CHAYODE ilivyo jidhatiti kuelimisha umma kuhusu umiliki ardhi

MIONGONI mwa mambo yanayoonekana kuwa sugu katika jamii, ni suala la kugombea ardhi. Suala hili hutokea ama baina ya nchi na nchi, kabila na kabila, wakulima na wafugaji, na hata kati ya ndugu na ndugu. Katika Makala haya Lilian Timbuka anaeleza zaidi.

HIVI sasa Mahakama mbalimbali nchini zimejaza kesi zinazohusiana na masuala ya migogoro ya ardhi. Mara nyingi kesi hizi zimekuwa baina ya wanafamilia au wana ukoo walioshindwa kupata muafaka wao wenyewe kuhusu eneo wanalokuwa wamedhulumiana au wameingiliana.

Kwa upande wa wafugaji huhitaji eneo kwa ajili ya malisho ya mifugo wao, wakati wakulima huhitaji eneo hilo kwa ajili ya kulima mazao, ama ya chakula, au ya biashara.

Hali hii ikichochewa na mabadiliko ya hali ya hewa, ndiyo kichocheo hasa cha mgogoro wa ardhi baina ya wakulima na wafugaji.

Tukigeukia upande wa mgogoro wa ardhi baina ya nchi na nchi, hii huja baada ya nchi moja kutaka kukalia na hata kuvuka mipaka ya nchi iliyopo na kuingilia eneo la nchi jirani kama alivyowahi kufanya fashisti Idd Amini wakati akiongoza Uganda alipovamia mipaka ya Tanzania, mwaka 1978.

Madhara ya mgogoro huu baina ya  nchi na nchi kugombea mipaka, ni makubwa kwa jamii.

Licha ya kuleta mtafaruku mkubwa miongoni mwa jamii, lakini pia migogoro kama hiyo huwafanya  watu wapoteze uhai, viungo vya miili na kuporomoka kwa uchumi katika jamii.

Migogoro ya ardhi ni suala linalokithiri miongoni mwa wakulima na wafugaji na mfano bora ni wafugaji wa jamii za Kimasai.

Mingine, ni migogoro inayohusisha koo na koo kama ilivyokuwa ikisikika kwa koo za Wanachari na Walenchoka wilayani Tarime.

Migogoro baina ya pande hizi imekuwa mikubwa kiasi cha  kusababisha mauaji ya watuwengi.

 Mikoa iliyoathirika kwa kiasi kikubwa na migogoro ya namna hii ambayo husababisha hata mauaji na wakimbizi wa ndani ya nchi, ni pamoja na Arusha, Morogoro na Mara.

Ugomvi baina ya Walenchoka na Wanchari mkoani Mara ulisababisha vifo na majereha kwa watu wengi. Hili ni jambo lilo bayana kwa Watanzania.

Miongoni mwa matukio ya kugombania ardhi ni lile  lililotokea mkoani Manyara katika wilaya ya Babati (enzi hizo Mkoa wa Arusha), wakati mkoani Mara makabila ya Walyanchori na Walyanchoka waliuana kutokana na kugombea ardhi ambapo ilisababisha zaidi ya vifo vya watu wapatao 35 na watu wengine zaidi ya 80 kupigwa mapanga na kuachiwa majeraha ambayo yamepelekea kuwa na vilema vya maisha na huko  Morogoro katika Wilaya ya Kilosa

Matukio kama hayo yalitokea baina ya wakulima na wafugaji yalisababisha madhara makubwa kwani kijiji kilichokuwa kikaliwa na wakulima zaidi ya 1’500, kiliteketezwa kwa moto.

Mapigano hayo hayakuisha kwa kijiji kuchomwa moto pekee, bali ilifikia wakati wakulima na wafugaji hao wakaanza kuuana kwa kutumia silaha kama vile mapanga, mikuki na sime na yakasababisha vifo vya watu ambao idadi yao kamili haikujlikana.

Hata hivyo, ilidaiwa kuwa takribani 45 walikuwa wameuawa. Japo watu wengine ambao idadi yao haikujulikana walidaiwa kuteketezwa kwa moto ndani ya nyumba zao.

Hivi sasa kuna fukuto lingine la mgogoro wa ardhi linalofukuta katika Kijiji cha Kibwaya kilichopo katika Wilaya ya Morogoro Vijijini.

Familia zipatazo 171 zimedaiwa kutakiwa kuhama katika kijiji hicho kutokana na kile kinachodaiwa kuwa kijiji kimeuzwa kwa raia mmoja mwenye asili ya Kiasia.

 Ardhi hiyo inayogombewa na wakazi hao ina ukubwa wa ekari zipatazo zaidi ya 1,000 ambazo wao wanazitumia kwa ajili ya kilimo na ufugaji.

Tatizo kubwa linakuja kuonekana kuwa ni wananchi walio wengi kutofahamu sheria za umilikaji ardhi japokuwa wapo wataalamu wa suala hilo hapa nchini.

Kutokana na matatizo kuongezeka kila wakati, hivi sasa vikundi na mashirika mbalimbali vimejitokeza kuelimisha umma kuhusu sheria za umilikaji wa ardhi hasa katika mikoa ambayo tatizo hilo imeonekana kushamiri.

Miongoni mwa vikundi hivyo ni Shirika la  Maendeleo kwa Vijana na Watoto  (CHAYODE), ambalo limeanza kutoa elimu ya haki ya umilikaji wa ardhi katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Morogoro.

Mkurugenzi wa CHAYODE, Ramadhani Omari Timu, anasema wakati shirika lake linaanzishwa mwaka 2000,lilikuwa na matarajio ya kuwaendeleza watoto na vijana katika masuala ya elimu, uchumi sanaa na utamaduni”.

“Shirika letu lililenga kushughulikia haki na maendeleo ya mtoto na kuwasaidia vijana katika shughuli zao halali ili kwajiletee maendeleo,” alisema.

Akaongeza kuwa, lengo lingine lilikuwa kuwaunganisha na kujenga ushirikiano miongoni mwa watoto na vijana wa Tanzania na sehemu nyingine duniani ili kuendeleza utamaduni wa Mtanzania.

Anasema shirika hilo pia limekuwa likiendesha shughuli za uhamasishaji kwa vijana kuanzisha vikundi vya uzalisahji mali kulingana na nafasi zao kama wakulima, wafanyabiashara na wasanii ili wajikomboe kiuchumi.

“Tumekuwa na shughuli nyingi ambazo tunazifanya kama vile kuandaa na kuendesha mafunzo kwa vijana juu ya shughuli wazifanyazo ili kuboresha na kuimarisha ujuzi wao na pia, tunafanya utafiti wa masuala ya kielimu, kiutamaduni, kiuchumi na kijamii unaoweza kuwasaidia watoto na vijana kuboresha maisha yao.”

Alisema katika kutimiza malengo yake, Shirika hilo la CHAYODE liliweza kubaini  matatizo ya ardhi yanayowaathiri sana watoto na vijana hasa wale wa vijijini ambao wanapohitimu masomo yao ya msingi au sekondari, hutegemea kilimo.

“Tumeona kuwa mtoto akikua anahitaji kumiliki ardhi, na pia hata vijana wanaohitimu masomo ya msingi au sekondari vijijini huhitaji kutumia ardhi katika shughuli za maendeleo,”anasema.

Anasema tatizo kubwa kwa makundi hayo lilikuwa katika suala la  kujua sheria ya kumiliki ardhi kwani wengi wamezoea kuwa alipokuwa analima baba yake, naye atalima hapo, yaani anarithi ardhi sasa inapotokea uvamizi matokeo yake huwa ni mapigano yanayoonekana siku hizi.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, watu wanaotetea haki za watoto na vijana wameona umuhimu wa kutoa elimu ya haki ya msingi ya kumiliki ardhi kwa wananchi na wameanzia na Mkoa wa Morogoro.

