Kijue Kilimo cha Kujinusuru

Maingilio: Katika toleo lililopita tuliona kuwa kilimo cha kujinusuru ni rahisi kukimudu kinakubalika katika jamii ni rahisi kutekeleza na kueneza kwa sababu jirani anaweza kuona afanyalo mwenzake. Sasa endelea.

Njia za kudhibiti mmomonyoko wa udongo

 

Udongo wa juu wa ardhi wa kawaida huondolewa na maji au upepo kwa ajili ya mmomonyoko wa ardhi ya juu ambayo ina rutuba nyingi ya kuifanya mimea iweze kustawi vizuri na hatimaye kutoa mavuno mengi na bora. Tunajua kuwa udongo ulio chini ya tabaka la juu hauna rutuba ya kutosha ya kuwezesha mazao kustawi vizuri. Kutoweka kwa udongo wa juu toka shambani au bustani kwa njia ya mmomonyoko ni hasara kubwa sana, kwa vile kunasababisha upungufu wa mavuno. Hivi basi lazima kuzingatia hifadhi ya ardhi ikiwa mkulima anataka kupata mazao bora.

Njia za kuhifadhi ardhi zinaweza kutumiwa kwa kutegemea hali ya hewa, mazingira ya eneo kama ni maeneo ya mwinuko au tambarare. Hata hivyo zinaweza kutumika njia mbili au tatu katika shamba moja.

Ziko njia kuu mbili za kuhifadhi ardhi. Njia za asili au za kienyeji na njia ya kisasa ambazo zimefanyiwa utafiti yakinifu na wataalamu.

 

Njia za asili

 

Huko Mbinga wenyeji wake walilazimika kubuni kilimo cha ‘ngoro’ au ‘Ingoro’. Sehemu kubwa na wilaya hiyo ina miteremko mikali. Wataalamu wakongwe kama akina Bike (1938), Stenhouse (1994), Temu na Bisanda (1966) wanaeleza kuwa Wamatengo walilazimika kutumia kilimo hicho ili kuhifadhi udongo mzuri ulio katika miteremko hiyo. Ngoro hulimwa na kuchimba vishimo katika miteremko hiyo.

Ngoro hulimwa kwa kuchimba vishimo katika miteremko na kupanda mazao kama maharage,mahindi, ngano, kwenye kingo za vishimo hivyo. Mkulima alifyeka shamba, halafu alipanga nyasi zilizokatwa katika mistari kwenda juu mpaka  chini; na toka upande wa kushoto kwenda kulia. Ukitazama toka mbali majani hayo yanaonekana kama masega ya asili. Kisha mkulima alipindua udongo wa chini kuwa juu na chini ya udongo wa juu kukaa nyasi na udongo wenye rutuba.

Nyasi zilizofunikwa hugeuka kuwa mboji na polepole udongo wenye rutuba huongezeka. Maji ya mvua  yakisimama katika vishimo hivyo vidogo vidogo na hivi kulinda unyenyekevu wa ardhi na kukinga mmomonyoko wa ardhi.

Tunaelezwa pia kuwa wahehe na Wabena ambao waliishi huko Iringa walisifika sana kwa ulimaji wa vinyungu katika mabonde na kandokando ya mito ambamo walipanda maharagwe, viazi mviringo.

Mtindo huu wa  ulimaji ni wa matuta ambao hutunza maji na unyevunyevu. Zaidi ya hayo huzuia mmomonyoko wa udongo.

Itaendelea

Chozi la Matumaini kwa Watoto walioathirika kwa UKIMWI (2)

Na Pd. Richard Mjigwa

Sehemu hii ya awamu ya kwanza ya mradi wa Kijiji cha Matumaini, kunatarajiwa kujengwa Maabara ya kisasa kwa ajili ya uchunguzi wa Ugonjwa wa UKIMWI na maendeleo yake.

Ama kwa hakika kituo hiki kitasaidia kutoa habari katika mapambano dhidi ya janga la UKIMWI kwenye mikoa iliyoko Kanda ya Kati.

