 13), kama ilivyo ada, utadumu kwa siku 40.

Lengo kuu la kila mfungo ni kufanya toba na malipizi kwa sababu ya madhambi ambayo wanadamu wanayatenda. Kimsingi kipindi cha Kwaresima ni wakati maalumu wa kumrudia Mungu kwa kukikiri na kuyatubu makosa yetu.

Katika kipindi hiki, waamini wanaalikwa, pamoja na mambo mengine, kumtafuta Mungu katika Neno lake, katika Sakramenti zake na hasa katika Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu.

Pili, wanahimizwa kufanya matendo ya toba na huruma kwa ajili ya wenzetu. Tunahimizwa pia kujibidisha kwa kuongeza muda wa kusali kwa ibada na kwa nia zaidi na pia, kufunga na kujinyima mambo yasiyo ya lazima katika maisha tukiyatoa kama sadaka.

Kama alivyosema Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi Mhashamu Amedeus Msarikie wakati wa Ibada ya majivu katika Kanisa la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), kipindi hiki ni muhimu kutumika kama mwanzo wa kuendesha ushirikiano na uwajibikaji imara.

Ni wajibu kuanzia sasa kuona kuwa jukumu la mwingine, ni jukumu lako pia. Uungwana hapa utadhihirika kwa mtu kufanya jambo jema bila kutegemea ujira wa fadhila yake. Moyo wa kujitolea unahitajika kuimarishwa zaidi kwa Wakatoliki na Wakristo wengine kuanzia kipindi hiki.

Hata hivyo, licha ya thamani na umuhimu wa kipindi hiki kutambulika kwa upeo mpana namna hiyo, bado wapo baadhi ya watu wasioujua mvema Mfungo wa Kwaresima.

Hao, wanaamini kuwa mfungo kama ulivyo mfungo, ni kujinyima kula na kunywa baadhi ya vyakula na vinywaji huku mambo mengine katika maisha yakiendelea kama ilivyokuwa awali kabla ya kupakwa majivu kwa ajili ya kuuanza mfungo.

Ni vema ikaeleweka bayana kuwa Mfungo wa Kwaresima haulengi kumfunga mtu asile wala kunywa. Kama alivyosema Katibu wa Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padre Andrew Luanda, kung'ang'ania kufunga kula na kunywa pekee matokeo yake ni kukonda na pengine kujisababishia uwezekano wa kifo kitokanacho na madhara ya njaa.

Kwa ufupi kipindi cha Kwaresima hakina budi kuwa mwanzo wa kutubu, kujuta, kujikosoa na kuomba radhi kwa Mungu kutokana na makosa yote ambayo wanadamu tumemtendea.

Kipindi hiki hakipaswi kuwa cha kujionesha machoni pa watu kuwa umefunga . Hii ni sawa na kusafisha glasi kwa nje huku ndani ni chafu.

Ni kipindi cha kukusudia kabisa kutoyarudia tena madhambi yote uliyokuwa ukiyatenda. Hapo ndipo maana halisi ya kufunga na kujinyima inapoanza kudhihirika hasa unapokuwa mwaminifu si machoni pa watu pekee, bali hasa kwa Mungu.

Ni kipindi muafaka cha kuachana na mambo hatari kiroho na kimwili ambayo ni ujambazi, wizi, ulevi, uzururaji, rushwa, zinaa, ukatili, ubakaji, uzembe, utoaji mimba, uchawi, ushirikina, mauaji ya vikongwe, uharibifu wa mazingira, udanganyifu, udini, ugaidi, utapeli, uchu wa madaraka, matumizi ya dawa za kulevya na mifumo ya ubaguzi.

Sasa ni wakati muafaka wa kujenga na kuimarisha tabia ya upendo kwa mwingine kama mwenyewe unavyojipenda. Ni wakati wa kuwasaidia wenye shida bila kuchoka wala kukata tamaa ni wakati wa kujenga na kudumisha ukarimu ili Yesu atakapofufuka wakati wa PASAKA, tufuke pamoja naye kiroho.

Basi, Wakatoliki na Wakristo wote kipindi hiki kitumike kujenga zaidi, kuimarisha na kuuonesha uungwana wetu wafuasi wa YESU KRISTO. uaminifu wa kujinyima yote yanayopingana na Mungu na kuahidi kutoyarudia huku ukidumu katika sala na maombi, ndio maana halisi ya MFUNGO WA KWARESIMA.

Kwaresima hii tufunge kwa nia

Ndugu Mhariri,

Pole sana na kazi napenda kuchukua nafasi hii kutoa yangu maoni machache kwa wakristu wenzangu wote ambao tupo katika mafungo ya Kwaresma.

Tunapoamua kufunga kwa nia kwa kweli Mungu atatusikiliza matatizo yetu na atatusaidia. Kwa wale ambao wanafunga tu ili mradi wasionekane na watu kuwa wao wapo tofauti na wenzao au wanafunga ili kutimiza wajibu tu, kwa kuwa ni sheria mtu afunge tu hapo hujafanya chochote, bali unapoteza tu muda wako.

Ninaposema kufunga si kufunga kabisa kula chakula la hasha, sio lazima kufunga kula ingawa kuna wale ambao wana uwezo wa kufanya hivyo. Hiyo pia si mbaya ila unaweza kufunga kadiri unavyoweza cha maana sana unafunga vile vitu ambavyo unapenda mfano labda umezoea kunywa kilauri kila siku na kiti moto unaamua kuacha kula na badala yake hizo fedha unamsaidia mtu ambaye hana uwezo. Kuna watu ambao wana shida kuliko wewe ingawa sisi binadamu shida hazifanani hata kidogo maana wewe ukiwa una shida hii mwenzako atakuwa na shida kubwa kuliko yako hivyo basi ni vema kabisa katika mwezi huu wa mfungo tujitoe kwa wenzetu kuwasaidia kwa hali na mali bila kujali kuwa huyu ni wa jinsia gani au dini gani. Tukubali kushiriki mateso ya wenzetu kwa hali na mali kwa niaba ya Kristo.

Na pia ni vizuri kuombea amani duniani kwa jumla kuna wenzetu ambao kila siku iendayo kwa Mungu ni vita yaani hakuna hata amani si kama sisi tunaweza kuamka asubuhi na kutembea kadiri unavyotaka wenzetu hata kutoka nje hawathubutu kutokana machafuko ya vita ambavyo mara nyingi vyanzo vyake havina kichwa wala mkia. Mfano mzuri ni hapa Tanzania hivi majuzi tu kumetokea machafuko huko Mwembechai, sasa basi tuombe Mungu hayo machafuko yasiendelee maana kidogokidogo mwishowe kutageuka uwanja wa vita. Hivyo ndugu zangu, katika mfungo huu tumwombe Mungu atuepushie mabalaa yanayoanza kujitokeza.

Nawatakia mafungo mema

Mrs. M. Fertgerald

Dar es Salaam