Anasema Shirika hilo la CHAYODE lilianzia kutoa elimu ya haki ya ardhi katika Wilaya ya Kilombero, Morogoro ambapo alisema  mafunzo yanatolewa kwa viongozi wa vikundi vya sanaa ambao watavifundisha vikundi vyao huko vijijini.

“Tumeendesha mafunzo ya haki ya ardhi kwa viongozi wa vikundi mbalimbali vya sanaa ili wakayatumie katika vikundi vyao, kuwaelimisha wananchi wa maeneo yao,” anasema kiongozi huyo.

Alisema wanatumia zaidi sanaa katika shughuli zao kutokana na ukweli kwamba hiyo ni njia rahisi ya kufikisha ujumbe kwa wanajamii.

Timu alisema mafunzo hayo ya haki ya ardhi yalifanyika katika Tarafa ya Mang’ula katika Wilaya ya Kilombelo ambapo mara baada ya mafunzo hayo, wananchi walipata nafasi ya kuona michezo ya kuigiza inayoonesha migogoro ya ardhi na wao waliweza kutoa maoni yao juu ya utatuzi wa migogoro hiyo.

Mafunzo hayo yalilenga hasa katika utamaduni na sanaa, sanaa kwa maendeleo, uongozi wa vikundi vya sanaa, wanawake na maendeleo ya vijana na wanawake, sheria ya ardhi namba 4 na 5 ya mwaka 1999.

Vatican yachambua Mkutano wa Maendeleo Endelevu (2)

Na Mwandishi Wetu

 

Inatoka Toleo Lililopita

Umaskini wa kupindukia unachochea ukiukaji wa haki za binadamu ulimwenguni. Katika kwenda sambamba na kanuni ya uziada, maskini ni lazima wasikilizwe juu ya masuala mbalimbali na wawe ni kiini cha mipango mahali walipo, kitaifa na kimataifa kwa ajili ya maendeleo endelevu. Watu wanaoishi katika umaskini lazima wachukuliwe kama washiriki watendaji. Watu hawawezi kuwa vyombo lakini ni lazima wawe wahusika wakuu wa maisha yao ya baadaye, wenye uwezo wa kuwa “wakala wa maendeleo yao wenyewe” na “katika hali maalumu za kiuchumi na kisiasa, kufanya ubunifu ambao ni tabia ya binadamu na ambayo juu yake utajiri wa mataifa unategemea.” Juhudi yoyote inayochangia katika maendeleo ya watu inatakiwa kushughulikia mahitaji ya mtu kiroho na kimwili.

Moja ya vitu muhimu kwa uwepo wa mwanadamu ni maji. Leo idadi kubwa ya watu wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji na ukosefu wa huduma za usafi. Wajibu wa msingi wa kuweka usawa na matumizi endelevu, utunzaji na usimamizi wa rasilimali za maji uko mikononi mwa serikali.

Katika mapambano ili kuondoa umaskini, maji hutimiza dhima muhimu si tu kuhusiana na afya lakini pia kama nyenzo muhimu kwa uzalishaji. Maazimio ya mkutano huu wa Dunia lazima yashughulikie changamoto hii ya upatikanaji wa rasilimali hii itoayo uhai kwani ikiachwa bila kushughulikiwa, kifo ndio kitakuwa matokeo kwa wale wasioweza kupata maji.

Kipaumbele kikubwa kingine katika maendeleo endelevu ni maendeleo vijijini. Maeneo ya vijijini yanabeba zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote ulimwenguni na watu maskini wanaoishi katika maeneo haya mara nyingi hukosa huduma za msingi za jamii.

Kuendelea kukua kwa miji siku hizi mara kadhaa kumekuwa ni sababu kwa watu wanaoishi vijijini kusahauliwa. Lakini kwa hakika ni kiwango kikubwa cha umaskini katika maeneo ya vijijini kilichochangia kiasi kikubwa kwa watu kuhama kutoka vijijini kwenda mijini.

Tukichunguza sana kanuni ya uziada, utawala bora ni moja ya vitu muhimu katika vita dhidi ya umaskini. Utawala bora unapaswa kuwa kwa faida ya pamoja. Ili utawala bora ufanikiwe lazima kuwepo na ushirika mpya unaoendeleza uwekezaji katika watu na katika miundombinu na hiyo itawezesha ushiriki wa wananchi katika maamuzi yanayohusu maisha yao. Ukithaminishwa katika mazingira haya, mfumo wa kidemokrasi kadiri unavyopigana kuhakikisha unakuwepo uwezekano wa ushiriki wa wananchi katika kufanya uchaguzi wa kisiasa na kuwa na sauti katika utawala.Huu ni mchakato unaoitwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili bila kuegemea upande wowote wa jamii ambao umejikita katika uumbaji wa miundo ya ushiriki na wajibu shiriki, yote mawili ni muhimu kwa utawala bora.

Utawala unaweza kuitwa mzuri iwapo matarajio ya binadamu yanashughulikiwa kuelekea kwenye ushiriki wenye ubunifu katika serikali na katika jamii. Katika mazingira ya jumuiya ya kimataifa, utawala bora huhitaji kwamba mataifa yote yakiwemo masikini na madogo sana, kufikia utoaji maamuzi katika vyombo ambavyo huamua sera na kukuza ushirikiano wa kimataifa, na sio taifa moja kujichukulia uamuzi.

Itaendelea toleo lijalo

Lijue Shirika la Kipapa la Misioni  (PMS)

l Ni muunganiko wa mashirika manne

MARA nyingi watu mbalimbali wakiwemo waamini wa Kanisa Katoliki na wale wenye mapenzi mema, wamekuwa wakisikia ama kusoma kwenye vyombo mbalimbali vya habari juu ya Shirika la Kipapa la Misioni (PMS). Ili ufahamu kwa undaji juu ya Shirika hili,ungana na Leocardia Moswery,SAUT, katika makala yake.

 KATIKA kuhamasisha na kuelimisha waamini duniani kote ili washiriki kazi na shughuli za Misioni kwa sala, sadaka na michango ya mali na fedha, Uongozi wa Kanisa Katoliki Duniani ulianzisha Shirika la Kipapa la Misionn (PMS).

Shirika hili linaloongozwa na Baba Mtakatifu na Maaskofu, lina jumuisha matawi manne  ambayo lengo lake ni  kuhamasisha kila  Mkristo kutambua kuwa ni  mmisionari, mhubiri wa Habari Njema kwa wengine kwa kadiri ya nguvu na uwezo wake, kwa kadiri ya wito na vipaji vyake.

Mashirika hayo ni pamoja na Shirika la Uenezaji Injili (Propagation of Faith), Shirika la Kimisionari la  Utoto wa Yesu (Missionary Childhood), Shirika la Mtakatifu Petro Mtume (St. Peter the Apostle) na Shirika la Umoja wa Wamisionari (Missionary Union).

 

 Shirika la Uenezaji Injili (Propagation of Faith)

 

Shirika hili lilianzishwa na msichana mmoja, Maria Paulina Jaricot.

Tangu utoto wake,Maria ambaye alizaliwa Julai 22 ,1799 katika sehemu ya  Lyons, Ufaransa, alipata mafunzo ya imani katika shule za Kanisa Katoliki.

Kabla ya kuanza kupata mafunzo hayo ya imani,Maria  baada ya kumaliza shule akiwa na umri wa miaka 14 alianza maisha ya anasa, ya kujipamba kwa mavazi kulingana  na mitindo ya wakati ule.

Alikuwa na kipindi kifupi cha uchumba, baadaye alipatwa na ugonjwa na katika mahangaiko yake hayo, mama yake akafa mnamo mwaka 1816.

Tangu wakati huo Maria  aliamua kutoa maisha yake kwa Mungu akaamua kufunga nadhiri ya usafi wa moyo, na akanza kuvaa mavazi kama ya wafanyakazi maskini.

Pia, aliamua kwenda kufanya kazi hospitalini ili kuwasaidia na kuuguza wagonjwa maskini waliokuwa hawajiwezi kabisa.