Kijiji hiki cha Matumaini kitakuwa pia na kituo cha watoto wadogo pamoja na shule ya msingi itakayokuwa inawahudumia hata watoto majirani, ili kuweza kutoa matumaini zaidi katika tunu ya maisha. Kijiji hiki kinapokea watoto yatima na wale walioathirika kwa Virusi vya UKIMWI kutoka mikoa ya Dodoma, Morogoro na Singida. Lakini nafasi ikiruhusu watoto kutoka sehemu nyingine za nchi watapewa nafasi pia.

Ujenzi wa Kijiji hiki cha Matumaini ni ishara wazi ya jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anavyoweza kubadili miradi ya kibinadamu, ili kukidhi mipango ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Hiki ni kijiji ambacho imani na sala vinakumbatiana. Huu ni mwelekeo chanya wa kupambana na janga la ugonjwa wa UKIMWI, kwa kuchochea matumaini kwa siku za usoni.

 Haya ni mapambano mazito yanayoyajumuisha makundi mbali mbali katika jamii, ili kupambana kufa na kupona dhidi ya gonjwa la UKIMWI, kwa upande wa Serikali na dini mbali mbali. Watoto ni tumaini la mwendeleo wa Kanisa na taifa kwa ujumla. "Huu kwa hakika ni utajiri wa jamii yoyote ile". Haya ni maneno mazito yaliyotolewa na Mhashamu Askofu Mkuu Luigi Pezzuto, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, wakati wa mahubiri yake. "Upendeleo kwa watoto katika historia ya maisha ya Kanisa si jambo geni sana, kwani tayari kuna mtu aliyetangulia kuonesha njia na huyo si mwingine bali ni Yesu Kristu mwenyewe", alisema Askofu mkuu Pezzuto.

Awamu ya pili ya Kijiji cha Matumaini ni kuhakikisha kwamba mpango huu unawanufaisha watoto yatima walioathirika na UKIMWI wapatao mia nne, lakini ambao bado wanayo nafasi ya kuishi pamoja na ndugu na jamaa katika mazingira ya mkoa wa Dodoma. Watoto hao watahudumiwa huko huko wanakoishi kwa kupatiwa ushauri nasaha, elimu pamoja na huduma ya matibabu.

Kwa vile hakuna mtoto aliyejichagulia kubaki yatima, basi Kijiji cha Matumaini kitatoa pia msaada wa kiuchumi katika kuboresha matumaini ya maisha ya watoto hao.

Watoto hao pia watapata nafasi ya kutumia huduma mbali mbali zinazotolewa na Kijiji cha Matumaini kama zilivyobainishwa katika awamu ya kwanza.

Akitoa shukrani zake za dhati kwa Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, Mkuu wa mkoa wa Dodoma Bw. Isidori Shirima, aliwashukuru Masista hao kwa jitihada zote walizofanya hadi kufikia hapo na kwamba, Serikali itaendelea kushrikiana na Kanisa katika kumhudimia mwanadamu.

Ufunguzi wa Kijiji cha Matumaini lilikuwa ni tukio la aina yake katika kuleta matumaini mapya kwa wale walioathirika na gonjwa la UKIMWI. Tabasamu lililosindikizwa na mafuriko ya machozi lilionekana miongoni mwa wageni waalikwa, hasa pale watoto hao walioathirika na UKIMWI walipokuwa wanacheza na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw. Isidori Shirima kana kwamba ni watoto wa familia yake. Busu la upendo lilipotolewa kwa watoto watatu wanaofungua Kijiji hiki cha Matumaini na Mhashamu Askofu mkuu Luigi Pezzuto na Mkuu wa Mkoa Bw. Isidori Shirima liliwaacha wengi wakiogelea katika dimbwi la machozi ya matumaini.

Awamu ya tatu ya Kijiji cha Matumaini ni utoaji wa Ushauri nasaa kwa wanawake wajawazito ili kuchunguza maambukizo ya Virusi vya UKIMWI kabla ya kujifungua, ili waweze kusaidiwa kujifungua salama na hivyo kupunguza uwezekano wa maambukizo kwa watoto ambao hawajazaliwa.

Wanawake wajawazito wapatao ishirini na tano wataweza kuhudumiwa kwa mara moja katika Kijiji cha Matumaini juma moja kabla ya kijifungua na juma moja baada ya kijifungua, ili waweze kupewa mbinu mbadala katika kuwatunza watoto wao bila kuwanyonyesha maziwa ikiwa kama wameathirika na Virusi vya UKIMWI.