Kwa kuitikia  mwito wa kaka yake aitwaye Phileas, aliyekuwa Mmisionari kuhusu  mahitaji na matatizo ya Wamisionari, Maria alikusanya wasichana wafanyakazi wa viwanda vya mji wa Lyons  katika jumuiya ya sala, wakajitolea kwa hali na mali kutegemeza misioni.

Paulina alitambua wazo hilo na ghafla mwaka 1819, alipata wazo na mwanga wa kuunda vikundi vya watu kumi, ambao watakuwa 100 na baadaye 1000 na kila kikundi na kiongozi wake.

Kila mwanachama atakuwa na wajibu wa kusali kila siku na kutoa mchango wa kila juma kwa misioni.

Shirika la Paris la Wamisioni lilipokea wazo la Paulina na yeye alipatwa na matatizo na upinzani mwingi na akaamua kujitenga na hata shirika lilipoanzaishwa rasmi Mei 3, 1822, jina lake halikutajwa.

Paulina hakukata tamaa alianzisha vikundi vya sala na vya kitume ambavyo ni pamoja na LORETO (Shirika la Watawa kwa Misioni), Maisha ya Rozari kwa kuombea Misioni, na hata Maktaba kwa Walei ili wafahamu habari za Kanisa na za Misioni.

Vile vile, alinzisha hata  benki kwa ajili ya wafanyakazi wa Lyons. Lakini juhudi zake hazikuleta mafanikio  kwa vile benki ilifilisika na Paulina alipoteza mali zake zote, akawa maskini na 1862 akiwa na umri (63) alikufa.

Zipo hatua za kumtaja Mtakatifu kwani hatua ya kumtaja ‘Mwenyeheri’ imekamilika.

Shirika la Kimisionari la  Utoto wa Yesu (Missionary Childhood)

Shirika hili  ambalo lengo lake kuu ni kufundisha watoto imani, kulinda na kutetea haki za watoto na kutoa misaada kwa watoto wanaoteseka, lilianzishwa Mei 9, 1843 na Askofu Charles de Forbin Janson, ambaye alipata elimu safi  ya Kanisa Katoliki.

Baada ya kumaliza masomo yake, Charles ambaye alizaliwa  Novemba 3, 1785, nchini Ufaransa katika familia tajiri, alipewa kazi na Serikali ya Ufaransa kujifunza kuwa Balozi katika  nchi yake.

Macho yake yaliona mateso ya Kanisa la Ufaransa ambapo  makanisa pamoja na nyumba za Watawa ziligeuzwa kuwa mapokeo ya kale na watoto wengi walikuwa hawajui  tena imani ya dini yao.

Baada ya kuona hivyo, alimua kuwa Padre na kumtaka dereva wake ampeleke katika Seminari ya Mtakatifu  Sulpice kitu ambacho kiliwashangaza watu wote.

Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 23.

Wakati akiwa Seminari, Charles alipenda kujifunza habari za misioni na akaanza kuwafikiria mamilioni ya watoto duniani ambao  hawakuwa na mtu wa kuwafundisha habari za Mungu.

Akiwa na umri wa miaka 38, Charles aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Nancy na akaonesha uhodari wake katika kufundisha watu dini.

Askofu Charles alitoka  China kama mmisionari, lakini Baba Mtakatifu alimwambia anahitajika zaidi Ufaransa ili kujenga upya imani huko.

Mwaka 1839, wimbi la watu wenye kuwachukia maklero likavamia nchini kote Ufaransa.

Askofu Charles akafukuzwa kutoka jimboni kwake na kukimbilia mafichoni. Akiwa mafichoni aliweza kutembelea eneo la Amerika na Canada akihubiri bila kupumzika.

Aliporundi Ufaransa, Askofu Charles, alifanikiwa kukutana na Paulina Maria Jaricot  Mwanzilishi wa Shirika la Uenezaji Injili Duniani.

Kukutana kwake na Paulina, kulimfanya Askofu Charles aone umuhimu wa kuhamasisha watoto wa Urafansa ili wasaidie kazi za Misioni kwa sala zao na kwa michango yao ya fedha.

Askofu Charles alitambua kuwa, hayupo tena mwenyewe katika kufikisha Injili kwa watoto, bali yupo pamoja na jeshi kubwa la watoto wamisionari.

Shirika hili la Kimisionari la Utoto wa Yesu linafanya kazi zake duniani kote kupitia kwa Maaskofu, mapadre, watawa, wamisionari wakiwasaidia watoto wanao teseka,  maskini,  wasio na makazi, wagonjwa, waliotupwa ili watoto wote wajisikie wanapendwa na Mungu.

 Shirika la Mtakatifu Petro Mtume (St. Peter the Apoltle) Hili ni Shirika linalojishughulisha na elimu ya waseminaristi, manovisi, mapadre na watawa ambalo mara nyingi huboresha elimu na malezi yao.

Mwanzilishi wa Shirika hili ni binti mmoja wa Kifaransa, Jean Bigard aliyezaliwa Desemba 2, 1859.

Akiwa na umri wa miaka 19, alimua kuacha anasa za kidunia na ubatili wake na kujitoa kikamilifu kwa kazi ya Mungu.  Jean na Mama yake Stephanie walianza kuchangia mfuko wa kuwasaidia mapadre wazalendo wa nchi za misioni kwa ajili ya masomo na mahitaji yao ya kila siku.

Waliomba misaada kutoka nyumba hadi nyumba, wakaomba na sala zao wakaandika maandishi kuelezea uhitaji mkubwa wa seminari katika nchi kama Japan.

Pia, Jean alitoa urithi wake kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa jipya Ujapani lililopewa jina la Mtakatifu Fransis Xavieri.

Ijapokuwa kazi ya Jean ilithaminiwa na Maaskofu wa nchi za Misioni, Maaskofu wa nchi ya Ufaransa hawakupenda kusaidia.

Ni baada ya miaka mingi ya mapambano, ndipo Maaskofu wa Ufaransa walipokea Shirika lake la Mtakatifu Petro Mtume  (mwaka 1886).

Mpaka mwaka 1903 alipofariki mama yake Jeann Mama Stephinie Bigard, tayari walikuwa wamekusanya kiasi kikubwa cha fedha kwa kuwaelimisha mapadre wa misioni.

Baada ya kifo cha Stephinie, Jean alishindwa kuendeleza shirika na akaamua kulikabidhi kwa wamisionari Wafransiskani.

Baada ya hapo, Jeann alijiunga na nyumba ya watawa.

 Shirika la Umoja wa Wamisionari (Missionary Union) Lilianzishwa mwaka 1916 na Padre Paulo Manna, kwa kuwaunganisha mapadre pamoja.

  Shirika hili  ambalo kibali chake kilitolewa na Baba Mtakatifu Benedikti wa 15, lina malengo ya kuwaunganisha mapadre, watawa na walei katika kusali pamoja na ndugu na dada zao wenye kufanya kazi za misioni.

Pia, shirika hili ni moyo wa mashirika mengine kwa vile linachochea roho ya umisionari na kutoa elimu ya misioni kwa mapadre, watawa, waseminaristi, manovisi na walei ambao wanahusika katika kuhamasisha na kupandikiza roho ya umisionari katika Taifa la Mungu.

UCHAMBUZI WA KITABU

Tamthilia na Ulimwengu Ulivyo Sasa (2)

Kitabu:            MORANI.

Mwandishi:     Emmanuel Mbogo.

Mhakiki:        

Projest M. Christopher

 

Inatoka Toleo lililopita

 

Nungu na Mlemeta ambao tayari tumekwisha elezwa kuwa ni kupe na mkia wa ng’ombe na kazi ya kupe ni kunyonya kile asichopanda ili mradi yeye ashibishe tumbo lake. Watu hawa wanawapa watu wakati na hali ngumu.

Pesa ndogo wanayoipata haifai kitu kwani bidhaa zote ni bei mbaya.  Huu wala sio utani hata kidogo, uhalisi upo katika jamii zetu na ndio maana Mwandishi suala hili likamshughulisha ipasavyo. Tumeshuhudia Tanzania ikipanga  kununua ndege ya Rais na pia rada ya nchi kwa ajili ya usalama.

Serikali ina nia njema, lakini ifikirie ni mamilioni mangapi yatakayotolewa kugharamia vyombo hivyo huku wakulima wakilia na bei ndogo ya kahawa kwa shilingi 40/- kwa kilo na wakati uti wa mgongo wa taifa ni kilimo.

Kila siku wimbi la ujambazi linaongezeka hata mpaka vyombo vya dola vimeshukiwa kufanya hujuma hizo, sababu kubwa ni utawala usio mbadala: mazao hayana soko, ajira hamna, bidhaa bei ghali, kodi inadaiwa, tumbo linadai unategemea mtu atafanya nini? Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni matajiri kwa mali asili aliyowapa Mungu lakini utajiri huu umeishia mikononi mwa wachache. Je hali hii haioti mizizi hapa kwetu?

 

Rushwa:

 

Pamoja na kufanya magendo kunyonya jasho la wenzao na kuhujumu uchumi, bado rushwa imekithiri na kuonekana kuwa silaha ya wakubwa dhidi ya wanyonge. Mlemeta na Yusufu wanapinga kuliweka jina la Nungu katika orodha ya wahujumu uchumi kwa sababu wamepewa ruhusa kama anavyosema Jalia:

“Mlemeta kama wewe umenunuliwa sio mimi” (Uk. 13). Jaji anahukumu visivyo  kwa maana amepewa rushwa isingekuwa hivyo, basi Jaji yule angeweka wazi uovu wa Nungu. Badala yake, kibao kinageukia makabwela kuwa ndio wahujumu.

Msanii anasema: “... Mhujumu uchumi mkubwa! Eti kukutwa nyumbani kwake na tenga mbili za kisamvu na dawa tatu za kolgeti” (Uk. 35).

Hii imetupa picha halisi kuwa ukandamizaji ni nyenzo ya wakubwa kwa Makabwela. Hakimu hakuona walaolundika fedha ughaibuni, wenye hoteli Marekani, wanaovusha karafuu, kahawa na tanzanite kwa magendo, badala yake kaona wenye tenga mbili za kisamvu!

Hili ndilo tatizo linalozifanya nchi zetu zishindwe kuendelea na kusababisha vita kwani  daima rushwa ni adui wa haki. Na haki isipokuwepo ndipo mtutu hushikwa ili kuitafuta kwani haki haipatikani ila kwa ncha ya upanga.

Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sierra Leone na Madagascar vita inapiganwa kwa sababu kuna upande mmoja usioutendea haki upande mwingine.

Hapa Tanzania tumeona baadhi ya viongozi wala rushwa wakitiwa nguvuni, lakini wengine wakihamishwa idara badala  ya kutiwa nguvuni. Maskini Makatibu Kata na viongozi wa mitaa ndio wanaotiwa nguvuni wala sio wale vigogo. Kamati na tume mbali mbali za kuchunguza wala rushwa zimeundwa, lakini jibu mpaka sasa tunalisubiri wakati muda unayoyoma.

 

Usaliti:

 

Dhana hii pia ni kikwazo cha maendeleo. Mlemeta na Yusufu walipewa kazi ya kuwa Wanakamati, Kamati ya kubaini wahujumu uchumi, wanamsaliti Jalia na jamii kwa jumla uliyowapa shughuli hii kwa kuwaamini.

Mlemeta anamtamkia waziwazi Dongo kuwa: “Unaweza kumkamata Mzee, lakini mimi sikubaliani na wewe” (UK.12). Pia, usaliti ni ule wa Nungu kwa Aisha. Nungu alistarehe na Aisha mpaka usiku wa manane pale Night Club Bar huku akijua dhahiri kuwa ni mwanafunzi na bado yu mikononi mwa wazazi.

Kukosa kwake siku nyingi shuleni kunamfanya afukuzwe shuleni na pia nyumbani. Anapokuja nyumbani kwa Nungu na kumweleza hayo, Nungu anasema: “Kakufukuzia kwangu ?… Mpumbavu mkubwa…!” (Uk. 26).

Sakata hili haliishii hapo, hatimaye wanaachana: “Vipi mzungu wako? Alinishagaza na mie nikamshiti” (Uk.32). Chanzo cha kufukuzwa kwa Aisha ni Nungunungu, lakini anakataa kupokea matokeo ya starehe yao. Kabla hajafukuzwa, walikuwa chanda na pete.

“Indiketa” kwa wanafunzi na vigogo naziwasha! Enyi wanafunzi nani kawafundisha tabia hii hamwoni kuwa mnawasaliti wazazi wenu? Enyi vigogo, viongozi na wengine waacheni wanafunzi wasome ushawishi wenu wa fedha, lifti na madoido mengine uwe kikomo. 

Ukweli ni kwamba katika jamii yetu, usaliti upo hasa kuanzia mtu na mtu mpaka mtu na kikundi cha watu. Viongozi waliopewa dhamana na wananchi ya kuwakilisha mawazo na matatizo ya serikalini, Unashindwa kuwa karibu na waliokutuma, shida zinazowakabili utazijua vipi?

 

Ujasiri:

 

Pamoja na njaa, kiu na hali mbaya ya msituni, Mzee, Malongo na Mzee Mapoto wanaendelea na safari yao ya kulitafuta Dongo na nguzo ya Uswezi pia.

Jalia mwanamke wa pekee anayetisha asiyeogopa kitisho chochote, anakabiliana na Yusufu na Nungu pale wanapoleta matata.

“...Jalia ananikata mtama mimi!” (Uk 14). “Nitakuua” (Uk. 38). Jalia alimkata ngwala Yusufu alipojaribu kupambana naye. Pia, alimpiga Nungu pindi walipokutana mlangoni pale Sunlight Bar ambapo inawezekana Nungu alipoteza maisha.

Hapa sio kweli kuwa uhalisia haupo, upo ila kwa kiasi kidogo  kwani katika jamii yetu ni wanawake wachache wawezao kuwa kama Jalia na Hadikwa.

Kila kazi ya fasihi ina manufaa kwa jamii ikitegemea jinsi msanii alivyoiweka wazi na kuwafunua macho hadhira juu ya lile linalijiri katika jamii yao. Ndio maana msanii ni zao la jamii na ni mwanajamii na huiandikia jamii yake.

Mtazamo wa Kikatoliki kuhusu namba za Biblia(2)

Inatoka Toleo lililopita

Namba saba:  Kibiblia namba hii ina maana zifuatazo:

i.Utilimilifu au Ukamilifu

ii. Jumla ya 3 jumlisha 4

iii. Utimilifu unaoongoza mtiririko wa muda:

- Wiku moja ni siku saba

Wiki moja na siku saba; Mwaka wa Jubilei ni (7X7) + 1= 50.

Maana nyingine ni Mashemasi saba walioteuliwa ili kugawa huduma (mahitaji) ya kila siku – (Matendo 6:5); Mwinjili Mathayo anaipendelea sana namba saba katika Injili yake; Kitabu cha Ufunuo wa Yohane kinaitaja na kuirudia sana namba hii saba.

 

Namba Nane (8): Kibiblia namba hii inadokeza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na Uhai au maisha mapya:  Rejea wale watu wanane waliobakia na kukombolewa kwenye safina ya Nuhu.

Pia, inadokeza Siku ya nane baada ya mtoto kuzaliwa ni siku ya kutahiriwa- hivyo ni uhai mpya, maisha mapya, mwanzo mpya na pia, Daudi alikuwa ni mtoto wa nane wa Yesse.

 

Namba Kumi (10): Kibiblia namba hii inadokeza mintarafu Ujazo au utimilifu tele, ukamilifu rejea vidole vyote vya mikono miwili ya mwanadamu; Amri Kumi za Mungu; Mababu wa Israeli kabla ya ile Gharika Kuu pamoja na Pembe kumi za yule mnyama aliyeonekana na Dani.