Ujenzi wa Kijiji cha Matumaini ulianza mwezi Juni mwaka jana. Hadi sasa zaidi ya dolla za Kimarekani zipatazo laki sita zimekwisha tumika katika shughuli za ujenzi. Baadhi ya nyumba zimekamilika na tayari zimeanza kutumika, bado ujenzi uko mbioni kukamilisha majengo yaliyobaki.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili amekuwa ni kati ya wafadhili wakuu wa Kijiji hiki cha Matumaini. Yeye amechangia ujenzi wa nyumba moja ambayo tayari imeanza kutumika. Wafadhili wengine ni Kikundi cha "AMICI delle Mission" kutoka Bagnolo Mella nchini Italia pamoja na wafadhili wengine wa ndani na nje ya nchi ambao wanapenda chozi la matumaini libaki katika sakafu ya mioyo yao. Watoto Hassani na Amani ndiyo sehemu kubwa ya ufanisi katika Kijiji hiki cha Matumaini.

Ni matumaini ya Masista Waabuduo Damu Azizi kwamba, watawapatia watoto hao matibabu, matunzo na zaidi ya hayo pendo la kifamilia katika kipindi hiki wanaposafiri pamoja kwenye hii hija ya matumaini. 

sababu zinazo changia kushamiri kwa uchumba  sugu (2)

    Na Mwandishi Wetu

Sababu ya Tatu :

 Ukosefu wa kipato.Siku hizi  kuna ukosefu  mkubwa wa fedha na ajira hasa miongoni mwa vijana. Hali hii inachangia sana  ‘uhalalishaji’ wa uchumba sugu eti kwa vile uchumba sugu unapunguza gharama za mahari na harusi.

Rejea bei  ya ‘Mbuzi ya sale’ – kati  ya Wachaga

Bei  ya Ngo’mbe 40 wa mahari kati ya Wasukuma.

 

a)     Je huu ni                    ukweli ?

 Huu si ukweli hata kidogo. Kwa nini ? baadaye gharama huwa kubwa zaidi.

Gharama za talaka, ‘utengano, uchangudoa, uchunaji mabuzi. Mayatima wa UKIMWI, watoto wa mitaani ni kubwa kuliko zile za awali !!!.

 b)    Vile vile, kimaadili kama bado mmoja anayo dhamiri safi, hai na sahihi atapaswa kulipiwa uvunjaji timamu na wa makusudi wa sheria za Mungu na Kanuni za Kanisa.

c)     Kiuchumi, usuria  na mtengano na hata talaka utapswa kulipiwa zaidi – hata mara nne zaidi kama Zakayo alivyofanya : Soma Luka 19 :9

d)     Makabila mengi yamepunguza sana kima cha mahari.

 

Sababu ya Nne :

 Leo hii vijana wengi wanaoishi maisha ya uchumba sugu wanadai ‘kila mmoja anafanya hivyo’

a)     Je huu ni                    ukweli ?

 

Hapana, si kila mtu au kijana hapa Tanzania anaishi maisha ya uchumba sugu. Mara kwa mara hasa kutokana na saikolojia ya vionjo vyao, vijana wengi katika urika wanaweza ‘wakaipenda’ na ‘kuushabikia’ mtindo huo wa maisha ya uchumba sugu.

b)     Je si kweli kuwa Kristo amesema bayana kuwa mlango au njia ya kwenda mbinguni ni nyembamba ?

c)     Je  hatuoni umuhimu wa sheria, kanuni na miongozo katika maisha na Kanisa hasa katika kutuongoza tupende na kutenda tu  yale yaliyo mema ?

d)     Fundisho kutoka katika kielelezo cha kiafya.

Hebu tujaribu kufikiri kuwa kipo kijiji kimoja mahali fulani hapa Tanzania au Afrika. Katika kijiji hiki umri wa juu kabisa wa kuishi ni miaka 23 tu! Aidha, kati ya watoto wachanga sita, wanne hufa kabla ya kufikia umri wa miaka 5. Je ni nani angalikubali kushabikia lishe hiyo duni au desturi za kijiji hicho?