Namba Kumi na Mbili (12): Kibiblia namba hii ni muhimu sana kwani inaelezea Miezi kumi na miwili ya mwaka; Taifa la Waisraeli (Wayahudi) lilikuwa na makabila kumi na mawili, Ufunuo 7:5-8 na kwamba Yesu alichagua mitume kumi na wawili

Inadokeza pia kuwa, Yerusalemu Mpya imejengwa katika misingi kumi na miwili na ina milango kumi na miwili; Nyota kumi na mbili katika kile kilemba cha mwanamke, katika Kitabu cha Ufunuo. Rejea Ufunuio 12:13 na 14. Hivyo, 12 x 12= 144 – waliokombolewa duniani na Wafuasi 72 waliotumwa na Yesu 12x 6.

 

Namba Arobaini (40): Kibiblia namba hii ina maana muhimu sana na inatumika mara kadhaa:

Waisraeli waliihusisha na kukadiria miaka 40 kama kizazi kimoja kutokana na mang’amuzi yao. Ni dhahiri kuwa wapo baadhi ya Waisraeli walioweza kufikia miaka sabini au themanini. Hata hivyo, kutokana na lishe au tabia duni, wengi walifikia miaka 40 hasa wakati wa kipindi cha Musa.

Pia, Nuhu alikaa katika safina kwa siku 40; Namba hii 40 inahusishwa na kipindi cha taabu, dhiki, majonzi, kasheshe, adhabu, simanzi, misiba, toba, mateso, shida na toba kwa Waisraeli: Mfano, Gharika Kuu ilidumu kwa siku 40; Waisraeli walikaa na kutangatanga jangwani kwa miaka 40; Musa alikaa mlimani Sinai kwa siku 40; Eliya alitumia siku 40 kufikia Mlima Sinai na Watu wa Ninawi walipewa siku 40 watubu.

Mfano mwingine ni ule wa Yesu kukaa jangwani kwa siku 40 akifunga na kusali; na Kristo Mfufuka alikaa kwa siku 40 kabla ya kupaa mbinguni. Hivyo, zipo siku 40 kati ya Pasaka na Kupaa.

 

Namba Hamsini (50): Kibiblia hii ni namba inayoelezea: Furaha: Siku 50 baada ya kuvuna mashambani ni kipindi cha furaha, shangwe na nderemo.

Shukrani: Mwaka wa 50 yaani (7x7)+1 ni mwaka wa kutoa shukrani kwa Mungu.

Pentekoste- Siku 50 baada ya ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo- Mavuno ya Ukristo.

 

Namba sabini (70): Kibiblia namba hii inadokeza:-

Utimilifu, ujazo- usiopimika wala kufahamika na akili ya mtu wa kawaida (10x7) kadiri ya Wayahudi.

Ukamilifu: Waana wa Israeli wanawakilishwa mbele ya Mungu na Wazee 70. Pia, Kadiri ya Biblia, dunia ilikuwa na watu 70 wengi ajabu- kadiri ya utambuzi wa kiwango cha hesabu za Kiyahudi.

Pia, Wana wa Yakobo (Israeli) walioingia Misri walikuwa 70; Miaka 70 inachukuliwa na Mwandishi wa Zaburi kama muda tosha na mrefu wa binadamu kuishi hapa duniani na Yesu anawataka wafuasi wake wasamehe 7x70 yaani bila mwisho bila kikomo:

Wazazi kulea leo,ni kulelewa kesho

l Watoto wasipozingatiwa, hatma ya Tanzania ya kesho itakuwaje?

l Askofu Mkuu: Kuvunjika kwa ndoa na Umasikini, ni chanzo cha tatizo

Na John Pinini, Tabora

“Hatupendi na tunaona uchungu sana kuwaona watoto hao wazuri wakiendelea kusumbuka mitaani kwa kuishi maisha ya hatari katika mabehewa ya treni, vibaraza vya maduka na sehemu zingine ambazo zinahatarisha maisha yao, tunasikia uchungu kwa kuishi maisha hayo ndiyo sababu Shirika letu limeanzisha kutuo hiki ili wapate msaada wa malezi,” anasema Mkurugenzi wa Kituo cha  St. Fransis de Sale (S.F.S.) Children’s Home.

Anaongeza, “Tunawakuta wakiwa katika hali mbaya wengine wakiwa nusu uchi, wanaombaomba na kuokota chakula katika mapipa ya takataka, miili yao ikiwa imejaa upele na vidonda, hawaogi wala hawapigi mswaki, hawapati chakula cha kutosha wala matibabu, wanahisi kutengwa na jamii, imepelekea watoto wengi kuingia mitaani kujitafutia mahitaji yao wangali wadogo na hivyo kuishia kuwa ombaomba.

S.F.S. Children’s Home ni Kituo cha kulelea watoto wa mitaani kilichopo katika Kata ya Ipuli mjini Tabora. Kituo hiki kimefungua ukurasa mpya wa maisha ya watoto hao baada ya kuzinduliwa rasmi na hivyo, kuwawezesha kuwa na uhakika wa kupata huduma muhimu kama malazi, chakula, elimu na afya.

Kituo hicho kilichoanzishwa kwa madhumuni ya kuwasaidia watoto wasio na makazi maalumu mjini Tabora,  kilizinduliwa rasmi mwezi Agosti mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Abbas Kandoro.

Kimekuwa mfano kwa jamii hususan mji huo katika suala ziama la kuwapenda na kuwathamini watoto wa mitaani.

Kituo hiki kimeanzishwa na Wamisionari wa Shirika la Mtakatifu Francis wa  Sale, lililopo mjini humo.

 Lengo la Kituo hicho ni kuwasaidia watoto wa mitaani  ili waishi kwa furaha kama watoto wengine  wanaoishi katika familia zao.

Alisema watoto hao pia wanahitaji malezi bora bila ubaguzi ili waandaliwe kuwa raia wema wa baadaye watakaolitumikia vema Kanisa na Taifa. “Hivyo, kuna haja ya kuwasaidia ili wakue na kuvitumia vipaji walivyopewa na Mungu,” alisema.

Kuendelea kuwaacha watoto hao bila kuwasaidia ni kuandaa tabaka la vijana watakao kuwa chanzo cha vitendo viovu kama ujambazi, uvutaji bangi, watumiaji wa dawa za kulevya, wabakaji, wakabaji na hata watakaoshiriki vitendo vingine viovu vinavyoiletea aibu jamii ya kitanzania.

Anasema kwa sasa kituo hicho kina watoto 48 kati yao, wasichana ni 16 na wavulana ni 32 ambao wengi wao wana umri wa kati ya miaka 5 hadi 15.

Kituo kinawapa huduma hizo muhimu kwa kuamini kuwa, watoto wakisaidiwa wataonesha na hata kuviendeleza vipaji vyao mbalimbali vitakavyo lililetea faida Taifa, ameongeza.

Padre Kurian, Mkurugenzi wa Kituo hicho anasema kuwa, katika kuwaandalia mazingira bora ya kielimu, kituo hicho kinatoa mafunzo ya kusoma na kuandika kwa watoto ambao hawajui kusoma kabla ya kuwapeleka katika shule mbalimbali za msingi.

Aidha, ameongeza kuwa kituo hicho kina mpango wa kuwaendeleza zaidi kielimu watoto hao kwa kuwapeleka katika vyuo vya ufundi stadi na hata kwa wale watakaobahatika kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

Akizungumzia huduma ya afya, Mkurugenzi huyo ambaye pia ni Padre wa Shirika la Mtakatifu Francis wa Sale, anasema kwamba Kituo kiko makini juu ya afya za watoto hao na kwamba huwapatia matibabu katika hospitali maalumu ya Ipuli kila inapohitajika.

Anasema kwa  kuwapa huduma bila ubaguzi na kwa kuzingatia upendo, wamekuwa wakipata taarifa zaidi za watoto wanaohitaji kusaidiwa na kuwafikia.