Hayupo. Hivyo basi, sisi kama Wakristo tunaona faida za kuishi maisha ya Sakramenti ya ndoa, basi tufanye hivyo hata kama inaonekana kuwa siku hizi ni wachache wanaochagua kilicho chema.

Sababu ya tano

 

Vijana wengi wanaamini kuwa maisha ya uchumba sugu ndiyo njia pekee ya kumpata mwenzi wa ‘kufaa’ kwa wakati uliopo.

Moja ya njia nzuri za kupima uwezekano wa kuishi pamoja kama mume na mke ni kuangalia jinsi wanavyoweza kustahimili matatizo dhidi yao.

Mara nyingi wasichana wanafikiri kuwa mapenzi kabla ya ndoa ndio ‘mbinu’ au ‘njia’ muhimu ya kumpa mwenzi. Mwishoni wasichana wengi hupata mimba na kuachika.

Yote haya huwaletea majuto makubwa maishani!.

 

Sababu ya sita:

 Siku hizi vijana wengi wanadai kuwa maisha yao ya uchumba sugu hayamwumizi mtu yeyote!

 

Je huu ni ukweli?

 Si ukweli hata kidogo. Ni jambo lililo dhahiri na wazi kabisa kuwa maisha ya uchumba sugu husababisha makovu mengi ya kisaikolojia kwa familia nzima. Utafiti unaonesha kuwa wazazi wengi wa pande zote huumia na kusononeka sana mara wanaposikia kuwa watoto wao wanaishi maisha ya uchumba sugu.

Aidha, wengi wao hunyimwa kupokea Ekaristi Takatifu kutokana na uamuzi wa maisha ya uchumba sugu wa watoto wao. Wazazi hao hujuta na kukumbuka jitihada za malezi kwa watoto wao hasa walipokuwa wadogo.

 

Sababu ya Saba

 Leo hii wanasema kuwa Kanisa sehemu nyingi linaonekana kuwa ‘kimya’ kuhusu uchumba sugu.

 Je huu ni ukweli ?

Kimsingi Kanisa haliko kimya. Linakemea sana hali hiyo hata hivyo, Yuda Iskariote alimsaliti Kristo. Je hali hii ilihalalisha usaliti huo ?

Mtakatifu Paulo naye aliwaasa na kuwagombeza wale wakristo wa Kanisa la Pergamo kutokana na tabia  yao  ya uasherati (Ufunuo 2 :15).

Tabia ya uasherati inakemewa aghalabu mara 14 katika kitabu cha Ufunuo peke yake.

Rejea Ufunuo 2 :15, 20-23 ; 21 :8 ; 22 :15). Mtakatifu Paulo anatukumbusha kuwa Wayahudi 23,000 waliangamizwa kutokana na uasherati (Rejea 1Kor 10 :8) Rej pia 1Kor 6 :9-10).

Ama kweli mapadre, wachungaji na walezi wanaowajibu mkubwa na wa pekee kabisa wa kukemea maisha  ya uasherati na uchumba sugu.

 

Sababu ya nane :

 Wapo baadhi ya vijana wanaohalalisha uchumba sugu kwa kile wanachodai kuwa haiwezekani kubadilika tena.

 

Je huu ni mwono sahihi ?

 Hapana, Mtakatifu Augustine wa Hippo alifaulu kubadilika na kufikia hatua ya juu ya utakatifu mwishoni mwa maisha yake.

 Basi vijana tuelewe kuwa kamwe hujachelewa  kuachana na upotovu, nenda ukaungame na kufanya toba

Daima huruma ya Mungu ipo kwa wale wanaomkimbilia na kufanya uongofu wa kweli. Tuzingatie ukweli  huu hasa katika mwaka huu wa  toba.

SATF ilivyo jizatiti kuwasaidia watoto yatima

WATOTO yatima wanahitaji msaada kama walivyokuwa wakipata kutoka kwa wazazi wao. Katika makala haya ya Mwandishi Joseph Kiboga anaeleza jinsi shirika liitwalo Social Action Trust Fund (SATF), linavyobeba jukumu hilo nchini.

MTOTO mwenye wazazi huridhika na maisha, hujiona yuko huru kwa sababu hupata mahitaji ya msingi kama vile elimu, chakula na malazi kulingana na uwezo wa wazazi wake. Lakini mtoto huyo huyo hukata tamaa, hujiona mpweke na mwenye kila aina ya shida anapopoteza wazazi hao.

Mahitaji ya mtoto, awe na wazazi au asiwe nao hayabadiliki, yanabaki ni vile vile kwani bado atahitaji kula, kujisitiri na kupata elimu ya kumwezesha kupambana na maisha.

Kutokana na mahitaji hayo, ndio maana wengi waliopoteza wazazi wao, huondoka nyumbani kwao kwenda mitaani kutafuta misaada mbalimbali itakayowawezesha kukidhi mahitaji yao. Hilo ni tatizo kubwa la kijamii katika nchi masikini kama Tanzania.

Kutokana na tatizo hilo kuongezeka siku hadi siku, mashirika kadhaa yasiyokuwa ya kiserikali, yameanza kujitolea kusaidia watoto wa namna hiyo katika harakati zake za kuondokana na tatizo hilo.

Moja ya mashirika hayo ni lile liitwalo 'Social Action Trust Fund' (SATF), ambalo limetumia mamilioni ya pesa kuhakikisha watoto hao wanapata elimu.

Mkurugenzi wa shirika hilo, Bw. Valentin Rweyemamu, anasema tatizo la watoto yatima ni kubwa licha ya jitihada zinazofanywa na shirika lake.

Anakiri kuwa shirika lake kusaidia  idadi ndogo ya watoto ikilinganishwa na wale wanaohitaji msaada.

 Bw.Rweyemamu anasema idadi ya watoto yatima nchini haipungui milioni moja, hivyo kufanya msaada unaotolewa na SATF  kutokidhi mahitaji halisi.

Kwa kutumia  msaada kutoka shirika la  Misaada la Serikali ya Marekani (USAID), limewezesha watoto yatima kupata misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupatiwa elimu.

Anasema tangu SATF ianze kuwasaidia yatima, watoto wameweza kusoma bila matatizo japo hawana wazazi.

Kuanzia Aprili mwaka 1998 shirika lilipoanzishwa, Bw. Rweyemamu anasema bodi ya wadhamini  iliidhinisha sh. milioni 600 ili zitumike kuwasaidia watoto yatima.

Mwaka  juzi anasema shirika liliwezesha  watoto yatima 10,621 kupata elimu katika shule mbalimbali katika mikoa 12 Tanzania Bara.

Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 263, ikilinganishwa na watoto 3,717, waliosaidiwa mwaka 1999.

Mikoa iliyonufaika  ni Pwani, Dar es Salaam, Iringa, Kagera, Kilimanjaro, Lindi, Mbeya na Morogoro. Mingine ni Mwanza, Ruvuma, Tabora na Tanga.

Mwaka jana  Bw. Rweyemamu anasema shirika lilitenga milioni.300 kuwahudumia watoto hao wakiwemo wa shule za sekondari ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 50 tofauti na mwaka juzi ambapo sh.  milioni 200 zilitumika.

Msaada wa mwaka jana ulisaidia  mikoa 14, mikoa miwili ikiwa ni mipya kuingizwa kwenye mpango huo, mikoa hiyo ni Kigoma na Mtwara.

Akieleza sababu ya ongezeko hilo, Bw. Rweyemamu  anasema limechangiwa na ongezeko la msaada wa  pesa kutoka sh. milioni 100, mwaka 1999 hadi kufikia sh. milioni 200 Mwaka juzi.

Sababu nyingine anasema ni kule kuweka viwango vya matumizi kwa kila mtoto, ambavyo mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) ambazo wanashirikiana nazo zilipashwa   kuzingatia.

Anasema viwango hivyo viliwekwa baada ya kubaini kuwa NGOs, nyingine zilisaidia idadi ndogo ya watoto mwaka 1999, na kujikuta zikitumia  pesa nyingi kwa kila mtoto.

Ili kuhakikisha pesa zinawafikia walengwa,Bw. Rweyemamu anasema  mashirika yanayohusika yanatakiwa kupeleka picha za watoto wanaosaidiwa, majina yao, shule wanazosoma, sahihi za wakuu wa shule na wahusika wengine.