“Idadi ya watoto hao katika mji wa Tabora imekuwa kubwa na inayoongezeka kwa kasi kutokana na kukosekana kwa ushirikiano wa malezi katika jamii au familia zao…Hii ndiyo inawafanya watoto watoroke nyumbani kwao”.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusu tatizo la watoto wa mitaani katika mji wa Tabora, baadhi ya wakazi wa mji huo wamesema kuwa umaskini, ulevi wa kupindukia, uzazi usio wa mpango na UKIMWI ni kati ya sababu zinazochangia kuongezeka kwa watoto wa mitaani.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw. Abbas Kandoro, anasema umaskini umechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa watoto wa mitaani katika mji huo na nchini kote kwa jumla.

Amesema hali hiyo ya umaskini imesababisha watoto wengi kukimbia familia zao na kuingia mitaani kwa lengo la kupata unafuu wa maisha.

“Iwapo familia zitafanikiwa kuupiga vita umaskini, tatizo la watoto wa mitaani litapungua maana sasa watatulia katika familia zao kwani wana uhakika wa kupata mahitaji muhimu,” alisema.

Naye Mkazi wa Kata ya Gongoni mjini humo, Bw. Alfred Mallugu, anasema ulevi wa kupindukia na uzazi usio na mpango ni kati ya  sababu ambazo zinachangia katika kuwepo kwa watoto wa mitaani mjini Tabora.

Amesema tabia ya baadhi ya wazazi ya kubobea katika ulevi na kusahau majukumu yao katika familia, ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya tatizo la watoto wa mitaani.

Hata hivyo, Padre Kurian, anasema uzoefu umeonesha kuwa, wengi wa watoto hao wanatoka katika mikoa ya jirani ya Kigoma, Shinyanga na Dodoma ambao huingia katika mji huo kwa njia ya reli.

Analitaja kundi lingine kuwa ni la watoto wanotoka katika wilaya jirani na mji huo yaani Nzega, Urambo na Sikonge.

Anasema watoto hao hukimbilia katika mji huo ambao ni makutano ya njia ya reli kutoka katika mikoa hiyo kwa lengo la kutafuta kazi ndogondogo, na pindi wanapokosa kazi hizo, ndipo huanza kuzurura mitaani kujitafutia riziki.

Aidha, amesema kuwa kituo hicho kitaendelea kuelekeza nguvu zake katika kuwasaidia watoto hao ili kuisaidia Serikali katika kupambana na tatizo la watoto wa mitaani.

“Serikali pekee haiwezi kumaliza tatizo hilo la watoto wa mitaani, inahitaji kusaidiwa na taasisi (asasi) mbalimbali ili kuokoa maisha ya watoto hawa”, amesisitiza.

Anaongeza kuwa, endapo jamii nzima itaelewa umuhimu wa kuwasaidia watoto wa mitaani, itakuwa rahisi kupunguza kasi ya ongezeko la watoto hao nchini kwani wao wanawakuta katika mazingira magumu na ya kusikitisha.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Vijana, Aziza Sleyum Ally, anasema kuibuka kwa maambukizo na vifo vya watu kutokana na ugonjwa wa UKIMWI, kumesababisha familia nyingi kukosa viongozi na hali hiyo kusababisha wanafamilia kusambaratika.

“Hali ni mbaya zaidi kwa familia ambao zimeondokewa wazazi wote wawili na kuacha watoto wadogo bila mtu wa kuwaongoza. Matokeo yake watoto hao wanajiingiza katika biashara na hatima yake kuishia kuwa watoto wa mitaani,”anasema.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora Mhashamu Mario Abdallah Mgulunde, anadokeza kuwa kuvunjika kwa maadili na ndoa katika jamii ni moja ya sababu zinazosababisha kuwa na watoto wa mitaani, ambao kutokana na kukosekana kwa malezi ya wazazi au walezi wao, wanajikuta wakiishi katika maisha yasiyo na msaada na kukata shauri kuingia mitaani.

Amesema udhaifu wa baadhi kushindwa kuishi maadili ya dini au jamii, unawakosesha dira ya kuwaongoza katika maisha yao na matokeo yake ni kuishi katika mifarakano ya kifamilia hali inayosababisha watoto kukimbia makwao.

Mmoja wa watoto wanaoishi katika kituo hicho, Toyi Musa (5), anaamini kuwa kufiwa na wazazi kunachangia watoto kwenda kuishi mitaani kutokana na kukosekana kwa malezi ya dhati kutoka kwa jamaa inayorithi dhamana hiyo.

Mtoto huyo ambaye awali alikuwa akiishi na wazazi wake katika kijiji cha Kazulamimba mkoani Kigoma, anasema kuwa kama isingekuwa kufiwa na wazazi wake, yeye na dada yake Ashura Musha (9) wasingeweza kuondoka kijijini kwao na kukimbilia mjini Tabora.

Mtoto huyo amesema kuwa walilazimika kuondoka kwao baada ya kufiwa na wazazi wao na hivyo, kukosa mtu wa kuwatunza na kukimbilia mjini Tabora kwa lengo la kutafuta kazi.

“Tulikuwa tunaishi na wazazi wetu, lakini baada ya wao kufariki tulikosa mtu wa kututunza, tukaamua kupanda treni tukaja Tabora kutafuta kazi tuliambiwa huku kuna kazi”, ndivyo anavyoelezea mtoto huyo.

Kila mmoja katika jamii kwa kutumia upendo wa kimungu ulipo ndani yake, awasaidie watoto hawa ili wamjue Mungu na kuishi maisha mema kiadilifu.

Mwisho ulitolewa mwito kwa jamii nzima kutoa kipaumbele katika suala zima la malezi kwa watoto, hasa wale waliopoteza wazazi wao; kwani wao wanahitaji kupewa matumaini na upendo zaidi.

ECAWIDNET: Mtandao unamkomboa mwanamke asinyanyaswe

VIKUNDI mbalimbali duniani vikiwemo vya  Kitaifa na Kimataifa, vimepiga hatua katika suala zima la kumkomboa mwanamke. Moja ya vikundi hivi ni Mtandao wa Maendeleo ya Akinamama chini ya Kanisa Katoliki katika nchi za Afrika Mashariki na Kati (ECAWIDNET). Katika Makala haya, Mwandishi Dalphina Rubyema anaeleza zaidi.

HIVI sasa mataifa mbalimbali duniani yanaoonekana sasa kuithamini kazi kubwa inayofanywa na mwanamke tofauti na siku za nyuma ambapo mwanamke alionekana hana manufaa yoyote mbele ya jamii mbali na kuwa kama chombo cha starehe na uzalishaji mali katika familia.

Enzi hizo, mwanamke alichukuliwa kama kiumbe asiyehitaji haki na usawa zaidi ya kuolewa na kuzaa watoto pamoja na kumstarehesha mumewe.

Hata miongoni mwao, baadhi ya wanawake hawakuwa na chaguo lolote katika kumpata mume, mbali na chaguzi na maamuzi yaliyofanywa na wazazi wao.

 Kazi za mwanamke hazikuishia hapo, bali pia wanawake walitumika kama chombo cha kuzalishia mali.

Ni dhahiri kuwa licha ya kazi kubwa waliyoifanya ikiwa ni pamoja na maandalizi ya mwanzo hadi mwisho ya shamba, bado baada ya mavuno kuuzwa na pesa kupatikana, ni baba pekee aliyekuwa ndiye maamuzi mkuu na wa mwisho juu ya matumizi ya pesa hiyo.

Wanawake hawakushirikishwa kabisa katika masuala ya elimu na kama ilitokea wakasomeshwa, basi namba yao ilikuwa ni ndogo  ikilinganishwa na namba ya wanaume.

Lakini, kadri siku zilivyozidi kuendelea, ndivyo mashirika mbalimbali duniani yalivyoona umuhimu wa kumkomboa mwanamke.

Tanzania haikuwa nyuma katika suala hilo. Nayo ilisimama kidete kuhakikisha kuwa, mwanamke anapata haki na heshima anayostahili kama ilivyo kwa wanamme.

Katika kuhakikisha mwanamke anapata elimu, Serikali ilianza kutoa nafasi za upendeleo katika shule na vyuo mbalimbali vikiwemo vile vya Elimu ya Juu.