“Misaada yetu inasaidia watoto wetu kupata elimu, tunawalipia karo, vitabu, sare za shule, usafiri na gharama nyingine,” anasema, Bw.Rweyemamu.

Anasema  kwa kuanzia SATF inatoa misaada kwa watoto yatima wa shule za msingi ili watoto hao, walau waweze kujua kusoma na kuandika.

Anasema wanafunzi walioanza nao shule za msingi kwa kuwagharamia, mwaka huu, wameanza kuwapeleka  sekondari.

“Baadhi ya watoto wetu tuliowasomesha wameweza kufaulu mitihani ya darasa la saba,” anasema na kuongeza:

“Baadaye watakaoshinda vizuri kwenda Chuo Kikuu tutawasaidia kuwapeleka huko”.

Kuhusu msaada unaotolewa katika mkoa wa Pwani, Bw.Rweyemamu anasema shirika lake linashirikiana na Chama cha Afya ya Msingi kwa wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (SHDHEPHA) kuwahudumia watoto hao.

Anasema mwaka jana, SATF ilikabidhi kwa SHDHEPHA, sh. milioni 10, hivyo kuweza kusomesha watoto 973.

Kwa mwaka huu, SATF imetoa sh.milioni 15, na kuwa msaada huo utaweza kuwasaidia walengwa wengi zaidi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa  Pwani, Bw Nicodemus Banduka anasema msaada unaotolewa na SATF katika mkoa huo umeweza kuwasaidia watoto wengi walengwa.

Anasema kasi ya ugonjwa huo, ni kubwa hivyo kufanya idadi ya watoto yatima kuongezeka mara kwa mara.

Bw. Banduka anasema 1998, mkoa huo ulikuwa na wagonjwa  420;  1999 waathirika 1056 na mwaka jana wagonjwa 5,405.

Hata hivyo anasema idadi hiyo inaweza kuwa mara tano kwani takwimu zilizopo kwa sasa zinakanganya.

“Mkoa wetu unaweza kuwa wa tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa, ingawa takwimu za zamani zinasema mkoa ni wa sita kitaifa,” anasema, Bw.Banduka.

Akieleza sababu ya kuongezeka kwa ugonjwa huo, Bw. Banduka anasema ni barabara kuu ya kwenda mikoani na kuzidi kukua kwa mji wa bagamoyo.

Bw. Banduka anasema mwaka jana, watu 3248 walipimwa damu  na 368 sawa na asilimia  11.4, walipatikana na virusi vya ugonjwa huo.

Ili kuhakikisha mkoa huo unapunguza kasi ya UKIMWI, anasema mkoa unaendesha kampeni ya uelimishaji watu ili wabadili tabia.

Mbali na mkakati huo, anasema wameanzisha kitengo cha kupima watu ugonjwa huo kwa siri, na majibu hayo yanakuwa siri ya daktari na mhusika.

Akieleza mbinu waliojiwekea kudhibiti maambukizo ya virusi kutoka kwa mama mjamzito kweda kwa mtoto, Bw. Banduka alisema wanawake wote wajawazito mkoani humo watakuwa wakipatiwa vidonge.

Anasema tayari mkoa umekubaliana na shirika moja la Hispania  linalojulikana kama Doctors of the World  litakalokuwa likitoa vidonge hivyo.

Ni wazi kuwa vidonge hivyo vitasaidia watoto wasipate maambukizo ya virusi hivyo wakati wa kuzaliwa au kwa kunyonya maziwa ya mama zao.

Mwalimu wa shule ya Twende Pamoja ya Kibaha, Bw. Julius Mbonea mbele ya Bw. Banduka na Bw.Rweyemamu alisema kuwa mkoani humo kuna watoto yatima waliokwisha anza kuonesha dalili za ugonjwa huo.

Mwalimu huyo,  anasema serikali iwatafutie dawa za kurefusha siku za kuishi ambayo yametangazwa kuwa tayari yanauzwa nchini.

Mbali na kuwa na dalili za ugonjwa huo, Bw. Mbonea anasema watoto wengi yatima hawana makazi na kuiomba serikali kuwapatia makazi ya kuishi..