Serikali ya Tanzania haikuishia hapo, bali pia ilianza kuwashirikisha wanawake katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Hadi sasa wanawake wanapewa nafasi za uongozi na kuna wanawake wengi wenye nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwa ni pamoja na uwaziri, ubunge wa kuchagulia na hata wapo wabunge wa viti maalumu na viongozi katika nyanja mbalimbali.

Aidha, wanawake nao kwa upande wao hawapo nyuma katika kutetea maslahi yao na sasa wameunda vikundi mbalimbali vya kuwakomboa kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na hata kijamii.

Vikundi hivi vimeanzia ngazi ya shina hadi ngazi ya kimataifa.

Moja ya vikundi vyenye hadhi hii ya kimataifa ni Mtandano wa Maendeleo ya Akinamama katika Afrika Mashariki na Kati (ECAWIDNET).

Mtandao huu ulioanzishwa mwaka 1993, unavijumuisha Vitengo vinavyohusika na masuala ya Maendeleo ya Akinamama katika nchi za Umoja na Ushirikiano katika Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika nchi za Mashariki mwa Afrika (AMECEA).

Madhumuni ya kuanzishwa kwa Mtandao huu unaozihusisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Eritrea, Sudan, Ethiopia, Malawi na Zambia ni kuimarisha umoja na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ukiwamo ujuzi na utaalamu.

Waratibu wa Vitengo vya Maendeleo ya Wanawake katika nchi husika, ni wahusika wakuu katika mpango huu.

Tangu mtandao huu uanzishwe mambo mbalimbali yamekwisha fanyika. Miongoni mwa mambo hayo ni warsha za mafunzo, wanachama wa mtandao huo kubadilisha vifaa vya kufundishia, kuweka bayana mipango mbalimbali ya kuendeleza Mtandao pamoja na uandaaji wa vitabu mbalimbali vilivyobeba ujumbe wa kumkomboa mwanamke.

Miongoni mwa vitabu hivyo, ni  Unyanyasaji Dhidi ya Wanawake cha mwaka 1996 na kitabu cha Wanawake na Usawa cha mwaka 2001.

Mikakati ya Mtandao huo kama ilivyoainishwa na Kamati Tendaji ilipoketi nchini Tanzania Julai 9 hadi 13 mwaka jana, ililenga kutoa changamoto ya kuwakomboa wanawake kulingana na mazingira wanayoishi kwa hivi sasa kuanzia ngazi ya Taifa hadi Kimataifa.

Vile vile, Mtandao huo unalenga kuhakikisha unalinda na kuendeleza haki za mwanamke pamoja na kumkomboa mwanamke kiuchumi ambapo suala zima la uanzishaji wa vikundi vya kuweka na kukopa, linahamasishwa.

Vile vile, ECAWIDNET inaweka nguvu zaidi katika suala zima la kupinga unyanyasaji wa mwanamke likiwemo suala la kutahiriwa na kurithiwa.

Katika kuhakisha Mtandao huu unafanya kazi yake kama inavyo takiwa, kila mwaka hufanyika Mkutano ambao huwashirikisha wawakilisha kutoka nchi mbalimbali zinazounda Mtandao huu na mkutano huu hufanyika nchi moja baada ya nyingine.

Mwaka huu, mkutano huo umefanyika Septemba Mosi hadi 14, nchini Malawi.

Mratibu wa ECAWIDNET, Bibi Oliva Kinabo, anasema pamoja na mambo mengine, mkutano huo ulilenga kuangalia “Mafundisho ya Kanisa Katoliki kwa Jamii”.

Anasema katika mkutano huo liliangaliwa suala zima la nafasi ya mwanamke katika mafundisho ya Kanisa kwa jamii.

Anasema Tanzania iliwakilishwa na wajumbe watatu ambao ni Mratibu wa Mtandao wa Maendeleo ya Akinamama nchini (WID) (Bibi Oliva Kinabo mwenyewe), Mratibu wa WID, Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Bibi Bertha Kayila na Mratibu wa WID Jimbo Kuu la Arusha, Bibi Mackrine Rumanyika.

Anasema pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo pia walitembelea vikundi mbalimbali vya akina mama nchini Malawi ambapo walishuhudia shughuli zinazofanywa na vikundi hivyo.

Anavitaja  vikundi vilivyotembelewa kuwa ni Mt.siliza kilichopo kwenye Jimbo Katoliki la Lilongwe.

Bibi Kinabo anasema kikundi hiki ambacho kipo chini ya usimamizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lilongwe, lengo lake ni  kuwainua wanawake kiuchumi na kijamii kwa kuwapa mafunzo na mikopo yenye riba nafuu.

“Wanakikundi wanafundishwa jinsi ya kuendesha miradi midogo midogo likiwemo suala la kazi za mikono,” anasema Bibi Kinabo.

Aidha, washiriki hao walitembelea kikundi cha MAU ambacho kinahusika na masuala ya uzazi wa mpango kwa njia ya asili.

Anasema katika mkutano huo wa siku 12, maamzi na mapendekezo ya washiriki yalikuwa ni kupinga kwa kauli moja suala la kuendelea kuwanyanyasa wanawake na watoto likiwemo suala la usafirishaji wa makundi haya kwa lengo la unyanyasaji.

“Unajua kuna baadhi ya watu ambao wanatoa wanawake na watoto sehemu moja kwa ahadi za kuwapatia kazi inayofaa, lakini wakisha wafikisha wanakotakiwa, hufanyishwa kazi zinazodhalilisha utu wao,” alisema.

Vile vile washiriki hao walitoka na msimamo kuwa, watu wa jinsia zote bila kujali rangi, wala umri  wana haki sawa mbele ya macho ya Mungu, hivyo katika kupambana na suala zima la UKIMWI kila mmoja anatakiwa awe na maamuzi juu ya mwili wake.

Hata hivyo, Mratibu huyo wa ECAWIDNET anasema kuwa baadhi ya nchi zilizopo kwenye Mtandao huo, hazishiriki mikutano katika muda unaotakiwa kulingana na hali ya kisiasa katika  nchi zao.

Mfano mzuri ni nchi ya Sudan, mwaka jana nchi hiyo haikupata mwakilishi kutokana na kuchelewa kutolewa kwa visa ya kusafiria.

Vile vile anasema kuwa miongoni mwa nchi wanachama wa mtandao huo, hazina uhusiano mzuri hali inayofanya nchi hizo zisiwe wenyeji wa mkutano.

“Mfano Eritrea na Ethipoia ni chui na paka, kwa hiyo ukifanyia mkutano Eritrea huwezi kupata mshiriki kutoka Ethiopia, vile vile ukifanyika Ethiopia huwezi kumpata wa Eritrea. Hivyo, ili wahusika wote wahudhurie mkutano, inabidi nchi hizo mbili zisiwe wenyeji wa mkutano,” anasema.

Mkutano huo uliofanyika nchini Malawi, ndiyo uliomchagua Bibi Oliva Kinabo kuwa Mratibu wa Mtandao huo, kabla ya hapo alikuwa Katibu wa Mtandao.

Neokatukumenato si Dhehebu, wala Ulokole ndani ya Ukatoliki

Historia ya Kanisa imeingia sasa katika milenia ya tatu ambapo Kanisa limeendelea kuwapo, kumshuhudia Kristu na kuwasaidia watu kukomaa katika ujuzi na imani kwa Mungu.

Njia mbalimbali zimejitokeza ndani ya Kanisa ili kulifanya Kanisa kuendelea kutimiza azma yake ndani ya nyakati zinazobadilika, bila kubadilika kwa mafundisho ya Kristu.Neokatukumenato ni moja ya njia hizo ambazo sasa Kanisa linazifanyia uchunguzi ili kuuona mchango wake katika kuitamadunisha tunu hii ya Imani. Katika makala hii Padre SIFFREDUS RWECHUNGURA wa Parokia ya Mt. Yosefu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, anafafanua zaidi juu  ya Utume wa jumuiya hii.

Njia ya Neokatekumenato ni nini?

Tunaweza kuieleza Njia ya Neokatekumenato kwa njia mbili; kwanza kutokana na neno lenyewe; pili kutokana na utume wake.

Neno Neokatekumenato linaonekana kama neno geni sana kwetu. Lakini tukichunguza zaidi tutagundua kwamba si neno geni sana, kwani tumeishasikia maneno kama ‘wakatekumeni’, ‘katekumeni’, n.k Kimsingi neno hili asili yake ni maneno hayo. Neno Neokatekumenato limeundwa na maneno mintilafu mawili: ‘neo’ na ‘katekumenato’.

'Neo' ni neno la kilatini maana yake ‘mpya’. Katekumenato ni malezi au kipindi cha ukatekumeni. Mkatekumeni ni yule ambaye  anaandaliwa kwa ajili ya ubatizo. Kwa hiyo tunaweza kusema Neokatekumenato ni katekumenato mpya ; ikiwa na maana kwamba siyo tu inajumuisha wale wanaojiandaa kubatizwa bali ni zaidi ya hao kama tutakavyoona hapo mbele tutakapoelezea utume wake.

Kwa upande mwingine tunaweza kuielezea njia ya Neokatekumenato kufuatana na maneno ya Baba Mtakatifu Yohana Paulo wa pili aliyoyasema katika waraka wake ‘Ogniqualvota’ wa Agosti 30, 1990 : ‘ Naitambua Njia ya Neokatekumenato kama utaratibu endelevu wa malezi ya kikatoliki yaliyomuafaka kwa jamii yetu na kwa nyakati zetu’.

Kimsingi Njia ya Neokatekumenato nia yake au utume wake ni kumsaidia Askofu wa Kanisa mahalia kama njia mojawapo ya utekelezaji kijimbo wa kazi za uingizaji katika Ukristu na elimu endelevu katika imani kwa wahusika kama wanavyoagizwa na Mababa wa Mtaguso wa pili wa Vatikano na Magisteria ya Kanisa.

Kwa maana hiyo, Njia ya Neokatekumenato inaweza kuelezwa kuwa ni makusanyiko wa shughuli zifuatazo :

-          Neokatekumenato au katekumenato baada ya ubatizo ;

-          Elimu au malezi endelevu katika imani

-          Katekumenato kwa wale ambao bado hawajabatizwa ;

Sasa tuangalie kiundani zaidi shughuli hizi za Njia ya Neokatekumenato.

 I.  Neokatekumenato au katekumenato baada ya ubatizo

 Walengwa

Kama nilivyosema awali, njia ya Neokatekumenato ni nyenzo iliyo chini ya Askofu mahalia kuwasaidia waliobatizwa kuishi kwa ukamilifu ahadi zao za ubatizo. Kwa maana hiyo wafuatao waweza kufaidika na chombo hiki:

-          Waliolegea katika imani;

-          Ambao hawakuinjilishwa au kupata katekesi vya kutosha

-          Wanaotaka kukua na kukomaa katika imani.

-          Wanaotoka katika madhehebu mengine ambayo hayako katika ushirika kamili na Kanisa Katoliki.

 Hii inawajumuisha hata mapadre na watawa ambao wanataka kuishi kwa ukamilifu ahadi zao za ubatizo kwa njia ya Neokatekumenato. Katika kufanya hivyo huweza vilevile kutoa huduma mbalimbali kwa wahusika kufuatana na wito au nafasi zao, mfano kuongoza ibada mbalimbali n.k

 

Jumuiya za Neokatekumenato

 

Neokatekumenato  huendeshwa parokiani katika jumuiya ndogondogo zinazoitwa ‘jumuiya za Neokatekumenato’ chini ya uangalizi na malezi ya paroko wa parokia husika pamoja na wasaidizi wake.

 

Utaratibu wa kujiunga na jumuiya za Neokatekumenato

 

Jumuiya za Neokatekumenato huanzishwa parokiani kwa mwaliko wa Paroko.

Makatekista ambao ni waamini ambao tayari wamo katika jumuiya za Neokatekumenato huja kwenye parokia husika na kuwaalika waamini kuja kusikiliza katekesi. Halafu kufanya ‘katekesi za mwanzo’ ambazo huendeshwa kwa kipindi cha miezi miwili. Katika kipindi hiki cha miezi miwili katekesi  hizi hufanyika mara mbili kwa juma kwa muda wa saa moja kila mkutano. Kipindi hiki cha katekesi za mwanzo humalizika kwa mkutano na kuishi pamoja wa siku tatu ambao hufanyika kwenye nyumba  mbalimbali za mafungo. Katika mkutano huo huzaliwa jumuiya ambayo huanza kutembea chini ya miguu au misingi mitatu ambayo ni muhimu kwa maisha ya Kikristu kama walivyosisitiza Mababa wa Mtaguso wa pili wa Vatikano: yaani Neno la Mungu, Liturujia (Ekaristi) na Jumuiya.

 

Neno la Mungu, Liturujia (Ekaristi na Jumuiya)

 

Kwa kuadhimisha ibada ya Neno la Mungu mara moja kila juma, ambamo wahusika hushiriki kikamilifu kwa kuandaa, halafu kutoa mwangwi- yaani mang’amuzi baada ya kuoanisha Neno la Mungu na maisha halisi ya mhusika- polepole wahusika hutambua hali ya mapungufu, hali ya dhambi, lakini vilevile hugundua huruma na upendo wa Mungu alio nao kwa mdhambi. Kwa njia hiyo mhusika huweza kuanza safari ya wongofu (toba) akisaidiwa na neema kutokana na sakramenti za Kanisa hasa Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi. Polepole huanza kuonja uhuru halisi (uhuru waw ana wa Mungu) na kuanza kugundua na kuishi ahadi zake za ubatizo ambazo huwa dhahiri katika jumuiya na jamii kwa ujumla.

 

II.       Elimu au malezi endelevu katika imani

 

Kugundua na kuishi ahadi zako za ubatizo sio kazi ya siku moja, ndio maana tunahitaji malezi endelevu katika imani. Malezi yanayotumiwa na njia ya Neokatekumenato si mengine bali ni kuendelea kuazimisha Neno la Mungu kila juma na kuadhimisha Ekaristi.

Ibada hizi hufanyika katika jumuiya ndogo ndogo za Neokatekumanato ambamo mhusika akisaidiwa kwa Neno na Ekaristi, vile vile  husaidiwa na wanajumuiya wenzake kwa kumuita kwa wongofu hasa anapotambua kwamba anashindwa kwa namna moja au nyingine kuwapenda wengine katika jumuiya.

Kwa njia hiyo wanajumuiya huwa kioo au nyenzo wao kwa wao kujitambulisha hali zao za mapungufu na kwa njia hiyo kukimbilia msaada wa neema ya Mungu kwa njia mbalimbali. Pole pole ishara za ‘umoja na upendo’ huanza kuwa dhahiri katika jumuiya, ishara ambazo kristu alisema zitawafanya watu watambue kuwa sisi ni wafuasi wake na kwamba alitumwa na Mungu (Taz. Yoh. 13,34-35 na Yoh 17, 21-23).

 

III  Katekumenato kwa wale ambao hawajabatizwa

 

Njia ya Neokatekumenato vilevile ni chombo cha kumsaidia Askofu kwa uingizaji katika ukristu kwa wasiobatizwa. Wahuska hushiriki katika ‘katekesi za Mwanzo, na baadaye huendelea kushiriki Neno la Mungu katika jumuiya . Wakatekumeni hutumia mafundisho kutoka mababa wa Kanisa, hati mbalimbali za Mtaguso wa pili wa Vatikano na Magisteria, Katekisimu ya Kanisa Katoliki na mafundisho kutoka waandishi wa masuala ya kiroho waliokubaliwa na Kanisa. Huendelea na mafundisho hayo mpaka Kanisa linapowaona wako tayari kupokea ubatizo.

 

Itaendelea toleo lijalo